Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARILEO. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARILEO. Onyesha machapisho yote

Ijumaa, 25 Mei 2012

LLOYD NCHUNGA AJIUZULU UONGOZI WA YANGA JANA.

MWENYEKITI wa Yanga, Lloyd Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kuanzia jana.

Kujiuzulu kwa Nchunga itakuwa furaha kwa Baraza la Wazee la Yanga, ambalo karibu mwezi mzima sasa limekuwa likimshikia bango Nchunga aachie madaraka kwa madai ya timu hiyo kufanya vibaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika mapema mwezi huu, ambapo Yanga ilishika nafasi ya tatu.
Image

Lloyd Nchunga.

Pia itakuwa imewarahisishia kazi baadhi ya wanachama wa Yanga, ambao walikutana makao makuu ya klabu hiyo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani na kutangaza kumpindua Nchunga, uamuzi ambao ulipingwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba ni kinyume cha Katiba.

Uamuzi huo wa Nchunga kujiuzulu aliutangaza jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake jengo la NSSF, Dar es Salaam na kwamba amefanya hivyo kwa maslahi ya Yanga.

Alisema uamuzi wake wa kujiuzulu umekuja wakati walishakubaliana kwenye kikao cha
Kamati ya Utendaji ya Yanga kwamba wajumbe wengine waliobaki wasijiuzulu hadi mkutano mkuu wa wanachama Julai 15 mwaka huu, lakini mazingira yamemfanya afikie uamuzi huo na kwamba anajua wenzake watasononeka sana.

“Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo,” alisema.

Nchunga aliorodhesha mafanikio mbalimbali ambayo uongozi wake uliyapata tangu aingie madarakani Julai 2010, ambayo ni Ngao ya Hisani mwaka 2010, ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2010/2011 na ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka 2011.

Pia alisema chini ya uongozi wake waliua uteja kwa Simba, ukiacha matokeo mabaya ya kufungwa mabao 5-0 waliyoyapata kutoka kwa Simba Mei 6, mwaka huu.

“Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu mabao 5-0, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.

Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia.

“Siwatuhumu wachezaji moja kwa moja, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema. “Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!

“Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika hoteli mbalimbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.

“Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula
kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia,” alisema Nchunga.

Alieleza kuwa Jumapili baadhi ya wanachama wa Yanga walikutana na kutangaza mapinduzi, ambayo hata hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliyakataa.

Hata hivyo alisema baadhi ya wazee walikaririwa na kituo kimoja cha redio wakisema Yanga bora ishushwe daraja au kufungiwa kuliko Nchunga kuendelea kuongoza.

“Hii imenikumbusha hekima za Mfalme Suleiman akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wagawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.

“Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika uenyekiti wa Yanga kwani ni klabu
ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya Katiba yetu.

“Vile vile siko tayari kuona klabu yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi. Natumaini Kamati ya Utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya Katiba ya Yanga pamoja na Bodi ya Wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka
kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi.

“Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapohitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Nchunga.

Nakala ya taarifa ya kujiuzulu ameituma kwa wadhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume,
Francis Kifukwe na Yusuf Manji kwa taarifa.

Nchunga ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alishinda uenyekiti wa Yanga Julai mwaka 2010.

Katika uchaguzi huo nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilienda kwa Davis Mosha. Walioshinda katika ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Ally Mayai, Mzee Yusufu, Sara Ramadhani, Tito
Osoro, Mohamed Bhinda, Charles Mgondo, Salum Rupia na Theonest Rutashoborwa.

Hata hivyo Mosha alijiuzulu mwaka jana, wakati Mayai, Mzee Yusuph, Bhinda walijiuzulu hivi
karibuni kulipoanza shinikizo la kuung’oa madarakani uongozi wa Nchunga.

Rutashoborwa alifariki dunia

Alhamisi, 17 Mei 2012

RC MWANZA AAGIZA POLISI WASHUGHULIKE NA TUKIO LA KADA WA CHADEMA KUNG'OA SIKIO KWA KUNG'ATA.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ameiagiza Polisi mkoani hapa kuchukua hatua zinazostahili kwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Ilemela, Abel Mwesa baada ya kutuhumiwa kumng’ata na kuondoa kipande cha sikio la mkazi wa kitongoji cha Nyabiti.

Ndikilo ametoa agizo hilo baada ya mlalamikaji, Lazaro Nolbert kufika ofisini kwake na kutoa malalamiko hayo ambayo aliyaripoti katika Kituo cha Polisi Mwatex tangu Aprili 26, mwaka huu, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Haya ndio mambo yanayolichafua Jeshi la Polisi, mtu ameripoti wiki mbili zilizopita hadi leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa huku akipokea barua za vitisho, jamani hebu chukueni hatua ili jeshi hilo liendelee kuaminiwa na wananchi,” alisema Ndikilo.

Alisema inaonesha baadhi ya maofisa wa Polisi wanaficha taarifa za matukio kwa maslahi binafsi na ndio maana tukio hilo halijafika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Akisimulia tukio hilo, mkazi huyo kitongoji cha Nyambiti, Lazaro Norobert (25), alidai kuwa sikio lake limeng’atwa na kuondolewa kabisa na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Abel Mwesa baada ya kukosa chumba kwenye nyumba ya kulala wageni ya Amani inayomilikiwa na mzazi wa Lazaro.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya mkuu wa mkoa juzi, alisema amelazimika kufika ofisini hapo baada ya kukosa ushirikiano kutoka Polisi, kwani aling’atwa sikio hilo Aprili 26, mwaka huu na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Nyakato Mwatex na kupewa RB namba Ny/RB/3059/2012.

Alisema siku hiyo ya tukio, Katibu huyo alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa ameambatana na mwanamke ambapo alimkuta kijana huyo nje na kumuomba chumba na kujibiwa kuwa yeye hahusiki.

Baada ya kumjibu, alidai Abel alimwambia kuwa ana kiburi na kuwaita makamanda wenzake waje kumshughulikia ambapo walifikia na kuanza kumpiga na kisha yeye Abel alimvuta sikio na kisha kumng’ata na kuondoka na kipande cha sikio lake. Alisema baada ya tukio hilo alimkamata mtuhumiwa mmoja na kumfikisha katika Kituo cha Polisi cha Mwatex, lakini aliporudi kesho yake alikuta ametolewa kwa dhamana.

Alisema Katibu huyo pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabiti baada ya tukio hilo, alianza kupokea barua za vitisho kuwa siku zake za kufa zinakaribia iwapo ataendelea kumghasi.

Aliamua kutoa taarifa Ofisi ya Mtendaji ambapo aliandikiwa barua na kwenda kutoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako alipewa RB namba MW/Rb/4579/2012 ya shambulio la kudhuru mwili.

Alisema kwa kuwa awali alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mwatex na hakupewa ushirikiano na Polisi hadi kupokea barua za vitisho hivyo, ameamua kulifikisha suala hilo kwa mkuu wa mkoa ili apate msaada zaidi kwani hata nyumba ya kulala wageni ya mama yake wametishia kuichoma moto

Jumapili, 13 Mei 2012

MATEJA WAYATEKA MAKABURI YA SINZA, WAUZA MAKABURI YALIYOZIKWA ZAMANI.

KWA kipindi kirefu sasa, usimamizi wa makaburi ya Sinza, Dar es Salaam umekuwa chini ya mikono ya mateja (watumiaji wa mihadarati) wanaoendesha biashara haramu ya maeneo ya makaburi yaliyokwishatumika ili kujipatia kipato.

Picha ya Maktaba; Msiba wa Dokta Remmy.

Kwa sababu ya kukosa utu na ufukara uliopitiliza, mateja hao wasiopungua 15 wamekuwa wakiendesha biashara hiyo waziwazi kwa miaka nenda rudi na hivyo kufanya wazoeleke kwa baadhi ya wakazi wa maeneo jirani na makaburi hayo, pamoja na wateja wanaofika kutafuta huduma ya maziko.

Kutokana na kuzoeleka huko na kwa sababu ya kutokuwa na tabia ya kukwapua vya watu kama wafanyavyo mateja wengine katika vituo vya mabasi na kwingineko, wa kwenye makaburi hayo wanapewa ushirikiano na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa dau wanalolitaja na hivyo kuligeuza eneo hilo kuwa lao la kudumu kibiashara.

Uchunguzi wa gazeti hili uliothibitishwa na baadhi ya mateja hao, wakazi wa eneo hilo, viongozi wa mitaa na watu waliopotelewa na makaburi walimozikwa ndugu zao, umethibitisha kuwapo uozo mkubwa katika makaburi hayo ‘yanayomilikiwa’ na genge hilo kama sehemu ya kujiingizia kipato isivyo halali.

Aidha, imethibitika kuwa mateja hao wasio na tabia ya kuibia mtu wala kudhuru wanaoingia na kutoka kwenye makaburi hayo kusaka huduma ya maziko, hufukua makaburi ya waliozikwa kuanzia miaka miwili iliyopita kurudi nyuma na kuzika maiti wapya huku wakifahamu kuwa eneo hilo limejaa na linastahili kuachwa huru.

Kwa maelezo ya mateja waliozungumza na HABARILEO, wafu wanaowafukua zaidi ili kupata
makaburi ya wazi ni watoto wachanga bila kujali walizikwa lini pamoja na watu wazima waliozikwa kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Mateja walonga
Kwa masharti ya kutotajwa gazetini, baadhi ya mateja waliozungumza na HABARILEO kwa nyakati tofauti makaburini hapo, walidai kuishangaa Serikali kwa kusahau kuwapelekea vifaa vya afya kwa kuwa kazi wanayoifanya ni ya hatari kiafya.

Jumapili, 29 Aprili 2012

KADA WA CHADEMA ACHINJWA HUKO ARUMERU.


MWENYEKITI wa Chadema wa kata ya Usa River w i l a y a n i Arumeru mkoani hapa, Msafiri Mbwambo (32) mkazi wa Lake Tatu, ameuawa kwa kuchinjwa na kiwiliwili kutelekezwa makaburini na watu wasiojulikana.

Tukio hilo linalohusishwa na masuala ya kisiasa, lilitokea juzi saa tatu usiku eneo la Mukidoma,
Usa River, ambako wauaji wanadaiwa kutumia panga kumchinja Mbwambo na kutokomea.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walidai kuwa kabla ya tukio Mbwambo alikuwa na wenzake wakistarehe kwa vinywaji, lakini yeye hakuwa anakunywa chochote lakini ghafla alipigiwa simu na watu hao, wakidai kuwapo wanachama wa CCM waliotaka kurudisha kadi na kujiunga na Chadema.

Taarifa zilidai kuwa Mbwambo alichukua pikipiki na kuwafuata, lakini hakurudi hadi mwili wake ulipokutwa umetelekezwa kando ya barabara makaburini, pikipiki na vitu vingine vikiwa eneo hilo bila kuchukuliwa na wauaji.
R I P Mbwambo.
Hata hivyo, chanzo cha tukio hilo hakijajulikana ila taarifa za awali zinahusisha masuala ya
kisiasa, kwani baada ya uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki kumalizika, malumbano ya kisiasa na kukamiana yaliendelea eneo hilo.

Katika uchaguzi huo wa Aprili mosi, Joshua Nassari wa Chadema aliibuka mshindi akimbwaga
mshindani wake mkubwa, Sioi Sumari wa CCM baada ya jimbo hilo kumpoteza mbunge wake,
Jeremiah Sumari ambaye ni baba mzazi wa Sioi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alithibitisha kutokea tukio hilo
na kudai kuwa, polisi bado wanafanya uchunguzi na hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika mochari ya hospitali ya mkoa ya Mount Meru kwa
uchunguzi zaidi

Jumamosi, 28 Aprili 2012

KIKWETE KUPANGUA BARAZA LA MAWAZIRI, NI BAADA YA KIKAO CHA NEC JANA.

Rais Kikwete akiwa kwenye Kikao Cha Kamati Kuu Ya CCM jana
RAIS Jakaya Kikwete, amewasilisha kwenye Kamati Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), taarifa yenye azma ya kulipanga upya Baraza la Mawaziri ili kuwawajibisha Mawaziri waliotajwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusika na ubadhirifu wa rasilimali za umma.

Pamoja na Baraza la Mawaziri, Rais Kikwete katika taarifa hiyo kwa Kamati Kuu, ameeleza pia nia yake ya kupangua watendaji wakuu wa Wizara wakiwemo Makatibu Wakuu na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, waliotajwa pia na CAG kuhusika na ubadhirifu huo.

Kutokana na kuibariki taarifa hiyo iliyowasilishwa na Rais Kikwete kwa Kamati Kuu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete ameshauriwa na Kamati hiyo kulisuka Baraza hilo mapema iwezekanavyo.

Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Taifa, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari kwamba pamoja na taarifa hiyo ya Rais, Kamati Kuu pia ilipokea na kuzijadili taarifa na maazimio ya Kamati ya Wabunge wa CCM na Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM juu ya kilichotokea kwenye Bunge lililomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.

“Pamoja na taarifa hizo Kamati Kuu imepokea taarifa ya jinsi Rais alivyojipanga kuchukua hatua za kuwawajibisha Mawaziri na Watendaji wa Serikali na wale wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali, Kamati za kudumu za Bunge na wabunge bungeni, “ alisema Nape.

Alisema Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa serikali yao na inapongeza juhudi za serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa na Bunge hilo.

Kwa mujibu wa Nape, Rais Kikwete pamoja na kuhudhuria sherehe za Muungano, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda juzi mchana, ambaye alimpatia taarifa ya kile kilichotokea bungeni Dodoma hadi kufikia hatua ya Kamati ya Wabunge wa CCM, kuwataka Mawaziri waliotajwa kwenye taarifa ya CAG kuwajibika.

Alichukua nafasi hiyo kupuuza taarifa za chini kwamba kambi ya upinzani bungeni ndiyo iliyosababisha shinikizo hilo, akisema taarifa ya CAG imeweza kupelekwa na kujadiliwa bungeni kutoka na mfumo aliouasisi Rais Kikwete wa kutaka taarifa ya CAG kuwa wazi zaidi kuliko ilivyokuwa awali ikiwa ni pamoja na kupelekwa bungeni kwa uwazi ili kujadiliwa.

“Hili ni vizuri likafahamika. Rais hajaishia hapo tu, hata ule mfumo wa maofisa wa CAG kuwa na ofisi kwenye majengo ya serikali kama kwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa) sasa haupo. Rais ameweka mfumo ambao wakaguzi hawa sasa wanakuwa na ofisi nje ya majengo ya serikali ili wanapokuja kuwakagua watendaji wa serikali wawe huru,” alisema Nape.

Ingawa Nape hakuwataja lakini katika kikao cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Mawaziri saba walibanwa na Wabunge wa CCM wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu na hivyo kukididimiza chama hicho kisiasa.

Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo alituhumiwa na wabunge wengi kuwa si mwadilifu na
anaongoza kutumia fedha za umma. Mkulo pia alituhumiwa kuuza mali za Serikali kiholela bila kulishirikisha Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC). Ripoti ya CAG ya mwaka uliopita wa fedha imetoa mifano ya viwanja vilivyouzwa na Mkulo bila kuishirikisha CHC.

Waziri mwingine ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda ambaye wizara yake inatuhumiwa kutumia Sh bilioni moja kwenye Maonesho ya Nane Nane. Mwingine ni Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami na Naibu wake Lazaro Nyalandu ambao wanatuhumiwa kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango (TBS).

Kwenye orodha hiyo yumo Waziri Jumanne Maghembe ambaye ni Waziri wa Kilimo anayeelezwa kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa bodi ya Pamba ambao wametafuna Sh bilioni 2 zilizotolewa na Serikali kuwalipa wakulima wa zao hilo baada ya kutokea mdororo wa uchumi.

Pia yumo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye wizara yake imetajwa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa imegubikwa na rushwa katika ununuzi wa mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura.

Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika ambaye wizara yake kwenye taarifa ya CAG
imeonesha kufanya madudu kutokana na ulaji uliokithiri kwenye halmashauri za wilaya anashutumiwa kushindwa kuchukua hatua kwa watendaji wa chini yake badala yake amekuwa anawahamisha vituo vya kazi wabadhirifu hao.

Habari hizo pia zilimtaja Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige ambaye wizara
yake imegubikwa na kashfa ya majangili kuua tembo wengi mwaka jana kuliko wakati
wowote ule kuwahi kutokea. Utata wa ugawaji wa vitalu vya kuwindia pia ni kashfa
ambayo imekuwa inaitafuna wizara hiyo kwa muda mrefu. Nape hakusema kama Mawaziri hao wataguswa na fagio hilo la Rais Kikwete au la.

Nape alisema pamoja na Mawaziri hao waliotajwa, Rais anaweza kuchukua mwanya huo kuwapangua Mawaziri na watendaji wengine wa serikali anaoona mchango wao katika kuiendesha serikali umekuwa mdogo kuliko anavyohitaji.

Mbali ya hilo, Nape alisema Kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye serikali ya Mapinduzi Zanzibar na imewapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa jinsi walivyojadili taarifa hiyo na imeipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa hiyo na kuanza kuifanyia kazi.

Katika hatua nyingine Kamati Kuu ya Taifa ya CCM, imewateua wanachama wake watano kuwa Kaimu Makatibu wa Mikoa wa chama hicho baada ya serikali kuunda mikoa mipya mitano ya Geita, Njombe, Simiyu, Katavi na Mjini Magharibi, Zanzibar.

Nape aliwataja walioteuliwa kuwa ni Hilda Kapaya, Shaibu Akwilombe, Hosea Mpagike, Alphonce kinamhala na Aziz Ramadhan Mapuri, ambao vituo vyao vya kazi vitatajwa baadaye

Jumatano, 18 Aprili 2012

KAMATI YA MAZISHI YA KANUMBA YASEMA PAMOJA NA UMAARUFU WAKE KANUMBA HAKUWA TAJIRI.

KAMATI ya mazishi ya aliyekuwa msanii maarufu nchini, Steven Kanumba, imesema imetumia Sh milioni 70 kugharimia maziko yaliyofanyika Aprili 10.

Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 7 na kuzikwa siku tatu baadaye kwenye makaburi ya Kinondoni na maelfu ya wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani.

Marehemu Kanumba enzi za uhai wake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtitu Gabriel alisema jana kwamba kamati hiyo iliyoratibu mazishi ya msanii huyo tangu Aprili 7, ilikusanya michango na ahadi za takribani Sh milioni 90 huku gharama za mazishi hadi maziko vikigharimu Sh 70,502,000.

Akitoa mchanganuo huo, Mtitu alisema Kamati yake ilitumia Sh 52,102,000 na ahadi za malipo ya vifaa ambazo ni Sh 18,400,000 na zilitumika kwa vifaa mbalimbali zikiwamo taa, jukwaa, viti na maturubai.

Alisema Sh milioni nne zilizobaki kutokana na zilizokusanywa zilikabidhiwa kwa mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa na Kamati haijatimiziwa ahadi ya Sh milioni 15.5.

Alipoulizwa kama Kanumba ameacha mali ya Sh milioni 700, Mtitu alisema pamoja na msanii huyo kuwa na jina kubwa, lakini alikuwa masikini na si tajiri kama ilivyokuwa inafikiriwa.

“Pamoja na jina la Kanumba kuwa kubwa, hakuwa na fedha, na ndiyo maana baada ya kutoka kuhifadhi mwili wake Muhimbili, tulijikusanya na kujipanga kuhakikisha tunampumzisha kwenye nyumba ya milele kwa heshima ya hali ya juu na hili tumelifanikisha,” alisema Mwenyekiti huyo.

Pamoja na kukanusha ‘kuchakachua’ fedha zilizokusanywa, Mtitu alisema Kamati yake ilianza ikiwa haina hata Sh 100 na kulazimika wanakamati kubeba gharama za awali.

“Tulitambua mchango mkubwa wa Kanumba enzi za uhai wake, tuliona iko haja ya kufanya yote haya, tulianza tukiwa hatuna hata Sh 100, ingawa baadaye Kamati ilichangia gharama za awali ambazo zilipatikana miongoni mwa wajumbe wenyewe,” alieleza.

Akizungumzia kushindwa kutoa nafasi kwa wananchi kuaga mwili wa Kanumba, Mtitu alisema Kamati ilikadiria kuwa watu wapatao 40,000 wangehudhuria kutokana na idadi ya watu ambao walikuwa wakifika msibani, lakini wingi wa watu na ufinyu wa muda siku hiyo ndivyo vilifanya utaratibu ukatizwe.

“Wakati wa mazishi tulikuwa tunahudumia waombolezaji 3,000 mpaka 4,000 kwa siku, hivyo tukaweka makadirio ya watu 40,000 siku ya maziko, lakini watu waliojitokeza walikuwa wengi na ikawa vigumu kutoa nafasi kwa wote kuaga, hasa kutokana na wingi na mazingira yalivyokuwa na muda pia,” alifafanua.

Kamati iliyoratibu shughuli zote za mazishi iliundwa na wadau wa filamu, wasanii, wafanyabiashara, ndugu na marafiki wa Kanumba, aliyekuwa mwigizaji nyota wa filamu nchini na aliyevuma pia katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Kifo chake kilikuwa cha utata baada ya kudaiwa kuwa na ugomvi na mwigizaji wa kike, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake.

Lulu tayari amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya msanii huyo.

Katika hatua nyingine, Gabriel alisema katika kumuenzi Kanumba, wanafikiria kuandaa Tuzo za kutambua kazi za sanaa ya maonesho na filamu, ambazo wataziita kwa jina la Tuzo za Steven Kanumba

Ijumaa, 6 Aprili 2012

LEMA ASEMA HATAKATA RUFAA JUU YA HUKUMU YA KUVULIWA UBUNGE.

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) akiondoka kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Arusha baada ya kusikiliza hukumu yake ambapo mahakama hiyo ilitengua matokeo ya uchaguzi uliopita na kumvua ubunge jijini humo. (Picha na Marc Nkwame).

Jumanne, 7 Februari 2012

WAZIRI ATIMULIWA NA NYOKA KANISANI.

Mh. Aggrey Mwanri kushoto akiwa na Askofu Thomas Laizer(Picha na Maktaba)
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, juzi
alitimua mbio kunusuru maisha yake na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Sanya Juu, mtaa wa Kilingi.

Hali hiyo ilitokea baada ya tukio la nyoka kutoka kusikojulikana kuingia kanisani humo huku Naibu Waziri akijiandaa kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa hilo. Tukio hilo lilitokea katika ibada ya saa nne iliyokuwa ikiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, ambayo pia ilikuwa ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.

Mwanri aliyekuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kuendesha harambee hiyo ya Kanisa la Kilingi, akiwa na mkewe meza kuu, aliwashangaza waumini alipokimbia akiwa amenyanyua mikono juu. Kutokana na kuibuka kwa nyoka huyo, waumini walikimbizana na kiumbe huyo kwa mawe na viti bila kujali kama walikuwa ibadani, huku Askofu na wachungaji wengine wakiendelea kusali na waumini kutakiwa kurejesha utulivu katika ibada.

Hata hivyo, jitihada za waumini za kumkimbiza nyoka huyo kutaka kumwua hazikufanikiwa, baada ya kutoweka asionekane tena, jambo lililoacha simulizi la ni kwa jinsi gani alifika mahali hapo. Awali mgeni rasmi wa harambee hiyo, alikuwa awe Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, lakini kutokana na kubanwa na shughuli za sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa CCM, alishindwa kufika.

'Habarileo' lilishuhudia Mwanri ambaye pia ni Mbunge wa Siha akikimbia huku akitamka maneno ya “shindwa kwa Jina la Yesu wewe shetani, shetani shindwa kwa Jina la Yesu,” huku wageni wengine waalikwa wakianguka chini wakijiokoa.

Jumatano, 21 Desemba 2011

WANASIASA WAILAUMU TAKUKURU

WANASIASA wameinyooshea vidole Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(TAKUKURU), wakitaka wajisafishe ili iaminike na kurudisha heshima yake katika jamii.

Wakichangia mada iliyotolewa na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka Takukuru, Mary Mosha katika mafunzo ya viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu Uongozi, Uwajibikaji na Utawala Bora, wanasiasa hao walisema kuwa Takukuru ni chanzo cha rushwa nchini.

Ms Mary Mosha, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma Takukuru.


Akichangia mada hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye alisema kwa sasa Takukuru harufu yao mtaani siyo nzuri.


Nape alisema katika hata mambo ya kawaida yanayoonekana yana mazingira ya rushwa ikiwemo miradi ya maendeleo, maofisa wa Takukuru wamekuwa wakidai wanaendelea na uchunguzi huku wananchi wakizidi kuwalalamikia.


“Takukuru harufu yenu mtaani kwa sasa siyo nzuri, wakati mwingine inaonekana wazi mnatumika kusafisha watu, sasa itafika mahali watu wataona Takukuru ni mzigo maana wanalipwa fedha za walipa kodi, lakini kazi yao haionekani,” alisema Nape.


Alisema watu wamekuwa wakiona rushwa ni ya uchaguzi wakati kuna rushwa mbaya zaidi kwa
baadhi ya watumishi kutumia rasilimali pasipo mpangilio au kwa malengo ambayo hayakukusudiwa bila kuchukuliwa hatua zozote.


“Kwa sasa tunaona rasilimali hazitusaidii kwa sababu wanaowajibika kuzisimamia hawatimizi wajibu wao, inatupasa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kwa sababu Takukuru mkiendelea hivi wananchi watawachukia sana,” aliongeza Nape.


Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema adui mkubwa wa rushwa nchini ni Takukuru yenyewe kwa kuwa uwajibikaji wao ni mbovu na viongozi wake hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.


Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Lifa Chipaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa TADEA, alisema rushwa haipo tu ndani ya vyama, bali hata ukwepaji wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara ni rushwa.


Chipaka alisema watumishi wa Takukuru wamekuwa wakilipwa fedha nzuri, wakipewa magari ya kifahari ya kutembelea na nyumba nzuri, lakini hakuna wanachokifanya katika jamii.


Mapema, akitoa mada yake, Mosha alisema kama vyama vya siasa visipodhibiti rushwa ndani ya vyama vyao, vitashindwa kudhibiti hata nje ya vyama na hivyo kusababisha kupatikana viongozi wasiofaa.

Jumapili, 4 Desemba 2011

MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWALIMU AWASUMBUA POLISI SUMBAWANGA.

MKAZI wa Mazwi mjini Sumbawanga, Yusuph Ahmad 'John' (20) ambaye anatuhumiwa kumuua mwalimu wa Shule ya Msingi Kianda, juzi alizua kizaazaa baada ya kufanikiwa kwa
muda kutoroka akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa tisa mchana mjini hapa . Mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake
anadaiwa kumuua kwa kumnyonga mwalimu Richard Emilly (50) katika kitongoji cha
Chiluba kilichopo eneo la Mazwi mjini hapa.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Isuto Mantage amethibitisha kukamatwa tena kwa mtuhumiwa huyo na anatarajiwa kupandishwa kizimbani kesho baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Inadaiwa kwa ushirikiano wa raia wema mtuhumiwa huyo aliweza kukamatwa na askari Polisi
huku wenzake wakidaiwa kufanikiwa kutoroka na kujificha kusikojulikana, lakini muda mfupi
baada ya kufikishwa kituo cha Polisi mjini hapa kwa mahojiano akiwa chini ya ulinzi mkali wa
polisi aliweza kutoroka na kuanza kukimbia.

Polisi Dar es salaam wakiwa kazini.(Picha na Maktaba)


Hali hiyo ilisababisha kizaazaa mjini hapa hususani maeneo hayo ya kituo cha Polisi pale wananchi walipojitokeza na kushuhudia mtuhumiwa huyo akichanja mbuga akielekea eneo la Hospitali ya Mkoa huku polisi wakipuliza filimbi wakiashiria kutoroka kwa mtuhumiwa huyo.
“Sijawahi kuona `live’ nimezoea kuona kwenye video leo nimeshuhudia; ilikuwa kama kuona mkanda wa video mtuhumiwa huyo baada ya kutoroka alianza kukimbilia eneo la Hospitali
ya Mkoa huku wengi wetu tukiwa tumepigwa na butwaa kwa muda,“ alisema shuhuda aliyejitambulisha kwa jina moja la Jackson, mkazi wa eneo la Kizwite mjini hapa.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa baada ya kufika eneo hilo la Hospitali ya Mkoa aliparamia ukuta
uliozunguka eneo la hospitali hiyo ambapo alishukia ndani ya eneo la hospitali na kisha akapanda juu ya mti mrefu uliopo kwenye eneo hilo na kujificha kwenye matawi yake.
Huku akiwa amejificha kwenye matawi mtini, polisi wenye silaha waliosheheni kwenye magari kadhaa kukabiliana naye walifika eneo hilo la hospitali na kuanza msako mara moja bila mafanikio.
Wakiwa wamekata tamaa na kujiandaa kuondoka eneo hilo ndipo mtuhumiwa alipojirusha kutoka mtini na kutua kwenye paa la moja ya majengo hospitalini hapo.
Mwandishi wa habari hizi naye alifika eneo hilo na kushuhudia mtuhumiwa akiwa anajirusha kutoka mtini na kutua salama kwenye paa la jengo mojawapo hospitalini hapo ndipo umati uliokusanyika eneo hilo walipoanza kupiga kelele wakionesha alipo mtuhumiwa.
“Wote tulijua ameondoka eneo hili la hospitali nadhani aliingiwa na hofu akidhani tumemwona
kumbe wapi, kama angevumilia kujificha kwenye matawi yale ya mti ule hadi usiku halafu akaamua kushuka hakuna ambaye angeweza kumshuku,“ alisikika akisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.


Mtuhumiwa aliwekwa tena chini ya ulinzi mkali huku akipata mkong’oto wa nguvu kutoka kwa
askari Polisi.
“ Bila shaka wamemuumiza sana vipi kama wangemchukua tu bila ya kumpiga kikatili vile? “
Alihoji mmoja wa mashuhuda aliyekerwa na kitendo cha askari Polisi kuanza kumpatia kipigo mtuhumiwa huyo.
Kamanda Mantage alisisitiza kuwa, Polisi inaendesha msako mkali ili kuwabaini watuhumiwa
wengine wanaohusika katika mauaji ya mwalimu huyo

Jumatano, 30 Novemba 2011

HUKUMU KESI YA JERRY MURO NA WENZAKE KUTOLEWA LEO.

BAADA ya kesi inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake kuunguruma kwa zaidi ya mwaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo inatarajiwa kuhitimishwa kwa kutolewa hukumu.

Muro na washitakiwa wenzake Deogratius Mgasa na Edmund Kapama, wanadaiwa katika kesi hiyo kuomba na kutaka kupokea rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Michael Wage.

Kwa mara ya kwanza, Muro, Kapama na Mgasa walipandishwa kizimbani Februari 5, mwaka jana na kusomewa mashitaka yao na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali, Boniface Stanslaus akisaidiana na mwendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincolin mbele ya Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe.

Jumanne, 29 Novemba 2011

CHADEMA WAFIKIA MUAFAKA NA KIKWETE JUU YA MUSWADA WA KATIBA MPYA.

Image
Rais Kikwete akiagana na ujumbe wa CHADEMA ukiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe baada ya kumaliza mzungumzo ya siku mbili juzi na jana Ikulu na kufikia makubaliano kadhaa juu ya uundwaji wa Katiba mpya.
MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge hivi

karibuni utasainiwa na Rais Jakaya Kikwete kama ilivyopangwa.
Hali hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa jana kati ya Rais na Kamati ndogo ya Chadema iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe.
Kususia mjadala wa Muswada huo kwa wabunge hao wa vyama hivyo, ulitokana na madai yao ya kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni wakidai haukuwa umesomwa na wananchi na kuuelewa, hivyo kukosa kuuchangia, lakini walikataliwa na Spika Anne Makinda.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa jana Ikulu Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutakuwa na haja ya sheria hiyo baada ya kusainiwa kuendelea kuboreshwa, ili ikidhi mahitaji ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.
Pia kutakuwa na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba mpya.
Awali ilielezwa kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya uelewano ambapo Rais Kikwete aliwahakikishia Chadema kuwa yeye na Serikali yake wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.
Kulingana na hatua iliyofikiwa jana, Rais atasaini Muswada huo kuwa sheria ambayo inatarajia kuanza kutumika Desemba mosi, lakini wakati ikiendelea kutumika, kutakuwa na fursa ya kuifanyia marekebisho endapo haja itajitokeza.
Hili si jambo jipya kwa masuala ya uandishi wa Katiba mpya, kwani hata ya Kenya ilipitishwa na mpaka sasa zipo taarifa kuwa imeshafanyiwa marekebisho mara 11 kutokana na mahitaji yanayoibuka kwa kuzingatia mazingira na muktadha.
Makubaliano ya jana, yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imeanza kuibuka kwa Chadema na makundi mengine kutaka kufanya maandamano nchi nzima, kupinga Muswada huo kusainiwa na kushinikiza urejeshwe bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza.

Ijumaa, 25 Novemba 2011

HAKIMU AWAWAKIA MAWAKILI WASOFIKA MAHAKAMANI KUWA ATAPAMBANA NAO.

Aliyekuwa Mhasibu TRA -Justice Katiti
HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waliyalwande Lema ametangaza mgogoro na mawakili wa washitakiwa katika kesi ya ya wizi wa Sh bilioni 3.8 inayomkabili mhasibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Justice Katiti na wenzake wanne.


Kesi hiyo Novemba 24 ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuendelea kusikilizwa, ndipo Lema alipotangaza kuwa atafanya ukorofi kwa wakili ambaye hatafika mahakamani katika tarehe ambazo atakuwa amepanga kusikiliza kesi hiyo.


Lema alitoa onyo kwa mawakili hao kuwa wasipofika mahakamani siku hizo hatasimamisha usikilizwaji au kuahirisha kesi, hivyo wawepo vinginevyo atafanya ukorofi na ametoa taarifa mapema.


“Kawaelezeni mawakili wenzenu, yule pasua kichwa ametangaza ukorofi, sitaki kuandika tu kwenye jalada hapa nasema kabisa asiyefika mahakamani, mimi nitaendelea na kesi na mteja wake atakuwa hana mwakilishi,” alisema Lema.


Lema alisema kifo tu au ugonjwa ndivyo vitakavyomfanya asisikilize kesi hiyo, lakini si mawakili wa washitakiwa kutokuwepo mahakamani katika siku hizo ambazo ni kuanzia Desemba 6 hadi 8, mwaka huu.


Katika mashtaka yao wanadaiwa Mei na Novemba mwaka 2008 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kuiba Sh bilioni 3.8 za TRA na kuzihamishia kwenye akaunti za kampuni mbalimbali na za watu binafsi

Alhamisi, 24 Novemba 2011

MFANYAKAZI TRA KORTINI KWA WIZI SHILINGI MIL. 944/-

T R A Boss, Mr. Kitilya.
MFANYAKAZI wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Sangu John amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka 132 akidaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 944, mali ya mwajiri wake kwa njia za udanganyifu pamoja na kulipa mishahara hewa.


Mashitaka hayo alisomwa jana mbele ya Hakimu Aloyce Katemana na mawakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincon, Osward Tibabyekomya wakisaidiana na Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro.


Mashitaka yalikuwa ni ya kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri wake, kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kusababisha hasara kwa mamlaka hiyo ya Sh 944,169,330.


Katika mashitaka ya kwanza, John alidaiwa Juni 19, 2006 katika ofisi za TRA Makao Makuu Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam kwa nia ya kudanganya, alighushi orodha ya malipo ya mshahara kwa mwezi huo, akionesha wafanyakazi hewa tisa wa shirika hilo walitakiwa walipwe Sh 12,000,000 huku akijua si kweli.


Katika mashitaka ya kutumia nyaraka kumpotosha mkuu wake wa kazi, alidaiwa mojawapo ni Juni 20, 2006 katika ofisi za TRA akiwa mwajiriwa, aliwasilisha orodha hiyo kwa mkuu wake wa kazi akidai kwamba wafanyakazi hao walitakiwa kulipwa fedha hizo huku akijua sio kweli.


Mashitaka mengine alidaiwa kwa nia ya kudanganya ambapo alijipatia kutoka Benki ya NBC fedha hizo akijidai kuwalipa watu hao kwa mshahara wa Juni 2006. Katika mashitaka, mengine alidaiwa kudai malipo hayo hewa miezi mingine kuanzia Juni 2006 hadi Agosti 2009.


Mashitaka mengine John alidaiwa alighushi nyaraka kuonesha mishahara ya wafanyakazi wa TRA, Novemba ni Sh 2,207,122,430 akijua sio kweli, alidaiwa kuendelea kumdanganya mwajiri wake katika miezi mingine katika kipindi hicho akionesha mishahara tofauti na iliyokuwa ikistahili wafanyakazi wa TRA kwa mwezi.


Aidha, mshitakiwa huyo alishitakiwa pia kwa kufanya mchezo huo aliisababishia hasara Mamlaka ya Mapato Tanzania ambayo ndio ilikuwa mwajiri wake Sh 944,169,330.


Alikana mashitaka yote na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa nusu ya fedha hiyo, Sh 472,084,665. Kesi hiyo imepangwa kutajwa Desemba 5, mwaka huu na upelelezi haujakamilika.

Ijumaa, 28 Oktoba 2011

SIMU YA MKONONI YAMTAMBULISHA ALIYEKUFA KWENYE AJALI YA MOTO WA BASI.

Ajali ya basi iliyotokea juzi.

WAKATI mabaki ya miili ya watu 12 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi la Deluxe yakizikwa jana, mmoja wa abiria waliokufa katika ajali hiyo, Salome Benjamin (24) alitoa simu yake itumike kutoa taarifa kwa ndugu zake.

Salome, mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma, ameelezwa kuwa aliwapa mashuhuda hao simu hiyo na kuwataka wawasiliane na ndugu zake kwamba imeshindikana kwake kuokolewa hivyo wasihangaike.

Akisimulia jana jinsi mwanawe alivyokufa, baba mdogo wa Salome, Michael Isamuhyo alisema shuhuda aliyetumia simu ya mwanawe aliwaeleza kuwa, Salome kabla ya kufa, aliwataka wasihangaike.

Isamuhyo aliyezungumza na gazeti hili, alisema shuhuda huyo aliwaeleza kuwa Salome kabla ya kufa alitokea dirishani upande wa kulia na kupiga kelele ya kuomba msaada.

Shuhuda huyo kwa mujibu wa Isamuhyo, alisema walikwenda kumsaidia lakini walishindwa kwa kuwa alinasa sehemu ya miguu ndani ya basi hilo.

“Shuhuda alituambia kuwa, wakati wanamvuta, walibaini kuwa hawataweza kumuokoa kwa kuwa sehemu ya miguu ilinasa na alipoona hawezi kuokolewa, alirusha simu nje kwa shuhuda huyo.

“Baada ya kutoa simu hiyo, alimtaka atueleze sisi ndugu zake kuwa ameshindikana kuokolewa ili tusihangaike,” alieleza kwa uchungu Isamuhyo.

Baba wa Salome, Benjamin Magige akizungumzia msiba huo alisema; “Nimempoteza mtoto wangu wa pekee wa kike, nimebaki na mdogo wake wa kiume tu, walikuwa wawili pekee, nina uchungu sana.

“(Salome) alikuwa amalize chuo keshokutwa tu, ni maumivu makubwa kwa familia, mama yake kaja lakini hawezi kuzungumza, huu si wakati wa Serikali kufumbia macho ajali hizi, tuumie wote na tuhakikishe zinakoma,” alisema Magige huku akilia.

Maiti hao walizikwa katika makaburi yaliyochimbwa kwa kuambatana katika eneo la Air Msae walipozikwa abiria 25 waliokufa katika ajali ya basi ya Air Msae mwaka 1999, umbali wa kilometa takribani 10 kutoka ilipotokea ajali hiyo.

Alhamisi, 27 Oktoba 2011

WALIOKUFA AJALI YA BASI JUZI KUZIKWA KABURI LA PAMOJA LEO

MIILI ya watu 12 walioteketea kwa moto katika ajali ya basi la Deluxe Coach iliyotokea Misugusugu mkoani Pwani juzi, watazikwa leo na Serikali kwa heshima zote katika kaburi moja katika eneo la Air Msae mjini Kibaha.
PICHA MBAYA
Maiti iliyoungua ikiondolewa.
Eneo hilo ndipo walipozikwa watu waliopata ajali ya basi la Air Msae lililokuwa likitokea Arusha kuja Dar es Salaam miaka ya 1990.


Uamuzi huo umefikiwa jana katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mwantumu Mahiza kutokana na miili hiyo kuharibika vibaya na kushindwa kutambulika.
Gari iliyoteketea kwa moto.
Akizungumzia mazishi hayo jana, Mahiza alisema kabla ya maziko, miili ya watu hao itachukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya vinasaba (DNA) ili vifanikishe utambuzi wao.


Taarifa kutoka Hosptali Teule ya Tumbi, zilieleza kuwa hata wananchi waliokwenda kujaribu kutambua ndugu zao, walishindwa kufanya hivyo kutokana na kuharibika kwa miili hiyo ambayo baadhi imekuwa majivu.


Kutokana na hali hiyo, Mahiza aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kufanikisha kuwatambua ndugu zao, kwa kupeleka vitu kama nguo ambazo ndugu zao walizitumia siku chache kabla ya ajali hiyo.


"Tunaomba wananchi walioondokewa na ndugu zao katika ajali hii watoe ushirikino kwa kuleta vitu kama soksi, shati, khanga au viatu alivyokuwa anatumia ndugu yao hivi karibuni ambavyo havijafuliwa ili visaidie kutambuliwa baada ya kupimwa kwa njia ya vinasaba,” alisema Mahiza.


Ofisa Habari wa Hosptali Teule ya Tumbi, Rose Mtei alisema kuwa majeruhi waliofikishwa katika hospitali hiyo ni 36 ambapo 35 waliruhusiwa na mmoja aliyelazwa anaendelea vizuri.

Jumatatu, 24 Oktoba 2011

SERIKALI IWE MAKINI, ALBINO WAMEANZA KUUAWA TENA.

MLEMAVU wa ngozi aliyekatwa mkono wake wa kulia na watu wasiojulikana, Kulwa Lusana (16), amesimulia alivyojikuta akiwafukuza wavamizi hao, huku akilia na kuwaomba wamrudishie mkono wake.

Kulwa ametoa maelezo hyao Polisi jana na kuongeza kuwa juhudi hizo za kudai kurudishiwa mkono wake, hazikuzaa matunda, kwani wakataji hao walizidi kutokomea gizani na kumuacha akitapatapa.

Baada ya kupoteza matumaini ya kuupata mkono wake, Kulwa alisimulia kwamba akiwa anagugumia kwa maumivu makali, alikimbilia kwenye nyumba ya baba yake ambapo aligongana naye mlangoni na wote kuanguka chini.

Mlemavu huo alifanyiwa unyama huo juzi saa 7 usiku katika Kijiji cha Mbizi, Kata ya Segese wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Diwani Athumani alisema watuhumiwa hao walivunja mlango na kuingia ndani kwa albino huyo na kuanza kumshambulia na kumjeruhi sikio na baadaye wakakata mkono wake wa kulia na kuondoka nao.

Kwa mujibu wa Kamanda Athumani, albino huyo alipiga kelele ya kuomba msaada kwa baba yake, Lusana Nkola ambaye hata hivyo wakati akitoka katika harakati za kumuokoa mtoto wake huyo, alipigwa jiwe kichwani akaanguka chini.

Alisema baada ya kufanyiwa unyama huo, watu hao waliufunga mkono huo kwenye mfuko na kuanza kukimbia nao na kutokomea pasipo julikana na kumuacha albino huyo akigugumia kwa maumivu makali.

Kutokana na tukio hilo, Polisi inamshikilia Petro Nkola mkazi wa kijiji cha Mtukula Runzewe wilayani Bukombe ambaye ni baba mdogo wa mlemavu wa ngozi, Kulwa Lusana (16).

Hata hivyo, Kamanda Athumani hakutaka kueleza kwa undani sababu za kumshikilia baba huyo zaidi ya kufafanua kuwa ni kwa mahojiano zaidi na uwezekano wa kuwapata watuhumiwa wengine waliotoroka na mkono wa mlemavu huyo.

Kulwa kwa sasa yupo katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama akiuguza jeraha lake na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda Athumani aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watu wote watakaowadhani kuwa ni washiriki wa tukio hilo la kinyama alilofanyiwa mtoto huyo.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku chache tu baada ya mlemavu mwingine wa ngozi, Adam Robert (14) kujeruhiwa kwa kukatwa na sime mkono wa kushoto na kunyofolewa vidole vya mkono wa kulia huko katika Kijiji cha Nyaruguguna wilayani Geita, mkoani Mwanza.

Katika tukio hilo la Geita, baba mzazi na mama wa kambo wa mtoto huyo, wanashikiliwa kwa tuhuma hizo.

Ijumaa, 21 Oktoba 2011

YANGA YAPANDA NGAZI MOJA KUELEKEA KILELENI.

 Image






YANGA ya Dar es Salaam imezidi kunogesha mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuifunga Toto African mabao 4-2.

Kutokana na matokeo ya mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga sasa imefikisha pointi 18 na kupanda kutoka nafasi ya nne hadi ya tatu kwenye msimamo.

Azam FC iliyokuwa ikishika nafasi ya tatu imeshuka kwa ngazi moja, ambapo Azam pia ina pointi 18, lakini inazidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga ipo mbele mchezo mmoja zaidi ya Azam.

JKT Oljoro inaendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19, huku Simba yenyewe ikiongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 24, ambapo zote zimecheza mechi kumi.

Katika mchezo wa jana, Yanga ambayo ina udugu wa kihistoria na Toto African ya Mwanza
ilienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao hayo yalifungwa na Haruna Niyonzima dakika ya nane, Kenneth Asamoah dakika ya 12 na Jerry Tegete dakika ya 21 yote yakifungwa kwa mashuti.

Toto iliyokuwa ikionekana kuzidiwa kipindi cha kwanza ilicharuka dakika za mwisho na kupata
bao dakika ya 82 mfungaji akiwa Mohammed Soud.

Wakati mashabiki wakiamini mchezo huo ungemalizika kwa matokeo hayo ya mabao 3-1, Asamoah aliongezea Yanga bao la nne dakika ya 85 kabla ya Soud naye kupachika la pili dakika
ya 89.

Yanga ingeweza kupata mabao mengi zaidi lakini umaliziaji haukuwa mzuri kwa kushindwa
kulenga lango kila walipokaribia golini.

Hali hiyo pia iliikumba Toto Africans ambayo kwa nyakati tofauti wachezaji wake Soud,
Phabian James na Bakari Kigodeko walishikwa na kigugumizi cha miguu walipomkaribia kipa
Yaw Berko

Jumatano, 19 Oktoba 2011

BABA NA MAMA WAKAMATWA KWA KUMSHAMBULIA MTOTO WAO ALBINO GEITA.

Mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kwegyir akitokwa machozi baada ya kumuona kijana Robert Tangawizi (14) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) alivyojeruhiwa mkono wa kushoto na kisha kunyofolewa vidole vitatu vya mkono wa kushoto, wakati alipomtembelea hospitalini Geita mkoani Mwanza. (Picha na David Azaria)

.WATU watano wakiwemo baba mzazi na mama wa kambo wa kijana mlemavu wa ngozi, Adam Robert, wamekamatwa na Polisi wilayani Geita Mkoa wa Mwanza, kwa tuhuma za kumjeruhi
kwa kumkata mapanga na kumnyofoa vidole vitatu kijana huyo, mkazi wa Kijiji cha Nyaruguguna.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Liberatus Barlow, amethibitisha kukamatwa kwa
watuhumiwa hao, lakini alikataa kuwataja majina.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, zimeeleza kuwa miongoni mwa wanaoshikiliwa ni pamoja na mganga maarufu wa jadi, Rumanyika Yesu (49).

Wengine kwa mujibu wa taarifa hizo ni pamoja na baba mzazi wa Adam, Robert Tangawizi (36),
mama wa kambo wa majeruhi huyo ambaye amekuwa akimlea kwa siku nyingi, Agnes Majala (29).

Pia baba mkubwa wa Adam, Andrew Tangawizi (52) na mkazi wa kijiji hicho, Machibya Alphonce (30). Taarifa hizo zimeeleza kuwa baba mzazi amekamatwa kutokana na maelezo ya mtoto na mazingira ya tukio hilo.

Adam anadaiwa kueleza kuwa siku ya tukio, mtuhumiwa ambaye ametoroka na anatafutwa na Polisi, alitaka kufanya kitendo hicho machungani, lakini mtoto huyo alimzidi ujanja.

Katika maelezo hayo, Adam alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alimdanganyia kofia, lakini alikataa kabla ya kumtaka kuwapeleka ng’ombe kwenye nyasi nyingi ambapo kulikuwa na kichaka, lakini pia alikataa.

“Siku hiyo hiyo jioni mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwao na mtoto na kisha
akakaribishwa na baba mzazi na kuketi naye mahali walipokuwa wakiota moto (Kikome).

Ijumaa, 7 Oktoba 2011

WAZO LANGU-WAFUJAJI MALI ZA UMMA WAPATIWE DAWA YA KUDUMU.

UKWELI ulio wazi kuwa kuna wakati lazima nguvu za ziada zitumike kuhakikisha kuwa mambo mbalimbali yanaenda sawa hususani katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa katika matumizi ya rasilimali za umma.
Na Theopista Nsanzugwako.

Aidha, ni jambo la kawaida kusikia baadhi ya watumishi wa umma kumlalamikia mtumishi
mwenzao kwa vitendo vya kujilimbikizia mali kwa kutumia vibaya vyeo vyao na ofisi zao.

Kwa kuliona hilo, Rais Jakaya Kikwete aliamua kuipa jukumu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza watumishi wa umma ambao sio viongozi wanaotajwa kwa kujilimbikizia mali wakitumia vyeo vyao na ofisi walizokabidhiwa kuwahudumia wananchi.

Pia ameipa jukumu Sekretarieti hiyo kukamilisha mchakato utakaowezesha kutungwa kwa
sheria itakayotenganisha biashara na uongozi ili itumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema haitoshi kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza viongozi
namna walivyopata mali zao wakati kuna watumishi wengi wametajwa kumiliki mali nyingi
ambazo hazijapatikana kihalali.

Alisisitiza kuwa ili kupata ukweli usio na shaka kuhusu umiliki wa mali za watumishi na viongozi, kuna haja hivi sasa kwa Sekretarieti hiyo kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama
pamoja wananchi ili wathibitishe mali walizozitaja katika fomu za tamko la rasilimali, maslahi na madeni.

Alisema lengo la kuchukua hatua hiyo ni kufanya kuwepo kwa watumishi wenye maadili na uadilifu na sio wanaotumia ubabe, vitisho na wale wanaopenda rushwa na hivyo kupelekea nchi kukosa maendeleo.

Napenda kuunga mkono kauli ya Rais kushirikisha vyombo vya ulinzi kwani itakuwa rahisi katika kuwashirikisha katika vyombo vya sheria watakaobainika kutokana na ushahidi
utakaokuwepo.

Wakati Rais akisema hayo, Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema
Sekretarieti hiyo imeanza kupata mafanikio baada ya idadi ya viongozi wa umma wanaorejesha fomu kuongezeka kutoka viongozi 6,007 sawa na asilimia 76.8 katika mwaka jana hadi viongozi 8,465 ambayo sawa na asilimia 94 mwaka huu.

Alisema uundwaji wa Baraza la Maadili umesaidia kupokea malalamiko 41 dhidi ya ukiukwaji
wa maadili kwa viongozi ambapo tayari 24 walipatikana na hatia na kupewa onyo na wengine onyo kali.

Mimi binafsi naona bado Sekretarieti hiyo haijafanya kazi ambayo ni mategemeo ya
wananchi kutoka kwa Sekretarieti hiyo kwa kutoa hukumu itakayofanya watumishi na viongozi
wengine kuwa woga lakini siyo kwa kuwaonya tu.

Ni kweli wapo watumishi wa umma waliojilimbikizia mali kiasi ambacho hakuna wa kumfuatilia
na kujua uhalali wake, kama ilivyokuwa kwa maofisa Ardhi na wengineo.

Kama kuna sheria inawabana katika kutoa adhabu hizo ni vema mikakati ikafanya ili ziweze
kubadilishwa na kuwezesha wafujaji hao kufikishwa mahakamani na ikidhibitika mali hizo zitaifishwe.

Hakuna haja kuwa ikifika hatua hiyo hata kama tatizo hili halitaisha basi litapungua na viongozi
na watumishi wa umma kuogopa mali za umma kama ukoma na kutumika vyeo vyao vizuri.

Imefika wakati kwa Sekretarieti hiyo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha viongozi na watumishi wa umma wanaotumia majukumu yao vibaya kwa kujilimbikizia mali
au kupata mali isivyo halali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa