Kwirinus Mapunda, Songea
MADIWANI wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini wamesusia kikao kilichoitishwa na viongozi wa Chama hicho wilaya kwa kile kilichodaiwa ni mgomo wa kudumu kushinikiza kujiuzulu kwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Charles Mhagama.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana kwa nyakati tofauti nje ya Ofisi ya CCM ambapo kikao hicho kilipangwa kufanyika walisema kuwa wameshtushwa na taarifa ya kuitwa kwenye kikao hicho bila kuelezwa ajenda zake wala muda wa kukaa kikao hicho
Walisema kuwa walifika kwenye kikao hicho na walishindwa kuwaona baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao ndio waliowaita kitendo ambacho kinaonyesha ni dharau dhidi ya madiwani.
Baadhi ya Madiwani hao Christian Matembo wa Kata ya SeedFarm, Kurabest Mgwasa wa Kata ya Msamala na Faustine Mhagama wa Kata ya Mshangano walisema kuwa kiu kubwa ya madiwani ni kutaka kuona Charles Mhagama ambaye anadaiwa kuwa ni Mstahiki Meya anajiuzulu ili uchaguzi mpya uitishwe kwani kura alizopata wakati wa uchaguzi hazikuwa halali
“Tumechoka kuogopana ndani ya chama kwa kuwaacha wachache wawaburuze wengi kwa maslahi yaliyojificha kwani hatuwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa demokrasia vya kuwatisha madiwani waliotimiza haki yao ya kupiga kura za hapana kwenye uchaguzi wa umeya uliopita hivi karibuni kwa kuwaita ni wasaliti wa chama,” alisema Matembo.
Alisema kuwa madiwani wengi wamempigia kura za hapana Charles Mhagama, lakini tunashangaa kuona mtu huyo anatembelea gari ya Mstahiki Meya na kufanya kazi kama Meya wakati siku ya kupiga kura uchaguzi ulivurugika na kusababisha madiwani kushikana kutokana na kumkataa Mhagama.
Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama ambaye pia ni Katibu wa Madiwani wote wa CCM alisema kuwa kitendo cha viongozi wa CCM wilaya cha kupendekeza madiwani watano wa chama hicho wavuliwe uanachama ni kuongeza mpasuko ndani ya chama kwani kura walizopiga zilikuwa za siri hivyo kuwahukumu hao ni kuwanyanyasa na kuwanyima haki zao za msingi.
Mhagama alisema kuwa kanuni za kudumu za halmashauri zina eleza kuwa jambo lolote litakalofanyika kwenye kikao cha Baraza la Madiwani halipaswi kuhojiwa wala kujadiliwa na mamlaka nyingine hivyo CCM Wilaya ya Songea Mjini kupitia Kamati ya Maadili na Siasa kuwahoji Madiwani kwa kile kilichotokea kwenye Baraza ni kukiuka kanuni na kusababisha utendaji wa kosa kwa makusudi na kuendekeza makundi bila sababu ya msingi
.
Chanzo; Gazeti Mwananchi.
“Ili kulinda heshima ya Chama ni vema Charles Mhagama aridhie kujiuzuru nafasi hiyo ili uchaguzi urudiwe upya badala ya kuwanyanyasa baadhi ya madiwani wanaodaiwa kupiga kura za hapana na kusababisha diwani huyo kupitishwa kwa kura za hapana 14 na za ndiyo 12,” alisema Mhagama.
Alisema kuwa madiwani wataendelea kususia vikao vitakavyoitishwa na Chama na Halmashauri ya Manispaa ya Songea mpaka uitishwe uchaguzi mwingine ambapo madiwani watamchagua kiongozi watakaomuona anafaa na sio kulazimishiwa kiongozi wasiyemtaka.
Naye Diwani wa Kata ya Msamala Kurabest Mgwasa alisema kuwa Ccm Wilaya imependekeza Madiwani watano wavuliwe uanachama ambapo hatma yao ipo kwenye ngazi ya chama hicho mkoa, lakini cha kushangaza madiwani hao nao wameitwa kwenye kikao hicho jambo ambalo lingeweza kuleta vurugu kubwa.
Kwa upande wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Mjini Alfonce Siwale alikiri kuitisha kikao hicho ambacho kilipaswa kifanyike jana lakini kilishindikana kutokana na mahudhurio hafifu ya madiwani ambao hawakufika hata nusu yao.
Alisema kuwa madiwani wengi wameshindwa kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa wapo safarini na hivyo kikao hicho kimepangwa kufanyika Oktoba 11 katika ofisi za chama hicho na kueleza kuwa madiwani hao hawana mgomo wowote
Alieleza kuwa chama hicho kina madiwani 21, lakini waliofika kwenye kikao hicho walikuwa wanane na kufanywa kikao hicho kutofanyika na kwamba kwenye kikao hicho madiwani waliopendekezwa kufukuzwa na chama ndio waliojitokeza kwa wingi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni