AJALI sasa ni shetani aliyeukumbatia mkoa wa Mbeya, baada ya siku chache kupita tangu watu 14 wapoteza maisha kwa ajali ya Fuso la mnadani, watu wengine tisa wamekufa na wengine 12 kujeruhiwa katika ajali nyingine.
Watu hao wamepoteza maisha katika ajali iliyohusisha basi dogo la abiria aina ya Toyota Hiace namba T 219 ASQ na gari aina ya Prado namba T 155 ACQ yaliyogongana uso kwa uso katika barabara ya Mbeya - Tunduma.
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo amesema leo kuwa, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 usiku katika Kijiji cha Chimbuya, Mbozi mkoani Mbeya.
Kimolo amesema, dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo, alishindwa kulimudu kutokana na mwendo wa kasi na kuyumba kutoka upande wake hadi upande wa pili na kugongana na gari hilo lililokuwa likienda Tunduma kutoka Mbeya.
Kwa mujibu wa Kimolo, waliokufa na miili yao kutambuliwa na ndugu zao ni pamoja na wanafamilia Anna Mbembela na mwanawe Mariam Mrema na Rahabu Mwaijumba na mwanawe Leah Said.
Wengine ni Binaisa Mwashiuya, Baraka Mwansite na dereva wa Hiace ambaye hajafahamika jina lake, wakati Agness Mpoli alifia njiani wakati akikimbizwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.
Mkuu wa Wilaya aliwataja majeruhi wa ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Mbozi iliyopo katika mji mdogo wa Vwawa kuwa ni Frank Simbeye (25) mkazi wa Chimbuya, Emmanuel Sanga (16) wa Mlowo, Agness Anthony (28) wa Mbeya na wanawe Jacqueline na Victor Christopher.
Majeruhi wengine ni mkazi wa mji mdogo wa Tunduma Anastazia Mtumbo (19), Richard Ezekiel (miezi 10) na Chenny Mwembe (25) wa Chimbuya.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Charles Kumbi wakati Prado lilikuwa likiendeshwa na mmiliki wake, Emmanuel Kaila ambaye amelazwa katika hosptali ya Sifika mjini Vwawa akipata matibabu kutokana na kujeruhiwa vibaya.
Hata hivyo, mashuhuda hao walisema huenda ajali hiyo ilisababishwa na trekta lililokuwa eneo la tukio likiwa limebeba tangi la maji bila taa na dereva wa Hiace akitaka kulipita.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kutoa mwito kwa wadau kutambua kuwa usalama barabarani unaoweza kupunguza matukio ya ajali kama hizo ni jukumu la wote
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni