Wazungu na Waasia hawakutaka kutambua kuwa Tanganyika ni nchi ya Waafrika Katika makala iliyopita, Mwandishi MOHAMED SAID alielezea jinsi harakati za Uhuru zilivyowashikisha akina Hamza Mwapachu, Kasella Bantu na wengineo na baadaye akaongezeka Mwalimu Julius Nyerere aliyezitia nguvu zaidi harakati hizo…. KUONGEZEKA kwa Mwalimu Julius Nyerere kulitia nguvu sana baraza hii. Mijadala ya siasa miongoni mwa vijana hawa sasa ilivuka kutoka manung’uniko ya ndani ya nchi kama migomo ya wafanyakazi na matatizo ya ardhi ya Wameru na kuingia kujadili masuala ya kimataifa ya mrengo wa kushoto na hasa kuhusu kuwa na utawala wa Waafrika Tanganyika. Kwa ufupi mijadala sasa ililenga katika kuutokomeza utawala wa Waingereza katika Tanganyika. Nyerere alimwona Abdulwahid kama mtu mwenye akili sana, kijana aliyejiweza kihali na mtu mwenye moyo mkubwa usiokuwa na hasad wala choyo. Watu walioishi na marehemu Abdulwahid wanasema alikuwa mtu karimu sana hujapatapo kuona na mwenye haiba ya kupendeka. Abdulwahid alimuona Nyerere, kama mtu aliyeelimika vizuri kati yao na mwenye ustadi katika mijadala. Nyerere alipata nafasi ya kuifahamu dunia vizuri lau kama alikulia kijijini. Zaidi Nyerere alikuwa amepata uerevu wa siasa kutokana na uhusiano wake na Fabian Society, wakati alipokuwa mwanafunzi Uingereza. Mijadala mizito sana ilijitokeza katika vile vikao vya kila Jumapili wakati akili na ujuzi wa siasa wa Abdulwahid vilipopambana na uhodari wa majadiliano wa Nyerere. Abdulwahid alipata uzoefu mkubwa wa uongozi katika siasa nyumbani kwao kwa baba yake aliyeasisi African Association kisha wakati wa vita Burma na baada ya vita serikali ya kikoloni ilipomteua kuwa katibu wa kwanza wa chama cha wafanyakazi Dockworkers Union akiwa kijana mdogo wa miaka 24. Nyerere hakuwa na ujuzi wowote katika siasa ukimlinganisha na Abdulwahid. Wakati African Association Tabora kiliposhiriki katika mgomo wa mwaka 1947, ambao chanzo chake kilikuwa mgomo wa makuli Dar es Salaam, Nyerere hakujihusisha na harakati zile za wafanyakazi ingawa yeye ndiye alikuwa katibu wa African Association pale Tabora. Jukumu kubwa la mgomo ule lilibebwa na Salum Abdallah na wanachama wa kawaida katika African Association. Salum Abdallah baada ya kuundwa kwa TANU, mwaka 1955 alikuwa rais muasisi wa Tanganyika Railway African Union (TRAU), katibu akiwa Christopher Kassanga Tumbo. TRAU na TANU vilishirikiana vizuri sana katika kupambana na serikali ya kikoloni. Kutokana na Nyerere kuingia katika harakati zile pale New Street pakawa na kuheshimiana na mapenzi makubwa baina yake, Abdulwahid, Ally Sykes, Dossa Aziz na John Rupia. Kila Jumapili Nyerere alikuwa akisafiri kutoka Pugu hadi Dar es Salaam kuhudhuria baraza lile lililokuwa likijadili siasa za Tanganyika. Baada ya kikao, Dossa Aziz au Dunstan Omar alimrudisha Nyerere kwa gari hadi Pugu. Hivi ndivyo Nyerere alivyokuja kuingia ndani ya TAA Makao Makuu na hatimaye akaja kupendekezwa kugombea cheo cha juu kabisa cha uongozi wa chama mnamo Aprili, 1953. Uongozi wa TAA ulimpendekeza Julius Nyerere ili kukiimarisha chama kwa kuwa na Waafrika wenye elimu ya juu ndani yake. Ilibakia kwa Nyerere kukubali au kukataa. Kujadili siasa haikuwa sawa na kuongoza chama kilichokusudia kunyakua madaraka kutoka kwa serikali ya kikoloni. Hivi vilikuwa ni vita dhidi ya ukoloni na ilibidi mtu ajitayarishe kwa lolote ambalo lingetokea. Nyerere alikuwa ndiyo kwanza amerudi kutoka masomoni Uingereza mwaka uliopita na alikuwa anataka kutulia aanze maisha. Vijana wenzake wa mjini aliowakuta katika siasa pale Dar es Salaam kama Abdulwahid na mdogo wake Ally, na Dossa Aziz walikuwa watu wenye uwezo wao na wakiishi ndani ya mji wao ukilinganisha na yeye mgeni, tena amekulia kijijini Katika mazingira kama yale ya Dar es Salaam ya miaka ya mwanzoni 1950 Nyerere kamwe hangeweza kujijengea nguvu ya siasa bila ya kushikwa mkono na wenyeji. Uongozi wa TAA ulitambua thamani ya elimu ya Nyerere na uwezo wake wa uongozi kwa chama na nchi yenyewe hapo baadaye. Abdulwahid pamoja na viongozi wenzake wa TAA waliamini kwamba kuwa na Mwafrika aliye na elimu ya juu kama rais wa chama kungeimarisha uongozi wa TAA na kutoa sura nzuri machoni mwa serikali ya kikoloni na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa uliokuwa ukitembela Tanganyika. Nyerere amenukuliwa kusema kuwa ilikuwa dhamira yake kufundisha kwa muda kisha aingie kwenye siasa. Hatimaye Nyerere alishawishiwa kukubali kuchukua jukumu la kuongoza TAA. Uchaguzi baina ya aliyekuwa rais wa TAA, Abdulwahid na mwalimu wa shule asiyefahamika vyema pale mjini, Julius Nyerere, ulifanyika kwenye Ukumbi wa Arnatouglo tarehe 17 Aprili, 1953. Nje ya uongozi wa TAA ambao ulimpendekeza kugombea nafasi hiyo, Nyerere alikuwa mgeni kabisa kwa wote aliokuwa akiwaomba kura zao. Maisha ya Nyerere katika siasa yalianza hapo. Nyerere alikuwa mgeni na alikuwa hana historia ya kuongoza mapambano ya umma dhidi ya serikali ya kikoloni. Ukoo wa Sykes ulikuwa unatambulikana katika siasa za Dar es Salaam kwa takriban robo karne. Ukoo huu ndiyo ulioanzisha na kuongoza vyama vyote viwili, African Association na Al Jamiatul Islamiyya. Ukoo wa Sykes ulikuwa unafahamika kwa kuongoza mapambano dhidi ya serikali. Ushahidi wa haya unapatikana katika nyaraka kati ya ukoo huu na serikali ya kikoloni. Katika kipindi cha miaka zaidi ya ishirini, serikali kwa nyakati tofauti, kati ya mwaka 1929 hadi 1953 ilikuwa na barua za Kleist Sykes na za mwanaye Abdulwahid wakiwa viongozi wa African Association kuhusu madhila tofauti yaliyokuwa yakiwakabili wananchi. Uchaguzi ulikuwa kwa kunyoosha mikono. Denis Phombeah aliyekuwa akifanya kazi pale Arnatouglo ndiye alikuwa msimamizi wa uchaguzi. Phombeah aliwaomba Abdulwahid na Nyerere kutoka nje ya ukumbi ili uchaguzi uanze. Wiki nzima kabla ya uchaguzi Phombeah alikuwa akizunguuka mji mzima na pikipiki yake akimfanyia kampeni Nyerere. Lakini kwa hakika hakukuwa na haja ya kufanya hivyo. Uongozi wa ndani wa TAA wa Abdulwahid, Ally, Dossa Aziz na Rupia ulikuwa tayari umekwishaamua kumpa Nyerere urais wa chama. Inawezekana labda kwa kuwa Phombeah hakuwa katika wandani wa TAA yeye hakujua uamuzi uliokuwa umepitika. Kwa hakika uchaguzi huu ulikuwa kutimiza utaratibu tu, mambo yote yalikuwa yamepangwa na yakapangika |
KARIBU KATIKA BLOGU HII YA KUELIMISHA, KUBURUDISHA NA KUONYA KUPITIA MADA MBALIMBALI NA HATA PICHA. ONGEZA MAHUSIANO KWA KUJUMUIKA NA WENZIO HAPA.UNAWEZA TUMA PICHA NA MAELEZO KWA ANUANI HII;mkuu74@gmail.com
Alhamisi, 6 Oktoba 2011
KISA CHA KAMBARAGE NYERERE 1952
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni