Naibu Waziri wa Ujenzi Dk. Harrison Mwakyembe, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kuingia ofisini humo kuanza kazi, kutokana na afya yake kuimarika. Mwakyembe amekuwa akitibiwa nchini India kwa muda mrefu. Picha na Zacharia Osanga Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe akiwa amevalia kofia ya pama alisema: “Si kwamba sijambo, bali nimepona kabisa baada ya kugundulika na maradhi hayo na kutibiwa.” BAADA ya utata wa muda mrefu wa ama Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amelishwa sumu au la, jana Mbunge huyo wa Kyela, aliweka hadharani ugonjwa wake akisema unafahamika kitaalamu kwa jina la Popular Scleroderma huku akisisitiza: “Sasa nimepona kabisa.” Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo mwaka jana yalizidi kumtikisa na Oktoba 9, Serikali iliamua kumpeleka Hospitali ya Appolo, India kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi. “Nimerudi juzi kutoka India na daktari wangu ameniambia nimepona, nilikuwa nasumbuliwa na maradhi ya ‘Popular Scleroderma’ iliyosababisha ‘skin disorder’ (ngozi kutokuwa katika hali ya kawaida), lakini kwa nguvu za Mungu nimepona, namshukuru Mungu.” Kuhusu sumu Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kulishwa sumu, Dk Mwakyembe alikataa kuzungumzia hilo akisema anasubiri uchunguzi ulioagizwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha. Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema angependa kuona uchunguzi huo unakamilika haraka na ripoti yake inatangazwa kwa umma. Alisema yuko tayari na anasubiri tume hiyo ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri Nahodha imhoji ili atoa kile kilichomo katika ripoti ya daktari wake. Dk Mwakyembe alisema anachoshukuru hadi sasa ni kwamba afya yake imeimarika kutokana na shinikizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza Serikali kumpa kipaumbele wakati wote akiwa nchini na India hatua ambayo imemwezesha kufika hapo alipo. Kutokana na hali hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka wananchi wote wakiwemo wa jimboni kwake Kyela kuondoa wasiwasi akisema sasa yupo imara kwa ajili ya ujenzi wa majukumu ya taifa. “Ninaomba wapiga kura wangu wa Kyela waache jazba, wawe na subira juu ya matatizo yangu. Wiki ijayo nitakwenda kuzungumza nao ili niweze kuwaeleza matatizo yaliyokuwa yananisumbua, lakini sasa hivi niko fit,” alisema. Mtaalamu auzungumzia Mtaalamu wa afya ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ugonjwa huo wa ‘Popular Scleroderma’ unasababishwa na chembechembe hai nyeupe kushambulia kitu kigeni kilichoingia kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya ngozi. Alisema chembechembe hizo zinaweza kusababisha ngozi ya mwili kuharibika... “Ni magonjwa yanayosababishwa na chembechembe hai nyeupe kujikataa zenyewe na kusababisha ugonjwa wa ngozi na mifupa.” Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe kuhusu ugonjwa wake imefungua ukurasa mpya hasa baada ya baadhi ya wanasiasa kuamini kuwa hakuwa na tatizo jingine bali, amelishwa sumu. Tayari Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba ambaye alitoa ripoti akisema Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu kama inavyodaiwa, amefanyia uchunguzi madai hayo na kukabidhi jalada lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ili afungue kesi. Kauli ya Sitta Mmoja wa wanasiasa waliodai kuwa Dk Mwakyembe amelishwa sumu, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alipoulizwa jana juu ya kauli hiyo mpya ya Dk Mwakyembe alisema hana cha kuzungumza. Januari 28, mwaka huu akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Dar es Salaam Sitta alisema Dk Mwakyembe amelishwa sumu. Akizungumza kwa utaratibu, Sitta alisema hana mengi ya kuzungumza kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa isubiriwe ripoti kutoka India ambako alikuwa akitibiwa. “Dk Mwakyembe si anatibiwa India?,” alihoji na kuendelea, “Nadhani umeshapata jibu, tusubiri… acha huko India waendelee na uchunguzi wao, siwezi kusema lolote zaidi ya hilo nililokuambia.” Dk Mwakyembe alianza kuugua Oktoba 9, mwaka jana na alitibiwa Apollo hadi aliporejea Desemba 11, mwaka jana. Alirejea tena India kuendelea na matibabu hadi Ijumaa iliyopita aliporudi na kusema kuwa amepona. Matatizo yake ya kiafya yamesababisha mvutano baina ya viongozi wa Serikali. Wakati Manumba akisema ripoti kutoka Wizara ya Afya ilionyesha hakupewa sumu, waziri mwenye dhamana na afya Dk Haji Mponda alimkana. Pia Waziri Nahodha ambaye ana dhamana na jeshi hilo la polisi, alikana ripoti hiyo ya DCI Manumba na kutaka aulizwe mwenyewe alikoitoa huku akisema uchunguzi alioagiza bado unaendelea |
KARIBU KATIKA BLOGU HII YA KUELIMISHA, KUBURUDISHA NA KUONYA KUPITIA MADA MBALIMBALI NA HATA PICHA. ONGEZA MAHUSIANO KWA KUJUMUIKA NA WENZIO HAPA.UNAWEZA TUMA PICHA NA MAELEZO KWA ANUANI HII;mkuu74@gmail.com
Jumanne, 20 Machi 2012
MWAKYEMBE ASEMA AMEPONA UGONJWA ULIOMSUMBUA.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni