Jumapili, 16 Oktoba 2011

SAFU-POLISI WANAPOTIA FORA KWA RUSHWA INASIKITISHA SANA.

SIKU zote tumelalamikia polisi kuwa wanaongoza kwa rushwa.

Ni sekta ambayo inaendekeza ‘mshiko’ na wakati mwingine hadi askari hao wanalitia aibu Jeshi letu zuri la Polisi.

Polisi wanadai rushwa bila ya aibu, angalia walivyomfilisi huyu mfugaji wa Iyumbu huko Singida hadi akauza ng’ombe wake 31 ili awatulize watumishi hao wa vyombo vya Dola kwa kumbambikia kesi.
Shedrack Sagati


Mzee Shigela kabambikiwa kesi na hiyo inatokana na utajiri wake lukuki wa ng’ombe alionao. Watumishi hao wa vyombo vya Dola wakaona watakula wapi zaidi kwa huyo mzee tajiri wa ng’ombe.

Wakaamua kumwingia na kumbambikia kesi kibao, mara kapatikana na fuvu na mifupa ya binadamu, mara kapatikana na ngozi ya simba na chui.

Kwa mtu wa kijijini masikini ambaye hajui sheria katika hali hiyo unadhani atafanya nini? Kisa hiki cha Singida kinasikitisha sana!

Kwamba kinawahusisha polisi wawili na raia watatu waliofanya unyama wa namna hii kuamua kumfilisi mfugaji huyo wa kijijini.

Angalia yumo Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kitongaoji na mkazi wa kijii hicho ambaye nadhani yeye kuingizwa kwenye kesi hiyo inawezekana katika eneo hilo ndiye mjuaji kuliko raia wengine.

Kashfa hii kwa polisi sio ngeni, raia wamekuwa wanalalamika kuwa polisi wanawabambikia watu kesi na hata wakilalamika kwa wakubwa wao hakuna hatua zinazochukuliwa na vigogo wa Jeshi hilo.

Mara ngapi raia wamelalamikia namna trafiki wanavyopiga mabao daladala na mabasi yanayoenda mikoani na nchi jirani.

Kuna hatua yoyote imechukuliwa? Zaidi ya trafiki kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine?

Tena ukiandika zaidi mambo ya polisi, wanakuwekea bifu kuanzia juu hadi chini na wanatafuta namna ya kukubana kama ilivyofanyika kwa paparazi mmoja baada ya kuanika uozo huo wa polisi wa Usalama Barabarani.


Hilo ndilo Jeshi tulilo nalo kwamba wale wa juu kwa kuwa hawaendi mstari wa mbele kuwakamata wahalifu au kukamata magari, wanawapa majukumu ya kupeleka mgawo kwa hao polisi wadogo.

Tunasikia kwa trafiki anayeshindwa kutimiza lengo la kukusanya mshiko anahamishwa au anapelekwa FFU.

Kwamba kupelekwa kwa kikosi hicho cha fanya fujo uone kwa polisi ni kama adhabu. Inakuwa adhabu kuwa wewe polisi badala ya kuzungumza na makondakta wa mabasi utaenda kulinda kwenye mabenki usiku na kwenye majumba ya wakubwa huko Masaki, Mikocheni na Oysterbay.

Ni katika hali ya namna hiyo trafiki hawaogopi tena kula mlungula, polisi wengine nao hawaogopi kula mlungula.

Leo mtuhumiwa akipelekwa selo ya Polisi ataingia bure lakini kutoka hadi pesa imtoke. Licha ya kuwa dhamana ni haki ya raia, lakini polisi huwezi kutoka hivi hivi kwa kuwa sheria inaruhusu hivyo.

Utawekewa mikwara mingi ambayo itakulazimu tu utoe kitu kidogo ndipo utolewe rumande. Nani anapenda aendelee kusota huko wakati pesa ni maua tu!

Hayo yanafanyika kando kidogo tu ya wakuu wa vituo ambao ofisi zao ziko karibu na kaunta za Polisi. Wanasikia mazungumzo yanavyoendelea kati ya raia na polisi husika.

Lakini hakuna anayekemea kwani hata huyo mkuu wa kituo naye kapitia huko huko. Awakemee vijana wake watakula wapi?

Eti kwa sababu mishahara na posho wanazolipwa hazitoshi kumudu maisha yao ya kila siku. Na kwa kuwa hawana muda wa kufanya biashara, kipato chao cha ziada ni lazima wakipate kwa njia haramu ya rushwa. Hilo ndilo Jeshi letu bwana.

Chombo ambacho kimepewa dhamana ya kulinda raia na mali zake. Leo tena hawa sio walinzi wa amani bali ni wabambikizaji wa kesi ili waweze kupata kitu kidogo.

Tunasubiri kwa hamu kwa polisi hao wa Iyumbu tuone hatua zitakazochukuliwa. Huwezi kujua kama huo mlungula wamekula na mabosi wao hakuna kitakachoendelea. Kesi hiyo itaenda na baadaye mfugaji huyo atapozwa kidogo na maisha yataendelea kama kawaida

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni