Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARI LEO. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARI LEO. Onyesha machapisho yote

Jumanne, 24 Aprili 2012

ARCADO NTAGAZWA AFIKISHWA KISUTU JANA KWA TUHUMA ZA UTAPELI

WAZIRI wa zamani wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Arcado Ntagazwa (65), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu mashitaka ya kujipatia mali ya Sh milioni 74 kwa njia ya udanganyifu.

Arcado Ntagazwa.

Katika kesi hiyo iliyosomwa mahakamani hapo jana, Ntagazwa anashitakiwa pamoja na mtu anayedaiwa kuwa ni mtoto wake, Dk. Webhale Ntagazwa (29) na Seneta Julius Miselya (60).

Baada ya kusomewa mashitaka na kuyakana, waliachiwa kwa dhamana isipokuwa Miselya ambaye hakuwa ametimiza masharti ya dhamana kwa wakati huo.

Wakisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Liud Chamshama, Mwendesha Mashitaka Wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya alidai kuwa Ntagazwa na wenzake hao walijipatia mali hiyo kwa udanganyifu.

Walidaiwa kuwa Oktoba 22, 2009 maeneo ya Mikoroshini Msasani katika Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa kwa nia ya udanganyifu walijipatia kofia 5,000 na fulana 5,000 kutoka kwa Noel Severe zenye thamani ya Sh milioni 74.

Ilidaiwa na Komanya kuwa washitakiwa hao walimdanganya Severe kuwa bidhaa hizo wangezilipa baada ya mwezi mmoja tangu kupewa mzigo huo, jambo ambalo hawakulitekeleza.

Washitakiwa hao walikana mashitaka yao na wakili wa Ntagazwa, Alex Mgongolwa aliomba dhamana kwa wateja wake akidai kuwa Ntagazwa ni mtu anayeaminika, kwa kuwa alipata kuwa Waziri na Mbunge kwa muda mrefu.

Wakili wa Serikali hakuwa na pingamizi kwa washitakiwa kupewa dhamana kwa sababu mashitaka wanayokabiliwa nayo yanadhaminika kisheria.

Hakimu Chamshama naye hakuwa na pingamizi, hivyo kutoa dhamana kwa washitakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano.

Washitakiwa walitakiwa kutoa Sh milioni 12 taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama na kukabidhi mahakamani hapo hati zao za kusafiria

Jumatatu, 20 Februari 2012

MAJAMBAZI WAIPEKUA MAITI.

MAJAMBAZI wamevamia na kuteka gari lililokuwa likimsafirisha maiti kutoka Mpanda mkoani Rukwa kwenda mkoani Mara na kumpekua maiti wakitafuta fedha na vitu vya thamani.

Utekaji huo ulifanyika Ijumaa iliyopita saa saba usiku katika eneo la Mtakuja Manispaa ya Tabora wakati wafiwa wakisafirisha mwili wa mtumishi wa Halmashauri ya Mpanda kwenda Musoma kwa maziko

 
Mkuu wa wilaya ya Tabora Mussa Chang'a(mwenye suti)


Akisimulia mkasa huo jana, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Moshi Musa Chang'a alisema baada ya gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser mali ya halmashauri hiyo kufika Mtakuja, walikuta mawe yamepangwa barabarani na liliposimama, ghafla kundi la majambazi lilitokea porini likiwa na mapanga na marungu na kuteka gari hilo.

Alisema baada ya kuteka gari hilo, waliwapekua waombolezaji waliokuwa wakisindikiza msiba na kuwapora zaidi ya Sh milioni mbili na simu za mkononi.

Chang'a alisema majambazi hao kabla ya kupora fedha hizo, waliwashambulia waombolezaji hao kwa marungu na ubapa wa mapanga na kuwasababishia majeraha madogo.

“Baada ya kumaliza kuwapora waombolezaji hao, ndipo wakaanza kuipekuwa maiti kwa lengo la kupata fedha zaidi au kitu chochote kilichokuwa kimefichwa kwenye jeneza hilo ili wakichukuwe,” alisema Chang’a.

Kwa mujibu wa Chang'a, muombolezaji mmoja alikuwa ameficha simu yake akatoa taarifa kwake na kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpanda ambao walifikisha taarifa hizo Polisi Tabora waliofika eneo la tukio usiku huo.

Alisema polisi walipofika eneo la Mtakuja, hawakuwakuta majambazi hao na tayari wameanzisha msako wa kuwabaini majambazi hao.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Tabora alisema majambazi hao hawako mbali na eneo la Mtakuja na kuwataka wananchi watoe taarifa Polisi ili wawakamate na kuwafikishwa katika vyombo vya sheria.

Alisema kila mwananchi wa Kata ya Mtakuja ana wajibu wa kushirikiana na Jeshi hilo ili kutokomeza kikundi hicho kinachosumbua watu mara kwa mara hasa nyakati za usiku.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Antony Rutta amekiri kutokea kwa uporaji huo na kuwataka wananchi kuwafichua watu wanaofanya uhalifu huo.

Aliwataka wananchi watoe taarifa hizo kwa siri ili Serikali ichukue hatua madhubuti kupambana na wahalifu hao ikiwemo kuwafikisha mahakamani watuhumiwa

Jumatano, 15 Februari 2012

MALI ZA VIGOGO 60 KUHAKIKIWA NA TUME YA MAADILI YA VIONGOZI.

WAZIRI wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ni miongoni mwa viongozi 60 watakaohakikiwa mali zao kuanzia Jumatatu.

Kwa mujibu wa Sekretarieti ya maaduili ya Viongozi wa Umma, wengine watakaohakiiwa ni pamopja na wakurugenzi, wabunge, madiwani na makanda wa Polisi wa mikoa.

Mbunge wa Ubungo, Mh. John Mnyika.

Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji Salome Kaganda, al;isem,a jana Dar es Salaam kwamba kazi hiyo itakamilika Machi mosi katika kanda sita na makao makuu, Dar es Salaam.

Wengine watakaohakikiwa katika awamu ya kwanza pamoja na Sitta na Mnyika ni, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Injinia Stella Manyanya na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu.

Pia Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario, Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Liberatus Sabas na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Massaburi.

Kadhalika yumo Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Charles Nyamrunda, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovic Mwananzila na Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu.

Kanda zitakazohusika na uhakiki huo ni Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Kusini.

Jaji Kaganda alisema, kutokana na idadi ya viongozi kuwa kubwa, sekretarieti itaanza na uhakiki wa viongozi 60 wenye nyadhifa tofauti na kazi hiyo itafanywa kwa mujibu wa sheria na wanasheria waliobobea wa sekretarieti hiyo na wachunguzi.

“Sheria ya Maadili inamtaka kila kiongozi wa umma anayehusika na sheria hii, kutoa taarifa za mali na madeni katika kipindi cha siku 30 baada ya kupewa wadhifa na kila mwisho wa mwaka yaani ifikapo Desemba 31,” alisema Jaji Kaganda.

Alisema, mwitikio wa urejeshaji wa matamko ya kukiri mali na madeni ya viongozi umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 22.5 kutoka wastani wa asilimia 60 kwa mwaka 2010.

Jaji Salome aliwataka viongozi wote waliopangiwa kufanyiwa uhakiki kutoa ushirikiano wa kutosha kwa maofisa wa Sekretarieti ili wafanikishe kazi hiyo.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kushirikiana na Sekretarieti kutoa taarifa zitakazosaidia kugundua mali zilizofichika ambazo zinasadikika kuwa za viongozi wa umma wanaoguswa na Sheria ya Maadili.

Alisisitiza kuwa, viongozi waliotajwa kuhakikiwa wasifikiri kuwa wametajwa na wengine na waepuke matapeli ambao wanaweza kuwafikia wakiwataka kutoa rushwa ili wasihakikiwe wakijidai kuwa wao ni maofisa wa Sekretarieti.

Kuhusu vigezo vilivyotumika kuanza na viongozi hao, Jaji Kaganda alisema Sekretarieti iliteua sampuli bila kuzingatia vigezo, katika kila kanda na kupata viongozi hao na kuzingatia kanuni za uwazi ili kila mwananchi ajue kinachofanyika.

Katibu Msaidizi, Idara ya Viongozi wa Siasa, Coletha Kiwale alisema kazi ya uhakiki ni ya kawaida na viongozi waliotajwa hawana tuhuma yoyote bali ni moja ya utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti.

Alisema viongozi wanaohusika wamepelekewa barua na maelekezo yanayostahili na kutakiwa kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazosaidia uhakiki huo.
Mali ni kosa?

Katika hatua nyingine, Jaji Kaganda alisema katika kikao cha Baraza la Maadili kilichokutana mwaka jana kuhoji baadhi ya viongozi ambao hawakujaza fomu ya kutambulisha mali zao, hawakufikia kutoa adhabu ya kufukuzishwa kazi kwa kiongozi yeyote badala yake wapo waliopewa onyo kali.

Jumapili, 22 Januari 2012

MKE WA MTU SUMU, DEREVA WA BODABODA AFUMANIWA NA KUUWAWA KIKATILI HUKO MPANDA.

DEREVA wa pikipiki za kukodi maarufu kama 'bodaboda', Mussa Kimbei (43), ameuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga na wananchi baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na mke mdogo wa mfanyakazi wake.
Dereva bodaboda wa Uganda(picha na maktaba)

Inadaiwa kuwa marehemu ambaye ni mkazi wa eneo la Kichangani mjini Mpanda alikuwa pia akimiliki shamba la tumbaku ekari nane na ekari nne za shamba la mahindi katika Kijiji cha Kambanga ambapo aliajiri walinzi na vibarua wanane.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, mauaji hayo yalitokea
juzi saa tano usiku shambani kwa marehemu katika kitongoji hicho cha Kambanga baada ya
kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa msimamizi wa shamba lake aitwaye Christopher
Bonge.

Mantage alisema mbali ya kumuua kikatili kwa kumcharanga vipande vipande kichwa kwa
mapanga, wananchi hao walichoma moto vibanda vitatu vya kukaushia tumbaku na kufyeka
mashamba yake ya tumbaku na mahindi kisha wakateketeza pikipiki yake kwa moto.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini, baadhi
ya madereva wa bodaboda ambao wanadai kuwa marafiki wa karibu wa Kimbei, wanadai kwa muda mrefu Kimbei alikuwa akituhumiwa kufanya mapenzi na wake za wanakijiji hao wa Kambaga.

“Kimbei ambaye ameacha wake wawili na watoto tisa, inadaiwa alikuwa akitumia fedha zake baada ya mauzo ya tumbaku kurubuni wake za wanakijiji hao. Huyu mke mdogo wa msimamizi wa shamba lake walikuwa na uhusiano wa kimapenzi wa muda mrefu,” alisema mmoja wa madereva hao.

Jumapili, 8 Januari 2012

MTUHUMIWA WA MAUAJI AKAMATWA BAADA YA MIAKA MINNE.

JESHI la Polisi wilayani Nkasi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji, Charles
Mwananjela (38) maarufu kama `Topaz’.

Mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa kwa takribani miaka minne.

Kamanda Isuto Mantage katikati.

Mtuhumiwa huyo anayedaiwa alikuwa dereva teksi na mkazi wa kitongoji cha Kipundu mjini Namanyere, Nkasi alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwaka 2009 kwa tuhuma za mauaji ya
Mboje Masesa (60) mkazi wa Shishiyu, Shinyanga.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Isuto Mantage mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa tisa mchana mjini Namanyere baada ya kuamua kurejea mjini hapo huku akidhani kuwa polisi walishasahau tukio hilo la mauaji.

“Mtuhumiwa huyu ambaye miaka minne iliyopita alikuwa dereva teksi mjini Namanyere anadaiwa kuwa alishiriki mauaji hayo yaliyotendeka Septemba 21, 2009 saa saba usiku katika pori lililopo katikati ya vijiji vya Mkole na Ipanda wilayani Nkasi.

“Yeye (mtuhumiwa ) akiwa pamoja na wenzake watano ambao tayari tumeshawakamata na kuwafikisha mahakamani walimshambulia mzee huyo pamoja na mkewe kwa marungu na kumuua pale pale,“ alisema Mantage.

Inadaiwa kuwa usiku huo wa tukio mtuhumiwa na wenzake hao pia walimshambulia mke wa marehemu ambaye alizirai kwa zaidi ya saa tano ambapo baadaye alizinduka akiwa hospitalini.

Kamanda Mantage alibainisha kuwa uchunguzi wa awali ulibaini kuwa mtuhumiwa na wenzake walikuwa wamekodiwa na Moshi Malambo ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa marehemu,
akidaiwa kutaka kumrithi mke wa marehemu pia mali zake ikiwa ni pamoja na ng’ombe

Jumatano, 14 Desemba 2011

BADO UTATA WAGUBIKA KIFO CHA KONSTEBO DAVID ALIYEJIUA LINDONI NMB.

Askari Polisi wakijaribu kuwatawanya wananchi waliokuja kushuhudia tukio hilo la askari kujiua nje ya Makao Makuu ya Benki ya NMB mtaa wa Azikiwe na Jamuhuri.

ASKARI Polisi, Konstebo David Selemani (22) aliyejiua kwa kujipiga risasi jijini Dar es Salaam inadaiwa kabla ya kuchukua uamuzi huo, aliwasiliana na ndugu zake wengi wakiwemo ambao hakuwa amewasiliana nao kwa muda mrefu.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile ambaye kwa mujibu wake polisi inaendelea na uchunguzi kubaini sababu za kufanya hivyo, alisema hatua hiyo iliwashangaza ndugu hao.


Shilogile alisema uchunguzi unaofanyika ni pamoja na kuwasiliana na kampuni ya simu ya mtandao aliokuwa akiutumia ili kufahamu mtu aliyekuwa akiwasiliana naye kabla ya kujiua.


Kwa upande wa ndugu na marafiki wa askari huyo waliozungumza na gazeti hili kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa maziko, walisema wanaendelea kujiuliza maswali bila majibu juu ya sababu za jamaa yao kuchukua uamuzi huo.


Katika kuaga mwili wa Konstebo David katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, mmoja wa ndugu aliyejitambulisha kwa jina moja la Danny, alisema siku moja kabla ya kujiua, alizungumza naye kwa simu akimtaka waonane.


“Mimi shughuli yangu ni dereva, na kwa bahati mbaya siku hiyo nilikuwa safarini, hivyo nilimtaka wakaonane na kaka yangu ili wazungumze kama kulikuwa na jambo la haraka la kuzungumza, sababu nilijua lingeweza kupatiwa majibu na kaka,” alisema Danny.


Alisema siku iliyofuata, akiwa njiani kurudi Dar es Salaam, alishitushwa kupata taarifa za msiba wa David, suala alilodai kuwa limemuacha na maswali mengi juu ya kile kilichosababisha ajiue.

Jumapili, 20 Novemba 2011

KIKWETE AWANANGA WANASIASA, WATANZANIA WATATOA MAONI YAO JUU YA UANDIKWAJI WA KATIBA MPYA.

Rais Kikwete akihutubia Wananchi kupitia Wazee wa Dar es salaam juzi ambapo aliongelea mambo mbalimbali ikiwemo uundwaji wa Katiba mpya.


KATIBA mpya ya Tanzania itaandikwa na Watanzania wenyewe kwa kupitia maoni yatakayotolewa nao kwa Tume itakayoundwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka huu.


Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete alipozungumza na Taifa
kupitia wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.


Alisema kila Mtanzania atapewa fursa ya kutoa maoni yake kwa Tume ambayo ataiunda
kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar mara Muswada wa marekebisho ya Katiba uliopitishwa
jana na Bunge la Jamhuri utakapokuwa umesainiwa.


Alisisitiza, k w a m b a T u m e haitaacha kusikiliza maoni na hoja ya kila mtu atakayependa kushiriki kuchangia, lakini hayo yatafanyika kwa kuzingatia sheria.


“Katiba iliyopo itafuatwa, kwa sababu ndiyo iliyopo kwa sababu kubadili Katiba lazima ya zamani iwepo, hivyo itafuatwa na kuzingatiwa katika mchakato mzima wa kupata Katiba mpya,” alisema Rais.


Tume kuteuliwa na Rais Juu ya malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wanaharakati pamoja na wanasiasa, hususan wa upinzani kwamba yeye hastahili kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa kuandika Katiba, Rais alishangaa.


Alisema hii si mara ya kwanza kwa Rais kuunda Tume kama hiyo, kwa sababu hata waliomtangulia walipata kufanya hivyo akitolea mfano wa Rais wa Kwanza Mwalimu Nyerere ambaye aliunda tume kama hiyo mara tatu; mwaka 1963, 1964 na 1965


Akifuatiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye aliunda mara moja mwaka 1992 chini ya Jaji Francis Nyalali na Benjamin Mkapa mara moja ya Jaji Robert Kisanga.


Alisema Katiba iliyopo inampa mamlaka ya kuuda Tume hiyo, ambayo alisema itajumuisha watu wa kada mbalimbali na kufuatiwa na Bunge Maalumu la Katiba, ambalo litajumuisha wanasiasa wakiwamo wabunge, wawakilishi na watu wengine 300.


Kuhusu hoja kwamba Zanzibar isipewe fursa sawa na Tanzania Bara, Rais aliponda hoja hiyo, akisema udogo wa nchi si hoja na kinachotakiwa ni ushirikishi kwa usawa.


“Hizi ni nchi huru zenye hadhi sawa-udogo si hoja, Shelisheli ina watu 84,000, lakini ni Taifa huru, hivyo mkiamua kuungana nayo, lazima mnakuwa na haki sawa pia,” alisema Rais.


Katiba ya sasa si mbaya Pamoja na kutaka kuja na Katiba mpya, lakini alisema Katiba ya sasa si mbaya, kwani imewalea Watanzania kwa muda mrefu katika mazingira ya amani na utulivu na kupiga hatua kubwa ya maendeleo kuliko ilivyokuwa miaka 50 iliyopita.


“Tunachotaka kukifanya sasa ni kuhuisha Katiba itakayofanana na Tanzania ya sasa. Katiba ya miaka 50 ijayo ambayo itaendelea kudumisha amani na utulivu,” alisema.


Alisema katika mchakato huo, kuna mambo ambayo yatatakiwa kujadiliwa na hasa kulindwa, kwa kuwa ndizo tunu za Taifa.


Aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwapo kwa nchi na mipaka yake; Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Bunge; Mahakama; umoja; mshikamano na usalama; haki za binadamu; usawa mbele ya sheria; uhuru wa kuabudu na kuaminiana.


Alisema hayo yatazungumzwa kwa maana ya kulindwa na si kutaka kubomolewa, kuvunjwa au kukiukwa.

Jumapili, 16 Oktoba 2011

SAFU-POLISI WANAPOTIA FORA KWA RUSHWA INASIKITISHA SANA.

SIKU zote tumelalamikia polisi kuwa wanaongoza kwa rushwa.

Ni sekta ambayo inaendekeza ‘mshiko’ na wakati mwingine hadi askari hao wanalitia aibu Jeshi letu zuri la Polisi.

Polisi wanadai rushwa bila ya aibu, angalia walivyomfilisi huyu mfugaji wa Iyumbu huko Singida hadi akauza ng’ombe wake 31 ili awatulize watumishi hao wa vyombo vya Dola kwa kumbambikia kesi.
Shedrack Sagati


Mzee Shigela kabambikiwa kesi na hiyo inatokana na utajiri wake lukuki wa ng’ombe alionao. Watumishi hao wa vyombo vya Dola wakaona watakula wapi zaidi kwa huyo mzee tajiri wa ng’ombe.

Wakaamua kumwingia na kumbambikia kesi kibao, mara kapatikana na fuvu na mifupa ya binadamu, mara kapatikana na ngozi ya simba na chui.

Kwa mtu wa kijijini masikini ambaye hajui sheria katika hali hiyo unadhani atafanya nini? Kisa hiki cha Singida kinasikitisha sana!

Kwamba kinawahusisha polisi wawili na raia watatu waliofanya unyama wa namna hii kuamua kumfilisi mfugaji huyo wa kijijini.

Angalia yumo Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kitongaoji na mkazi wa kijii hicho ambaye nadhani yeye kuingizwa kwenye kesi hiyo inawezekana katika eneo hilo ndiye mjuaji kuliko raia wengine.

Kashfa hii kwa polisi sio ngeni, raia wamekuwa wanalalamika kuwa polisi wanawabambikia watu kesi na hata wakilalamika kwa wakubwa wao hakuna hatua zinazochukuliwa na vigogo wa Jeshi hilo.

Mara ngapi raia wamelalamikia namna trafiki wanavyopiga mabao daladala na mabasi yanayoenda mikoani na nchi jirani.

Kuna hatua yoyote imechukuliwa? Zaidi ya trafiki kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine?

Tena ukiandika zaidi mambo ya polisi, wanakuwekea bifu kuanzia juu hadi chini na wanatafuta namna ya kukubana kama ilivyofanyika kwa paparazi mmoja baada ya kuanika uozo huo wa polisi wa Usalama Barabarani.

UKATILI KWA ALBINO WAANZA UPYA HUKO GEITA

VITENDO vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) vimeibuka tena wilayani Geita mkoani Mwanza, baada ya mlemavu mmoja wa ngozi kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kulia pamoja na kukatwa mkono wa kushoto.
Mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Albino.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Nyaruguguna, Kata na Tarafa ya Nyang’hwale ambapo mlemavu huyo, Adam Robert (14), mwanafunzi wa darasa la nne, alivamiwa na kukatwa mkono wa kulia na kisha kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kushoto.

Akisimulia mkasa huo, mlemavu huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita akiuguza majeraha yake, alisema alikumbwa na mkasa huo saa 1:40 usiku akiwa nyumbani
kwao ambapo alivamiwa na mtu mmoja waliyekuwa wanakula naye chakula nje ya nyumba.

Akizungumza kwa shida katika kitanda namba 5 alikolazwa, alisema siku ya tukio saa 12 alifika nyumbani kwao mtu huyo akidai amekwenda kuangalia ng’ombe wake waliokuwa wamepotea ambapo walianza maongezi na yeye juu ya upotevu wa ng’ombe hao.

‘‘Wakati tuko nje na baba, mtu huyo alifika na kubisha hodi kisha tukamkaribisha tukampa kiti akakaa ndipo akaanza kutueleza kuwa anawatafuta ng’ombe wake waliopotea machungani.

Tukaendelea kuzungumza naye hadi tulipoletewa chakula hapo nje tukaanza kula,’’ alisema
na kuongeza: ‘‘Ghafla mvua ikaanza kunyesha ikabidi tuhamie ndani, baba akawa amechukua ugali akatangulia ndani mimi nikabeba mboga yule mtu akabeba kiti chake, wakati tunaingia ndani nilikuwa katikati ya baba na mtu huyo, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida kabla sijaingia ndani yule mtu akanishika na kunivuta nje”.

Alisema baada ya kuvutwa mtu huyo alianza kumkata mkono wake wa kushoto upande wa begani wakati huo akiwa amelala chini akijitupatupa na baada ya kuona ameshindwa kuukata na kuunyofoa mkono kuanzia kwenye kiganja, akaacha na kuanza kuukatia tena kwenye kiwiko.

“Aliposhindwa pia kuukatia kwenye kiwiko aliamua kuugeukia mkono wangu wa kulia na kukata vidole vyangu vitatu vya mkono huo na kuvinyofoa kabisa, wakati huo baba alishindwa
afanye nini akabaki kukimbilia huku na kule na wakati huo kaka yangu alikuwa amejificha kwenye nyumba nyingine na kilichonishangaza sana ni kwamba pamoja na kupiga sana kelele za kuomba msaada hakuna mtu hata mmoja aliyejitokeza kwa ajili ya kuja kunisaidia,” aliongeza kusema.

Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa mlemavu huyo, Robert Tangawizi (36) alisema wakati tukio hilo linatendeka alikuwa kama vile amechanganyikiwa na kushindwa kabisa kumuokoa mwanawe muda wote wa purukushani kati yake na mhalifu huyo na kwamba alishikwa na bumbuwazi na hasa baada ya kumuona mtu ambaye walikuwa wanakula naye chakula kwenye meza moja amegeuka mhalifu kwa mwanawe.

Alhamisi, 29 Septemba 2011

AJALI YAUA TISA HUKO MBEYA

AJALI sasa ni shetani aliyeukumbatia mkoa wa Mbeya, baada ya siku chache kupita tangu watu 14 wapoteza maisha kwa ajali ya Fuso la mnadani, watu wengine tisa wamekufa na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali nyingine.

Watu hao wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace namba T 219 ASQ na gari aina ya Prado namba T 155 ACQ yaliyogongana uso kwa uso katika barabara ya Mbeya - Tunduma.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo amesema leo kuwa, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 usiku katika Kijiji cha Chimbuya, Mbozi mkoani Mbeya.

Kimolo amesema, dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo, alishindwa kulimudu kutokana na mwendo wa kasi na kuyumba kutoka upande wake hadi upande wa pili na kugongana na gari hilo lililokuwa likienda Tunduma kutoka Mbeya.

Kwa mujibu wa Kimolo, waliokufa na miili yao kutambuliwa na ndugu zao ni pamoja na wanafamilia Anna Mbembela na mwanawe Mariam Mrema na Rahabu Mwaijumba na mwanawe Leah Said.

Wengine ni Binaisa Mwashiuya, Baraka Mwansite na dereva wa Hiace ambaye hajafahamika jina lake, wakati Agness Mpoli alifia njiani wakati akikimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.

Mkuu wa Wilaya aliwataja majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi iliyopo katika mji mdogo wa Vwawa kuwa ni Frank Simbeye (25) mkazi wa Chimbuya, Emmanuel Sanga (16) wa Mlowo, Agness Anthony (28) wa Mbeya na wanawe Jacqueline na Victor Christopher.

Majeruhi wengine ni mkazi wa mji mdogo wa Tunduma Anastazia Mtumbo (19), Richard Ezekiel (miezi 10) na Chenny Mwembe (25) wa Chimbuya.

Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Charles Kumbi wakati Prado lilikuwa likiendeshwa na mmiliki wake, Emmanuel Kaila ambaye amelazwa katika hosptali ya Sifika mjini Vwawa akipata matibabu kutokana na kujeruhiwa vibaya.

Hata hivyo, mashuhuda hao walisema huenda ajali hiyo ilisababishwa na trekta lililokuwa eneo la tukio likiwa limebeba tangi la maji bila taa na dereva wa Hiace akitaka kulipita.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kutoa mwito kwa wadau kutambua kuwa usalama barabarani unaoweza kupunguza matukio ya ajali kama hizo ni jukumu la wote

Jumanne, 27 Septemba 2011

MBUNGE NA MADIWANI CHADEMA WACHUKUA POSHO YA VIKAO VYA BARAZA LA MADIWANI ARUSHA.

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema amekiri kusaini na kuchukua posho ya kikao cha Baraza la Madiwani mwishoni mwa wiki, lakini akatetea uamuzi huo akisema alikwenda kuzima
njama za kufukuzana.
Mh. Godbless Lema


Lema na madiwani wenzake watatu wa Chadema, walishiriki katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Arusha, kinyume cha msimamo wao wa kutohudhuria vikao hivyo.

Mapema mwaka jana, Lema na madiwani wote wa Chadema wa Jiji la Arusha waliweka msimamo wa kutomtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo na kutohudhuria vikao vyote vya Baraza la Madiwani kwa madai kuwa Meya huyo hakuchaguliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni na kuhudhuria vikao ni kumtambua.

Lakini Ijumaa iliyopita, Lema na madiwani Isaya Doita (Ngarenaro), Crispin Tarimo (Sekei) na Sabina Francis (Viti Maalumu), walihudhuria kikao hicho na kupokea posho kwa malipo ya kuhudhuria kikao.

Lema alikiri alisaini posho hiyo yeye na wenzake na kudai kulikuwa na njama za kutaka kuwafukuza madiwani wa Chadema kwa kukosa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo bila ya kuwa na taarifa yoyote na kwa mujibu wa sheria na kanuni wangetimuliwa.

Alisema kwa kufanya hivyo siyo kama wamebadilisha msimamo wao wa kutomtambua Meya
Lyimo na Naibu wake, Estomii Mallah, isipokuwa ilibidi wafanye hivyo kutegua mtego wao wa madai ya kufukuzwa madiwani.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomii Chang’a alisema madiwani wa Chadema walipewa posho baada ya kuhudhuria kikao hicho na wala hakukuwa na njama za kutaka kuwafukuza kama alivyodai Lema

Alhamisi, 1 Septemba 2011

PIKIPIKI ZA BIASHARA MARUFUKU KUINGIA KATIKATI YA JIJI LA DAR

KIKOSI cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam, kimepiga marufuku biashara ya usafiri wa pikipiki maarufu ‘bodaboda’ kuingia katikati ya Jiji ili kupunguza msongamano.
Pikipiki za biashara hazitakiwai mjini, labda ya binafsi kama hii.


Kutokana na hatua hiyo, kikosi hicho kitaanza kuwakamata wafanyabiashara hao watakaoingia jijini mara baada ya kumalizika kwa Sikukuu ya Idd El-Fitr.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa kikosi hicho, Vitus Nikata alisema ni marufuku kufanya biashara hiyo katikati ya mji.

Alisema suala hilo liko wazi lakini kwanza walikuwa wakitoa elimu kwa wasafirishaji hao kwa kuwa wengine hawajui kama hilo ni kosa.

“Katika kamatakamata yetu tutawatambua waendesha bodaboda hizo kutokana na namba za usajili kwa kuwa za biashara ni nyeupe na za watu binafsi ni njano hivyo hakuna atakayetudanganya,“ alisema.

Aliwataka wafanyabiashara hao kufuata sheria za Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kujali maeneo yao ya kufanya biashara ili kuepusha usumbufu.

Jumapili, 26 Juni 2011

POLISI RUVUMA WAIBUA MTANDAO WA WASAFIRISHAJI BINADAMU.

MKONO mrefu wa Jeshi la Polisi nchini, umewanasa watuhumiwa wawili wa biashara ya kusafirisha binadamu nje ya mipaka ya nchi.

Watuhumiwa hao ni wakazi wa Bombambili katika Manispaa ya Songea mjini hapa. Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Mwalimu wa Shule ya Msingi Makambi ya mjini hapa.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika na biashara ya kusafirisha watu, wakiwamo wanafunzi wa kike kwenda katika nchi jirani, ikiwamo ya Msumbiji.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda ambaye amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Nolasco Mgalula (31) ambaye ni Mwalimu na Suzana Onesmo. Polisi wanasema kwamba waliwakamata watuhumiwa hao Juni 22 mwaka huu.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mtandao huo kutoka kwa raia wema.

Aidha wazazi wa wasichana hao walikumbwa na wasiwasi baada ya kutowaona mabinti zao ndipo walipotoa taarifa za kupotelewa katika Kituo cha Polisi cha Songea mjini.

Kamanda Kamuhanda aliwataja kwa majina wasichana waliotoroshwa (majina tunayahifadhi) na kusema walipelekwa Msumbiji kwa lengo la kufanya biashara za kuuza baa na wengine kufanya kazi ya ukahaba katika madangulo maalumu.

Watoto waliotolewa taarifa wamebainika kuwa ni wanafunzi wa kidato cha pili katika shule za sekondari zilizopo mjini hapa.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha Polisi wamesema kwamba jitihada za kuwapata mabinti hao na kuwarudisha hapa nchini zinafanyika kwa kushirikiana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Niasa nchini Msumbiji.

Alifafanua kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kuufuatilia mtandao huo kwa ukaribu zaidi ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinapingana na haki za binadamu na sheria ya elimu nchini kwa kuwa waliofanyiwa kitendo hicho ni wanafunzi.

Alitoa rai kwa wazazi na walezi wa watoto wanaosoma mkoani hapa kuwa waangalifu kwa mabinti zao kujihusisha na watu waovu hasa wakati huu ambao mwingiliano wa watu kutoka nchi jirani ya Msumbiji umekuwa mkubwa baada ya kujengwa kwa Daraja la Mkenda katika Kata ya Mitomoni, Songea Vijijini linaloziunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji

Jumapili, 22 Mei 2011

MAITI WASUSWA TARIME, WANASIASA WAGEUZA MTAJI WA VYAMA VYAO.

Maiti waliosuswa Tarime waharibika
Imeandikwa na Samson Chacha, Tarime;

UTATA wa mazishi ya watu wanne kati ya watano waliouawa baada ya tukio la kuvamia Mgodi wa North Mara wilayani hapa Mei 16 umeendelea, baada ya ndugu wa marehemu kuendelea kususa miili huku ikiendelea kuharibika katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya.

Hadi Mei 21, ni mwili mmoja tu uliochukuliwa, huku mingine minne ikibaki mochari, kwa maelezo kwamba, ndugu wa marehemu wanamsubiri mganga wao na wanasheria ambao ni viongozi wa Chadema, Mabere Marando na Tundu Lissu.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili linazo zinasema, wanandugu hao wamekataa kuchukua miili hiyo mpaka itakapochunguzwa, huku uchunguzi ukishuhudiwa na Marando na Lissu.

Miili ambayo mpaka jana ilikuwa haijachukuliwa ni ya mwanafunzi Emmanuel Magige wa
Nyakunguru, Chacha Ngoka mkazi wa Kewanja Nyamongo na waliokuwa wakazi wa Mugumu, wilayani Serengeti, Mwikwabe Marwa na Chawali Bhoke.

Mwili pekee uliochukuliwa na kuzikwa ni wa Chacha Mwasi wa Bisarwi Komaswa. Kutokana na kususia maiti, Kamishna wa Jeshi la Polisi anayeshughulia masuala ya Operesheni, Paul Chagonja, amesema jeshi lake linasikitishwa na baadhi ya wanasiasa kuingilia matatizo ya Makosa ya Jinai kwa kushawishi wafiwa kususia miili ya ndugu zao wakati inazidi kuharibika hospitali.

“Hakuna polisi aliyemfuata mtu yeyote aliyeshambulia askari wetu kwa mawe na silaha za jadi, pia hatujakataa kuwa waliouawa hawakupigwa risasi na polisi, sasa huyo mganga anayesubiriwa anatarajia kuja kuandika kuwa wameuawa na nini, kama si siasa kavu ya kusumbua ndugu za marehemu?” alihoji.

Chagonja alisema baadhi ya ndugu wa marehemu walitaka kuchukua miili ya ndugu zao, lakini baadaye wakasema wanasubiri daktari wao na wanasheria Marando na Lissu wafike kushuhudia, lakini tangu Jumatano zimekuwa zikitolewa ahadi za uongo huku miili ya marehemu hao ikiharibika.

Aliongeza kwamba, tayari Polisi ina taarifa kuwa, wafiwa wamehifadhiwa nyumbani kwa Diwani wa Chadema Mjini hapa (jina tunalo) na kuna ndugu vijijini wameshindwa kufanya shughuli zao za kujipatia kipato wakisubiri kuzika kwa sababu ya kukwamishwa na wanasiasa.

Kamishna Chagonja alisisitiza kwamba, Polisi inafanya uchunguzi wa mauaji hayo na kama itabainika kuwa askari walioua walifanya makusudi, sheria itafuata mkondo wake na hawezi kutoa hukumu kwa kuangalia upande mmoja.

Alisema kuna askari zaidi ya saba waliojeruhiwa kwa mawe akiwamo Mrakibu Simon Mrashani na Mrakibu Msaidizi Hassan Maya na wenzao watano.

Aidha, magari ya Jeshi yaliharibiwa kwenye mapambano hayo kati ya polisi na watu zaidi ya
800 waliovamia mgodi kutaka kupora mawe ya dhahabu.

Wakati ikiwa haijafahamika siku ambayo wanandugu hao wataridhia kuchukua miili ya ndugu zao, Mkuu wa Wilaya, John Henjewele, ameonya kwamba endapo ndugu wa marehemu hao watashindwa kuchukua miili hiyo na kuizika, Serikali itazika.

Aidha, aliwaonya wanasiasa, hususani wa Chadema wanaotajwa kujiingiza na kuligeuza tukio hilo kuwa la kisiasa, akiapa kwamba Serikali haitafumbia macho wanaochochea uhalifu.

Mei 20 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), alirushiwa mawe na kundi la watu katika mji mdogo wa Sirari aliposhawishi vijana wa mji huo kujiunga na maandamano ya chama hicho Mei 21, wakati wa kuchukua miili ya watu wanne, ambayo bado iko mochari.

Tukio hilo lilitokea siku chache baada ya Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kupitia CCM, Amos Sagara, kupigwa mawe walipokwenda Nyamongo kuwapa pole wafiwa.

Sirari ni ngome ya Sagara ambaye pia ni Diwani wa Sirari, hivyo kutimuliwa kwa mawe kwa Lema kulitafsiriwa kuwa ni kulipa kisasi baada ya vijana wa eneo hilo kuchukizwa na kitendo cha Diwani wao kupigwa Nyamongo na wafuasi wa Chadema