Monday, 27 June 2011
Waziri wa NIshati na Madini William Ngeleja akiwa bungeni, jana wabunge walimshutumu kuwa tokea ateuliwa katika nafasi yake hakuna alichokifanya katika wizara yake
Kizitto Noya na Habel Chidawali, Dodoma
WABUNGE wameibana Serikali na Shirika la Umeme nchini(Tanesco), wakitaka majibu ya kina kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kuhusu ukiritimba wa shirika hilo la umma, mikataba mibovu, mgawo wa nishati ya umeme na bei yake.
Hayo yalitokea jana mjini hapa wakati wa semina iliyoandaliwa na Ngeleja kwa wabunge hao kuhusu uendeshaji wa sekta ya umeme nchini.
Wabunge waliochangia mjadala huo walionyesha kukerwa na huduma mbovu za Tanesco wakieleza kuwa haziridhishi huku baadhi yao wakilalamikia bei kubwa ya umeme.
Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene alimjia juu Ngeleja na kueleza kuwa ndiye chanzo cha tatizo hilo kwa kuwa sera na mipango yake havitekelezeki.
“Kila mwaka unakuja na mipango hiyo hiyo, naweza kusema kuwa tangu Ngeleja uwe waziri, hujatusogeza hata hatua moja,”alisema.
Aliongeza:“Ngeleja huna jambo lolote ambalo umelifanya tangu ulipoingia katika wizara hii, kila siku ni michakato ambayo haina majibu. Watanzania wanataka umeme siyo porojo, acheni porojo za makabrasha ya karatasi.’’
Simbachawene, ambaye pia ni mwenyekiti wa Bunge alimwambia Waziri Ngeleja kuwa taifa linataka umeme na siyo mipango isiyotekelezeka ambayo haiwasaidii kuwaondolea umaskini wananchi
Naye Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) aliitaka Serikali ieleze kwa nini mitambo ya Dowans iliyozua mjadala mzito nje na ndani ya Bunge kutokana na kile kilichoelezwa kukosa ubora sasa inaendelea kutumika.
“Mimi nashindwa kuelewa, hivi tatizo kwenye mitambo ya Dowans ilikuwa nini? Maana tulielezwa kuwa ni mibovu na haina viwango, lakini hivi juzi alikuja Mwarabu akazungumza na Rais (Jakaya Kikwete) na sasa tunaambiwa kuwa mitambo hiyo ni bora sana…tatizo ilikuwa kweli mitambo au mtu, nataka majibu”alieleza.
Juma Nkamia, ambaye ni Mbunge wa Kondoa Kusini (CCM), alihoji mantiki ya bomba la gesi kutandazwa kutoka Mtwara hadi Tanga wakati kuna maeneo mengi njiani ikiwamo Kanda ya Kati, ambayo hayana nishati hiyo ya gesi au hata umeme.
“Kwa nini bomba litoke Mtwara lipite Dar es Salaam mpaka Tanga? Hivi Kanda ya Kati mnaionaje? Kwa nini lisipite huku? Hivi ni kwa sababu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco (William Mhando) anatoka Tanga au kwa sababu Makamba (Januari) , ambaye ni Mwenye,kiti wa Kamati ya Bunge ya Nishatianatoka huko?”alihoji.
Baada ya kauli hiyo, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage alisimama na kuomba taarifa, kisha akasema, “Sio sahihi kusema hivyo kwani Makamba na Mhando ni watekelezaji tu wa mipango siyo wapangaji. “
Mwenyekiti wa semina hiyo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Diana Chilolo alikazia hoja ya Mwijage akisema, "Utungaji wa sera unaanzia kwenye wizara na baadaye inakuja Baraza la Mawaziri na mwisho kwenye Kamati za Bunge.
Kamati ina wajumbe 27 na Makamba hawezi kuwaburuza wenzake 26,”alisema Chilolo na kuongeza:
“Na mimi ni mwanamke, mbunge kwa miaka 15 sasa. Siwezi kuburuzwa na mtu mmoja.”
Baadaye, Nkamia aliilipua Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na Maji (Ewura), akisema ni taasisi inayotumia vibaya fedha za umma kwa kulipana posho za vikao huku ikiwa haina utendaji uliotukuka.
“Posho ya ofisa wa Ewura kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni kubwa kuliko nauli ya mbunge kwenda Marekani. Mimi nimewahi kuwa mwandishi wa habari na mara kadhaa tumekuwa tukisikia Ewura wamekamata mafuta yaliyokuwa chini ya viwango. Hebu leo watuambie mafuta hayo huwa wanayapeleka wapi?”Alihoji.
Katika mchango wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR- Mageuzi) alipinga mpango wa Tanesco wa kupeleka umeme wa uhakika mkoani Kigoma mwaka 2016 akisema ni mbali mno na hiyo itaathiri mradi wa kutengeza saruji uliopangwa kuanza mkoani humo.
Alisema katika kipindi kifupi alipatikana mwekezaji kutoka Marekani, lakini alishindwa kuwekeza katika kiwanda ambacho kingezalisha saruji kwa wingi na kufanya bei ya bidhaa hiyo kupungua kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo, mbunge huyo aliwataka Tanesco kutafuta fedha hata kama ni kwa kukopa, ili kutimiza malengo yao na kwamba fedha hizo zitaingia katika utaratibu wa tozo kupitia makampuni ya simu za mikononi.
Kafulila alisema kulingana na idadi kubwa ya Watanzania wanaotumia simu za mikononi, deni hilo linaweza kulipwa ndani ya miaka mitatu.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) alitaja chanzo cha kukwama kwa maendeleo ya Tanesco kuwa ni mikataba mibovu inayoingiwa na watalaamu wa shirika hilo.
Lissu alilaani utaratibu mbovu wa shirika hilo wa kupitisha maji kwenye mabomba na umeme juu ya nguzo, lakini wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wanasikia na kuona faida kwa wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia aliitahadharisha Serikali kuhusu mpango wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Tanga akisema anaamini hawatakubali kwani wanaona mpango huo hauna faida kwao.
“Watu wa Kusini hawatakuwa tayari kuona mabomba ya gesi yakipita katika mashamba na karibu na nyumba zao wakati wao hawanufaiki na mpango huo,”alisema Ghasia.
Ghasia alisema kitendo hicho kinawakwaza na kuwavunja moyo wananchi wa maeneo hayo jambo litakalochangia kuhujumu miundombinu hiyo.
Akijibu hoja ya Mrema kuhusu Dowans, Waziri Ngeleja alisema,”Mheshimiwa Mrema, ili maisha yaende ni vyema watu wakasahau historia ile. Tuliitana majina mbalimbali, lakini sasa tunasema hivi:
“Serikali haikununua mitambo hiyo, imesema inataka umeme. Ikatokea kampuni ikaiona mitambo hiyo kuwa ni bora na kuiambia Serikali itaizalishia umeme.
"Sasa kwa kuwa sisi tunachotaka ni umeme hatuna sababu ya kuhoji tena mitambo hiyo ya Dowans,”alisema.
Ngeleja, pia alimwomba Waziri Ghasia kuwa mtu wa kwanza kuwashawishi wakazi wa Kusini ili waupokee mradi huo wa kuweka bomba la gesi kwa kuwa mipango ya Serikali inafanywa kwa awamu.
“Mipango hiyo inafanywa kwa awamu. Tunaomba ndugu zetu wa Kusini wakubali bomba lipite ili awamu hii imalizike,”alisema.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo alisema Tanesco inakabiliwana changamoto nyingi ikiwamo tatizo la mgawo wa umeme uliotokana na kupungua kwa kina cha maji katika mabwawa yanayozalisha umeme.
Alisema bwawa la Mtera litafungwa mwezi Agosti mwishoni kutokana na uhaba huo wa maji, lakini Serikali inajitahidi kuweka mipango ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya kupunguza tatizo hilo
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni