Jumanne, 13 Septemba 2011

WAVAMIZI SALASALA KUONDOLEWA KWA NGUVU NA SERIKALI.

Waliovamia Salasala kuondolewa kwa nguvu

Serikali imesema itawaondoa kwa nguvu watu waliovamia maeneo ya Salasala, wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam yalipokuwa machimbo ya kokoto kwa kuwa eneo hilo ni la serikali na hakuna aliyeuziwa.
Hayo yalisemwa jana na ofisa mahusiano wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Muhowera, wakati akizungumza na NIPASHE wakati akitoa  ufafanuzi kuhusiana na mgogoro wa kiwanja hicho.


Muhowera alisema walishatoa taarifa kwa wavamizi hao kuwa waondoke, lakini cha kushangaza mpaka sasa hawajatekeleza agizo hilo la serikali.

“Muda wowote kuanzia sasa zoezi la kuwaondoa watu hao litafanywa na Manispaa,” alisema afisa huyo habari na kuongeza: “Wameonyesha dharau kwa serikali, hali hiyo haiwezi kuvumilika,” alisema Muhowera.

Alisema awali eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya BENACO kwa ajili ya kuchimba madini na baada ya muda wao kwisha, eneo hilo limebaki kuwa mali ya serikali.

Wananchi wa eneo hilo wameshikilia msimamo wao kuwa eneo hilo ni mali yao kwani waliuziwa na uongozi wa serikali ya mtaa wao.

Hata hivyo, viongozi hao wa serikali ya mtaa wameshindwa kutoa maelezo ya kujitosheleza kuhusu hatua ya kuwamilikisha wakazi wake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni