Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MWANANCHI. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MWANANCHI. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 3 Machi 2013

FATOU BENSOUDA ATEMBELEA TANZANIA, NI MWENDESHA MSHTAKA MKUU WA ICC



Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda alipofika Ikulu jijini Dar es Salaam 
Na Fidelis Butahe
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda, ametua nchini jana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya ICC imekuja ikiwa ni miezi sita tangu Serikali ya Tanzania ilipopelekwa katika mahakama hiyo, iliyoko The Hague,  Uholanzi kwa madai ya kukiuka haki za binadamu.

Malalamiko hayo maalumu yalipelekwa ICC na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Septemba 28 mwaka jana, baada ya kutokea kwa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na watu wengine 23.

Taarifa ya LHRC ilieleza kuwa pamoja na watu hao kuuawa, Serikali ilishindwa kuwachukulia hatua wahusika.

Mbali na kuishtaki Serikali ICC, kituo hicho cha Sheria na Haki za Binadamu pia kilipeleka mashtaka kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu.



Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba, alisema kuwa walifungua mashtaka hayo ili kuzitaka mamlaka hizo za kimataifa kufanya uchunguzi na kuichukulia hatua stahiki za kisheria dhidi ya Serikali ya Tanzania.

Jana Rais Jakaya Kikwete alikutana na Bensouda na kufanya mazungumzo na baadaye walipiga picha za pamoja nje ya Viwanja vya Ikulu,  akiwa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi.

Katika maelezo yake Bisimba alisema: “Tumepeleka mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu.”

“Tunatarajia kuona uwajibikaji wa viongozi wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa njia yoyote ile. Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na kujiuzulu, kuachishwa kazi na kufikishwa Mahakamani,” aliongeza Dk Bisimba.

Gazeti hili lilipomtafuta Jaji Werema kuzungumzia ujio wa Bensouda alisema kuwa Mwendesha Mashtaka huyo alikuwa mgeni wa Rais Kikwete, hivyo hawezi kueleza kilichozungumzwa.

“Alikuwa mgeni wa Rais, lakini kubwa nililolisikia ni kwamba alikuja kusalimia kwa sababu tangu alipoteuliwa hakuwahi kuja Tanzania,” alisema Werema.

Kama ilivyokuwa kwa Werema, naye Feleshi  alikwepa kuzungumzia ujio huo wa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, huku akisema jambo hilo linaweza kutolewa ufafanuzi na Ikulu.
Kwa Hisani ya Gazeti la Mwananchi.

Jumamosi, 29 Desemba 2012

HUKUMU UILIYOMREJESHA LEMA BUNGENI YAPINGWA NA WASOMI.

MWANAZUONI aliyebobea katika sheria, Profesa Issa Shivji na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla wamekosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, wanasheria hao walisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu wakiongozwa na Nathalia Kimaro, Salum Massati na Bernard Luanda, inapingana na sheria.

Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa Lema, Method Kimomogoro amepinga madai hayo akisema wanaoipinga pengine hawajapata nafasi ya kuliangalia kwa undani suala la haki ya mpiga kura kupinga matokeo mahakamani.

Profesa Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri zilizopo.
Alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi, Katiba ya nchi na Mahakama, vinampa haki mpiga kura kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980), vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,” alisema Profesa Shivji.

Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mahakama Kuu Tanzania iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Walalamikaji walishinda.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lema, iliamua kwamba hukumu katika kesi ya Mgonja ilikosewa kwani si sahihi kwamba mtu yeyote bila kujali mahali alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo lolote nchini hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna yoyote.

Lakini Profesa Shivji aliitetea hukumu hiyo ya Mgonja akisema imekuwapo kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwamba kwa muda wote huo imekuwa ikifuatwa katika uamuzi wa mashauri mbalimbali, huku akisisitiza kuwa Mahakama haiwezi kuifuta kirahisi tu.

Profesa Shivji alisema mpiga kura ni mwananchi na kwa vyovyote ana masilahi katika uchaguzi husika na hivyo anatarajia kuona uchaguzi ambao ni huru na wa haki.
“Hivyo huwezi kusema hahusiki na nani kashinda au kashindwa kwa kuwa uchaguzi ni muhimu katika kujenga na kukuza demokrasia,” alisema Profesa Shivji.

Chama cha Wanasheria
Kwa upande wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali wakizungumzia kutofurahishwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na wengi tunajiuliza kama siyo, sababu ya kuwa mpiga kura ni ipi nyingine inampa haki mpiga kura kupinga matokeo?”

Stolla alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005, inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

“Mwaka 2002, sheria zote zilifanyiwa marekebisho na baadaye mwaka 2005, Bunge likatunga sheria mpya inayoitwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ikafuta ya mwaka 1985. Sheria hiyo na marekebisho yake, ndiyo inayotawala uchaguzi hadi sasa,” alisema.

Alisema hata kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo ya Uchaguzi ya mwaka 1985, tayari kulikuwa na uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja ambayo iliamua kuwa mpiga kura ana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

Jumatano, 12 Desemba 2012

WATATU WAKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI HUKO IRINGA

Pembe za ndovu 


Pembe hizo zilizoelezwa kuwa zimetokana na tembo 39 wenye thamani ya Sh934.8 milioni, zilikamatwa juzi saa 12 jioni, baada ya gari lililokuwa na shehena ya mzigo huo kushtukiwa na askari waliokuwa katika Kituo cha Ukaguzi cha Igumbilo kilichopo Iringa Mjini.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema jana: “Watuhumiwa walikamatwa kutokana na kusita kusimamisha gari lao baada ya kushukiwa na askari. Haina shaka kwamba tembo hao waliuawa katika uwindaji haramu unaodaiwa kuendelea mkoani Mtwara,” alisema Kamanda Kamuhanda na kuongeza: “Askari walipolisimamisha gari hilo, dereva alijifanya anasimama, lakini baadaye akaanza kulikimbiza ndipo polisi walipoanza kulifukuza.”


Kamuhanda alisema kutokana na gari hilo kuwa na mwendo wa kasi kuliko la polisi, walilazimika kuchukua gari la msamaria mwema aina ya Toyota Land Cruiser na kuendelea kulikimbiza.“Wakati wanalifukuza gari hilo, askari waliwasiliana na polisi wa Kituo cha Ruaha Mbuyuni ambao waliweka kizuizi.”


Kamanda Kamhanda alisema baada ya kufika eneo hilo na kubaini kizuizi hicho, dereva wake aligeuza gari hilo kwa kasi na kuanza kurudi.


Alipofika mbele kidogo, watuhumiwa walilitelekeza na kukimbilia kichakani.Kitendo hicho kiliwavuta baadhi ya wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo na baada ya kufika hapo, walishirikiana na polisi kuingilia kichakani kuwasaka watu hao na kuwakamata muda mfupi baadaye.


Kamanda huyo alisema polisi waliokuwa wakilifuatilia gari hilo, walilipekua na kukuta pembe hizo zenye uzito wa kilo 211.6.
“Thamani ya pembe hizo ni Sh186,680,000. Lakini gharama za jumla kwa tembo 39 waliouawa ni Sh934,830,000,” alisema.


Kamanda Kamuhanda alisema mbali na kuwashikilia watu hao watatu, polisi inaendelea na kufanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika zaidi wa uharamia huo.
“Tunaamini bado kuna watu nyuma yao, siyo rahisi hao waliokuwa wanasafirisha, kuwa ndiyo waliokuwa wamewawinda tembo hao,” alisema na kuongeza;


“Sisi tunaendelea na uchunguzi na utakapokamilika tutawafikisha watuhumiwa wote mahakamani. Si kweli kwamba hawa waliokuwa wakisafirisha ndiyo wameingia kwenye mbuga za wanyama na kuua wao wenyewe,” alisema.


Kamanda huyo alisema mbali na pembe hizo za ndovu, katika upekuzi huo, polisi walibaini aina mbili za namba za usajili wa gari lililokuwa limebeba shehena hiyo ya nyara za Serikali.
“Watuhumiwa walitumia namba mbili za gari. Wakati gari hilo linapita eneo la Igumbilo, lilikuwa na namba tofauti na zilizokutwa Ruaha. Hali hii ilifanya kazi ya kutambua gari kwa kutumia namba kuwa ngumu, lakini aina ya gari na rangi vilisaidia,” alisema

Jumapili, 9 Desemba 2012

MAJAMBAZI WAPORA MAITI NA WAOMBOLEZAJI HUKO SINGIDA.

WAVUNJA GARI,JENEZA,WAMPEKUA MAREHEMU,WAPORA SH20 MILIONI
 
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora  takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi mkoani Singida,  majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na jeneza lililokuwa na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi  wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na kumpekua marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa msafara uliokuwa ukisafirisha maiti,  Makaranga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya SUA.
Akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa lilitokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa Singida kwenye kona maarufu kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani Mara.  
Alisema kuwa gari hilo pamoja na jeneza, lililobeba viongozi wa wanafunzi sita na viongozi wengine wanne lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao walibeba bunduki mbili aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.  
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele na kumparaza kwa panga usoni dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo vyote na kutuamuru kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” alisema Makaranga.  
Makaranga alisema kuwa katika tukio hilo, aliporwa Sh2 milioni alizokabidhiwa azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara huo, Sh8.8 milioni zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa  mwenzao na jumla ya Sh9 milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo mifukoni mwao.  
“Pia tuliporwa simu  zetu zote  za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.  
Makaranga aliyeeleza kuwa anafanya kazi za kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa na majambazi hao kuwa ni pamoja na yeye, dereva wao na kiongozi wa wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na uongozi wa SUA ili watume gari lingine na kukarabati jeneza lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama, watahakikisha watu waliofanya unyama huo, wanakamatwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.  
“Nimesikitishwa sana na tukio hili, inaelekea sasa binadamu tunaanza kutoka kwenye utu na kuhamia kwenye vitendo ambavyo binadamu wa Mwenyezi Mungu hawezi kuthubutu kuvifanya. Watu wanafikia hata kufungua jeneza na kuanza kulisachi,” alisema  Mlozi akionyesha masikitiko

Jumamosi, 10 Novemba 2012

HOJA YA ZITTO KABWE YAKUBALIWA NA BUNGE.

NGUVU za Serikali za kutaka kuifuta hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya nchi, jana zilishindwa baada ya wabunge kadhaa kumgomea Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kufanya hivyo.
Dalili za Serikali kutaka kuzima hoja hiyo zilianza baada ya Jaji Werema kusimama na kutoa mapendekezo ya kufuta vipengele muhimu.
Hatua hiyo ilizusha mvutano mkali, huku baadhi ya wabunge wakisema Serikali inataka kuifuta hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Mapendekezo ya Werema
Katika mapendekezo yake, Jaji Werema alipendekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye kipengele katika hoja hiyo ya Zitto ambacho kiliitaka Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia ili kupitia Kitengo cha Assets Recovery Unit irejeshe nchini mabilioni ya fedha yanayomilikiwa na Watanzania katika benki za Uswisi na maeneo mengine yote ambayo hufichwa fedha ili kukwepa kodi.
Jaji Werema alitaka pendekezo hilo liondolewe kwa maelezo kuwa mamlaka za uchunguzi ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Usalama wa Taifa zinalifanyia kazi suala hilo.
Eneo jingine katika hoja ya Zitto ambalo Jaji Werema alipendekeza lifanyiwe marekebisho ni kuwapiga marufuku viongozi wa Serikali na watoto wao pamoja na Watanzania wengine kufungua akaunti nje akisema suala hilo litashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya fedha za kigeni.
Pia alitaka pendekezo lililomo katika hoja ya Zitto cha kutaja akaunti za watu wenye fedha benki za nje na kuzichapisha katika vyombo vya habari lifanyiwe marekebisho kwa kuondolewa.
Alisema suala hilo ni gumu na linakwenda kinyume na sheria za benki zinazotaka kutunza siri za wateja wao.
Kuhusu pendekezo la kuitaka Serikali katika Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2013/13 kuanzisha kodi maalumu ‘Financial Transaction Tax’ ya angalau asilimia 0.5 ya thamani ya ‘transaction’ ili kuweza kuwa na rekodi za uhakika fedha za ndani na zinazotoka nje ya nchi, Werema alitaka lifutwe akisema hiyo inahitaji utafiti wa kutosha.
Alisema ofisi yake imechukua siku nyingi kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ikiwemo kwenda Uswisi na kwingineko na kwamba itashirikiana na vyombo binafsi vya uchunguzi kufanya kazi hiyo.
Pendekezo jingine lililopingwa na Jaji Werema lilikuwa ni kuitaka Serikali kuwabana Watanzania wenye fedha nje ya nchi waeleze walikozipata akisema kazi hiyo inaweza kufanywa na Takukuru.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (kushoto) akimwonyesha Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo baadhi ya ushaidi aliokuwa nao wa hoja yake binafsi inayoitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya watanzania walioficha fedha haramu nje ya nchi, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Wabunge wamshukia
Baada ya kutoa mapendekezo hayo, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisema anamshangaa Mwanasheria Mkuu kwa kufanya marekebisho ambayo yanaizima hoja ya Zitto.
Huku akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge, alisema Mwanasheria Mkuu anataka kuua hoja hiyo na kwamba mapendekezo yake yanakwenda kinyume na kanuni ambazo zinataka kila badiliko katika hoja liwiane na jambo linalojadiliwa.
“Hoja ya mabadiliko ya Mwanasheria Mkuu kuondoa mapendekezo hayo, kwa maoni yangu yanakinzana na Kifungu 53 (3) (4) cha Kanuni za Bunge, kinachopendekeza kuwapo kwa mabadiliko na siyo kufuta hoja.
Alisema hatua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya kupendekeza mabadiliko hayo ni kufuta hoja jambo ambalo alisema ni kinyume cha kanuni. Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mtu ambaye anaweza kuiondoa hoja ni mtoa hoja na si mtu mwingine yeyote.
Alimtaka Spika kutumia busara yake kumzuia Mwanasheria Mkuu kufuta hoja hiyo muhimu kwa mustakabali wa nchi.
Baada ya maelezo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisimama na kuunga mkono mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu, huku akielekeza ‘makombora’ kwa Lissu kuwa anachokisema kinapingana na mtoa hoja Zitto, ambaye anakubaliana na Mwanasheria Mkuu.
Hata hivyo, Zitto alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa hakubaliani na mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu yanazima hoja yake.
Baadaye Lukuvi alisema anaunga mkono pendekezo moja katika hoja ya Zitto la Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya uchunguzi katika Bunge la 11 na kwamba ili kasi hiyo iende vizuri yashirikishwe pia kampuni binafsi ya uchunguzi.
Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), alipinga pendekezo la kuiondoa hoja hiyo na kuunga mkono azimio kwamba Bunge liiagize Serikali kufanya uchunguzi huo na ripoti yake iwasilishwe katika Bunge la 11 na ikishindwa, Bunge liunde kamati ndogo ya kufanya kazi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia, aliuanga mkono mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisema vyombo vya uchunguzi viachiwe kuchunguza mabilioni ya fedha yaliyopo nje ya nchi.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alipinga akisema mapendekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yalikuwa na lengo la kuua hoja hiyo akisema wabunge watafanya dhambi kubwa kuiondoa hoja hiyo ya msingi.
Sendeka alitaka hoja hiyo iboreshwe kwa kumtaka Zitto awataje hadharani watu ambao wameficha fedha nje ya nchi ili Watanzania wawafahamu... “Ukiwataja hawa hoja yako itakuwa na mashiko, tusaidiane na wala siyo fedheha kuwataja.”
Alitaka kamati iundwe kuchunguza jambo hilo ili ukweli ujulikane.
Baada ya kubanwa na wabunge, ndipo Jaji Werema alisimama na kulegeza msimamo wake kwa kurejesha pendekezo la Serikali kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi vya nje pamoja na wachunguzi binafsi kufanya kazi hiyo.
Alikubali pia pendekezo la kuitaka Serikali kuja na mkakati wa kueleza nini imekifanya katika Bunge la 11.
Aliwataka wabunge wote wenye majina ya watu walioficha fedha nje ya nchi kuyapeleka Takukuru au wamkabidhi yeye.
Baada ya hapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisimama na kusema hoja ya Zitto haikuwa mbaya na kusema Mwanasheria Mkuu pia alikuwa na nia njema.
Alisema Serikali haiwezi kumficha mhalifu akisema kama mtu ameiba atachukuliwa hatua bila ya kumwonea haya. Aliungana na Mwanasheria Mkuu kutaka Serikali iachiwe jambo hilo ilifanyie kazi.
Akihitimisha mjadala huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema hoja ya Zitto haijatupwa bali, inaingia kwenye utaratibu wa Serikali wa kuyatekeleza maazimio hayo.
Alisema Serikali itapaswa kutoa taarifa ya utekelezaji wa hoja ya Zitto katika Bunge la 11 la Aprili) mwakani na kama ikishindwa, Bunge litaunda kamati kufanyia uchunguzi maazimio hayo.

Msimamo wa Zitto
Akizungumza baada ya uamuzi huo wa Bunge, Zitto alisema ameridhishwa na hatua hiyo akiamini kwamba itafanyiwa kazi.
Alisema amefurahi pia kwa kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kwa hoja yake kufanyiwa kazi na Bunge

Jumapili, 2 Septemba 2012

RAIS KIKWETE AFAFANUA JUU YA MGOGORO WA MPAKA WA MALAWI NA TANZANIA.

Rais Jakaya Kikwete
Tausi Mbowe
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kuwa mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa baina ya Tanzania na Malawi, utamalizwa kwa mazungumzo huku akisema chimbuko la mzozo huo ni mkataba wa Heligoland uliowekwa na wakoloni .

Akihutubia taifa kupitia hotuba yake ya kila mwezi, Rais Kikwete alisema kuwa siyo makusudio yake, wala ya Serikali kutafuta suluhisho la suala hilo kwa nguvu za kijeshi.

“Nawahakikishia Watanzania wenzangu kuwa, hatuko vitani na Malawi na wala hakuna maandalizi ya vita dhidi ya jirani zetu hawa kwa sababu ya mzozo wetu wa mpaka katika ziwa...  Ondoeni hofu na endeleeni na shughuli zenu za ujenzi wa taifa letu kama kawaida, ” alisisitiza Rais Kikwete.

Alisema kuwa alipokutana na Rais wa Malawi, Joyce Banda mjini Maputo, Msumbiji Agosti 18, 2012 alimhakikishia kuwa Tanzania haina mpango wa kuingia vitani na Malawi.

Rais Kikwete aliwataka wanasiasa kuepuka kauli au matendo yatakayovuruga mazungumzo na kuchochea uhasama kati ya nchi hizo mbili jirani na rafiki, huku akisisitiza kuwa kuna mafanikio makubwa ya kumaliza mzozo huo kwa njia ya mazungumzo kuliko njia ya vita, kwa kuwa kwa kufanya hivyo badala ya kupata suluhisho inaweza kuwa ndiyo mwanzo wa mgogoro mpana zaidi.

Alisema utata kuhusu mpaka katika Ziwa Nyasa haukuanza leo na kwamba ulikuwapo tangu wakati nchi hizo mbili zikiwa bado zinatawaliwa na wakoloni na kuendelea hata baada ya uhuru.

Chimbuko la mzozo
Rais Kikwete alisema chimbuko la mzozo wa mpaka uliopo sasa, baina ya nchi hizo mbili ni makubaliano baina ya Waingereza na Wajerumani kuhusu mpaka baina ya nchi hizo yaliyofanywa Julai Mosi, 1890, ambayo yalijulikana kama Mkataba wa Heligoland, (The Anglo-Germany Heligoland Treaty) ambayo yalitiwa saini Berlin, nchini Ujerumani baina ya Waingereza na Wajerumani.

Alisema wakoloni hao walikubaliana kuhusu mipaka baina ya makoloni yao na wakoloni wengine waliopakana nao, ambapo ndiyo makubaliano yaliyoweka mipaka ya Tanganyika na ile ya Zanzibar .

Rais Kikwete alisema kuwa kwa upande wa Ziwa Nyasa, Waingereza na Wajerumani walikubaliana kuwa mpaka uwe kwenye ufukwe wa nchi ya Tanzania kwa maana hiyo ziwa lote likapewa nchi ya Malawi na kwa upande wa Mto Songwe mpaka ulikuwa ufukweni upande wa Malawi kwa maana hiyo mto wote ukawa upande wa Tanzania.

Alisema katika kipengele cha Sita (Article VI) cha mkataba huo, wakoloni hao walikubaliana kufanya marekebisho ya mpaka mahali popote kama itakuwa ni lazima kufanya hivyo, kulingana na mazingira na hali halisi ya mahali hapo.

Alisema mwaka 1898 Tume ya Mipaka iliundwa na kuanza  kazi katika Mto Songwe kuhakiki mpaka baina ya Tanzania  na Malawi, ambapo ilikubaliana kuhamisha mpaka kutoka ufukweni mwa Mto Songwe upande wa Malawi na kuwa katikati ya mto.

“Baada ya uhakiki katika eneo hilo kukamilika, mwaka 1901 mkataba mpya ulisainiwa kuhusu mpaka huo...Tume iliendelea na kazi yake katika Ziwa Tanganyika na kuhamisha mpaka kutoka ufukweni hadi katikati ya ziwa na mkataba mpya kusainiwa mwaka 1910,” alisema.

Rais Kikwete alisema bahati mbaya tume hiyo haikufanikiwa kufanya uhakiki wa mpaka katika Ziwa Nyasa kutokana na kutokea kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kati ya mwaka 1914 hadi 1918 ambapo baada ya vita hivyo na Ujerumani kushindwa, Baraza la Umoja wa Mataifa liliikabidhi Uingereza udhamini wa Tanganyika na kwamba Uingereza ikawa inatawala Malawi na Tanganyika.

Alisema wakati Tume ya Uingereza na Ujerumani ilipokuwa imekufa, Tume ya Mipaka kati ya Uingereza na Ureno iliendelea na kazi na matokeo yake mwaka 1954, Uingereza na Ureno zilitengua mkataba wao wa mwaka 1891 ulioweka mpaka wa Ziwa Nyasa katika ufukwe wa mashariki ya ziwa, yaani kwenye ufukwe wa Msumbiji na kuuhamishia katikati ya ziwa.

Alisema jambo la kustaajabisha ni kuwa, Waingereza walioona umuhimu na busara ya kurekebisha mpaka kati ya Malawi na Msumbiji, hawakuona umuhimu wa kufanya hivyo kati ya nchi ya Tanzania na Malawi licha ya watu kutaka ufafanuzi kwa sababu inasemekana kati ya mwaka 1925 na 1938, taarifa ya Uingereza kwa Umoja wa Mataifa ziliweka mpaka katikati ya ziwa.  Lakini, kuanzia mwaka 1948 mpaka ukawekwa tena ufukweni.

“Mwaka 1959, 1960 na 1962, suala la mpaka wa Malawi lilijitokeza tena na kujadiliwa na Bunge la Tanganyika, wakati ule lilijulikana kuwa Baraza la Kutunga Sheria, (Legislative Council – LEGCO)," alisema.

Alisema hoja iliyotolewa ilikuwa kwamba Serikali ya Tanganyika ijadiliane na Serikali ya Nyasaland kupitia Serikali ya Malkia wa Uingereza ili ufumbuzi upatikane.  Wakoloni hawakujali na wala hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka Tanganyika ikapata uhuru wake Desemba 9, 1961 na Malawi kupata uhuru wake mwaka 1964.”

Rais Kikwete aliongeza kuwa, wakati Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961, mjadala kuhusu mpaka wa Tanganyika na Malawi uliendelea bungeni, hata hivyo iliamuliwa kwamba isubiriwe mpaka Malawi wapate uhuru ili yafanyike mazungumzo baina ya nchi mbili huru.

Alisema kuwa tangu wakati huo Tanzania haikukata tamaa katika awamu zote za uongozi imekuwa ikijitahidi kuendelea na jitihada za kumaliza mgogoro huo.

Kikwete alisema tume ya sasa itatoa mapendekezo kwa marais wa nchi hizo mbili, ambayo yatakuwa msingi wa majadiliano baina yao.  Alisisitiza umuhimu wa kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Sensa
Akizungumza kuhusu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, Rais Kikwete alisema mpaka sasa mwelekeo ni mzuri na ugumu ulioonekana kuwepo pale mwanzoni uliendelea kupungua siku hadi siku kadri utekelezaji wa zoezi ulivyokuwa unaendelea hivyo ana matumaini makubwa kuwa Sensa ya mwaka huu itakuwa na mafanikio mazuri.

Alitoa wito kwa wale wote ambao hawajahesabiwa wafanye hivyo katika siku zilizoongezwa ikiwa ni pamoja na wao wenyewe kupeleka taarifa zao kwa wenyeviti wao wa Serikali za mitaa au vijiji.

Alisema amearifiwa kwamba kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa, matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi kuhusu idadi ya watu na jinsia zao yatatolewa mwishoni mwa mwaka huu

Jumatano, 8 Agosti 2012

TANZANIA IMEJIDHATITI KWA LOLOTE KUTOKANA NA CHOKOCHOKO ZA MALAWI KUHUSU ZIWA NYASSA.


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,Edward Lowassa
Reginald Simon na Daniel Mjema, Dodoma
KAMATI ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imesema Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani na Malawi kama italazimika kufanya hivyo.Akizungumza mjini Dodoma jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Edward Lowassa alisema kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Tumepewa maelezo na jeshi letu na tumeridhika kuwa ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na limejipanga vizuri sana kwa uhakika, kiakili na kivifaa,” alisema Lowassa.

Kabla ya Lowassa kuzungumza na waandishi wa habari, alifanya kikao cha faragha kilichohusisha pia wajumbe wa kamati hiyo na makamanda wa JWTZ walipofika bungeni kutoa taarifa kwa kamati hiyo.
Hata hivyo, katika tamko hilo Lowassa alisema Tanzania inatarajia mgogoro huo utamalizika kwa njia za kidiplomasia kwa sababu Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa muda mrefu.

“Ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na kama ilivyo ahadi yao (JWTZ), wako tayari kulinda mipaka ya nchi yetu hadi tone la mwisho. Tunasali sana tusifike hapo,” alisema Lowassa na kuongeza: “Tunategemea hatutafika huko, lakini kwa heshima ya nchi yetu kama ikibidi kufika huko (vitani) tutafika kulinda mipaka yetu”.

Mwenyekiti huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, alisema kama Tanzania itafikishwa mahali itabidi damu ya Watanzania imwagike, nchi iko tayari kulinda mipaka yake kwa nguvu.Alisema kama itabidi kuingia vitani, itatumia umoja na mshikamano wa Watanzania wa mwaka 1978 wakati wa Vita na Uganda kulinda mipaka ili kulinda heshima ya nchi.

Alisema mwaka 1978 wakati Rais wa Uganda, Idd Amin na majeshi yake walipochukua sehemu ya Tanzania na kujitangazia ni mali yake, ilichukua hatua kumfukuza Amin.

“Alijitangazia sehemu ile ni mali ya Uganda hutegemei nchi ikae kimya, hutegemei Watanzania wanyamaze wakati nchi yao imetekwa, tulichukua hatua tukamfukuza hadi nchini kwake.”
Lowassa alisema Kamati ya Bunge inajua madhara ya kiuchumi yaliyotokana na Vita ya Idd Amin na kwamba vita yoyote ikipiganwa lazima kunakuwa na madhara ya kiuchumi.

Hata hivyo, alisema anaamini mgogoro huo hautafika huko na kusisitiza kuwa, lakini ikibidi JWTZ ni moja kati ya majeshi bora duniani na ni jeshi lililojiandaa vizuri kwa lolote.
“Wako tayari sisi ni moja kati ya jeshi lililojiandaa vizuri na jeshi bora duniani na la kujivunia. Tuko imara kiakili na kivifaa tena vya kisasa,” alisema Lowassa.

Alisema kamati yake inaunga mkono msimamo ulitolewa bungeni juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuhusu mgogoro huo na kwamba ndiyo kauli rasmi ya Serikali.
Juzi, Waziri Membe alizionya kampuni za kigeni za Malawi zilizoingia katika ardhi ya Tanzania eneo la Ziwa Nyasa kutafiti mafuta na gesi kusitisha mara moja.

Akiwasilisha makadirio ya wizara yake, Membe alisema upo ushahidi kuwa ndege tano za utafiti za Malawi ziliruka anga la Tanzania na kutua katika Ziwa Nyasa upande wa Tanzania.Membe alisema pamoja JWTZ kutoruhusu ndege hizo za Malawi kuingia na kutua eneo hilo la Ziwa Nyasa, bado ziliingia na kutua kinyume kabisa cha sheria za kimataifa.

“Wenzetu wa Malawi wanadai Ziwa Nyasa lote lipo Malawi na msingi wa madai yao ni mkataba wa Heligoland wa mwaka 1890 na sisi tunasema mpaka uko katikati ya Ziwa.”

Membe alisema hata mgogoro wa mpaka kati ya Cameroon na Nigeria ulitatuliwa na Mahakama Kuu ya Dunia kuwa mpaka baina ya nchi hizo mbili upite katikati ya Ziwa Chad.

Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Patrick Kabambe alikaririwa na Redio Sauti ya Ujerumani akisema wataendelea na utafutaji mafuta licha ya onyo hilo la Tanzania.

Waziri huyo alisema ziwa hilo linaitwa Malawi na siyo Ziwa Nyasa na kwamba utafutaji wa mafuta na gesi utaendelea na hakuna wa kuwasimamisha. Alihoji, iweje Tanzania ishtuke sasa

Jumapili, 29 Julai 2012

HATARI JAMANI, WABUNGE WALA RUSHWA, TUTAENDELEA KWELI NCHI HII!!!?

SPIKA AVUNJA KAMATI YA NISHATI, WAZIRI AELEZA WALIVYOITAFUNA TANESCO
Kizitto Noya na Boniface Meena, Dodoma
WAKATI wabunge wakitoa tuhuma nzito dhidi ya wenzao wanaodaiwa kujihusisha na ufisadi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imebainishwa kuwa wabunge wenye tabia hiyo ni watano, watatu kutoka chama tawala CCM na wawili upinzani.

Habari zilizopatikana jana mjini Dodoma zimeeleza kuwa baadhi ya wabunge hao wanatoka katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, huku wengine wakitoka Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wabunge hao wamedaiwa kuwa wamekuwa wakitumia nafasi zao za ubunge na ujumbe wa kamati kufanya biashara na Tanesco na kutetea mafisadi ndani ya shirika hilo la umma.

Gazeti hili limefanikiwa kupata majina ya wabunge hao, ambayo leo hatutayataja kwa sababu za kitaaluma. 

Baadhi ya wabunge waliochangia hoja hiyo bungeni juzi na jana walisema kuwa, wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini hawapendi kuwataja kwa kuwa siyo wakati mwafaka.

Moto wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa jana na Mbunge Vita Kawawa wa Namtumbo(CCM) aliyeomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hili lijadiliwe na Bunge na kupendekeza kuwa, Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.

 “Waheshimiwa wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa kifungu cha 55 (3)f  mbunge au waziri anaweza kutoa hoja ili jambo fulani lijadiliwe. Sasa naomba kutoa hoja ya kujadili suala hilo," Kawawa alisema.

Aliliomba pia Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na kamati nyingine zilizolalamikiwa kwa rushwa. Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge. 

Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono Spika wa Bunge, Anne Makinda alisimama na kukubali hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na Madini.

Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.

"Ninakubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na zingine ambazo zitatajwa kwenye tuhuma hizo. Nalipeleka pia suala hilo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, halafu kama ni kutajwa (wabunge hao), basi tutapata mwongozo wa kamati hiyo." alisema Spika Makinda na kuongeza:

"Nasema kwa dhati kabisa, kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge hili. Wabunge mkae vizuri. Kama kuna baadhi yetu wanaenda huku na huku kujitafutia masilahi binafsi, tutawezaje kuisimamia Serikali?"

Mbunge Zedi
Baada ya Spika kutangaza kuvunja Kamati ya Nishati na Madini, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema kuwa ameshtushwa na uamuzi huo na anasubiri uamuzi wa Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge. 

"Nimeshtushwa sana na uamuzi huo, lakini tusubiri Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge," alisema Zedi.

Waziri Muhongo
Akihitimisha hoja ya wizara yake bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi vya Tanesco kama wajumbe, wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.

"Shirika liliwahi kulipa Pauni za Uingereza 50,000 kwa ajili ya kununua vipuri, lakini kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza;

“Hata katika nguzo za umeme kuna biashara inaendelea. Tunajua kuwa nguzo hizo zinazalishwa Iringa na kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka Afrika Kusini." 

Waziri Muhongo alisema kuwa mbali na ufisadi huo, baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini wamewahi kuliuzia shirika hilo matairi ya magari kwa bei kubwa, bidhaa ambayo hata hivyo alisema haina ubora unaokubalika.

"Baadhi ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco; niseme tu kuwa, hii siyo sahihi. Lakini niombe kwamba mjadala huu tuufunge kwa sababu, tayari tumekabidhi suala hilo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)" alisema Waziri Muhongo.

Waziri Muhongo pia alizungumzia jinsi baadhi ya watu na kampuni zinavyoiibia Tanesco kupitia mita za Luku ambapo aliwataja  watu hao kuwa ni pamoja na Shule za St. Mary's zinazodaiwa Sh10.5 milioni, Access Bank, Tawi la Tabata Matumbi Sh13.8 milioni na Hoteli ya Akudo Paradaise ya Kariakoo inayodaiwa Sh25.5 milioni.

Alisema kuwa baada ya kubainika kwa wadaiwa hao hutumia umeme kinyume na utaratibu,wahusika  wote walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi baada ya kufanyika kwa uchunguzi.

“Baada ya kufanya uchunguzi na kubaini kuwapo kwa watu wanaotumia umeme bila kulipia na kuisababishia Tanesco hasara, tumeamua kuwachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha polisi,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:

“Inaonyesha wazi kwamba wizi wa umeme wa Luku umekuwa ukifanyika mara kwa mara na kwamba baada ya kuwakamata hawa, uchunguzi utaendelea na wengine watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.”

Jenista Mhagama

Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kuwa, amepokea kwa masikitiko taarifa hizo za wabunge wa CCM kuingia katika tuhuma hizo, lakini akasema namna nzuri ya kushughulikia tatizo hilo ni vyombo vya dola kufanya uchunguzi makini ili kujiridhisha na kisha hatua za kisheria kufuatwa.

"Ni taarifa mbaya kwa kweli, lakini mimi niiombe Serikali itusaidie kufanya uchunguzi ili ukweli ubainike na hatua zichukuliwe," alisema Mhagama.

Jumamosi, 28 Julai 2012

BEI YA KUUNGANISHA UMEME IMESHUSHWA NA SERIKALI

NI KWA WALE WASIOHITAJI NGUZO, WA NGUZO MBILI KUTOZWA SH 800,000, WAZIRI MUHONGO, ASEMA MGAWO SAFARI HII HAUKUBALIKIBoniface Meena, Dodoma
 
SERIKALI imetangaza kushusha gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa viwango ambavyo ni kati ya asilimia 60 na 77 kwa wakazi wa vijijini na kati ya asilimia 29 na 65 kwa wananchi waishio sehemu za mijini.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali bila kujali mteja aliko.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma jana, waziri huyo alisema punguzo hilo ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio mijini.

Profesa Muhongo alisema pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema kwa wateja watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni zilizokuwa zikilipwa awali.

“Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”

Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.

Machi 18 mwaka jana, Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.

Kadhalika Mei 16 mwaka huu, akizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt Profesa Muhongo alisema: “Kipaumbele cha wizara kwa sasa ni kupata umeme wa uhakika wa bei nafuu na unaotabirika. Ni muhimu kuongeza watumiaji wa umeme kwa kuwa kwa sasa kwa takwimu za Tanesco ni asilimia 18.4 tu ya Watanzania wanaopata huduma hii.”

Wizi Tanesco Profesa Muhongo aliwataka wezi wa umeme kujisalimisha kabla hawajakamatwa kwani hata wakijificha watakamatwa tu. Alisema upotevu wa umeme unafanywa na baadhi ya wananchi wanaoshirikiana na wafanyakazi wa Tanesco kwa kushirikiana na vishoka. “Kuna rushwa iliyokithiri Tanesco, kuna wezi wanaowaunganishia watu umeme na kuliibia shirika, wakae chonjo kwani watakamatwa tu,” alisema Profesa Muhongo. kuhusu wizara hiyo, alisema mambo mengi yatafanyika kwa uwazi na haoni sababu za kila jambo kuwa ni siri. “Mnakaribishwa wizarani kila mtakapoona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, hatutakuwa na mambo ya kuficha tutakuwa wawazi,” alisema Profesa Muhongo.

Mgawo wa Umeme
Kuhusu suala la mgawo wa umeme, alisema hautakuwepo tena na haukubaliki kamwe.
“Waheshimiwa wabunge, suala la mgawo haliwezekani na halikubaliki,” alisema Profesa Muhongo. Alisema katika mwaka 2011/12, wizara iliendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini. Profesa Muhongo alisema hadi Juni, 2012 uwezo wa mitambo ya kufua umeme (installed capacity) ulikua megawati 1,375.74 (gesi asilia ikiwa ni asilimia 40, maji asilimia 41 na mafuta asilimia 19).

“Uwezo huo ni ongezeko la megawati 367 sawa na asilimia 36 ikilinganishwa na uwezo wa megawati 1,013.74 uliokuwepo Juni, 2011. Mahitaji ya juu ya umeme kwa mwaka 2011/12 yalifikia wastani wa MW 820.35 ikilinganishwa na MW 730 kwa mwaka 2010/11,” alisema.

Alisema Julai, 2011 wakati wa Bajeti ya wizara hiyo ilipowasilishwa, nchi ilikuwa katika mgawo wa umeme... “Mgawo huo ulitokana na upungufu wa umeme wa takriban megawati 300 uliosababishwa na upungufu wa maji katika mabwawa kwenye vituo vya kufua umeme. Kutokana na hali hiyo, Serikali ililazimika kuandaa mpango wa dharura wa kuondoa mgawo wa umeme nchini ulioridhiwa na bunge.” Alisema katika mpango huo, megawati 572 zilipangwa kuzalishwa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa. Alisema hadi kufikia Juni, mwaka huu uwezo wa ufuaji wa umeme kutokana na mpango huo wa dharura ulifikia megawati 422.

“Mitambo hiyo inajumuisha Symbion megawati 137, Aggreko megawati 100, IPTL megawati 100 na mtambo wa gesi asili wa Ubungo megawati 150," alisema. Alisema kutofikiwa kwa kiwango kilichokusudiwa,  kunatokana na kukosekana kwa mitambo ya megawati 150 ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) iliyokadiriwa kugharimu Dola za Marekani 162 milioni sawa na Sh256.20 bilioni. Alisema hadi kufikia mwishoni mwa Juni, mwaka huu lengo la kuondoa mgawo wa umeme lilifikiwa kwa asilimia 100.

Jumatano, 25 Julai 2012

MARANDA NA FALIJALA WAFUNGWA MIAKA MITATU JELA KWA KESI YA EPA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miaka 18 jela Kada wa CCM, Rajabu Maranda na binamu yake, Farijala Hussein katika kesi ya tuhuma za kuchota Sh2.2 bilioni za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rajab Maranda na binamu yake Farjala Hussein(mwenye jezi ya bluu)
Mahakimu wawili katika jopo la waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo waliwatia hatiani watuhumiwa kwa makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila kosa.

Kwa upande wake kiongozi wa jopo hilo, Jaji Fatuma Masengi aliwaachia huru washtakiwa hao kwa maelezo kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote saba yaliyokuwa yanawakabili.

Hata hivyo, hukumu hiyo haikuweza kuwaokoa watuhumiwa na hasa Farijala na Maranda watatumikia adhabu yao kwa miaka mitatu jela kwa kuwa adhabu zote walizopewa zitakwenda kwa wakati mmoja.

Tayari Maranda na Farijala wanatumikia kifungo kingine cha miaka mitano jela, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh1.8 bilioni za EPA, ambapo walihukumiwa na mahakama hiyo Mei 23, 2011.

Jopo lagawanyika
Jopo la mahakimu watatu lililokuwa likisoma hukumu hiyo liligawanyika na kusoma hukumu mbili tofauti, ambapo hukumu moja iliyoandaliwa na kusomwa na kiongozi wa jopo hilo, Jaji Masengi aliyewaachia huru washtakiwa.

Hata hivyo, katika hukumu ya pili, iliyoandaliwa na Hakimu Projestus Kahyoza na mwenzake Catherine Revocate iliwatia hatiani washtakiwa katika makosa sita kati ya saba yaliyokuwa yakiwakabili, na kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa.

Hata hivyo, wakati wakisoma hukumu hiyo, mahakimu hao walisema badala ya washtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 18, hukumu yao itaenda sambamba hivyo watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela.

Kabla ya hukumu
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, hakimu Kahyoza na mwenzake walipitia ushahidi uliotolewa na mashahidi sita wa upande wa  mashtaka  akiwamo mtaalamu wa maandishi, Joseph Mgendi ambaye aliweza kuangalia saini katika nyaraka halisi na zinazodaiwa kughushiwa,  ikiwamo hati ya usajili  ambapo alibainisha kuwa zilikuwa zimeghushiwa.

Pia walipitia utetezi uliotolewa wa mshtakiwa Maranda, ambaye aliyakana mashtaka yote saba yanayowakabili na kwamba, alikataa katakata kuwa hakuwahi kula njama na kughushi hati ya usajili wa Kampuni ya Money Planners & Consultant.

Hakimu Kahyoza alisema, Maranda alidai kuwa yeye hakuwahi kwenda Brela kusajili kampuni hiyo na kwamba, aliyewahi kwenda kusajili kampuni ni binamu yake, Farijala.

Hakimu Kahyoza alisema, Maranda katika utetezi wake alisema yeye hakuwahi kughushi hati yoyote hivyo, haikuwa rahisi kwake kutoa hati iliyoghushiwa pia, hakuwahi kuiba fedha BoT na wala hakuwahi kujipatia fedha yoyote kwa njia ya udanganyifu.

Kahyoza alifafanua kwamba, Maranda alidai mfumo uliotumika kuwaingizia fedha kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CBA uliendeshwa kihalali ndiyo maana, BoT hawakuwahi kulalamika hivyo, aliiomba mahakama imuone hana hatia.

Akisoma utetezi uliotelewa na Farijala, Hakimu Kahyoza alisema, Farijala naye alikataa  madai ya kughushi, kuwasilisha nyaraka bandia benki, kuiba fedha yoyote na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na aliiomba mahakama imwachie huru kwa sababu hana hatia.

Yasiyo na utata
Hakimu Kahyoza alisema kuwa mahakama ilibaini kuwapo kwa masuala yasiyokuwa na utata ambayo ni pamoja na kwamba Maranda na Farijala ni ndugu, waliwahi kufanya biashara pamoja na waliingiziwa fedha kwenye akaunti namba 0101379004 ya United Bank of Africa ambazo ni kiasi cha Sh2.2 bilioni.

“Baada ya kuweka msingi huo, mahakama ilijiuliza je, washtakiwa walikula njama ya kuiibia  BoT, walighushi hati ya usajili wa kampuni namba 150731, walighushi hati ya mkataba kati ya Kampuni ya Money Planners & Consultant  na Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani, waliwasilisha nyaraka za kughushi benki, waliibia BoT na kwamba je, walijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,” alihoji Kahyoza.

Hakimu huyo alisema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa,  hakuna utata kuwa hakuna mahali panapoonyesha washtakiwa ndiyo walikuwa wamiliki wa kwanza wa kampuni hiyo Money Planners & Consultant na kwamba majina yanayodaiwa kuwa ni wamiliki wa kampuni  hiyo ya Thobias  Kitunga na Paulo  ni majina ya uongo na ya kufikirika.

Alisema licha ya majina hayo kuwa ya kufikirika, mabadiliko ya kampuni hiyo ya Money Planners & Consultant hayakuwahi kufanyika na hata Brela hakuna kumbukumbu, hivyo saini zilizopo katika nyaraka za kampuni hiyo ikiwamo hati ya usajili ni za kughushi.

Alisema sababu ya kuthibitisha hilo ni kwamba, ofisi ni ileile iliyopo Magomeni Mapipa, Mtaa wa Iramba nyumba namba 7 hata baada ya mabadiliko.

“Hati hizo za usajili hazikusainiwa na Msajili wa Biashara toka Brela, Noel Shani bali zilisainiwa na washtakiwa wenyewe. Hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 333 na 335 (c) (e) vimetufanya tufikie hitimisho kuwa  washtakiwa walighushi nyaraka hizo,” alisema Hakimu Kahyoza.

Jumatatu, 9 Julai 2012

DK. ASHA ROSE MIGIRO AMALIZA UTUMISHI WAKE UN, AMEREJEA NCHINI LEO.



ASHA MIGIRO(DK.)
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa DK Asha-Rose Migiro

CHADEMA YASEMA SERIKALI YATAKA KUWADHURU DK. SLAA NA MNYIKA.

MBOWE ASEMA MPANGO HUO UNARATIBIWA NA KIGOGO WA USALAMA WA TAIFA, MKUCHIKA ASEMA NI TUHUMA NZITO, AZIVUTIA KASI Geofrey Nyang’oro
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),kimetoa tuhuma nzito kikidai kigogo mmoja (jina tunalo) wa Idara ya Usalama wa Taifa anaratibu mpango wa kuwaua viongozi wake waandamizi akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.


Kwa sababu hiyo, chama hicho kimeitisha kikao cha Kamati Kuu (CC) leo kujadili mambo mbalimbali na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe amesema ajenda kuu itakuwa kuzungumzia usalama wa viongozi wao kutokana na vitisho hivyo.
Kuhusu tuhuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika amesema tuhuma hizo ni nzito na atazijibu kwa maandishi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mbowe alitaja majina ya baadhi ya maafisa idara hiyo (majina tunayahifadhi) na kudai kuwa mmoja kati yao ndiye anayeratibu shughuli hiyo na tayari yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kuongoza  kundi linalotaka kumdhuru Mnyika.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema mbali na viongozi hao wawili, mwingine aliyedai kuwa anafuatiliwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema akidai kwamba, taarifa zinaonyesha kuwa wanafuatiliwa kwa saa 24.
Mbowe alidai kwamba idara hiyo ambayo haifanyi shughuli za siasa, inatumia ofisi yake vibaya kwa kufuatilia viongozi hao wakidhani chama hicho kina mambo ya siri kinayotaka kuyafanya katika nchi hii.
“Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao kwa wananchi na si vitisho,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunaomba wananchi waelewe kuwa viongozi wao wako hatarini, lakini Chadema hatutarudi nyuma katika kutetea haki  za wanyonge hata kwa kufa na hatuwezi kupeleka malalamiko yetu polisi sababu nao ni sehemu ya tatizo.”
Alisema chama chake kimekuwa kikihusishwa na mambo mengi ukiwamo mgomo wa madaktari unaoendelea na kusema Chadema hakiko nyuma ya mgomo huo na hakijawahi kukutana na kufanya kikao na madaktari.
“Wametuhusisha na mambo mengi na sasa wanasema tuko nyuma ya mgomo wa madaktari, taarifa hizo siyo za kweli na wala hatujawahi kukaa nao kikao chochote kujadili masuala yao, madaktari wana madai ya haki zao. Hapa tunaingia kwenye utaratibu wa kutesana ili kupata taarifa, mmesikia Dk Ulimboka aliteswa ili aseme Chadema iko nyuma ya mgomo,” alidai Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alisema suala la kutokuwa nyuma ya mgomo huo haliwanyimi fursa ya kutetea makundi ya watu wanaodai haki zao wakimwamo madaktari na kusema anaunga mkono tamko la viongozi wa dini.
“Viongozi wa dini wametoa tamko lao jana (juzi), wakitaka Serikali kuwarudisha madaktari na kumalizia suala hilo kwa njia ya mazungumzo,” alisema.
Alisema Chadema kinaunga mkono tamko hilo akisema si busara kuwa fukuza kwa sababu Serikali imetumia gharama kuwaandaa.
Dk Slaa anena
Kwa upande wake, Dk Slaa alisema Chadema kimeamua kutotoa madai yake polisi akidai kuwa imepokea madai mengi kutoka kwa viongozi na wanachama ya kutendewa visivyo lakini hakuna hata moja lililowahi kufanyiwa kazi.
Kuhusu kitisho la kuuawa alidai kwamba alianza kutishiwa siku nyingi na kusisitiza kuwa hilo haliwezi kuwanyamazisha.

“Taarifa za sasa wanaanza na Mnyika na kufuatia mimi, ninachosema wafanye watakavyo hatutaacha kufanya kazi yetu, hata nilipoibua tuhuma za EPA niliwaambia watuhumiwa wengine wa sakata hilo ni Usalama wa Taifa,” alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alitaja baadhi ya mambo ambayo alidai kuwa hayakushughulikiwa yalipowasilishwa polisi kuwa ni vinasa sauti alivyowekewa kwenye chumba alichokuwa amelala wakati wa vikao vya Bunge Mjini Dodoma.
Alisema vifaa hivyo vilichukuliwa na polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi lakini hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa hata kwake licha ya kuwa mhusika mkuu.
Mnyika: Namwachia MunguAkizungumzia madai hayo, Mnyika alisema anamuachia Mungu kwa kuwa ndiye aliyetoa uhai hata kwa hao wanaofikiria kutekeleza kitendo hicho.
Mnyika alidai kuwa baada ya kupata taarifa hizo ambazo alisema zimeandaliwa kwa ama kunyeshwa sumu au kuvamiwa na majambazi, alikutana na familia yake na uongozi wa chama chake ambao kwa pamoja wamemtaka aendelee na kazi ya kutetea rasilimali za taifa.
“Nilipopata taarifa hizi nimekutana na viongozi wangu wa chama na jana usiku (juzi), nilikutana na familia yangu, kwa pamoja wameniambia niendelee na kazi hii ninayoifanya kwani nimetumwa na wananchi na sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ”alisema Mnyika.
Kwa upande wake, Lema alisema  taarifa za kufuatiliwa na watu hao wanaodaiwa kuwa ni wa Usalama wa Taifa alizipata kwa mmoja wa vyanzo vyake kutoka serikalini.
“Nilipigiwa simu na mtu mmoja kutoka serikalini aliyeniambia kuna gari nyuma linanifuatilia, nilipogeuka niliona na kusimama kisha nikashuka na kubadili gari na lenyewe likaendelea kunifuatilia katika gari nililokuwa nimepanda,” alidai  Lema.

Lema alidai kwamba hata juzi asubuhi alikutana nalo katika nyumba aliyofikia na alipolikaribia watu hao walishusha vioo na kumsalimu wakimwita ni Mbunge wa Arusha aliyeko kwenye likizo.

Jumapili, 8 Julai 2012

MAJI YAGUNDULIWA SAYARI YA MARS.



WANASAYANSI wa anga kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta  uwezekano wa maisha katika sayari nyingine, mbali na dunia.Kuna imani kuwa kwenye sayari hizo, huenda zikapatikana raslimali nyingi kwa urahisi kuliko duniani ambako binadamu wameishi mamilioni ya miaka  hadi sasa.


Wataalamu hao wa anga wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda sasa na moja ya mambo muhimu wanayoangalia ni upatikanaji wa maji. Popote maji yanapopatikana, wanaamini maisha yanawezekana.Moja ya sayari ambayo wamekuwa wakiichunguza kwa miaka mingi sasa ni Mars, ambayo ni ya nne kutoka kwenye jua. Dunia ni ya tatu.


Sababu kuu za kuichagua sayari hii tofauti na zingine ni kwamba, hali ya hewa inatofautiana kidogo sana na ya dunia.


Sayari nyingine kama Mercury na Venus, zipo karibu zaidi na jua na hali ya joto iko juu kiasi kwamba hali ya maisha inaweza kuwa taabu.


Mars ambayo wanasayansi wanaipa jina la sayari nyekundu, ipo karibu na dunia, hivyo ni rahisi kufika iwapo wanasayansi watathibitisha iwapo maisha yanawezekana huko.


Wanaiita sayari nyekundu kwa sababu eneo kubwa la uso wake ni wa rangi nyekundu, tofauti na nyingine zilizomo kwenye mfumo wetu wa sayari.


Hakuna mwanasayansi  ambaye amethubutu kusafiri hadi kwenye sayari hiyo kutokana na ugumu wa kupata vyombo vya kuaminika, vinavyoweza kusafirisha watu kutoka duniani hadi Mars na kurudi salama.


Hata hivyo, hilo siyo tatizo kwa sababu wakibaini mazingira mazuri, utengenezaji wa vyombo hivyo hauwezi kuwapa taabu.


Kazi ya uchunguzi imekuwa ikifanywa kwa vyombo maalumu ambavyo havina watu lakini, vina uwezo wa kuleta mawasiliano duniani.


Pia wanatumia viona mbali katika mchakato huo  kuchunguza hali ilivyo kwenye sayari hii, ambayo kumekuwapo na hisia kwamba huenda waliwahi kuishi viumbe hai mamilioni ya miaka iliyopita lakini baadae mazingira yakabadilika na kuwa mabaya.


Uchunguzi unaonyesha kuwa, sayari hii ina mabonde mengi ambayo yanakila dalili kuwa awali yalikuwa yanatiririsha maji kama ilivyo mito hapa duniani.


Kwa muda mrefu, wanasayansi wamekuwa wakiichukulia sayari hiyo kuwa na mazingira ya jangwa yanayotokana na ukame wa muda mrefu.


Wagundua maji
Mwezi uliopita wanasayansi hao wamekuja na maelezo kwamba sayari hiyo ina kiwango kikubwa cha maji na mengi yapo mita chache kutoka uso wake.


Mmoja wa wanasayansi wanaochunguza sayari hiyo ni Profesa Jay Melosh wa Chuo Kikuu cha Purdue, nchini Marekani.


Yeye anasema uchunguzi huo umewapa imani kwamba siyo tu kwamba Mars ina maji bali kuna viumbe wadogo, mfano wa jamii ya bacteria ambao wanaendelea kuishi humo hadi leo hii.

Jumatatu, 21 Mei 2012

MAAFISA UHAMIHAJI WACHUNGUZWA KWA UKWASI WAO MKUBWA, TUME YAANZA KAZI RASMI LEO.


Vigogo Uhamiaji wana utajiri wa kutisha

TUME YA KUWACHUNGUZA YAANZA KAZI LEO, WAHAMISHIWA MIKOANI KIAINA
Mwandishi Wetu
KASHFA nyingine imeibuliwa katika Idara ya Uhamiaji.Taarifa mpya yenye kurasa tano, imewataja vigogo hao saba wakidaiwa kuwa na utajiri wa kutisha.Taarifa hiyo ambayo tunayo nakala yake, imedai kuwa vigogo hao wanamiliki mali na mamilioni ya shilingi katika akaunti zao binafsi.
Maofisa saba wametajwa kwa majina na vituo vyao vya kazi ambavyo ni Lindi, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na Moshi.
Tuhuma hizo zimekuja wakati Tume Maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za ufisadi na utoaji wa vibali bandia kwa wageni, ikitajwa kuanza kazi juzi. Hata hivyo, habari kutoka wizarani zinaeleza kuwa timu hiyo itaanza rasmi kazi zake leo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Uhamiaji, zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamemhoji meneja wa benki moja kubwa ya Moshi ili kupata ukweli wa madai kuwa kigogo mmoja wa Uhamiaji mwenye cheo cha Naibu Kamishna (DCI), anamiliki akaunti ya fedha za kigeni.
Kigogo huyo anahusishwa pia na mtandao wa utoaji vibali bandia kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi mkoani Kilimanjaro au kufanya kazi za kujitolea.
Ripoti hiyo imetaja taasisi 13, zikiwamo zisizo za kiserikali (NGO), hospitali na hoteli za kitalii zinazodaiwa wageni wake walipewa vibali bandia.
Mbali na kumhoji meneja huyo, inadaiwa pia walifanya mahojiano na uongozi wa kiwanda kimoja kinachodaiwa kukutwa na vibali bandia vya wageni 84.
Taarifa hizo zilidai kuwa maofisa wengine waandamizi wa Uhamiaji kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam walitarajiwa kuwasili Moshi juzi kuungana na wenzao.
Baadhi ya maofisa waliotajwa katika ripoti hiyo kwamba wana utajiri ni wale waliokumbwa na uhamisho katika idara hiyo, Kia miezi mitatu iliyopita.
Katika ripoti hiyo, kigogo mmoja mwenye cheo cha DCI anadaiwa kukutwa na Sh700 milioni katika akaunti yake, achilia mbali kumiliki mali za mamilioni.
Mbali na maofisa hao kumiliki mamilioni ya fedha taslimu, pia wanadaiwa ‘kufanya kufuru’ ya kununua magari ya kifahari, nyumba na viwanja.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuandikwa na Maofisa Uhamiaji wazalendo, imepinga hatua ya kuhamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, maofisa wanaotuhumiwa kukutwa na utajiri ambao haulingani na vipato vyao.
“Tunataka ufanyike ukaguzi wa kina wa vibali vyote vilivyotolewa kati ya 2009/2010, 2010/2011 hadi 2012 na taasisi zote zionyeshe nakala zake. 

Jumanne, 20 Machi 2012

MWAKYEMBE ASEMA AMEPONA UGONJWA ULIOMSUMBUA.


Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kuingia ofisini humo kuanza kazi, kutokana na afya yake kuimarika. Mwakyembe amekuwa akitibiwa nchini India kwa muda mrefu. Picha na Zacharia Osanga
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe akiwa amevalia kofia ya pama alisema: “Si kwamba sijambo, bali nimepona kabisa baada ya kugundulika na maradhi hayo na kutibiwa.”


BAADA ya utata wa muda mrefu wa ama Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amelishwa sumu au la, jana Mbunge huyo wa Kyela, aliweka hadharani ugonjwa wake akisema unafahamika kitaalamu kwa jina la Popular Scleroderma huku akisisitiza: “Sasa nimepona kabisa.”


Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo mwaka jana yalizidi kumtikisa na Oktoba 9, Serikali iliamua kumpeleka Hospitali ya Appolo, India kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.


“Nimerudi juzi kutoka India na daktari wangu ameniambia nimepona, nilikuwa nasumbuliwa na maradhi ya ‘Popular Scleroderma’ iliyosababisha ‘skin disorder’ (ngozi kutokuwa katika hali ya kawaida), lakini kwa nguvu za Mungu nimepona, namshukuru Mungu.”


Kuhusu sumu
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kulishwa sumu, Dk Mwakyembe alikataa kuzungumzia hilo akisema anasubiri uchunguzi ulioagizwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.


Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema angependa kuona uchunguzi huo unakamilika haraka na ripoti yake inatangazwa kwa umma.


Alisema yuko tayari na anasubiri tume hiyo ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri Nahodha imhoji ili atoa kile kilichomo katika ripoti ya daktari wake.


Dk Mwakyembe alisema anachoshukuru hadi sasa ni kwamba afya yake imeimarika kutokana na shinikizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza Serikali kumpa kipaumbele wakati wote akiwa nchini na India hatua ambayo imemwezesha kufika hapo alipo.


Kutokana na hali hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka wananchi wote wakiwemo wa jimboni kwake Kyela kuondoa wasiwasi akisema sasa yupo imara kwa ajili ya ujenzi wa majukumu ya taifa.


“Ninaomba wapiga kura wangu wa Kyela waache jazba, wawe na subira juu ya matatizo yangu. Wiki ijayo nitakwenda kuzungumza nao ili niweze kuwaeleza matatizo yaliyokuwa yananisumbua, lakini sasa hivi niko fit,” alisema.


Mtaalamu auzungumzia
Mtaalamu wa afya ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ugonjwa huo wa ‘Popular Scleroderma’ unasababishwa na chembechembe hai nyeupe kushambulia kitu kigeni kilichoingia kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya ngozi.


Alisema chembechembe hizo zinaweza kusababisha ngozi ya mwili kuharibika... “Ni magonjwa yanayosababishwa na chembechembe hai nyeupe kujikataa zenyewe na kusababisha ugonjwa wa ngozi na mifupa.”
Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe kuhusu ugonjwa wake imefungua ukurasa mpya hasa baada ya baadhi ya wanasiasa kuamini kuwa hakuwa na tatizo jingine bali, amelishwa sumu. Tayari Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba ambaye alitoa ripoti akisema Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu kama inavyodaiwa, amefanyia uchunguzi madai hayo na kukabidhi jalada lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ili afungue kesi.

Kauli ya Sitta

Mmoja wa wanasiasa waliodai kuwa Dk Mwakyembe amelishwa sumu, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alipoulizwa jana juu ya kauli hiyo mpya ya Dk Mwakyembe alisema hana cha kuzungumza.


Januari 28, mwaka huu akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Dar es Salaam Sitta alisema Dk Mwakyembe amelishwa sumu.


Akizungumza kwa utaratibu, Sitta alisema hana mengi ya kuzungumza kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa isubiriwe ripoti kutoka India ambako alikuwa akitibiwa.


“Dk Mwakyembe si anatibiwa India?,” alihoji na kuendelea, “Nadhani umeshapata jibu, tusubiri… acha huko India waendelee na uchunguzi wao, siwezi kusema lolote zaidi ya hilo nililokuambia.”


Dk Mwakyembe alianza kuugua Oktoba 9, mwaka jana na alitibiwa Apollo hadi aliporejea Desemba 11, mwaka jana. Alirejea tena India kuendelea na matibabu hadi Ijumaa iliyopita aliporudi na kusema kuwa amepona.


Matatizo yake ya kiafya yamesababisha mvutano baina ya viongozi wa Serikali. Wakati Manumba akisema ripoti kutoka Wizara ya Afya ilionyesha hakupewa sumu, waziri mwenye dhamana na afya Dk Haji Mponda alimkana.


Pia Waziri Nahodha ambaye ana dhamana na jeshi hilo la polisi, alikana ripoti hiyo ya DCI Manumba na kutaka aulizwe mwenyewe alikoitoa huku akisema uchunguzi alioagiza bado unaendelea

Jumatano, 15 Februari 2012

DK. MWAKYEMBE ARUDI TENA INDIA

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe anatarajia kuondoka nchini wakati wowote kwenda nchini India kwa ajili ya matibabu.

Dk. Mwakyembe kabla hajapata maradhi ya ngozi.
Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo Oktoba 9 mwaka jana, alilazimika kupelekwa katika Hospitali ya Appolo nchini India kwa matibabu zaidi.

Jana, vyanzo vya karibu na Dk Mwakyembe vilidokeza gazeti hili kwamba naibu Waziri huyo na Mbunge wa Kyela anatarajiwa kurudi Appolo, kwa ajili ya kuangalia kama matibabu aliyopata yameweza kumsaidia kwa kiwango gani.

Vyanzo hivyo vilivyo karibu na Dk Mwakyembe, vilifafanua kwamba anachokwenda kufanya India ni "Uchunguzi tu wa kawaida kuona maendeleo ya matibabu." 

Dk. Mwakyembe alipougua na kutibiwa India.
"Atarudi katika uangalizi wa kawaida, kwasababu amekuwa akipata matibabu hivyo lazima achunguzwe kuona dawa alizokuwa akitumia zimemsaidia kwa kiwango gani," alisema.

Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela, hivi karibuni alijitokeza na kutoa kauli nzito kuhusu chanzo cha maradhi yanayomsibu, huku Serikali ikiendelea kukaa kimya hata baada ya washirika wake wa karibu kusisitiza kwamba alipewa sumu.

Jumatatu, 23 Januari 2012

DK. SLAA USO KWA USO NA DK. KIKWETE, ILIKUWA JUZI IKULU YA DAR KATIKA MAZUNGUMZO YA KATIBA MPYA.

Mheshimiwa Rais Kikwete akisalimiana na Dk. Slaa juzi usiku Ikulu alipowakaribisha viongozi wa CHADEMA kwa mazungumzo mafupi juu ya Katiba mpya
.
RAIS Jakaya Kikwete amekutana na uongozi wa Chadema Ikulu Jijini Dar es Salaam, akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, kuzungumzia mchakato wa Katiba Mpya.Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili, mkutano huo ulifanyika jana kuanzia saa 10:30 jioni na kuendelea hadi usiku, lakini walifanya mapumziko mafupi saa tatu usiku.

Ujumbe wa Chadema uliokuwa wa watu wanane, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Wengine waliofuatana naye pamoja na Dk Slaa ni  Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, John Mnyika, Said Arfi, John Mrema, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari. Hadi tunakwenda mitamboni kikao hicho kilikuwa kinaendelea.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Slaa kukutana na Rais Kikwete tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao Dk Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34 akiwa nyuma ya Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, Dk Slaa hakuwahi kukutana na mkuu huyo wa nchi ana kwa ana.

Katika hafla ya kutangazwa matokeo ya urais iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Dk Slaa hakuhudhuria tofauti na ilivyokuwa kwa waliokuwa wagombea wenzake wote.

Dk Slaa, ambaye alikataa kuyatambua matokeo hayo, tangu wakati huo hawakuwahi kukutana rasmi na Rais Kikwete huku uvumi ukizagaa kwamba  kwamba mwanasiasa huyo amekuwa akijaribu kukwepa asikutane ana kwa ana na Rais Kikwete kwenye mazingira yoyote.

Katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipangalala, hivi karibuni Dk Slaa alidaiwa kumkwepa Rais Kikwete, kwa kutokwenda kukaa kwenye nafasi aliyoandaliwa jirani na kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Ilidfaiwa kuwa nyumba kulikofanyika shughuli za awali za mazishi, waandalizi waliandaa majukwaa mawili, moja maalumu kwa ajili ya wabunge huku jingine likiwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu ambalo alikaa Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.

Mbali ya kukaa viongozi hao, kulikuwa na nafasi ambayo ilikuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya Rais. Mbali ya nafasi hiyo, pia kulikuwa na kiti ambacho ilitegemewa kwamba Dk Slaa angekalia.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alidaiwa kukikwepa na kwenda kujichanganya katika jukwaa la wabunge na kiti hicho kubaki bila ya kukaliwa na mtu.

Hata hivyo Dk Slaa alikanusha uvumi huo na kudai kwamba asingeweza kwenda kukaa jukwaa alilokaa Rais Kikwete kwani yeye si kiongozi wa serikali hivyo kwa mujibu wa itifaki, asingeweza kumfuata Rais Kikwete na kwenda kumsalimia alipoketi.

Hii ni  mara ya pili kwa ujumbe wa Chadema kukutana na Rais Kikwete Ikulu  kuzungumzia mchakato wa Katiba Mpya

Jumatatu, 21 Novemba 2011

EWURA-BEI YA PETROLI YASHUKA DIZELI YAPANDA.

WAKATI bei ya petroli imeshuka dizeli na mafuta ya taa yamepanda, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza jana.


Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu imeonyesha kuwa petroli imeshuka kwa Sh22.86 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 1.12 na dizeli imepanda kwa Sh51.23 kwa lita ambayo ni sawa na asilimia 2.58 huku mafuta ya taa yakipanda kwa Sh46.45 kwa lita sawa na asilimia 2.35.


“Mabadiliko haya ya bei za mafuta hapa nchini yametokana na kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia na kupanda kwa bei ya dizeli na mafuta ya taa katika soko la dunia. Pia kushuka kwa shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani,” alieleza Masebu katika taarifa yake.


Alisema kuwa kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani alimradi ziwe chini ya bei ya kikomo.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya petroli kwa Dar es Salaam itakuwa ni Sh2,020, dizeli Sh2,034 na mafuta ya taa Sh2,021.


Jijini Arusha petroli itakuwa ikiuzwa kwa Sh2,104, dizeli itakuwa Sh2,118 na mafuta ya taa Sh2,105. Mbeya petroli itakuwa ikiuzwa kwa Sh2,127, dizeli 2,141 na mafuta ya taa yatakuwa ni Sh2,128. Mwanza petroli itauzwa kwa Sh2,170, dizeli Sh2,184 na mafuta ya taa Sh2,171.


Wiki mbili zilizopita Ewura, ilitangaza kupanda kwa bei ya petroli kwa Sh49.17, dizeli Sh2.69 na mafuta ya taa kwa Sh19.43. hadi jana, petroli ilikuwa ikiuzwa kwa Sh2,043, dizeli Sh1,983 na mafuta ya taa Sh1,975

Jumapili, 20 Novemba 2011

BUNGE LAMKAANGA JAIRO NA LUHANJO.

Luhanjo, Katibu Mkuu Kiongozi.


Neville Meena, Dodoma
KAMATI teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni, imewasilisha taarifa yake huku ikimkangaa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa, David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi  Philemon Luhanjo.Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Injinia Ramo Makani, aliliambia Bunge kuwa wengine wanaopaswa kuwajibishwa ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali, Ludovick Uttoh .
Makani alisema baada ya kufanya uchunguzi wake uliowezesha kuwahoji watu 146, imebainika kuwa utaratibu uliotumiwa na Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kutoka katika taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kusaidia upitishaji wa bajeti bungeni,  haukuwa wa kawaida na kwamba ulikiuka taratibu na sheria za fedha.
“Fedha zilizokusanywa zilikuwa kwa matumizi ambayo yasingehitaji uchangishaji kwa sababu yangeweza kugharamiwa na kasma zilizopo za wizara,” alisema Makani na kuongeza:
“Uchangishaji huo ulisababisha taasisi hizo kubebeshwa mzigo kwa kuwa hazina kasma mahususi kwa ajili ya kuchangia wizara kwa ajili ya maandalizi ya uwasilishaji wa bajeti bungeni”.
Alisema utafiti ulibaini kwamba Jairo akiwa Katibu Mkuu aliomba fedha kiasi cha Sh180 milioni kutoka taasisi nne ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lililoombwa Sh40 milioni, Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) Sh40 milioni, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) Sh50 milioni na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) Sh50 milioni.
Jairo, Katibu Mkuu Nishati na Madini.


Hata hivyo, kiasi kilichochangwa ni Sh140 milioni tu kutoka Tanesco, REA na TPDC wakati Ewura waligharamia chakula cha mchaka wa siku tatu pamoja na tafrija iliyokuwa imepangwa kufanyika baada ya kupitishwa kwa bajeti ambayo iliwagharimu Sh9.7 milioni.
Makani aliongeza kuwa uchunguzi zaidi ulibaini kuwa mbali na fedha hizo, kulikuwa na kiasi kingine cha Sh428.8 milioni kilichotoka katika Idara mbili za Wizara hiyo ambazo ni Idara ya Uhasibu Sh150.7milioni na Idara ya Sera na Mipango iliyotoa kiasi cha Sh278 milioni kwa ajili ya kusaidi upitishaji wa bajeti.
Alisema fedha zote hizo jumla yake ikiwa Sh568.8 milioni,  ziliingizwa kwenye akaunti ya taasisi ya GST iliyopo mjini Dodoma lakini akasema kati ya hizo, Sh150.7 milioni zilikuwa kwa ajili ya gharama za vikao na semina na kiasi kilichokuwa mahususi kwa ajili ya uwasilishaji wa bajeti bungeni kilikuwa ni Sh418.8 milioni.
Makani alibainisha kuwa maelezo waliyopewa na Wizara husika, walifikia uamuzi wa kuomba fedha hizo kutokana na fungu ambalo hutumika kwa ajili ya shughuli za bajeti kubakiwa na Sh35 milioni tu kati ya Sh207 milioni zilizokuwa zikihitajika.
Hata hivyo, alisema Wizara haikuzingatia kanuni husika za fedha katika kuomba fedha hizo, na kwamba Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo alipohojiwa na kamati hiyo, alisema utaratibu uliotumiwa kwamba si halali.
“Sababu zilizoifanya Wizara kuchangisha fedha haziwezi kutiliwa maanani kwa sababu hadi kufikia Juni 25, 2011 Wizara ya Nishati na Madini ilikwishakupata mahitaji yote ya fedha za uwasilishaji wa bajeti baada ya kupokea Sh171.5 milioni za matumizi mengineyo (OC) kutoka hazina,” alisema Makani.
Kughushi nyaraka
Kamati Teule ya Bunge pia ilibaini kwamba kulikuwa na vitendo vya kughushi na udanganyifu katika hesabu za gharama za uendeshaji wa semina ya wabunge ya Juni 26, 2011 ambayo iliendeshwa na Wizara ya Nishati na Madini.
Kamati hiyo ilibaini kuwa ili kufanikisha semina hiyo, Jairo aliziandikia tena taasisi nne ambazo ni REA, Ewura, TPDC na Tanesco kutoa Sh22 milioni kila moja na fedha zote zilikusanywa na kufikia kiasi cha Sh88 milioni, fedha ambazo zililipwa kwa mhasibu wa wizara, Hawa Ramadhani.
Alisema kwa mujibu wa barua hiyo, Jairo aliainisha kwamba bajeti ya semina hiyo ni gharama za ukumbi Sh39 milioni na posho kwa wabunge Sh46 milioni, hivyo kufanya mahitaji kuwa Sh85 milioni tofauti na kiasi cha Sh88 milioni kilichochangishwa.
Alisema maelekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Bunge kuhusu malipo hayo ni viongozi wa Bunge kulipwa Sh250,000, Wabunge Sh110,000, Wakuu wa Idara Sh80,000, Maofisa Sh50,000 na Watoa huduma nyingine Sh20,000.
“Kamati Teule ilibaini kwamba baadhi ya viwango vya posho vilikuwa tofauti na maelekezo ya Ofisi ya Bunge. Kwa mfano wakati wabunge walilipwa Sh110,000 kila mmoja, ilionekana kuwa mtumishi wa ngazi ya mhudumu alilipwa Sh120,000, badala ya Sh20,000, wakurugenzi walilipwa Sh180,000 badala ya Sh80,000 na maofisa wengine Sh150,000 badala ya Sh50,000," alisema Makani.