Jumatano, 21 Septemba 2011

WAKOREA WAPATIKANA NA HATIA YA KUTOA RUSHWA.

Boss wa Takukuru, Bw. Edward Hosea.

 Raia wawili wa Korea waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya kutoa rushwa, wamehukumiwa kwenda jela miaka mitano kila mmoja baada ya kukiri kosa mahakamani.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  mkoani Dodoma iliwafikisha mahakamani raia wawili wa Korea kwa kosa la kutoa hongo ya Shilingi 100,000 kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Waliofikishwa mahakani ni Yun Yong Sim na Kim Song Hul ambao wanakabiliwa na kosa la kutoa rushwa kwa ajili ya kumshawishi Mganga Mkuu, Godfrey Mtey ili aweze kuwapa kibali cha Zahanati yao ambayo ilifungiwa kutokana na kutokukidhi vigezo.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Hassan Momba, aliwahukumu washtakiwa kwa kosa la kutoa rushwa ya Shilingi 100,000 kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Kaimu Kamanda wa TAKUKURU mkoani Dodoma, Sostenes Kibwengu alisema kuwa raia hao waliwekewa mtego baada ya kupokea taarifa za jambo hilo ambapo walifanikiwa kuwatia mbaroni na kuwafungulia mashtaka ya kutoa rushwa mahakamani.

Kibwengu alisema kikosi chake chini ya Kamanda wa Mkoa, Eunice Mmari kilianza kutilia shaka nyendo za raia hao baada ya kupewa taarifa za siri na raia wema na viongozi wenyewe waliotaka kuhongwa.
Walifungiwa kutoa huduma katika Zahanati yao ambayo ipo eneo la Area C’ Manispaa ya Dodoma baada ya Wizara ya Afyana Ustawi wa Jamii  kubaini ilikuwa imejengwa na kutoa huduma chini ya kiwango, “Walifungiwa  ili warekebishe baadhi ya mambo yakiwamo mazingira pamoja na kuzuiwa kuuza dawa za asili ambazo hazikuwa na vibali ndipo walipoanza kuhaha kwa ajili ya kuweka mambo sawa kwa wakubwa,’’alisema mmoja wa watu wanaoishi karibu na eneo hilo.

Taarifa zinaonyesha kuwa mbali na kufungiwa kituo hicho, lakini raia hao walikamatwa na kuwekwa korokoroni ingawa siku mbili baadaye walionekana mitaani wakitafuta namna ya kunusuru biashara yao.

Kwa mujibu wa vyanzo kutoka Uhamiaji Mkoa wa Dodoma, raia hao hata vibali vyao si halali na kwamba wanaishi kwa kutumia ujanja ujanja kutoka kwa baadhi ya watu, “Ni kweli ningekuambia kikamilifu lakini msemaji hayupo hapa isipokuwa hata mimi naweza kusema uhalali wa wao kuishi hapa nchini ni wa mashaka mashaka lakini usinitaje,’’alisema mmoja wa wafanyakazi wa Uhamiaji.

Momba alisema ametoa hukumu hiyo mapema, kutokana na washtakiwa hao kutosumbua mahakama, baada ya kukiri kutenda kosa hilo, “Mahakama imeridhika pasipo na shaka yoyote, baada ya watuhumiwa wenyewe kukiri kosa lao, kuwa walikuwa wametenda kosa hilo, hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitano kila mmoja gerezani au watatakiwa kulipa faini ya Shilingi 500,000 kwa kila mmoja, kwa maana hiyo wote wawili watatakiwa kulipa ni Shilingi 1 milioni,’’ alisema Momba.

Hata hivyo, watuhumiwa hao kwa pamoja walilipa faini na kukwepa kwenda gerezani.

Hukumu ya watumiwa hao imekuja ikiwa ni siku moja tangu TAKUKURU waliposhinda kesi dhidi ya Ofisi Utamaduni wa zamani Manispaa ya Dodoma, Stansalaus Kobelo, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa kama hilo. Kobelo alihukumiwa juzi na mahakama hiyo kwa kosa la kutaka rushwa kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa Sekondari ya Jamhuri, ili kumsaidia mambo yake. Alilipa faini ya Shilingi 500,000/=

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni