Jumanne, 13 Septemba 2011

BAHARIA ASIMULIA KISA CHA AJALI YA MV SPICE KILIVYOTOKEA.

Baharia Rashid Said Rashid wa meli ya Mv. Spice Islander, iliyozama na kuua takribani watu 240 huku wengine 619 wakinusurika visiwani Zanzibar juzi, amesema waligawa maboya ya kujiokoa kwa abiria na kuwavalisha watoto kisha kuwaondoa melini kupitia madirishani kabla ya kuzama.



Akizungumza na NIPASHE akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, jana, alisema kabla ya meli hiyo iliyokuwa na mabaharia 12 kuzama majira ya saa 7:00 usiku wa Ijumaa iliyopita eneo la Nungwi, waliomba msaada kwa meli nyingine iliyokuwa inapita lakini hawakufanikiwa.

Said ambaye ni mkazi wa Shangani, alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kabla ya meli kupinduka, abiria walimtaka nahodha atoe taarifa kwao kama meli inazama na alifanya hivyo.

“Tulijaribu kufanya kila jitihada ili kuokoa hali hiyo, lakini tulishindwa na tukaamua tuiache meli na kuanza kutoka, hapo tena kila mmoja alikwenda kwa upande wake,” alisema.

Hata hivyo, alisema hafahamu kama mabaharia wenzake na nahodha wapo salama au wamekufa kwa sababu mara ya mwisho aliwaona kabla ya chombo kupinduka na kuzama.

“Kwa kweli siwezi kusema kama ni uzembe au la umefanyika, lakini wakati inatokea hali hii tulipishana na meli ya MV Jitihada na kuwapa ishara ya kuzama, lakini hawakutusaidia,” alisema baharia huyo.

Alisimulia kuwa walichukua jitihada mbalimbali za kuwapa ishara, lakini hawakufanikiwa na hawezi kusema kama walidharau au hawakuwaelewa walichokuwa wakikitafuta kutoka kwao.

IDADI YA VIFO YAFIKIA 240 

Hadi jana taarifa rasmi zilizema kuwa watu waliokufa katika ajali hiyo baada ya meli kuzama wamefikia 240.

Meli hiyo ilizama majira ya saa 7:00 usiku ilipokuwa ikitokea jijini Dar es Salaam kupitia Unguja ikielekea Pemba.

Takwimu hizo zilitolewa jana na Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, wakati akitoa maelezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, ambaye alifuatana na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Devis Mwamunyange.

Mwema alisema Serikali imeamua kupeleka wazamiaji kutoka nje ya nchi kusaidia kuchunguza kujua kama ndani ya meli hiyo kuna maiti zilizobaki.

Alisema Serikali imeamua kuzika maiti 39 baada ya kutotambuliwa na wahusika na kwamba kazi hiyo ilifanyika usiku wa kuamkia jana katika eneo la Kama, Wilaya ya Magharibi Unguja.

Aidha, alisema meli hiyo ilizama ikiwa na tani 160 za mzigo, ambapo tani 65 zilipakiwa katika bandari ya Dar es Salaam, wakati tani 95 zilipakiwa katika bandari ya Malindi.

source; nipashe

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni