Sweetbert Lukonge
KOCHA wa timu ya Tanzania, Jan Poulsen amelishutumu waziwazi Shirikishi la Soka nchini (TFF) kwa kuharibu mipango yake ya maandalizi ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2014.Poulsen aliondolewa kuifundisha timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' kwenye mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyomalizika hivi karibuni na Uganda kuibuka mabingwa.
Nafasi hiyo ya Poulsen walipewa makocha Charles Mkwasa na Jamhuri Kiwehlu ikiwa na wachezaji wa Tanzania Bara pekee kwa sababu Zanzibar nayo inashiriki michuano hiyo.
"Kazi yangu inakuwa ngumu sana kwa sababu tunatakiwa kujipanga kwa ajili ya mechi zetu za kufuzu 2012," Poulsen aliimbia BBC."Napopata fursa ya kuwa na wachezaji kwa muda mrefu ndivyo ninavyowafahamu zaidi. Muda uliobaki ni mfupi kabla ya kuanza kwa mechi za mchujo hapo Juni.
"Unaweza ukajiuliza kuna umuhimu gani wa kubadilisha timu kwa kiasi kubwa kwa ajili ya michuano ya Chalenji badala ya kuendelea kuwa na kikosi kile kile kilichocheza mechi mbili za mwisho dhidi ya Chad," alisema Poulsen.
Mdenmark huyo alikuwa kwenye jukwaa wakati Kilimanjaro Stars ikitupwa nje kwenye nusu fainali na Uganda na kuzomewa na mashabiki wake.Alipoulizwa kama ilikuwa na umuhimu wote kwa makocha hao ndani kuifundisha timu hiyo, Poulsen alisema.
"Sina uhakika kama ningeweza kufanya hivyo mimi. Lakini TFF wana sababu zao na jinsi wanavyotaka kuendeleza soka la Tanzania," alisema."Nafikiri tunatakiwa kujipanga kwa umakini na kuwa na mawasiliano mazuri kati yetu. Ni matumaini yangu mambo yatakuwa mazuri siku zijazo."
Akijibu madai hayo ya Poulsen, katibu mkuu wa TFF, Angatile Osiah alisema uamuzi huo ulitokana na kilio cha Watanzania wengi kutaka kocha asiifundishe Kilimanjaro Stars.
"Yeye ni kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania na sio Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars)," alisema Osiah.
Osiah alisema kuwa kufuatia hali hiyo Kamati ya Ufundi ya TFF ilikaa chini na kufikia uamuzi wa kutompa Poulsen nafasi hiyo na badala yake walipewa makocha wazawa.
"Ana uhuru wa kutoa mawazo na sisi hatuwezi kuyangilia, lakini uamuzi ulifanywa na Kamati ya Ufundi baada kuona ni jambo la msingi Kili Stars ikafundishwa na makocha wengine," alisema.Tanzania imefuzu kucheza hatua ya makundi katika harakati za kusaka tiketi ya kwenda Brazil 2014 baada ya kuitoa Chad.
Katika kundi lake ipo pamoja na Ivory Coast, Morocco na Gambia.Pia itakuwa na kibarua kizito dhidi ya Msumbiji Februari mwakani katika kampeni ya kutafuta kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2013 nchini Afrika Kusini |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni