Mabingwa wa sasa wa soka barani Afrika TP Mazembe, wamesema watakata rufaa kutokana na uamuzi wa Shirikisho la Kandanda Afrika- Caf, kuiondoa katika Ligi ya Ubingwa wa Vilabu kutokana na kumchezesha mchezaji asiyestahiki.
Wachezaji wa TP Mazembe.
Katika taarifa iliyotolewa muda mfupi baada ya uamuzi wa Kamati ya Maandalizi ya Caf kwa mashindano ya vilabu, klabu hiyo ya Congo imesisitiza haijavunja sheria kwa kumchezesha Janvier Besala Bokungu, ambaye klabu ya soka ya Simba ya Tanzania imemshutumu alivunja mkataba wake na klabu ya Esperance na kujiunga na Mazembe, hali iliyomfanya asistahili kucheza katika michuano ya Caf.
“Uongozi wa Mazembe unauona uamuzi wa Caf haukubaliki ndio maana haraka tutakata rufaa kutokana na uamuzi huo. Meneja wetu Mkuu Frederick Kitenge kwa sasa yupo Cairo akiangalia vipengele vyote vya kupata haki kwa klabu yetu,” Taarifa hiyo ya Caf imesomeka katika mtandao rasmi wa Corbeaux.
Iwapo rufaa ya Mazembe itagonga mwamba, watakosa nafasi ya kutetea ubingwa wao na pengine kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wa vilabu barani Afrika kwa mwaka wa tatu mfululizo, ambapo klabu hiyo imesema ndio lengo lao kuu msimu huu.
Simba Sports Club.
Katika hali nyingine, Chama cha taifa cha kandanda cha Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, kimetupilia mbali maombi ya Mazembe ya kutaka kuahirishwa mechi yake ya mwishoni mwa wiki dhidi ya DCMP, kwa sababu mabingwa hao wana ziara ya mazoezi nchini Brazil.
DCMP itadai pointi zote tatu iwapo Mazembe haitatokea uwanjani siku ya Jumapili. Kuna mashaka kama timu hiyo itasafiri kuelekea Marekani Kusini ili ikabiliane na DCMP.
Wachezaji wa TP Mazembe
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni