Jumamosi, 21 Mei 2011

KAHN APEWA DHAMANA.

Dominique Strauss-Kahn
Aliyekuwa Mkuu wa IMF Dominique Strauss-Kahn
Aliyekuwa mkuu wa shirika la fedha duniani, Dominique Strauss-Kahn, amepewa dhamana na jaji katika mahakama moja mjini New York.
Hii ni baada ya kushtakiwa rasmi kwa kujaribu kumbaka mhudumu wa hoteli moja.
Awali, Strauss-Kahn alijiuzulu kutoka kwa wadhifa wake kama Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Mawakili wa Bw Strauss-Kahn walisema yeye ni mtu mwenye heshima na kwamba hawezi kutoroka.
Mawakili wake wamemwambia jaji kuwa mkuu huyo wa zamani wa shirika la fedha duniani (IMF) yuko tayari kuwekwa chini ya kifungo cha saa 24 nyumbani na pia avalie kifaa cha elektroniki kitakachochunguza mienendo yake.
Mke wa Strauss-Kahn ambaye alikuwa mahakamani wakati wa kesi hiyo, alijitolea kutoa dhamana ya dola millioni moja.
Baada ya kipindi kifupi cha mapumziko jaji alikubali dhamana hiyo, lakini pia akapendekeza kutolewa kwa bima ya dhamana yake ya dola millioni tano.
Bali na kutoa dhamana, jaji aliamuru awekewe mlinzi mmoja aliyejihami wakati wote na pia asalimishe stakabadhi zake za kusafiri.
Strauss-Kahn sasa ameshtakiwa rasmi baada ya kikao cha baraza la uchunguzi, kilichohudhuriwa na mwanamke mwenye umri wa miaka 32 anayemtuhumu.
Baraza hilo liliamua kuwa Strauss-Kahn ana kesi ya kujibu.
Mwanamke aliyemfungulia mashataka ni raia wa Guinea, Magharibi mwa Afrika.
Strauss-Kahn amekanusha mashtaka yoke dhidi yake.
Anatarajiwa kufika tena mahakamani Juni sita, ambapo atatarajiwa kusema kama anakubali mashtaka dhidi yake au la.
Ikiwa, Strauss-Kahn, mwenye umri wa miaka 62, atapatikana na hatia, atahukumiwa kifungo cha miaka 25 jela.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni