Jumatatu, 17 Oktoba 2011

SIMBA YAONGOZA LIGI.

SIMBA imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania bara baada ya kuichapa African Lyon mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo umeifanya Simba sasa kukalia kilele ikiwa na pointi 21 ikifuatiwa na JKT Oljoro yenye pointi 19 na Azam ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 18.

Yanga iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 15.
Wachezaji wa Simba wakishambulia bao la tatu jana.


Wakati Simba ikiibuka na ushindi huo, habari za ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa imemtupia virago beki wake Kelvin Yondani.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa uamuzi wa kumtupia virago Yondani uliamuliwa na Kamati ya Utendaji iliyokutana karibu siku tano mfululizo wiki iliyopita.

“Taarifa rasmi zitatolewa na Mwenyekiti (Aden Rage) kesho (leo) lakini ameondolewa kwenye timu kwa utovu wa nidhamu, hakuonekana kambini tangu tulipocheza na Kagera mwezi uliopita,” alisema mtoa habari wetu.

Katika mechi ya jana, Simba ilipata bao la kwanza katika dakika ya 14 likifungwa na Felix Sunzu kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Oden Mbaga wa Dar es Salaam baada ya mchezaji wa Lyon Aziz Sibo kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Bao hilo la Simba lilidumu hadi mapumziko. Muda wote wa kipindi cha kwanza Simba ililiandama lango la Lyon kwa kasi huku mashuti ya Ulimboka Mwakingwe yakigonga mwamba mara mbili dakika ya 35 na 39 huku Lyon ikijibu mapigo mara nne lakini ilishindwa kufanya
madhara kutokana na safu yake ya ushambuliaji kutokuwa makini.

Emmanuel Okwi iliipatia Simba bao la pili dakika ya pili baada ya kuanza kipindi cha pili, alifunga kwa shuti kali kabla hajafunga bao la tatu katika dakika ya 51.

Dakika ya 57 Shomari Kapombe aliifungia Simba bao la nne akiunganisha mpira wa krosi wa Sunzu.

Katika mechi hiyo, Lyon ililazimika kumaliza mchezo pungufu baada ya mchezaji wake Bakari
Nzige kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuushika mpira kwa makusudi katika dakika ya 64, awali alikuwa na kadi ya njano.

Kipindi cha pili mechi hiyo ilisimama kwa dakika 15 baada ya kipa wa Lyon Noel Munishi kuzimia baada ya kugombana na Amri Kiemba, hakuweza kuendelea na mchezo na kupelekwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu zaidi.

Simba: Juma Kaseja, Nasoro Masoud, Juma Jabu, Juma Nyoso, Obadia Mungusa, Shomari
Kapombe/Gervas Kago, Ulimboka Mwakingwe/Amri Kiemba, Jerry Santo, Felix Sunzu/Mutesa Mafisango, Emmanuel Okwi na Uhuru Selemani.

African Lyon: Noel Munishi, Azizi Sibo, Sunay Juma, Shaaban Aboma, Bakar Nzige, Hassan Mwamba, Agustino Sino, Suleiman Kassim, Iddi Mbaga, Hood Mayanja na Semmy Kessy

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni