Jumanne, 24 Mei 2011

MTU NA BINAMU YAKE WAFUNGWA MIAKA MITANO JELA.


<>
 
<>
<>
<>
<>
 

Msafara wa gerezani ukianza, ndugu wakiangua kilio.
Wakiingia kwenye gari.

Rajabu Maranda na binamu yake Farijala Hussein.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana iligubikwa na vilio vya ndugu wa waliokuwa watuhumiwa wa kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.8 za Akaunti Maalumu ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Ndugu na jamaa wa Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambao ni mtu na binamu yake, waliangua vilio baada ya Mahakama hiyo kuwahukumu kifungo cha miaka 21 jela kutokana na kupatikana na hatia ya wizi huo.

Hiyo ni hukumu ya kwanza ya kesi za Epa zinazoendelea kusikilizwa katika Mahakama hiyo na wawili hao walianza maisha hayo mapya jana.

Pamoja na hukumu hiyo, jopo la mahakimu Ilvin Mugeta, Saul Kimela na Focus Bampikya, katika kuonesha uzito wa kosa, waliwaamuru wawili hao kurejesha fedha hizo serikalini vinginevyo watafilisiwa mali walizonazo.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya wenzake, Mugeta alisema ndugu hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manane ambapo sita yalithibitishwa na upande wa mashitaka na kukutwa na hatia.

Hata hivyo, kwa kuwa adhabu katika mashitaka hayo zinakwenda sambamba, akina Maranda watatumikia jela miaka mitano.

Akifafanua kuhusu kifungo hicho, Mugeta alisema katika mashitaka ya pili ya kughushi yaliyomhusu Maranda peke yake, atatumikia kifungo cha miaka mitatu.

Kwa yale ya tatu ya kughushi pia, Mugeta alisema wote watatumikia kifungo cha miaka mitano na kwa mashitaka ya tano ya kuwasilisha hati za uongo, watatumikia miaka miwili.

Kuhusu mashitaka ya sita ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, Maranda na mwenzake watatumikia kifungo cha miaka mitatu jela huku katika mashitaka ya nane ya kujipatia ingizo la fedha kwa njia za udanganyifu, watatumikia kifungo cha miaka mitatu.

Hata hivyo, mashitaka mawili, ya kula njama za kuiba na ya wizi, Mahakama iliyaondoa kwa sababu hayakuthibitishwa na upande wa mashitaka.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, mahakimu hao walitoa nafasi kwa upande wa mashitaka kutoa maoni yao ambapo Wakili Stanslaus Boniface, alidai kuwa ingawa washitakiwa hao hawana rekodi ya hatia, ni vyema wakapewa adhabu kali ili liwe fundisho kwa wengine.

Alidai anapendekeza adhabu hiyo kwa sababu fedha walizochukua ni nyingi na akaomba pia Mahakama iwaamuru wazirudishe kwa mwenyewe, ambaye ni Serikali.

Lakini wakili anayewatetea washitakiwa hao, Majura Magafu, aliomba wateja wake wapunguziwe adhabu na kudai kuwa washitakiwa hao walifanya makosa mengi kwa kutojua.

Akifafanua hoja hiyo, Magafu alidai kwamba wateja wake hawakupata maelekezo ya kutosha kutoka kwa taasisi husika. Alitoa mfano wa hati ya kuhamisha deni iliyopelekwa BoT, ambayo ilionekana kutokuwa na shaka yoyote na ndiyo maana fedha zikatolewa na kulipwa.

Alidai pia wateja wake wana matatizo ya afya, wanasumbuliwa na figo na hivyo mara kwa mara wanahudhuria matibabu, lakini pia wana familia kubwa zinazowategemea.

Wakili Magafu alidai ingawa Mahakama hiyo iliwakuta na hatia, bado ina nafasi ya kuwapa adhabu ya kifungo cha nje na si jela au kuwapa adhabu nyingine.

Lakini Hakimu Mugeta katika hukumu yake, alisema jopo lilizingatia hoja za mawakili hao katika kutoa adhabu hiyo ya miaka 21 jela, ambayo wataitumikia kwa pamoja ili iwe onyo kulingana na makosa yaliyofanywa.

Baada ya hukumu hiyo, ndugu waliofurika mahakamani hapo walilipuka kwa vilio huku wakitolewa nje ya Mahakama na askari kuwachukua Maranda na Farijala na kuwapeleka kwenye chumba cha mahabusu kusubiri usafiri na baadaye wakapelekwa Gereza la Ukonga.

Magafu alisema nje ya Mahakama kuwa hajaridhika na adhabu hiyo, na anasubiri nakala ya hukumu aipitie na kisha atajua nini cha kufanya.

Washitakiwa walikuwa wakidaiwa kutumia Kampuni yao ya Kiloloma & Brothers kuchukua fedha za EPA wakidai kuwa wamerithishwa deni na Kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai, India. Upande wa mashitaka uliwasilisha mahakamani mashahidi tisa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni