Jumatano, 14 Septemba 2011

MWENYEKITI SERIKALI YA MTAA KORTINI KWA RUSHWA YA LAKI MOJA.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Iringa, imemfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ilula-Mtua, William Ngandago (75), kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 100,000.

Mwenyekiti huyo anadaiwa kuomba na kupokea rushwa hiyo kutoka kwa Patrick Mtanga kama kishawishi ili aweze kumsaidia kumwekea dhamana ndugu yake, James Ndala, ambaye alikamatwa na Mwenyekiti huyo na kuwekwa katika mahabusu ya Polisi kituo cha Ilula.

Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo jana kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Iringa, Dainess Lyimo.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Bi. Restituta Kessy.

Ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru Mkoa wa Iringa, Restituta Kessy, aliyekuwa akisaidiana na Philemon Msegu kuwa William alikamatwa Julai 27, mwaka huu  katika Kijiji cha Ilula-Mtua, baada ya kudaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 100,000.

Baada ya upande wa mashitaka kutoa maelezo hayo, Hakimu Lyimo aliahirisha kesi hiyo na kuamuru mtuhumiwa kurejeshwa mahabusu hadi hapo kesi hiyo itakapotajwa tena Septemba 27, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni