Ijumaa, 25 Mei 2012

LLOYD NCHUNGA AJIUZULU UONGOZI WA YANGA JANA.

MWENYEKITI wa Yanga, Lloyd Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa huo kuanzia jana.

Kujiuzulu kwa Nchunga itakuwa furaha kwa Baraza la Wazee la Yanga, ambalo karibu mwezi mzima sasa limekuwa likimshikia bango Nchunga aachie madaraka kwa madai ya timu hiyo kufanya vibaya katika Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika mapema mwezi huu, ambapo Yanga ilishika nafasi ya tatu.
Image

Lloyd Nchunga.

Pia itakuwa imewarahisishia kazi baadhi ya wanachama wa Yanga, ambao walikutana makao makuu ya klabu hiyo makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani na kutangaza kumpindua Nchunga, uamuzi ambao ulipingwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba ni kinyume cha Katiba.

Uamuzi huo wa Nchunga kujiuzulu aliutangaza jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake jengo la NSSF, Dar es Salaam na kwamba amefanya hivyo kwa maslahi ya Yanga.

Alisema uamuzi wake wa kujiuzulu umekuja wakati walishakubaliana kwenye kikao cha
Kamati ya Utendaji ya Yanga kwamba wajumbe wengine waliobaki wasijiuzulu hadi mkutano mkuu wa wanachama Julai 15 mwaka huu, lakini mazingira yamemfanya afikie uamuzi huo na kwamba anajua wenzake watasononeka sana.

“Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo,” alisema.

Nchunga aliorodhesha mafanikio mbalimbali ambayo uongozi wake uliyapata tangu aingie madarakani Julai 2010, ambayo ni Ngao ya Hisani mwaka 2010, ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2010/2011 na ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka 2011.

Pia alisema chini ya uongozi wake waliua uteja kwa Simba, ukiacha matokeo mabaya ya kufungwa mabao 5-0 waliyoyapata kutoka kwa Simba Mei 6, mwaka huu.

“Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu mabao 5-0, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.

Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia.

“Siwatuhumu wachezaji moja kwa moja, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema. “Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!

“Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika hoteli mbalimbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.

“Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula
kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia,” alisema Nchunga.

Alieleza kuwa Jumapili baadhi ya wanachama wa Yanga walikutana na kutangaza mapinduzi, ambayo hata hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliyakataa.

Hata hivyo alisema baadhi ya wazee walikaririwa na kituo kimoja cha redio wakisema Yanga bora ishushwe daraja au kufungiwa kuliko Nchunga kuendelea kuongoza.

“Hii imenikumbusha hekima za Mfalme Suleiman akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wagawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.

“Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika uenyekiti wa Yanga kwani ni klabu
ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya Katiba yetu.

“Vile vile siko tayari kuona klabu yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi. Natumaini Kamati ya Utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya Katiba ya Yanga pamoja na Bodi ya Wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka
kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi.

“Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapohitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Nchunga.

Nakala ya taarifa ya kujiuzulu ameituma kwa wadhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume,
Francis Kifukwe na Yusuf Manji kwa taarifa.

Nchunga ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alishinda uenyekiti wa Yanga Julai mwaka 2010.

Katika uchaguzi huo nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilienda kwa Davis Mosha. Walioshinda katika ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Ally Mayai, Mzee Yusufu, Sara Ramadhani, Tito
Osoro, Mohamed Bhinda, Charles Mgondo, Salum Rupia na Theonest Rutashoborwa.

Hata hivyo Mosha alijiuzulu mwaka jana, wakati Mayai, Mzee Yusuph, Bhinda walijiuzulu hivi
karibuni kulipoanza shinikizo la kuung’oa madarakani uongozi wa Nchunga.

Rutashoborwa alifariki dunia

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni