Jumanne, 10 Mei 2011

KIKWETE AWATAKA MAWAZIRI KUELEZA MAFANIKIO YA SERIKALI

RAIS Jakaya Kikwete amesema mawaziri wamegeuka mifuko ya kufanyia mazoezi ya ngumi kwa kushambuliwa kutokana na tabia yao ya kushindwa kueleza mafanikio ya Serikali.

Mh. Rais Kikwete.

"Mmeshindwa kutetea mafanikio ya Serikali mpaka wanasema hatufanyi lolote kiasi cha kuonekana kweli hatujafanya kitu. Kuna mtaalamu alisema uongo ukizungumzwa sana unageuka ukweli.

"Tumeacha upotoshaji umefanywa bila kusahihishwa na sasa wananchi wanaichukia Serikali kwa sababu hawaelezwi kinachofanyika, lazima tuwe wa kwanza kusema taarifa zetu," amesema Rais Kikwete mjini Dodoma wakati anafungua semina elekezi ya viongozi na watendaji wakuu wa Serikali.

Amesema, tabia hiyo ya mawaziri imetoa mwanya kwa wasioitakia mema Serikali, kugeuza uongo kuwa ukweli.

Amewaagiza mawaziri hao kuwa wepesi kusahihisha upotoshwaji unapotokea kwa kuwa wakikawia kutoa taarifa sahihi, wanaigharimu Serikali.

Amekumbusha kuwa ,wataalamu wa habari na mawasiliano pia wanasema ukifanya kitu bila kuueleza umma, ni sawa na kutofanya jambo na kuhoji kwa nini mawaziri na makatibu wakuu wanashindwa kuwatumia maofisa habari kama wasemaji wa Wizara.

"Vyombo vya habari vipo, vinasubiri kupewa habari, lakini nyinyi hamtoi, mnabaki kulalamika eti vinapotosha.

"Mnawazuia maofisa wa habari kusema, kama ni lazima Waziri au Katibu Mkuu aseme, mbona siwasikii? Ndiyo maana wale vijana (maofisa habari) wamegeuka waandishi tu," amesema Rais Kikwete huku akiongeza kuwa hakumbuki lini mara ya mwisho kumsikia msemaji wa Wizara akitoa taarifa.

Amesema , mawaziri wengine hata wakiona upotoshwaji umefanyika, wanabaki kimya na kutoa mfano wa agizo la Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, kwa wizara mojawapo isahihishe upotoshaji.

Katika agizo hilo, Rais amesema, lilipofika katika wizara husika, badala ya kusahihisha upotoshaji uliotolewa, Waziri husika akapiga simu kwake na kuuliza kama ameagiza ufafanuzi utolewe.

"Waziri alinipigia simu akauliza eti hili umeagiza wewe? Nilimjibu pima mwenyewe," amesema Rais Kikwete na kuongeza kuwa inashangaza Waziri kaona upotoshaji na anauliza kuhusu kusahihisha.

"Katika jambo kubwa la Serikali, ni lazima Serikali iwasiliane na watu wake, wapeni fursa wasemaji, waingie katika vikao vya menejimenti na hata anapokuja mgeni, kama mnazungumza mambo ya Serikali kwa nini yeye asiwepo?" Amehoji.

Ametoa mfano wa Msemaji wa Ikulu ya Marekani kuwa amekuwa akitoa taarifa kila wiki na akiulizwa swali hasemi ngoja nikamuulize Rais Barack Obama kwa kuwa anajua kinachoendelea na hivyo anajibu tu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni