Jumapili, 1 Mei 2011

SHERIA IMECHUKUA MKONDO WAKE, SASA HAKI IONEKANE IMETENDEKA.

MKURUGENZI wa Hoteli ya Kitalii ya South Beach Hotel ya jijini Dar es Salaam, Bw. Salim Nathoo (53), amepandishwa kizimbani juma lililopita katika Mahakama ya wilaya ya Temeke. Nathoo ambaye ni mkazi wa Mikocheni ‘A’ alisomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Khasim Mkwawa wa mahakama hiyo.

Mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo alitambulika kwa jina la John Mwangiombo (32).

Upande wa Mashitaka uliongozwa na Mwendesha Mashtaka, Inspekta wa Polisi Dastan Kombe na kudai kuwa, washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 10 mwaka huu majira ya saa 6.30 usiku eneo la Mjimwema Kigamboni.

Washitakiwa hao walishirikiana kwa pamoja kumpiga na kumchoma moto kijana Lila Hussen (34) na kumsababishia kifo kwa kumuhisi mwizi mara alipoingia hotelini hapo.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kwa kuwa Mahakama hiyo haikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Kesi iliahirishwa hadi Mei 2, mwaka huu kwa kutajwa tena na washitakiwa watakwenda kujibu shtaka hilo mahakama kuu.

Awali imedaiwa kuwa marehemu Lila alichomwa moto na washtakiwa hao baada ya kuingia hotelini hapo kwa ajili ya kuwatafuta wageni wake raia wa kigeni aliowasindikiza hotelini hapo jana yake na mara alipoingia hotelini hapo kwa kuwa hakuwa na muonekano mzuri wa hadhi ya kuwa hotelini hapo mmiliki huyo alitoa agizo la kukamatwa kijana huyo kwa kudai ni mwizi na baadae walimmwagia mafuta na kumvisha tairi na kumchoma moto na alianza kuungua huku wageni wake wakiwa hawajui kinachoendelea.

Taarifa ziliwafikia jamaa zake anaofanya nao kazi maeneo ya feri na walifika hapo na kumuokoa kijana huyo na kumkimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu.

Na muda machache baadae mkurugenzi huyo alipogundua kuwa si mwizi na kuona alifanya makosa alianza hatua za kukimbia nchini na aliwezwa kukamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere na kufikishwa kituo cha polisi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni