Jumapili, 26 Juni 2011

OCEAN VIEW YACHEKA, SIMBA BADO YANUNA.

Haruna Moshi katika shikashika za mechi.

JINAMIZI la kutolewa kwenye michuano ya kimataifa bado limeendelea kuiandama Simba baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na Vital ‘O’ ya Burundi katika mechi ya michuano ya Kombe la Kagame iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Simba, wawakilishi wa Zanzibar, Zanzibar Ocean View jana walianza vema michuano hiyo kwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi Etincelles ya Rwanda.

Kwa upande wa mabingwa mara sita wa michuano hiyo Simba, wameingia uwanjani ikiwa ni wiki moja tu ipite tangu wang’olewe kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho na DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili iliyopita.

Katika mechi hiyo, Simba ilikianza kipindi cha kwanza kwa kuliandama lango la Vital ‘O’ lakini kuanzia dakika ya 35 mambo yalibadilika na wapinzani wao kutoka Burundi ndio waliokuwa wakishambulia na kukosakosa kumfunga mara kadhaa kipa Juma Kaseja.

Mchezo ulibadilika kipindi cha pili ambapo timu zilikuwa zikishambuliana kwa zamu lakini bila mafanikio ya kuzifumania nyavu.

Akizungumzia mechi hiyo kocha wa Simba Moses Basena alisema mchezo ulikuwa mzuri hasa ikizingatiwa kuwa wachezaji wake bado wana uchovu lakini anaimani watafanya vizuri mechi zijazo.

Naye kocha wa Vital ‘O’ Mousa Ally alisema ameridhika na matokeo kwa vile Simba ni timu kubwa na wamejitahidi kuibana isishinde.

“Simba ni timu kubwa na ndio maana leo tumecheza sana nyuma tukajitahidi kuibana isishinde lakini tukicheza na timu nyingine mtaona hatutacheza mchezo huu, nimefurahia kabisa matokeo,”alisema.

Nayo Zanzibar Ocean View ilipata bao lake la kwanza kupitia kwa Sabri Ramadhani katika dakika ya pili ya mchezo kwa kuunganisha pasi ya Saidi Rashidi kabla ya kuujaza mpira wavuni.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha safu ya ushambuliaji ya Etinceles ambapo katika dakika ya 23 walipata bao la kusawazisha kupitia kwa Muhir Clever.

Dakika ya 31 Sabri aliifungia timu yake bao la pili lakini Manirakiza Victorie aliisawazishia timu yake ya Etinceles bao hilo katika dakika ya 40.

Huku ikionekana mechi hiyo itaisha kwa sare, Selemani Haji aliipatia Zanzibar Ocean View bao la tatu na la ushindi katika dakika ya 85 na kuifanya timu yake iongoze kundi A ikiwa na pointi tatu ikifuatiwa na Simba na Vital ‘O’ zenye pointi moja kila moja na Etinceles ikiwa haina pointi mkiani

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni