Jumapili, 26 Juni 2011

POLISI RUVUMA WAIBUA MTANDAO WA WASAFIRISHAJI BINADAMU.

MKONO mrefu wa Jeshi la Polisi nchini, umewanasa watuhumiwa wawili wa biashara ya kusafirisha binadamu nje ya mipaka ya nchi.

Watuhumiwa hao ni wakazi wa Bombambili katika Manispaa ya Songea mjini hapa. Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na Mwalimu wa Shule ya Msingi Makambi ya mjini hapa.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika na biashara ya kusafirisha watu, wakiwamo wanafunzi wa kike kwenda katika nchi jirani, ikiwamo ya Msumbiji.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Michael Kamuhanda ambaye amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Nolasco Mgalula (31) ambaye ni Mwalimu na Suzana Onesmo. Polisi wanasema kwamba waliwakamata watuhumiwa hao Juni 22 mwaka huu.

Alisema kuwa Jeshi la Polisi liliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa za kuwapo kwa mtandao huo kutoka kwa raia wema.

Aidha wazazi wa wasichana hao walikumbwa na wasiwasi baada ya kutowaona mabinti zao ndipo walipotoa taarifa za kupotelewa katika Kituo cha Polisi cha Songea mjini.

Kamanda Kamuhanda aliwataja kwa majina wasichana waliotoroshwa (majina tunayahifadhi) na kusema walipelekwa Msumbiji kwa lengo la kufanya biashara za kuuza baa na wengine kufanya kazi ya ukahaba katika madangulo maalumu.

Watoto waliotolewa taarifa wamebainika kuwa ni wanafunzi wa kidato cha pili katika shule za sekondari zilizopo mjini hapa.

Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili baada ya upelelezi kukamilika.

Aidha Polisi wamesema kwamba jitihada za kuwapata mabinti hao na kuwarudisha hapa nchini zinafanyika kwa kushirikiana na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Niasa nchini Msumbiji.

Alifafanua kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kuufuatilia mtandao huo kwa ukaribu zaidi ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinapingana na haki za binadamu na sheria ya elimu nchini kwa kuwa waliofanyiwa kitendo hicho ni wanafunzi.

Alitoa rai kwa wazazi na walezi wa watoto wanaosoma mkoani hapa kuwa waangalifu kwa mabinti zao kujihusisha na watu waovu hasa wakati huu ambao mwingiliano wa watu kutoka nchi jirani ya Msumbiji umekuwa mkubwa baada ya kujengwa kwa Daraja la Mkenda katika Kata ya Mitomoni, Songea Vijijini linaloziunganisha nchi za Tanzania na Msumbiji

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni