Alhamisi, 17 Mei 2012

RC MWANZA AAGIZA POLISI WASHUGHULIKE NA TUKIO LA KADA WA CHADEMA KUNG'OA SIKIO KWA KUNG'ATA.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo ameiagiza Polisi mkoani hapa kuchukua hatua zinazostahili kwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Ilemela, Abel Mwesa baada ya kutuhumiwa kumng’ata na kuondoa kipande cha sikio la mkazi wa kitongoji cha Nyabiti.

Ndikilo ametoa agizo hilo baada ya mlalamikaji, Lazaro Nolbert kufika ofisini kwake na kutoa malalamiko hayo ambayo aliyaripoti katika Kituo cha Polisi Mwatex tangu Aprili 26, mwaka huu, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Haya ndio mambo yanayolichafua Jeshi la Polisi, mtu ameripoti wiki mbili zilizopita hadi leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa huku akipokea barua za vitisho, jamani hebu chukueni hatua ili jeshi hilo liendelee kuaminiwa na wananchi,” alisema Ndikilo.

Alisema inaonesha baadhi ya maofisa wa Polisi wanaficha taarifa za matukio kwa maslahi binafsi na ndio maana tukio hilo halijafika kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa.

Akisimulia tukio hilo, mkazi huyo kitongoji cha Nyambiti, Lazaro Norobert (25), alidai kuwa sikio lake limeng’atwa na kuondolewa kabisa na Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Abel Mwesa baada ya kukosa chumba kwenye nyumba ya kulala wageni ya Amani inayomilikiwa na mzazi wa Lazaro.

Akizungumza na waandishi wa habari mbele ya mkuu wa mkoa juzi, alisema amelazimika kufika ofisini hapo baada ya kukosa ushirikiano kutoka Polisi, kwani aling’atwa sikio hilo Aprili 26, mwaka huu na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Nyakato Mwatex na kupewa RB namba Ny/RB/3059/2012.

Alisema siku hiyo ya tukio, Katibu huyo alifika kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa ameambatana na mwanamke ambapo alimkuta kijana huyo nje na kumuomba chumba na kujibiwa kuwa yeye hahusiki.

Baada ya kumjibu, alidai Abel alimwambia kuwa ana kiburi na kuwaita makamanda wenzake waje kumshughulikia ambapo walifikia na kuanza kumpiga na kisha yeye Abel alimvuta sikio na kisha kumng’ata na kuondoka na kipande cha sikio lake. Alisema baada ya tukio hilo alimkamata mtuhumiwa mmoja na kumfikisha katika Kituo cha Polisi cha Mwatex, lakini aliporudi kesho yake alikuta ametolewa kwa dhamana.

Alisema Katibu huyo pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabiti baada ya tukio hilo, alianza kupokea barua za vitisho kuwa siku zake za kufa zinakaribia iwapo ataendelea kumghasi.

Aliamua kutoa taarifa Ofisi ya Mtendaji ambapo aliandikiwa barua na kwenda kutoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi ambako alipewa RB namba MW/Rb/4579/2012 ya shambulio la kudhuru mwili.

Alisema kwa kuwa awali alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mwatex na hakupewa ushirikiano na Polisi hadi kupokea barua za vitisho hivyo, ameamua kulifikisha suala hilo kwa mkuu wa mkoa ili apate msaada zaidi kwani hata nyumba ya kulala wageni ya mama yake wametishia kuichoma moto

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni