Lionel Messi ameshinda tuzo ya Fifa ya mwanasoka bora wa mwaka 2011 ya Ballon d'Or, na kuwa mchezaji wa nne katika historia duniani kushinda tuzo hiyo mara tatu. Mshambuliaji huyo kutoka Argentina mwenye umri wa miaka 24, aliwashinda Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na mchezaji mwenzake wa Barcelona, Xavi. Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson alishinda tuzo ya huduma kwa soka, huku meneja wa Messi, Pep Guardiola akipata tuzo ya kocha bora wa mwaka. Messi, ambaye aliwahi pia kushinda tuzo hiyo yenye hadhi mwaka 2009 na 2010, alikuwa mchezaji bora katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mwaka 2011, dhidi ya Manchester United, na pia alishinda ligi ya Uhispania, kombe la Supercopa la Uhispania, Kombe la Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la klabu mwaka jana
Teknolojia ya kutumia kamera katika goli huenda ikaanza kutumika katika ligi kuu ya Premier mwanzoni mwa msimu ujao wa 2012-13.
Halmashauri ya kimataifa ya chama cha mpira cha England itatoa uamuzi kama idhinishe mfumo huo ama la mnamo mwezi wa Machi 2012.Ikiwa itathibitishwa basi kiongozi wa FIFA Sepp Blatter anasema ligi za soka zitaweza kuutumia mwanzoni mwa msimu wa 2012-13 endapo utakua hauna kasoro wala hautagharimu fedha nyingi.
Mkuu wa ligi ya Premier ya England, Richard Scudamore amesema kwamba watautumia mfumo huo mara tu utakapoidhinishwa.
Teknolojia ya goli kuidhinishwa.
Blatter aliongeza kusema kwamba teknolojia hiyo inaweza pia kutumika katika michuano ijayo ya kombe la dunia la mwaka 2014 nchini Brazil .
Kwa miaka mingi mkuu huyo wa Fifa amekua akipinga matumizi ya teknolojia katika eneo la goli lakini inaelekea alibadili mawazo yake baada ya mabishano makali kuzuka mnamo mwaka 2010.













