Jumatatu, 17 Oktoba 2011

SUKARI YA MAGENDO YAKAMATWA HIMO MOSHI.

Daniel Mjema, Moshi
MAGARI 23 yakiwamo malori na mabasi ya abiria, yamekamatwa katika Mji mdogo wa Himo wilayani Moshi Vijijini, yakiwa yamesheheni sukari na mahindi yaliyokuwa yakivushwa kimagendo kwenda Kenya.Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa kinara wa biashara ya magendo ya sukari na mahindi na hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitaka nguvu zaidi kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) kukabiliana na biashara hiyo inayosababisha uhaba wa bidhaa hizo katika soko la ndani. 

Jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Absolom Mwakyoma alisema magari hayo yalikamatwa katika maeneo mbalimbali ya mpakani katika Mji wa Himo ambako kumekuwa na operesheni maalumu ya wiki moja.

Mwakyoma alisema kukamatwa kwa malori hayo kulitokana na ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na kikosi kazi kilichoundwa na Serikali kikiwashirikisha polisi.

Kamanda Mwakyoma alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro, inatarajiwa kukutana wakati wowote kuanzia leo kuzungumzia hatima ya malori hayo na magari mengine yaliyokamatwa.

Kamanda Abasalom Mwakyoma.

“Hatuwezi kusema yatataifishwa au la, hilo ni mpaka kamati ya ulinzi na usalama ikae na kupata pia ushauri wa kisheria kwa sababu sheria ya kutaifisha mali ya mtu ina mlolongo mwingi,” alisema Mwakyoma.

Hata hivyo, sukari yote iliyokamatwa itauzwa kwa bei elekezi ya Serikali ambayo ni kati ya Sh1,700 na Sh1,900 kwa kilo.

Agizo la RC
Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliamuru kukamatwa kwa malori yote yatakayoonekana yameegeshwa katika Mji mdogo wa Himo ambao umekithiri kwa biashara ya magendo.

Mji huo unaonekana kuwa na malori mengi kupita kiasi na muda wote wa mchana yamekuwa yameegeshwa lakini usiku wa manane ndiyo yanayotumika kuvusha sukari na mahindi kwenda Kenya.

Pamoja na jitihada hizo za Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kudhibiti uvushaji wa sukari kwenda nje ya nchi, lakini bado bei ya sukari haijashuka kwani bado inauzwa hadi Sh2,600 kwa kilo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni