Jumatano, 8 Juni 2011

POLISI WAUA TENA HUKO MKOANI MARA.




JESHI la polisi limedaiwa kufanya tena muaji Mugumu mkoani Mara ambapo safari hii, askari wa Kituo cha Mugumu wilayani Serengeti, wamedaiwa kumuua Nyitamboka Mwita (28) kwa  kumpiga risasi akiwa nyumbani kwake kwa madai ya kuwa ni jambazi.

Mauaji ya Nyitamboka ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyiboko, Kata ya Kisaka yaliyotokea Juni 6, mwaka huu yamekuja huku taarifa zikionyesha kuwa ni ya nne kufanywa na  polisi wa kituo hicho tangu Septemba mwaka 2010 hadi sasa.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Robert Boaz alipoulizwa alisema marehemu alitoka na panga na kumshambulia PC Sixbert kwa kukamata magazine na kumuangusha chini.Alisema  PC Rajabu akampiga risasi ya mkononi, lakini marehemu aliendelea kutaka kumshambulia na kwamba ndipo PC huyo akampiga risasi ya mgongoni iliyotokea kifuani na kumuua.

Alisema tukio hilo lilitokea saa 9:00 usiku na kwamba watu wengine wawili (majina yanahifadhiwa) walikamatwa katika msako huo. Watuhumiwa wote ni wakazi wa Kijiji cha Nyiboko na kwamba wanatuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha na kupora Tarime, Mwanza na Musoma.

Lakini mke wa marehemu, aliyejitambulisha kwa jina la  Benadeta Joseph, akisimulia mkasa huo, kwa maelezo kwamba alishuhudia tukio hilo, alisema kabla ya tukio,  saa 8;45 usiku, mumewe alitoka kwenye msiba nyumba ya jirani kwa mtu aliyetajwa kwa jina moja la Toli.

“Ghafla tulisikia mbwa wanabweka sana ikiashiria kuna watu nje ,mume wangu alilala kwa kuwa alikuwa amelewa, nikasikia milango
inagongwa kwa fujo sana, watu walisema wao ni polisi, waligonga sana bila kupumzika wengine madirishani,”alisema.

Alisema waliendelea kugonga wakisema, “wewe jambazi fungua, alikuwa uchi, nikamwamsha akakaa kitandani na kuuliza hao ni watu gani sungusungu au?, nikamwambia ni polisi akasema ngoja niende kuwasikiliza,”alisimulia Benadeta.

Shuhuda huyo aliliambia Mwananchi kuwa kutokana na kugonga kwa fujo mlango uliachia ukitaka kuanguka ambapo marehemu aliweka kiti kuzuia usianguke. Alisema kwa kuwa walikuwa wakigonga kwa fujo alitilia shaka hali hiyo na kutaka kuchukua panga, lakini aliamua kukubali kujisalimisha akiwa uchi.

“Alipotoka nje tu nikiwa nyuma yake nikasikia mlio wa risasi, mume wangu akapiga kelele wakampiga tena, akapepesuka na kuangukia nje ya uwanja,nikapiga kelele, wakapiga risasi juu na kuniamru kurudi ndani kulala,”alisema.

-Benadetha alibainisha kuwa kitendo hicho kiliwashtua wengine ambapo waliulizana, "mmempiga risasi, kwa nini mmemuua?," alisimulia.Alisema baada ya kuulizana walimmulika kwa tochi  kali na kuulizana kama ndiye waliyekusudia ambapo mmoja wa polisi hao alijibu kuwa ndiye na baada ya hapo waliita  gari la polisi aina ya pick up lililokuwa na rangi nyeusi alilodai lilikuwa limefichwa nje ya eneo lao.

"Wakati gari linaingia hapo nyumbani nililazimika kutoka na nguo ili kumstiri kwa kuwa alikuwa uchi, lakini polisi walinifukuza, walisema, unampelekea nani nguo, kwa sababu gani?, sisi tutambeba hivi hivi," alizidi kudai Benadeta akisema polisi hao walifanya hivyo wakijua mumewe ameishakufa.

Alisema hadi polisi hao walipoondoka hakuelezwa sababu za wao kuingia nyumbani kwao na kumuua mumewe, zaidi ya kumtishia kila alipotaka kujua kinachoendelea ambapo waliiondoka na kumwacha nyumbani hapo.

Hata hivyo alisema kuwa taarifa za polisi zinadai kuwa walimuua jambazi aliyekuwa wanapambana nao jambo alilosema siyo kweli.Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa taarifa hivi karibuni zilizodai mumewe anahusishwa na mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Borenga, Mchanake Maho mwezi Aprili ambaye alichinjwa na watu wasiojulikana.

“Kuna taarifa kuwa kijana mmoja anaitwa Julius alikamatwa Musoma akihusishwa na mauaji hayo na kuwa aliwataja watu mbalimbali na hata usiku kwenye tukio inasemekana ndiye aliyeulizwa kuwa ndiye huyu akakiri ndiye akiwa ameishauawa,”alisema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere DDH, Amosi Kittoh alikiri kupokea mwili wa marehemu huyo kwa ajili ya uchunguzi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni