Ijumaa, 7 Oktoba 2011

WAZO LANGU-WAFUJAJI MALI ZA UMMA WAPATIWE DAWA YA KUDUMU.

UKWELI ulio wazi kuwa kuna wakati lazima nguvu za ziada zitumike kuhakikisha kuwa mambo mbalimbali yanaenda sawa hususani katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa katika matumizi ya rasilimali za umma.
Na Theopista Nsanzugwako.

Aidha, ni jambo la kawaida kusikia baadhi ya watumishi wa umma kumlalamikia mtumishi
mwenzao kwa vitendo vya kujilimbikizia mali kwa kutumia vibaya vyeo vyao na ofisi zao.

Kwa kuliona hilo, Rais Jakaya Kikwete aliamua kuipa jukumu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza watumishi wa umma ambao sio viongozi wanaotajwa kwa kujilimbikizia mali wakitumia vyeo vyao na ofisi walizokabidhiwa kuwahudumia wananchi.

Pia ameipa jukumu Sekretarieti hiyo kukamilisha mchakato utakaowezesha kutungwa kwa
sheria itakayotenganisha biashara na uongozi ili itumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema haitoshi kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwachunguza viongozi
namna walivyopata mali zao wakati kuna watumishi wengi wametajwa kumiliki mali nyingi
ambazo hazijapatikana kihalali.

Alisisitiza kuwa ili kupata ukweli usio na shaka kuhusu umiliki wa mali za watumishi na viongozi, kuna haja hivi sasa kwa Sekretarieti hiyo kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama
pamoja wananchi ili wathibitishe mali walizozitaja katika fomu za tamko la rasilimali, maslahi na madeni.

Alisema lengo la kuchukua hatua hiyo ni kufanya kuwepo kwa watumishi wenye maadili na uadilifu na sio wanaotumia ubabe, vitisho na wale wanaopenda rushwa na hivyo kupelekea nchi kukosa maendeleo.

Napenda kuunga mkono kauli ya Rais kushirikisha vyombo vya ulinzi kwani itakuwa rahisi katika kuwashirikisha katika vyombo vya sheria watakaobainika kutokana na ushahidi
utakaokuwepo.

Wakati Rais akisema hayo, Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema
Sekretarieti hiyo imeanza kupata mafanikio baada ya idadi ya viongozi wa umma wanaorejesha fomu kuongezeka kutoka viongozi 6,007 sawa na asilimia 76.8 katika mwaka jana hadi viongozi 8,465 ambayo sawa na asilimia 94 mwaka huu.

Alisema uundwaji wa Baraza la Maadili umesaidia kupokea malalamiko 41 dhidi ya ukiukwaji
wa maadili kwa viongozi ambapo tayari 24 walipatikana na hatia na kupewa onyo na wengine onyo kali.

Mimi binafsi naona bado Sekretarieti hiyo haijafanya kazi ambayo ni mategemeo ya
wananchi kutoka kwa Sekretarieti hiyo kwa kutoa hukumu itakayofanya watumishi na viongozi
wengine kuwa woga lakini siyo kwa kuwaonya tu.

Ni kweli wapo watumishi wa umma waliojilimbikizia mali kiasi ambacho hakuna wa kumfuatilia
na kujua uhalali wake, kama ilivyokuwa kwa maofisa Ardhi na wengineo.

Kama kuna sheria inawabana katika kutoa adhabu hizo ni vema mikakati ikafanya ili ziweze
kubadilishwa na kuwezesha wafujaji hao kufikishwa mahakamani na ikidhibitika mali hizo zitaifishwe.

Hakuna haja kuwa ikifika hatua hiyo hata kama tatizo hili halitaisha basi litapungua na viongozi
na watumishi wa umma kuogopa mali za umma kama ukoma na kutumika vyeo vyao vizuri.

Imefika wakati kwa Sekretarieti hiyo kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha viongozi na watumishi wa umma wanaotumia majukumu yao vibaya kwa kujilimbikizia mali
au kupata mali isivyo halali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni