Ijumaa, 2 Machi 2012

'ASKOFU' AKAMATWA KWA RUSHWA ARUSHA

Thomas Mollel almaarufu Askofu.
WAKATI mwanachama wa CCM, Siyoi Sumari, akitangazwa mshindi katika mzunguko wa pili wa kura ya maoni Arumeru Mashariki, mfanyabiashara maarufu mkoani hapa anayechimba, kuuza na kununua madini aina ya tanzanite, Thomas Mollel ‘Askofu’ amekamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa madiwani.

Askofu huyo ambaye pia ni Diwani wa Mbuguni, Arumeru, alikamatwa usiku wa manane wa kuamkia jana kwa tuhuma hizo zinazohusiana na kura ya maoni ambayo ilipigwa jana na kumpa Siyoi ushindi wa kura 761 dhidi ya William Sarakikya ambaye alipata kura 361.

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, iliagiza kurudiwa kwa kura ya maoni ikihusisha wagombea hao baada yao na wengine waliojitokeza kutofikisha zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Arumeru Mashariki.

Katika kura hizo, Siyoi aliongoza kwa kupata kura 361 akifuatiwa na Sarakikya aliyepata kura 259. Kamati Kuu ilifanya uamuzi huo ili kupata mgombea ambaye atapata asilimia 50 au zaidi ya hapo.

Matokeo ya jana yalitangazwa na Msimamizi, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa. Wajumbe waliopiga kura walikuwa 1,124 ambapo kura mbili ziliharibika.

Askofu akamatwa Kuhusu Askofu kukamatwa, ilidaiwa kwamba alikutwa kikaoni akishawishi madiwani kwa rushwa ili wampigie kura ya maoni Siyoi, ili apate ridhaa ya CCM kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki.

Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto, alidai kwamba hadi jana walishamkamata Askofu na watuhumiwa wengine wawili.

Kasomambuto alidai kuwapo mtandao wa kutoa rushwa na kwamba Askofu alikabidhiwa kazi ya kushawishi kundi la madiwani hao na juzi juzi kukutana na baadhi yao kwenye kikao ambacho hakikuwa rasmi wala halali.

Aliwataja wengine waliokamatwa, kuwa ni Elirehema Kaaya ambaye awali aligombea katika mzunguko wa kwanza wa kura hiyo lakini alishindwa kwa kupata kura 205.

Ilidaiwa kuwa naye alihusika kushawishi waliompigia kura awali, ili wampigie Siyoi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana. Mwingine ni Ezekiel Mollel, ambaye ni Katibu wa Jumuiya ya Vijana ya CCM Wilaya ya Monduli.

“Wote watatu tunawashikilia na wako kwa uchunguzi zaidi na ukikamilika wote watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya rushwa,” alisema Kamanda huyo.

Aliongeza kuwa Elirehema ni Katibu Mwenezi wa CCM Nyamagana ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo. Alidai kwamba mtuhumiwa huyo baada ya kuhojiwa, alikutwa na tuhuma za kupewa jukumu la kushawishi kwa rushwa wajumbe waliompigia kura katika uchaguzi wa awali wapatao 205 ili wahamishie kura zao kwa Siyoi.



Kuhusu Mollel aliyekamatwa juzi, Kasomambuto alidaiwa kwamba alikutwa Arumeru akishawishi kundi la vijana wampigie kura Siyoi. Alisema Takukuru inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine zaidi ya watatu waliokimbia kutoka kikao hicho kwenye baa ya Levis katika kata ya Maji ya Chai, Arumeru.

Pia Takukuru inashikilia pikipiki mbili zilizokutwa eneo hilo; moja ikidaiwa kuwa ya Katibu Hamasa wa UVCCM Arumeru, John Nyiti.

Kuhusu madai kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo, aliwatuma Takukuru kukamata watuhumiwa hao, Mkuu huyo wa Mkoa alisema Takukuru ni taasisi inayojitegemea na hivyo hana mamlaka ya kuiagiza kufanya kazi. Aliwataka waliokamatwa kwa tuhuma hizo wajibu tuhuma zao kwa taasisi hiyo badala ya kutafuta mchawi.

“Mimi nasema Askofu na wenzake wajibu tuhuma zao; kama umekamatwa ugoni na mke wa mtu, usiseme hapa lazima fulani anahusika kunitaja, bali jibu tuhuma za kufumaniwa usitafute mchawi, kwa Takukuru sisi sote ni wateja wake,” alisema Mulongo.

Katika hatua nyingine, CCM Mkoa wa Arusha, imemfukuza kazi Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Leguruki iliyoko Arumeru, Antony Musani, baada ya kujiunga na Chadema.

Musani ambaye amekuwa Mkuu wa Shule hiyo inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM kwa miaka mingi, amefukuzwa baada ya kupoteza sifa ya kuendelea kuiongoza.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, amethibitisha kufukuzwa kazi mwalimu huyo na kusema hawezi kuendelea kuongoza shule inayomilikiwa na CCM huku akiwa Chadema. Musani alikuwa mmoja kati ya wagombea sita wa CCM wa ubunge, wakati kura za maoni zilizopigwa Februari 20 ambapo aliambulia kura 22 kati ya 1,034.

Baada ya kushindwa kura za maoni, Musani alihamia Chadema na katika kura za maoni za chama hicho akaambulia kura nane. Imeandikwa na John Mhala na Prisca Libaga, Arusha

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni