Jumatano, 4 Mei 2011

KUNDI LA HAMAS LALAANI MAUAJI YA OSAMA

Wamarekani wameendelea kushangilia kuuliwa kwa Osama bin Laden huku kiongozi wa kundi la Hamas la Palestina akilaani mauaji hayo. Picha na habari zaidi za jinsi Osama bin Laden alivyouliwa zimeanza kujitokeza.
Wamarekani wameendelea kushangilia kuuliwa kwa Osama bin Laden huku kiongozi wa kundi la Hamas la Palestina akilaani mauaji hayo. Picha na habari zaidi za jinsi Osama bin Laden alivyouliwa zimeanza kujitokeza.
Osama bin Laden ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda aliuliwa kwa kupigwa risasi ya jicho la kushoto baada ya kukataa kujisalimisha kwa majeshi ya Marekani.

Rais wa Marekani, Barack Obama pamoja na maafisa wake wa ulinzi na CIA walilifuatilia shambulizi la kumuua Osama bin Laden LIVE kupitia video zilizokuwa zikirekodiwa kwa kutumia video kamera zilizowekwa kwenye helmet za makomandoo wa Marekani walioivamia nyumba ya Osama.

Picha za tukio hilo zilizotolewa na televisheni ya ABC zilionyesha damu zikiwa zimetapakaa kwenye chumba ambacho Osama bin Laden alikuwemo.

Osama aliuliwa kwa kupigwa risasi kwenye jicho lake la kushoto. Maiti yake ilichukuliwa na kupelekwa kwenye kambi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan.

Baada ya vipimo vya DNA kuthibitisha kwa asilimia 99 kuwa mtu waliyemuua alikuwa ni Osama bin Laden baada ya kulinganishwa na vipimo vya DNA vya ndugu zake, maiti yake ilizikwa baharini baada ya Saudi Arabia na nchi zingine kuukataa mwili wake.

Helikopta moja kati ya nne za jeshi la Marekani zilizotumika kufanya mashambulizi toka angani, ilitunguliwa na roketi zilizorushwa na wapambe wa Osama bin Laden.

Nyumba aliyokuwa akiishi Osama ilikuwa takribani mita 200 toka kituo cha polisi na kilomita mbili toka kambi ya jeshi la Pakistan.

Taarifa ya Marekani ilisema kuwa maafisa wa Pakistan walikuwa hawajui kuwa Osama alikuwa amejificha kwenye jumba hilo lenye thamani ya dola milioni moja ambalo lilijengwa miaka mitano iliyopita likiwa na uzio mrefu wa kuta nene.

Wamarekani wameendelea kushangilia kuuliwa kwa Osama bin Laden ambaye alikuwa ndiye mtu aliyekuwa akitafutwa sana kuliko watu wote duniani.

Kiongozi wa Hamas katika ukanda wa Gazza, Ismail Haniyeh akiongelea kuuliwa kwa bin Laden alisema kuwa kuuliwa kwa bin Laden ni muendelezo wa umwagaji damu za Waarabu na waislamu unaofanywa na Marekani.

"Tunalaani kuuliwa kwa shujaa mtukufu wa Waarabu, Osama bin Laden na tunamuomba Mwenyezimungu amrehemu na kumweka mahali pema pamoja na waja wake wema", alisema kiongozi huyo wa Hamas.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni