Jumamosi, 14 Mei 2011

MUSEVENI AAPISHWA RASMI JUZI KUONGOZA UGANDA KWA MUHULA MWINGINE.

RAIS Yoweri Museveni ameapishwa kuanza ngwe ya nne ya kutawala taifa la Uganda huku akitambia mafuta yaliyopo nchini mwake ambayo yataanza kutumika miaka mitatu ijayo.
Wakati Rais huyo anaapishwa kwa mbwembwe zote, mpinzani wake Kizza Besigye alikuwa
anawasili nchini humo kwa ndege ya Kenya Airways na kulakiwa na mamia ya wananchi ambao baadaye waliunga maandamano kutoka mjini Entebbe kuelekea Kampala.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Magharibi maandamano hayo yalitawanywa na askari wa ulinzi wa Uganda kwa kutumia virungu, mabomu ya kutoa machozi na risasi.
Akizungumza na taifa baada ya kuwa amekula kiapo, Rais Museveni alitangaza mwelekeo na sera zitakazoongoza taifa la Uganda katika miaka mitano ijayo, ikiwa ni pamoja na kuifanya Uganda nchi yenye pato la kati ifikapo mwaka 2016.

Rais Museveni pia ameahidi kuufanya uchumi wa Uganda kuwa uchumi wa kisasa kwa kuelekeza nguvu zake katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwa ni pamoja na kuzalisha umeme wa kutosha kusukuma maendeleo ya nchi hiyo.

Aidha, ameahidi kuwa Uganda itaanza kutumia mafuta yake yenyewe katika miaka mitatu ijayo
baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha mafuta kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Akizungumzia bei kubwa za mafuta na chakula nchini humo, Rais Museveni alisema kero hizo
ni za muda mfupi na akatangaza baadhi ya hatua ambazo Serikali yake itachukua kupambana na kero.

Hatua hizo ni pamoja na nchi hiyo kuagiza mafuta ya bei nafuu kutoka Sudan Kusini kabla ya nchi hiyo kuanza kuzalisha mafuta yake.

Sherehe za kuapishwa kwa Rais Museveni zilihudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete ambaye
yeye na ujumbe wake ulirejea nchini jana jioni baada ya kumalizika kwa sherehe hizo.

Katika sherehe hizo zilizofanyika kwenye Viwanja vya Sherehe za Kitaifa vya Kololo mjini Kampala, Rais Kikwete alishuhudia Rais mteule Museveni akiapishwa na Jaji Mkuu wa Uganda, Jaji Benjamin J Odoki kushika madaraka ya kuongoza Uganda kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Rais Museveni amekuwa madarakani tokea mwanzoni wa mwaka 1986 wakati alipokamata madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi.

Wageni wengine waliokuwapo katika sherehe hizo zilizochukua kiasi cha saa nne kuanzia saa nne asubuhi ni pamoja na Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Rais Joseph Kabila wa DRC, Rais Mteule wa Nigeria Goodluck Jonathan, Rais Sheikh Shariff Sheikh Ahmed wa Somalia na Rais mteule wa Sudan Kusini Salva Kiir ambayo itapata uhuru wake Julai mwaka huu.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hizo ni Rais Mohammed Abdulaziz wa Jamhuri
ya Saharawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia Meles Zenawi, Rais Mstaafu wa Kenya Daniel Arap
Moi na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping.

Nchi za Zambia na Burundi zimewakilishwa na Makamu wa Rais, nchi za Misri, Namibia na
Rwanda zimewakilishwa na Mawaziri Wakuu, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Algeria imewakilishwa na spika wa mabunge ya nchi hizo na nchi za Djibouti, Afrika Kusini, Mozambique, Congo Brazzavile, India na Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) zimewakilishwa
na mawaziri.

Kabla ya kula kiapo katika sherehe hizo za kuvutia, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Injinia Dk. Badru Kiggundu alitoa tangazo rasmi ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Uganda uliofanyika Februari 18 mwaka huu, 2011.


Katika Uchaguzi Mkuu huo Museveni, Mgombea wa chama cha NRM alishinda kwa asilimia 68 akifuatiwa na Kizza Besigye wa chama FDC aliyepata asilimia 26.

Kizza Besigye, ambaye amekuwa akiwania uongozi wa taifa kwa mara tatu na ambaye amekuwa akiongoza maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha nchini aliwasili
Entebbe akitokea Kenya ambako alikuwa akitibiwa majeraha anayodai kuyapata katika
maandamano ya hivi karibuni.

Besigye, ambaye alikataliwa kurejea nchini Uganda juzi Jumatano, alirejea jana na kutumia
siku nzima kufika Kampala kutoka Entebbe katika njia ambayo kwa kawaida ni dakika 45.

Hata hivyo imedaiwa na vyombo vya habari vya Magharibi kwamba ilipofika mchana vikosi
vya usalama vilimzunguka Besigye na watu wake na kuwatawanya kabla ya kuudhibiti
msafara wake na kuuelekeza moja kwa moja makao ya chama chake.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi katika njiapanda kadhaa kwenye barabara ya Kutoka Entebbe kuelekea Kampala huku waandamanaji wakiwarushia askari mawe.

Besigye na viongozi wengine wa upinzani kwa takribani mwezi mzima wamekuwa wakiendesha
maandamano mara mbili kwa juma kupinga kupanda kwa bei ya chakula na mafuta na serikaliw
aliyosema imejaa rushwa.

Besigye ambaye alikuwa wa pili katika kinyang'anyiro cha kuwania uongozi wa Uganda akiwa
na asilimia 20 ya kura amesema kwamba hatamtambua Rais Museveni na serikali yake.

Yeye alisema kwamba Museveni na yeye walipata asilimia chini ya 50 na hivyo kulihitajika uchaguzi mwingine kumpata mshindi.

Rais Museveni ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa Marekani wapiga kura wengi wamempatia
kura kutokana na kuweza kuirejesha nchi hiyo katika amani akichangia kuwapo kwa uchumi
wenye nguvu baada ya vurugu za miaka mingi zilizosababishwa na uasi na serikali za kidikteta.

Rais Museveni akihutubia alishutumu wapinzani kwa kutaka kuvuruga mafanikio ambayo taifa
hilo inayo na kusema kwamba vurugu hizo zitadhibitiwa.
Pia alizungumzia mafanikio aliyopatikana katika utawala wake na kusema kwamba wanafunzi
milioni nane walipata nafasi ya elimu ukilinganisha na watoto milioni 2.5 mwaka 1986.

Pia aliahidi kukabiliana na rushwa. Museveni alishukuru wananchi waliokusanyika katika
uwanja uliofanyika kiapo na kusema anawashukuru kwa kumpatia asilimia 68 za kura kuendelea kuongoza nchi hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni