Alhamisi, 2 Juni 2011

SEPP BLATTER ACHAGULIWA TENA FIFA.

Sepp Blatter na Afrika

Sepp Blatter ameteuliwa tena bila ya kupingwa kwa kipindi kingine cha miaka minne kuwa Rais wa Shirikisho la soka duniani FIFA.
Sepp
Sepp Blatter mara tu baada ya kuchaguliwa tena

Kuteuliwa kwa Bw Blatter kunafanyika huku kukiwa na mgogoro mkubwa ndani ya shirikisho hilo kuhusu madai ya rushwa katika mchakato wa kuwania nafasi za kuandaa michuano ya kombe la dunia mwaka 2018 na 2022.
Je, Sepp Blatter anagusa vipi soka barani Afrika? Mwandishi wetu Mohammed Allie ameandika tathmini ifuatayo kutoka Cape Town, Afrika Kusini.
Jibu la swali hili, litategemea unaongea na nani.
Nchini Afrika Kusini, Sepp Blatter anachukuliwa kuwa ama ni shujaa au ni muovu.

Ukakamavu

Wapenzi wengi wa soka wa Afrika ya Kusini wanaamini kwamba ni kutokana tu na juhudi na ukakamavu wa Rais wa FIFA ndio hatimae bara la Afrika lilipata fursa ya kuandaa michuano ya kombe la dunia mwaka uliopita; ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya miaka 80 ya michuano hiyo, na kwa ajili hiyo daima watamshukuru raia huyo wa Uswisi mwenye umri wa miaka 75.
Baada ya juhudi za Afrika Kusini kuandaa michuano ya kombe la dunia ya mwaka 2006 kushindwa katika hali ya utata mkubwa, Blatter aliazimia kuhakikisha kuwa kombe la dunia linakwenda Afrika kwa kuanzisha mfumo wa kupokezana kati ya mabara ya dunia ambapo nchi tano za Afrika zilichuana kuwania nafasi ya kutayarisha michuano ya 2010 .

Heshima

Serikali ya Afrika ya Kusini ilimtunukia Blatter heshima kuu ya Oliver Tambo kwa mchango wake wa kupeleka michuano ya kombe la dunia nchini humo.
Wengine wanaamini Blatter aliiburuza kamati ya matayarisho pamoja na serikali kujenga viwanja vipya na miundo mbinu iliyohusika na kombe la dunia vilivyogharimu fedha nyingi bila ya lazima wakati nchi ilikuwa na mahitaji mengine muhimu katika nyanja ya afya, umeme, maji na usafi.

Dikteta

Wanatoa mifano ya viwanja ambavyo havitumiki sana nchini humo kama urithi wa fedha ziliopotezwa. Wakosoaji wake pia wanamuona Blatter kuwa ni mtu mjanja na dikteta ambae aliidhibiti vilivyo Afrika ya Kusini katika kipindi kabla na wakati wa michuano ya kombe la dunia.

Hata hivyo si siri kwamba Afrika imenufaika sana wakati wa enzi ya miaka 13 ya Blatter kama Rais wa FIFA.
Ilikuwa chini ya uongozi wake kwamba uwakilishi wa Afrika katika michuano ya Kombe la Dunia uliongezeka kufikia mataifa matano na baadae kiwango cha rikodi cha mataifa sita katika michuano ya mwaka 2010 baada ya kujumuisha mwenyeji Afrika Kusini.

Mafunzo

Wakati wa utawala wake FIFA imewekeza takriban dola nusu billioni barani Afrika kupitia huduma, vituo vya mafunzo, mkiwemo viwanja vinavyoweza kutumika majira yote pamoja na mipango ya kutoa mafunzo kwa waandishi habari na maafisa wa utawala.
Kwa mfano kituo cha maendeleo cha Rwanda, kimezaa matunda yake ya kwanza kwa timu ya vijana ya chini ya umri wa miaka 17 kufaulu kushiriki katika michuano ya kombe la dunia la vijana wa chini ya umri wa miaka 17 yatakayoanza nchini Mexico baadae mwezi huu.
Mchukie mpende, Fifa chini ya Sepp Blatter imetoa mchango mkubwa kwa bara la Afrika ambao umepindukia mipaka ya kandanda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni