Mabao mawili mazuri aliyofunga Robin van Persie yameiwezesha Arsenal kupata ushindi dhidi ya Sunderland katika uwanja wa Emirates.
Nahodha huyo wa Arsenal alifunga bao la kwanza katika sekunde ya 29 tangu mchezo ulipoanza, bao linaloonekana ni la mapema sana kufungwa katika Ligi Kuu ya England msimu huu.
Lakini ilionekana kama Sunderland ingepata pointi katika mchezo huo baada ya mchezaji wa zamani wa Arsenal Sebastian Larsson kusawazisha kwa mkwaju wa adhabu ya moja kwa moja katika dakika ya 30.
Lakini Van Persie ndiye aliyekuwa na kauli ya mwisho ya matokeo ya mchezo huo baada ya kufumua shuti la adhabu ya moja kwa moja katika dakika ya 82 na kuipatia Arsenal ushindi na pointi tatu muhimu ilizokuwa ikihitaji.
Arsenal imefikisha pointi 10 na kujisogeza nafasi ya 10.
Nayo West Bromwich Albion katika mchezo ulioanza mapema imefanikiwa kuzoa pointi tatu baada ya kuilaza Wolves mabao 2-0 na kufanikiwa kupata ushindi wa kwanza wa nyumbani na kujikwamu eneo la kushuka daraja.
Chris Brunt alikuwa wa kwanza kuipatia West Brom bao la kuongoza baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Billy Jones.
Kevin Doyle naye alikaribia kuipatia bao Wolves na Roger Johnson akapoteza nafasi nzuri ya kufunga baada ya kupiga mpira kichwa uliotoka nje.
Lakini mchezaji wa akiba Peter Odemwingie aliipatia West Brom ushindi dakika za mwisho na kuifanya Wolves ipoteze mchezo wa tano mfululizo wa ligi.
Kwa matokeo West Brom imefikisha pointi nane na wapo nafasi ya 12
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni