Jumapili, 13 Mei 2012

MATEJA WAYATEKA MAKABURI YA SINZA, WAUZA MAKABURI YALIYOZIKWA ZAMANI.

KWA kipindi kirefu sasa, usimamizi wa makaburi ya Sinza, Dar es Salaam umekuwa chini ya mikono ya mateja (watumiaji wa mihadarati) wanaoendesha biashara haramu ya maeneo ya makaburi yaliyokwishatumika ili kujipatia kipato.

Picha ya Maktaba; Msiba wa Dokta Remmy.

Kwa sababu ya kukosa utu na ufukara uliopitiliza, mateja hao wasiopungua 15 wamekuwa wakiendesha biashara hiyo waziwazi kwa miaka nenda rudi na hivyo kufanya wazoeleke kwa baadhi ya wakazi wa maeneo jirani na makaburi hayo, pamoja na wateja wanaofika kutafuta huduma ya maziko.

Kutokana na kuzoeleka huko na kwa sababu ya kutokuwa na tabia ya kukwapua vya watu kama wafanyavyo mateja wengine katika vituo vya mabasi na kwingineko, wa kwenye makaburi hayo wanapewa ushirikiano na watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulipwa dau wanalolitaja na hivyo kuligeuza eneo hilo kuwa lao la kudumu kibiashara.

Uchunguzi wa gazeti hili uliothibitishwa na baadhi ya mateja hao, wakazi wa eneo hilo, viongozi wa mitaa na watu waliopotelewa na makaburi walimozikwa ndugu zao, umethibitisha kuwapo uozo mkubwa katika makaburi hayo ‘yanayomilikiwa’ na genge hilo kama sehemu ya kujiingizia kipato isivyo halali.

Aidha, imethibitika kuwa mateja hao wasio na tabia ya kuibia mtu wala kudhuru wanaoingia na kutoka kwenye makaburi hayo kusaka huduma ya maziko, hufukua makaburi ya waliozikwa kuanzia miaka miwili iliyopita kurudi nyuma na kuzika maiti wapya huku wakifahamu kuwa eneo hilo limejaa na linastahili kuachwa huru.

Kwa maelezo ya mateja waliozungumza na HABARILEO, wafu wanaowafukua zaidi ili kupata
makaburi ya wazi ni watoto wachanga bila kujali walizikwa lini pamoja na watu wazima waliozikwa kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.

Mateja walonga
Kwa masharti ya kutotajwa gazetini, baadhi ya mateja waliozungumza na HABARILEO kwa nyakati tofauti makaburini hapo, walidai kuishangaa Serikali kwa kusahau kuwapelekea vifaa vya afya kwa kuwa kazi wanayoifanya ni ya hatari kiafya.



Teja wa kwanza aliyeshambuliwa na wenzake kwa maneno kwa kuzungumza mambo mengi tofauti na walivyokubaliana kulingana na kiasi walichotaka kulipwa, alidai kuwa wamekuwa wakifukua maiti wengine na kuwakuta wakitoa maji na wadudu kutokana na kuoza na hivyo kuhitaji vifaa kama glovu kwa ajili ya kuzuia maambukizi.

“Hapa ni maradhi tupu, kwa sababu maiti wengine hatujui walikufa kwa magonjwa gani na sisi
tunawafukua bila kuvaa zana zozote. Yaani tunawashika na kuwasogeza pembeni ili tupate pa
kuwazika wenzao sasa kama Serikali itaendelea kutuacha hivi basi itakuwa haina maana. Wa pili alidai kwamba wapo wanaofuata huduma hiyo huku wakijua kabisa kuwa kumejaa.

“Hatuwaambii kachimbe pale, tunawachimbia wenyewe na wanatulipa kwa maelewano, lakini tunaanza kwa Sh 150,000 na kelele zikizidi hatushuki zaidi ya Sh 120,000. Ndio hivyo eneo la peke yako litatoka wapi Dar es Salaam hii?” Alisema na kuhoji.

Alisema wapo kwenye eneo hilo kwa miaka mingi na kwamba wanajua makaburi yote yasiyo na ndugu wafuatiliaji. “Wapo waliotupa wafu wao hapa tangu miaka ya 2000, sasa hao ndugu yangu unatarajia watahesabika kuwapo hapa?

Mifupa yao tukiiona tunaiweka ndani ya kaburi na kuifukia halafu pembeni au juu tunazika mfu mpya”.

Teja aliyekuwa na fujo kwa wenzake akitaka habari isisemwe yote kwa undani kwa maelezo kuwa wao hawako katika eneo hilo kwa sababu ya ‘kuuza sura’, alidai kuwa makaburi kamwe hayajai, kwa sababu zinazojaa ni daladala zinazohesabiwa idadi ya vichwa.

Sambamba na maelezo hayo, walizungumzia alama zinazowekwa na ndugu wa marehemu wanapomaliza kuzika maiti wao na kusema hata misalaba ya chuma haizuii wao kuzika mtu kama kaburi halijaangaliwa kwa muda mrefu.

“We unafikiri nani anafanya usafi hapa, kama ndugu hawaji kung’oa majani kwenye makaburi yao mpaka yanakuwa msitu sisi tunafanya kazi hiyo na kunadi eneo. Misalaba na matofali hayo hayo tunayauza kwa wateja wapya na hatujawahi kupata tatizo lolote.

“Serikali yetu ndiyo hatuielewi, kwa sababu haitupi zana na ndiyo maana wakati mwingine tunalazimika kuchimba kwa majembe yasiyo imara na kuumia,” alisema teja wa nne aliyekuwa ameshika msalaba wenye jina linaloanzia na herufi H unaoonesha kifo kilitokea mwaka 2003.

Wasimamizi wa makaburi wazungumza

Kwa nyakati tofauti na kwa masharti ya kutotajwa gazetini kwa maelezo kuwa sio wasemaji wa Jiji, maofisa wanaohusika na huduma ya maziko katika Jiji la Dar es Salaam walisema hakuna makaburi yanayolindwa Dar es Salaam isipokuwa yana wasimamizi wanaofunga kazi saa 12 jioni.

Baadhi ya maofisa wa Jiji wanaohusika na huduma ya kuzika watu wasio na ndugu jijini humo walikiri kuwa na taarifa za kuwapo mateja katika makaburi ya Sinza na kueleza kuwa eneo hilo hawalishughulikii wao kwa kuwa linaangaliwa na Serikali ya Mtaa wa Sinza.

Ofisa mwandamizi anayesimamia makaburi ya Kinondoni alisema yeye si msemaji wa makaburini lakini akaweka bayana kuwa maeneo yote wanayoyasimamia wao hayauzwi kwa watu kwa sababu maziko ni haki ya kila mfu.

Alisema, “Tangu mwaka 1995 kodi ndogo ndogo zilipofutwa, hatukuwahi kumtoza mtu kwa ajili ya kaburi na wala hatuhusiki kuchimba kwa ajili ya wafu wenye ndugu. Sisi tunahangaikia wasio na ndugu tu hivyo yanayoendelea Sinza ni ya kusikitisha.

Baadhi ya watu waliokuwa makaburini hapo walilalamika makaburi ya ndugu zao kutoonekana na wengine wakidai kuibiwa alama walizoziweka pamoja na matofali.

Serikali ya Mtaa yafafanua
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza, Juma Mgandwa, alisema mateja hao walikuwepo kabla ya uongozi wao kuingia madarakani. “Hao walikuwepo tangu siku nyingi na ndiyo namna wanavyojipatia kipato”.

Aliongeza kwamba makaburi hayo yanahudumiwa na mitaa mitano na kwamba yako chini ya kata ya Sinza

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni