Ngassa
Calvin Kiwia na Imani MakongoroBAADA ya kupata nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Seattle Sounders ya Marekani, kiungo mshambuliaji wa Azam, Mrisho Ngassa amesema itakuwa kama ndoto katika maisha yake kucheza dhidi ya Manchester United.
Ngassa anayetajwa kuwa mshambuliaji mahiri katika kizazi hiki, anatarajiwa kuondoka nchini Julai 6, kwenda Marekani kwenye ma
Mrisho Ngassa
jaribio ya kucheza soka ya kulipwa na klabu hiyo kuanzia Julai 13 na ataivaa Manchester United inayofundishwa na Sir Alex Ferguson, Julai 20 kwenye Uwanja wa Qwest Field jijini Seattle.
Ngassa aliliambia gazeti hili jana jijini Dar es Salaam kuwa hakuwahi kufikiri hata siku moja katika maisha yake ya soka inaweza tokea kwake kucheza na dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester United na kusema lakini hiyo yote ni mipango ya Mungu.
"Ni historia mpya naweka katika maisha yangu ya soka, vile vile mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza dhidi ya klabu hiyo kubwa dunia," alisema Ngassa.
Alisema ni kama bahati kwake kupata nafasi hiyo kutokana na Tanzania kusheheni wachezaji wengi na wenye vipaji hivyo kuichukulia kama changamoto kwake kuongeza bidii katika mazoezi na kujituma zaidi.
"Sina budi kuongeza juhudi zaidi kwa kujituma katika mazoezi na kujitunza kama mchezaji, nafikiri nikizingatia yote hayo nitafanikiwa katika ndoto zangu nilizojiwekea za kufika mbali kisoka," alisema.
Alisema anaushukuru uongozi wa klabu ya African Lyon kutojali timu anayoichezea na kumpatia nafasi hiyo ya kwenda kufanya majaribio na klabu hiyo ya Marekani.
"Nafikiri uongozi wa African Lyon ni mfano wa kuigwa katika soka la nchi yetu kwa kitendo cha kiungwana walichokifanya kwangu," alisema.
Alisema uongozi huo ungeweza ukampa nafasi hiyo mchezaji wao Adam Kingwande, lakini umekubali uwezo wa Ngassa na kumpatia nafasi hiyo.
Hata hivyo aliwataka Watanzania kumuombea dua ili aweze kufuzu majaribio hayo na kujiunga na timu hiyo kwani atakuwa akiitangaza Tanzania.
Naye Makamu wa Rais wa timu hiyo, Lance Lopes, alisema kumchukua Ngassa ni kuthamini uwezo wake na mchango akiwa kwenye timu mbalimbali, ikiwamo ile ya taifa, Taifa Stars.
Alisema amekuwa akitumia akili nyingi kucheza soka, hivyo kwa kufanyiwa majaribio ya wiki mbili akiwa kwenye timu yao, hadi kwenye mechi ya kirafiki na mabingwa wa England na mabingwa mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Manchester United ni jambo la kuijivunia kwa historia ya soka Tanzania.
"Sisi kama wadau wa michezo hasa mpira wa miguu duniani, tunajisikia raha kumfanyia majaribio mchezaji wa Tanzania, Ngassa huku tukijua fika inaweza kuwa chachu kwake, ukizingatia kwamba Manchester United wataweka kambi kwetu kuanzia Julai 13, ikiwa ni maandalizi ya Ligi Kuu ya England.
"Huu ni wakati wake sasa wa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba nafasi hii anaitumia vyema, maana dunia nzima inaweza kumuona na kuthamini kipaji chake, ukizingatia kwamba yeye atakuwa mchezaji wa kwanza kufanya majaribio kwa timu kubwa inayokipiga pia na timu kubwa duniani,” alisema Lopes.
Naye Mwenyekiti wa timu ya Azam FC, Mohamed Said, alisema katika makubaliano hayo ya kumfanyia majaribio Ngassa hawajaangalia sana maslahi ya fedha zaidi ya kumuwekea ramani mchezaji wao.
Alisema endapo Ngassa anatafakiwa kufuzu kwenye timu hiyo, mafanikio yatakuwa kwa Tanzania nzima, huku akiitumia nafasi hiyo kumuasa mchezaji huyo mwenye kasi anapokuwa uwanjani.
Tumekuwa katika shauku kubwa ya kuona Tanzania inafanikiwa kuwa na wachezaji wengi duniani na kuwa na msaada na nchi, hivyo naamini uwezo wake ni mkubwa na unaweza kuwa na tija kwake.
Ni mchezaji mzuri, ndio maana amekuwa na msaada mkubwa kwenye timu mbalimbali, Azam FC, Yanga na hata anapokuwa kwenye timu ya Taifa, Taifa Stars, amekuwa akifanya vitu adimu kutokana na kipaji chake,” alisema.
Ngassa aliwahi kupata nafasi ya kufanya majaribio na klabu ya West ham ya Uingereza iliyokuwa ikinolewa na kocha Gionfranco Zola ambayo imeshuka daraja msimu huu lakini hakufanikiwa kufuzu majaribio hayo.
CHANZO; GAZETI MWANANCHI
Vijana wetu wanapojionyesha uwezo, ni furaha tele kwetu!
JibuFuta