Maiti waliosuswa Tarime waharibika
Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime;
UTATA wa mazishi ya watu wanne kati ya watano waliouawa baada ya tukio la kuvamia Mgodi wa North Mara wilayani hapa Mei 16 umeendelea, baada ya ndugu wa marehemu kuendelea kususa miili huku ikiendelea kuharibika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya.
Hadi Mei 21, ni mwili mmoja tu uliochukuliwa, huku mingine minne ikibaki mochari, kwa maelezo kwamba, ndugu wa marehemu wanamsubiri mganga wao na wanasheria ambao ni viongozi wa Chadema, Mabere Marando na Tundu Lissu.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo zinasema, wanandugu hao wamekataa kuchukua miili hiyo mpaka itakapochunguzwa, huku uchunguzi ukishuhudiwa na Marando na Lissu.
Miili ambayo mpaka jana ilikuwa haijachukuliwa ni ya mwanafunzi Emmanuel Magige wa
Nyakunguru, Chacha Ngoka mkazi wa Kewanja Nyamongo na waliokuwa wakazi wa Mugumu, wilayani Serengeti, Mwikwabe Marwa na Chawali Bhoke.
Mwili pekee uliochukuliwa na kuzikwa ni wa Chacha Mwasi wa Bisarwi Komaswa. Kutokana na kususia maiti, Kamishna wa Jeshi la Polisi anayeshughulia masuala ya Operesheni, Paul Chagonja, amesema jeshi lake linasikitishwa na baadhi ya wanasiasa kuingilia matatizo ya Makosa ya Jinai kwa kushawishi wafiwa kususia miili ya ndugu zao wakati inazidi kuharibika hospitali.
“Hakuna polisi aliyemfuata mtu yeyote aliyeshambulia askari wetu kwa mawe na silaha za jadi, pia hatujakataa kuwa waliouawa hawakupigwa risasi na polisi, sasa huyo mganga anayesubiriwa anatarajia kuja kuandika kuwa wameuawa na nini, kama si siasa kavu ya kusumbua ndugu za marehemu?” alihoji.
Chagonja alisema baadhi ya ndugu wa marehemu walitaka kuchukua miili ya ndugu zao, lakini baadaye wakasema wanasubiri daktari wao na wanasheria Marando na Lissu wafike kushuhudia, lakini tangu Jumatano zimekuwa zikitolewa ahadi za uongo huku miili ya marehemu hao ikiharibika.
Aliongeza kwamba, tayari Polisi ina taarifa kuwa, wafiwa wamehifadhiwa nyumbani kwa Diwani wa Chadema Mjini hapa (jina tunalo) na kuna ndugu vijijini wameshindwa kufanya shughuli zao za kujipatia kipato wakisubiri kuzika kwa sababu ya kukwamishwa na wanasiasa.
Kamishna Chagonja alisisitiza kwamba, Polisi inafanya uchunguzi wa mauaji hayo na kama itabainika kuwa askari walioua walifanya makusudi, sheria itafuata mkondo wake na hawezi kutoa hukumu kwa kuangalia upande mmoja.
Alisema kuna askari zaidi ya saba waliojeruhiwa kwa mawe akiwamo Mrakibu Simon Mrashani na Mrakibu Msaidizi Hassan Maya na wenzao watano.
Aidha, magari ya Jeshi yaliharibiwa kwenye mapambano hayo kati ya polisi na watu zaidi ya
800 waliovamia mgodi kutaka kupora mawe ya dhahabu.
Wakati ikiwa haijafahamika siku ambayo wanandugu hao wataridhia kuchukua miili ya ndugu zao, Mkuu wa Wilaya, John Henjewele, ameonya kwamba endapo ndugu wa marehemu hao watashindwa kuchukua miili hiyo na kuizika, Serikali itazika.
Aidha, aliwaonya wanasiasa, hususani wa Chadema wanaotajwa kujiingiza na kuligeuza tukio hilo kuwa la kisiasa, akiapa kwamba Serikali haitafumbia macho wanaochochea uhalifu.
Mei 20 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alirushiwa mawe na kundi la watu katika mji mdogo wa Sirari aliposhawishi vijana wa mji huo kujiunga na maandamano ya chama hicho Mei 21, wakati wa kuchukua miili ya watu wanne, ambayo bado iko mochari.
Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia CCM, Amos Sagara, kupigwa mawe walipokwenda Nyamongo kuwapa pole wafiwa.
Sirari ni ngome ya Sagara ambaye pia ni Diwani wa Sirari, hivyo kutimuliwa kwa mawe kwa Lema kulitafsiriwa kuwa ni kulipa kisasi baada ya vijana wa eneo hilo kuchukizwa na kitendo cha Diwani wao kupigwa Nyamongo na wafuasi wa Chadema
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni