Jumanne, 29 Novemba 2011

CHADEMA WAFIKIA MUAFAKA NA KIKWETE JUU YA MUSWADA WA KATIBA MPYA.

Image
Rais Kikwete akiagana na ujumbe wa CHADEMA ukiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe baada ya kumaliza mzungumzo ya siku mbili juzi na jana Ikulu na kufikia makubaliano kadhaa juu ya uundwaji wa Katiba mpya.
MUSWADA wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge hivi

karibuni utasainiwa na Rais Jakaya Kikwete kama ilivyopangwa.
Hali hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa jana kati ya Rais na Kamati ndogo ya Chadema iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe.
Kususia mjadala wa Muswada huo kwa wabunge hao wa vyama hivyo, ulitokana na madai yao ya kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni wakidai haukuwa umesomwa na wananchi na kuuelewa, hivyo kukosa kuuchangia, lakini walikataliwa na Spika Anne Makinda.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa jana Ikulu Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutakuwa na haja ya sheria hiyo baada ya kusainiwa kuendelea kuboreshwa, ili ikidhi mahitaji ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.
Pia kutakuwa na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba mpya.
Awali ilielezwa kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya uelewano ambapo Rais Kikwete aliwahakikishia Chadema kuwa yeye na Serikali yake wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.
Kulingana na hatua iliyofikiwa jana, Rais atasaini Muswada huo kuwa sheria ambayo inatarajia kuanza kutumika Desemba mosi, lakini wakati ikiendelea kutumika, kutakuwa na fursa ya kuifanyia marekebisho endapo haja itajitokeza.
Hili si jambo jipya kwa masuala ya uandishi wa Katiba mpya, kwani hata ya Kenya ilipitishwa na mpaka sasa zipo taarifa kuwa imeshafanyiwa marekebisho mara 11 kutokana na mahitaji yanayoibuka kwa kuzingatia mazingira na muktadha.
Makubaliano ya jana, yanamaliza sintofahamu iliyokuwa imeanza kuibuka kwa Chadema na makundi mengine kutaka kufanya maandamano nchi nzima, kupinga Muswada huo kusainiwa na kushinikiza urejeshwe bungeni kusomwa kwa mara ya kwanza.

Lakini pia kunatoa fursa pana kwa wawakilishi na wabunge kurudi kwa wananchi kuwahimiza kujitokeza kutoa maoni na mawazo yao kuhusu aina ya Katiba inayotakiwa na Watanzania wote.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilikubaliana kuwa ni jambo muhimu kwa mchakato huo kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani,
utulivu na umoja wa kitaifa.
Mkutano huo uliombwa na viongozi wa Chadema na Jumatatu iliyopita, ikaunda Kamati ndogo ya kumwona Rais, ikiongozwa na Mbowe huku wajumbe wengine wakiwa ni Mnyika, Makamu Mwenyekiti Bara, Said Arfi na Makamu Mwenyekiti Visiwani, Said Issa Mohamed.
Wengine ni Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mwanasheria wa Chama hicho, Tundu Lissu, wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri ya Chama hicho, John Mrema.
Upande wa Serikali katika mazungumzo hayo, uliwakilishwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
–Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani

Maoni 1 :

  1. I do not know the real story behind this but, As an outsider looking at the pic, UNAPATA HISIA "WAMEWEKA TAIFA LAO JUU KULIKO UWANACHAMA WAO KWA VYAMA MBALIMBALI"

    ... And that is just GOOD! Very very good indeed!

    JibuFuta