Alhamisi, 1 Septemba 2011

PIKIPIKI ZA BIASHARA MARUFUKU KUINGIA KATIKATI YA JIJI LA DAR

KIKOSI cha Usalama Barabarani mkoani Dar es Salaam, kimepiga marufuku biashara ya usafiri wa pikipiki maarufu ‘bodaboda’ kuingia katikati ya Jiji ili kupunguza msongamano.
Pikipiki za biashara hazitakiwai mjini, labda ya binafsi kama hii.


Kutokana na hatua hiyo, kikosi hicho kitaanza kuwakamata wafanyabiashara hao watakaoingia jijini mara baada ya kumalizika kwa Sikukuu ya Idd El-Fitr.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda wa kikosi hicho, Vitus Nikata alisema ni marufuku kufanya biashara hiyo katikati ya mji.

Alisema suala hilo liko wazi lakini kwanza walikuwa wakitoa elimu kwa wasafirishaji hao kwa kuwa wengine hawajui kama hilo ni kosa.

“Katika kamatakamata yetu tutawatambua waendesha bodaboda hizo kutokana na namba za usajili kwa kuwa za biashara ni nyeupe na za watu binafsi ni njano hivyo hakuna atakayetudanganya,“ alisema.

Aliwataka wafanyabiashara hao kufuata sheria za Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na kujali maeneo yao ya kufanya biashara ili kuepusha usumbufu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni