Ijumaa, 30 Septemba 2011

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI AWAJIBISHWE-PROF. LIPUMBA.

Siku moja baada ya Mahakama Kuu kusajili tuzo ya malipo ya Shilingi bilioni 111 kwa kampuni ya Dowans, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amemshauri Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na watendaji wake kwa kuisababishia nchi hasara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema kwamba Ngeleja na watendaji walioko chini yake ndio waliosababisha hasara hiyo ambayo sasa Serikali inapaswa kulipa hivyo ni lazima wawajibishwe mara moja.

“Wakati huu ambao Serikali imeshindwa kutatua tatizo la umeme, tunaongezewa gharama za kesi. Hili ni ombwe la uongozi ndani ya Serikali ya CCM, tangu Rais, mawaziri na watendaji wake. Nashangaa bado viongozi waliosababisha yote haya wako madarakani,” alisema Profesa Lipumba.
Prof. Ibrahim Lipumba.


Profesa Lipumba alisema tukio hilo ni matokeo ya ufisadi ndani ya Serikali kwa sababu Dowans ilitokana na mkataba wa Richmond ambao tangu mwanzo, TANESCO waliupinga, lakini baadhi ya viongozi wa Serikali wakashinikiza.

Vilevile, Profesa Lipumba aliilaumu kampuni ya uwakili ya Rex Attorney ya jijini Dar es Salaam kwa kile alichoeleza kuwa ilicheza mchezo wa kimaslahi pale ilipoishauri TANESCO kuvunja mkataba na Dowans kwa madai kuwa haukuwa halali huku ikiisaidia kampuni hiyo kupata mkopo katika benki ya Stanbic.

“Tanesco waliitumia Rex Attorney kupata ushauri wa kuvunja mkataba wa Dowans na TANESCO, lakini Rex hao wakaandika tena barua kwa Benki ya Stanbic ikitaka Dowans ikopeshwe Dola Milioni 20 za Marekani. Hawa ndiyo waliosababisha tushindwe kesi,” alisema Profesa Lipumba.

Juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilibariki malipo kwa Dowans baada ya kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), dhidi ya Tanesco na kampuni hiyo ya kufua umeme. Kwa uamuzi huo, Tanesco sasa inatakiwa iilipe Dowans kiasi cha Sh 111 bilioni badala ya Sh 94 bilioni za awali kwani inatakiwa kuilipa fidia hiyo na riba ya asilimia 7.5


source: http://www.wavuti.com/

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni