Alhamisi, 6 Oktoba 2011

JWTZ YAHOFIA UWEPO WA MAHARAMIA ZAIDI BAHARINI ENEO LA TANZANIA.

JESHI la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), limesema lina wasiwasi wa kuwepo kwa maharamia wa Kisomali ndani ya ardhi ya Tanzania.

Kutokana na hofu hiyo, limetangaza kuwa litawashikilia kwa muda na kufanya uchunguzi wa kina kubaini kama maharamia waliojaribu kuteka meli inayofanya utafiti wa mafuta katika bahari ya Tanzania walikotokea.
Msemaji wa JWTZ Lt. Col. Masoud K. Mgawe.(picha maktaba)


Wasiwasi huo umetolewa na maofisa wa ngazi ya juu wa JWTZ katika mkutano wao na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Jeshi, Upanga, Dar es Salaam.

Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Operesheni Brigedia Jenerali Mwanamakala Killo, Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi cha Wanamaji Kanali Maregesi Masanga na Msemaji wa Jeshi hilo, Kanali Kapambala Mgawe.

Maofisa hao hawakuficha wasiwasi wao wa uwezekano wa maharamia hao kutokea ndani ya ardhi ya Tanzania na kwamba kuna uwezekano pia mipango yote ya kutaka kuteka meli hiyo ikawa wameifanyia nchi kavu ndani ya Tanzania kabla ya kwenda baharini.

Wasiwasi wao unatokana na kuwepo wimbi kubwa la wahamiaji haramu kutoka Somalia ambao wakati mwingine wamekuwa wanakarimiwa na Watanzania kwa kuwaficha tayari kuwasafirisha nje ya nchi.

“Waswahili husema mipango nchi kavu, baharini tupa nyavu…hawa wanaweza kufanyia mipango katika ardhi yetu,” alisema Kanali Masanga.

Alisema wanahisi kuwepo kwa maharamia ndani ya nchi kwa vile ndani ya siku kadhaa kabla ya tukio la kutekwa kwa meli, vikosi vya JWTZ pamoja na vikosi vya nchi zingine zilizoko kwenye Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), meli za kijeshi zikiwemo za Afrika Kusini zilifanya doria eneo hilo ndani ya kilometa 300 na hawakuona kuwepo kwa chombo chochote hapo.

“Licha ya kuwa kwenye mazoezi ya SADC, lakini bado pia tulikuwa tunafanya doria na meli ya Afrika Kusini ilienda umbali wa kilometa 300 haikuona dalili za kuwepo chombo hicho, tunajiuliza hao watu walitokea wapi hiyo juzi? Walitokea nchi kavu au majini?

“Ndio maana tumeona tuwahoji kwanza tujiridhishe kama kweli ni maharamia au walikuwa na lengo lingine. Pia tujiridhishe kwa kutambua uraia wao na tukiona ni masuala kiraia, tutawakabidhi kwa Polisi,” alifafanua zaidi Kanali Masanga.

Alisisitiza kuwa maharamia hao wanaweza wakawa wamefanyia mipango ya kuvamia meli hiyo katika ardhi ya Tanzania, hivyo kuwaomba wananchi wawe makini na waache kuwakaribisha raia wa kigeni na kuwaficha katika majumba yao.


Akielezea hali ilivyo katika eneo ambalo meli hiyo ilitekwa, Kanali Masanga alisema meli hiyo ya Sams AllGood ni mali ya Kampuni ya Petro Gas ya Brazil na iko eneo hilo ikiwa inachimba kisima cha mafuta.

Alisema eneo la kufanya utafiti wa mafuta ndani ya eneo la Tanzania limegawanywa katika vitalu 12 na kwa sasa utafiti umefikia kwenye kitalu namba tano kilichoko Mashariki mwa Mafia.

Ni kutokana na hali hiyo, Kanali Masanga alisema Serikali ya Tanzania imeweka ulinzi imara katika maeneo ambako kunafanyika utafiti.

Alifafanua kuwa kwenye eneo hilo kuna meli za aina tatu ambazo baadhi zina walinzi, lakini hawaruhusiwi kuwa na silaha za kijeshi, zingine za utawala na moja ndiyo inayohusika na kuchimba kisima cha mafuta.

Naye Kanali Mgawe alisema maharamia hao walienda eneo hilo kwa kutumia boti ndogo ambayo baada ya wanajeshi wa Tanzania kuzima tukio hilo, hawakuiona tena boti hiyo.

“Hatujui ilikopotelea, pia hatujui kama ilikuwa peke yake au ilibaki na maharamia wengine.

Kuna baadhi ya watu walituambia waliona watu wawili ndani ya hiyo boti na taarifa zingine zinasema hakukuwa na mtu kwenye boti hiyo,” alisema Kanali Mgawe.

Alisema pia kuwa maharamia wanafika nchini baada ya pepo za baharini kuvuma kuelekea huku nchini hali inayovisaidia vyombo vyao kuletwa na pepo hizo.

Alisema kuanzia Oktoba hali ni ya wasiwasi kwani pepo zinazovuma baharini zinavisaidia vyombo vya maharamia kufika nchini kirahisi.

Hata hivyo, alisema JWTZ imejiimarisha kimafunzo na kimazoezi kudhibiti vitendo vyovyote vya kiharamia vitakavyofanywa ndani ya bahari ya Tanzania.

Eneo la bahari ya Tanzania lina maili za mraba 223,000 ambalo Kanali Masanga alisema ni vigumu kulifanyia doria na kuweka ulinzi wa saa 24.

Hivyo aliwataka wananchi kuwa makini na raia wa kigeni na kamwe wasiruhusu kuwahifadhi raia wa Kisomalia wanaofika kwa kisingizio cha kwenda nje ya nchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni