Alhamisi, 8 Septemba 2011

UJI WA CHUMA WAUNGUZA WATU SITA DAR ES SALAAM

WATU sita wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili baada ya kumwagikiwa na uji wa chuma katika ajali ya moto uliozuka katika kiwanda cha kufua vyuma Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema, moto ulizuka saa 4:00 usiku katika mashine ya kwanza ya kuyeyusha vyuma, baada ya uji wa chuma uliokuwa kwenye mtungi maalumu kuanguka na kumwagika chini.

Kinu cha myeyusho wa chuma.


Alisema uji huo uliwamwagikia wafanyakazi sita na kuwaunguza sehemu mbalimbali katika miili yao.

Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Mathayo Paul, Mohamed Khalfan ambaye ni raia wa Pakistani waliopata matibabu katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa na Jackson John ambaye bado amelazwa.

Wengine ni Shabani Juma (23), Sadiki Waswa (38) na Mner Hussein (40)ambaye ni raia wa Pakistani walihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Upelelezi unaendelea.

Katika tukio jingine huko Gongo la Mboto majira ya saa 3:30 usiku ulizuka moto katika nyumba ya Rashid Bilal (29) na kuteketeza nyumba yote na mali zilizokuwemo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile alisema chanzo cha moto huo hakijafahamika na mali iliyoteketea nayo haijafahamika.

Katika Wilaya ya Temeke, ulizuka moto katika vibanda tisa na vingine viwili vilivyokodiwa kwa ajili ya biashara.

Mabanda hayo yalikuwa yamezungukwa na nyumba ya Reginald Tesha ambaye ni mkazi wa Keko yenye namba CH 39/177.

Moto huo uliteketeza samani na mali zilizokuwemo ndani na chanzo bado hakijafahamika. Moto ulizimwa na kikosi cha uokoaji cha Jiji, hakuna madhara kwa binadamu na upelelezi unaendelea

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni