Jumatano, 21 Desemba 2011

WANASIASA WAILAUMU TAKUKURU

WANASIASA wameinyooshea vidole Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania
(TAKUKURU), wakitaka wajisafishe ili iaminike na kurudisha heshima yake katika jamii.

Wakichangia mada iliyotolewa na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma kutoka Takukuru, Mary Mosha katika mafunzo ya viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa kuhusu Uongozi, Uwajibikaji na Utawala Bora, wanasiasa hao walisema kuwa Takukuru ni chanzo cha rushwa nchini.

Ms Mary Mosha, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Umma Takukuru.


Akichangia mada hiyo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Nape Nnauye alisema kwa sasa Takukuru harufu yao mtaani siyo nzuri.


Nape alisema katika hata mambo ya kawaida yanayoonekana yana mazingira ya rushwa ikiwemo miradi ya maendeleo, maofisa wa Takukuru wamekuwa wakidai wanaendelea na uchunguzi huku wananchi wakizidi kuwalalamikia.


“Takukuru harufu yenu mtaani kwa sasa siyo nzuri, wakati mwingine inaonekana wazi mnatumika kusafisha watu, sasa itafika mahali watu wataona Takukuru ni mzigo maana wanalipwa fedha za walipa kodi, lakini kazi yao haionekani,” alisema Nape.


Alisema watu wamekuwa wakiona rushwa ni ya uchaguzi wakati kuna rushwa mbaya zaidi kwa
baadhi ya watumishi kutumia rasilimali pasipo mpangilio au kwa malengo ambayo hayakukusudiwa bila kuchukuliwa hatua zozote.


“Kwa sasa tunaona rasilimali hazitusaidii kwa sababu wanaowajibika kuzisimamia hawatimizi wajibu wao, inatupasa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake kwa sababu Takukuru mkiendelea hivi wananchi watawachukia sana,” aliongeza Nape.


Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema adui mkubwa wa rushwa nchini ni Takukuru yenyewe kwa kuwa uwajibikaji wao ni mbovu na viongozi wake hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.


Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe nchini, Lifa Chipaka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa TADEA, alisema rushwa haipo tu ndani ya vyama, bali hata ukwepaji wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara ni rushwa.


Chipaka alisema watumishi wa Takukuru wamekuwa wakilipwa fedha nzuri, wakipewa magari ya kifahari ya kutembelea na nyumba nzuri, lakini hakuna wanachokifanya katika jamii.


Mapema, akitoa mada yake, Mosha alisema kama vyama vya siasa visipodhibiti rushwa ndani ya vyama vyao, vitashindwa kudhibiti hata nje ya vyama na hivyo kusababisha kupatikana viongozi wasiofaa.



Alisema rushwa inaua misingi ya utawala bora, inasababisha kupoteza stahiki za watu, inasababisha kuwepo kwa matabaka na kuchangia kukosekana kwa amani.


Akitoa mada kuhusu wajibu wa vyama vya siasa katika kuimarisha demokrasia, Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Kamishna wa Polisi, Robert Manumba alisema kukithiri kwa migogoro ndani ya vyama vya upinzani yanaathiri utangamano wa Taifa na kuwataka
viongozi wa vyama kuhubiri na kuimarisha amani na usalama wa nchi.


Akichangia mada hiyo, Mwenyekiti wa Taifa wa UDP, John Cheyo alionya wanasiasa ambao
wamekuwa wakiwatumia vijana kufanya maandamano na vurugu na kuwataka wawatumie kwa maslahi ya nchi na si kwa kuvuruga amani.


“Vijana wa siku hizi wamekuwa wakitumika vibaya na ukiwaambia habari ya amani hawakuelewi ila ukiwaambia habari ya maandamano wanakwambia ni sa ngapi wala
hawaulizi ni kwa ujira gani, yana madhara gani au yana sababu gani,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki.


Pia aliitaka Serikali kuandaa bajeti kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato badala ya kuandaa bajeti ya kutegemea wahisani kwa kuwa nchi ina utajiri wa madini na hivyo haifai kuwa ombaomba

Maoni 1 :

  1. Nini tofauti katika polisi na jambazi? Ni msemo tu, itikadi na imani. Vinginevyo wanafanana tu barabara!

    JibuFuta