Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SIASA. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo SIASA. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 3 Juni 2012

NAPE NNAUYE ATIKISA SONGEA LEO


Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo kimeiteka Songea baada ya umati wa wananchi wa mji huo kujitokeza katika mkutano wa hadhara wa CCM uliohutubiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye  kwenye Uwanja wa Zimanimoto mjini Songea mkoani Ruvuma. Pichani, Nape akiwasalimia wananchi baada ya kuwasili kwenye uwanja huo. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma Cornel Msuha. Pia alipata fursa ya kuongea na Jumuiya za wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo mjini Songea. (Picha na  Bashir Nkoromo)

Ijumaa, 25 Mei 2012

MNYIKA ASHINDA KESI YA UCHAGUZI, NI MBUNGE HALALI WA UBUNGO.


Mh. John Mnyika alipokuwa anawasili Mahakama Kuu jana asubuhi.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kilikuwa katika furaha baada ya Mbunge wake wa Ubungo, John Mnyika kuthibitishwa na Mahakama Kuu kuwa Mbunge halali wa Ubungo jijini Dar es Salaam.

Ubunge wa Mnyika ulikuwa unapingwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa mgombea wa CCM, Hawa Ng’humbi.

Mahakama hiyo jana kupitia kwa Jaji Upendo Msuya, ilitamka kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni halali.

Aidha, Jaji Msuya alisema maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa kwa kuwa hakuthibitisha madai yake na kutakiwa kulipa gharama za kesi hiyo aliyoifungua mwaka 2010, siku chache baada ya kubwagwa na kijana huyo.

Awali kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Mahakama hiyo jana ilijaa wanachama na wapenzi wa Chadema na CCM na kusababisha askari Polisi kufanya kazi ya ziada ya kutanda kila mahali katika mahakama hiyo na katika Barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari ili kuimarisha ulinzi.

Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Msuya mahakamani hapo kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi ambapo pia amuru gharama za kesi hiyo kubebwa na Ng’humbi ambaye kabla ya kuwania ubunge mwaka 2010, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Jaji Msuya alisema Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na kutoa ushahidi kuonesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.

Alisema Ng’humbi na mashahidi wake aliowaita mahakamani, hawakuonesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa hapo kwamba yalitendeka na namna gani madai hayo yaliathiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 31, mwaka juzi.

“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii, lakini nimeshangaa ni kwa nini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,” alisema Jaji Msuya.

Alisema hakuelewa ni kwa nini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na kuhoji kama kweli madai hayo yalitokea, ni kwa nini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba cha majumuisho hawakulalamika?

Katika madai ya Ng’humbi ya dosari ya kura zaidi ya 14,000 alizodai hazieleweki zimetoka wapi, Jaji alisema alipata nafasi ya kuhesabu kura walizopata wagombea wote wa vyama vilivyogombea jimbo hilo ambavyo ni 16 na kubaini ilikuwa ni kosa tu la kibinadamu na halina uhusiano wowote na mdaiwa wa pili, Mnyika.

Kwa mujibu wa Jaji Msuya, fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi kwa kuwa ilikosewa kuandika.

Alisema Mnyika alitangazwa kuwa ni mshindi baada ya kupata kura 66,742 wakati Ng’humbi alipata kura 50,544 na wagombea wote kuwa kura 132,496.

Jaji Msuya alisema katika ushahidi wa Ng’humbi, hakuonesha ni vipi ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na vipi Mnyika alihusika na ongezeko hilo.

Kabla ya kuanza kuchambua hoja za Ng’humbi, Jaji Msuya aliwapongeza mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na kuhoji maswali ya msingi.

Alisema mawakili hao hawakupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na msingi wala kuwasilisha pingamizi zinazosababisha shauri kuwa na mlolongo mrefu.

Mnyika aliwakilisha na wakili Edson Mbogoro wakati wakili wa Ng’humbi alikuwa Issa Maige na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwakilishwa na Justus Mlokozi.

Kuhusu madai ya Ng’humbi kuwa alidhalilishwa kwa kuitwa fisadi na Mnyika katika mkutano alioufanya katika kampeni kwamba aliuza nyumba ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu wasichague CCM inakumbatia mafisadi, Jaji Msuya alisema hayakuwa na ushahidi.

Alifafanua kwamba Ng’humbi alidai maneno hayo yalizungumzwa na Mnyika katika mkutano uliokuwa na watu zaidi ya 500, lakini yeye hakuwapo. Kutokana na kukosekana kwa uwepo wake, Jaji Msuya alisema Mahakama haichukui maneno ya kuambiwa, bali mtu aliyesikia mwenyewe au kushuhudia.

“Katika watu wote hao 500 waliokuwa katika mkutano huo, hakuja hata mtu mmoja kutoa ushahidi na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.

Kuhusu madai kwamba Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa Chadema katika kujumlisha matokeo, Jaji Msuya alisema ushahidi pekee ni wa Ng’humbi na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi.

Alisema mbali na ulinzi, hata wagombea wengine wangelalamikia jambo hilo, lakini Ng’humbi hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.

Kuhusu madai kuwa Msimamizi wa Uchaguzi alitumia kompyuta za mkononi (laptop) za Mnyika badala ya kompyuta rasmi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na pia hazikukaguliwa kiasi cha kutia shaka kuwa pengine kulikuwa na taarifa zisizo rasmi katika kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na ongezeko lile la kura 14,000, Jaji Msuya alisema ushahidi umeonesha kuwa kompyuta hizo hazikutumika.

Alifafanua kwamba kompyuta zilizotumika zilikuwa za mawakala na kwamba katika madai hayo, Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi kuthibitisha akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajab Kiravu.

“Tofauti ya kura kama nilivyosema nimepiga hesabu na nimeona kuwa ni matatizo ya kibinadam na hakuna athari yoyote katika matokeo ya uchaguzi, ni shahidi wa tatu pekee aliyekuja kutolea ushahidi hili na Ng’humbi angeweza kuleta mashahidi zaidi,” alisema Jaji Msuya ambaye alianza kuisikiliza kesi hiyo kuanzia Aprili 19, mwaka huu na majumuisho ya pande zote yalifanywa Mei 4, mwaka huu.

Baada ya hukumu hiyo, Mnyika alikumbatiana na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye alikuwapo mahakamani hapo. Pamoja walitoka nje, Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema wakiimba na kushangilia kwa ushindi huo.

Hata hivyo, hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.

Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi ya Sh bilioni mmoja na kutaka kabla ya kusikiliza kesi kama hiyo, uchunguzi ufanyike kwanza ili ikionekana haina hoja za msingi, itupwe mapema.

“Mahakama imetenda haki na hii inaonesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani,” alisema Mbowe.

Naye Ng’humbi alisema amepokea uamuzi uliotolewa, lakini hawezi kusema lolote kwa sasa na kuwataka wana CCM wawe na utulivu kwa sababu anaamini ni watulivu na kama kuna jambo tofauti, atazungumza baadaye.

Hadi sasa, Mahakama imekwisha kutengua matokeo ya ubunge ya mwaka 2010 katika majimbo mawili pekee, Arusha Mjini kwa Godbless Lema wa Chadema na Sumbawanga Mjini lililokuwa la Aeshi Hilary wa CCM.

Majimbo ambayo kesi zao zilitupwa na mahakama na wabunge wake kuendelea na nafasi zao ni Segerea, Kasulu Mjini, Biharamulo, Singida Mashariki, Ilemela, Nyamagana, Kilwa Kusini, Muhambwe na Meatu

Ijumaa, 4 Mei 2012

RAIS J KIKWETE AMETANGAZA BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI MUDA MFUPI ULIOPITA, MANAIBU WAZIRI FEDHA NI WANAWAKE WAWILI


Dk J. Kikwete, Rais ametangaza Baraza jipya la Mawaziri leo.

Ifuatayo ni Orodha ya Mawaziri kamili waliobadilishwa tu au wapya walioteuliwa.
1.Shamsi Vuai Naodha-Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
2.Hussein Mwinyi- Afya
3.Chikawe Mathias-Katiba na Sheria
4.Emmanuel Nchimbi-Mambo ya Ndani
5.George Mkuchika- Utawala Bora
6.Dk. Chizza- Kilimo , Chakula na Ushirika.
7.Prof. J. Magembe-Maji.
8.Dk. Mwakyembe-Uchukuzi
9.Dk. Finela Mkangala- Habari, Vijana na Michezo.
10.Balozi Kagasheki Hamis- Maliasili na Utalii.
11.Dk. Kigoda-Viwanda
12.Dk. William Mgimwa- Fedha
13.Prof. Mwandosya- Waziri asiye na Wizara Maalum Ofisi ya Rais.
14.Dk. Sospeter Mgongo-Nishati na Madini.

Ijumaa, 6 Aprili 2012

ALIYEKUWA MBUNGE WA ARUSHA MJINI BW. LEMA HAIAMINI MAHAKAMA!!? IKULU YASEMA KAULI YAKE NI YA KIPUUZI.


Bendera ya Rais wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu
 Ikulu ya Tanzania imesema kuwa kauli aliyoitoa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juu ya kuihusisha Ikulu na Rais Jakaya Kikwete katika kesi hiyo ni ya kipuuzi.
IKULU
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema Rais Kikwete wala Ikulu haijawahi kuingilia kesi yake kwa namna yoyote ile, na wala haijawahi kutokea hata kwa kesi zingine zozote.
“Kwa hakika, haijapata kutokea Kikwete, tokea alipoingia madarakani, Desemba 21, 2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile, mwenendo wa kesi yoyote ile katika Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya hivyo wakati wote wa muda wake uliobakia wa uongozi,” ilisema Ikulu katika taarifa hiyo.
Aidha imeainisha kuwa si kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo.
Katika mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amedai kuwa Jaji Gabriel Rwakibalira imetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Ikulu.
“Kauli hii ya Lema ni upuuzi. Sio Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati kesi yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na Jaji Rwakibalira…Siyo kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo,” imefafanua taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa kauli ya Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa Mahakama ambao ni muhimili huru usioingiliwa na Serikali ama na Muhimili mwingine katika maamuzi yake. Lema amekuwa kiongozi kwa muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo hili kubwa na muhimu katika mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.
“Ni jambo lisilokuwa na mshiko wala tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Lema anajaribu kuingiza mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la kisheria ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Lema asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kumbebea msalaba huu. Badala ya kutafuta mchawi asiyekuwepo, ni vyema Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa hakutendewa haki akate rufani kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tunaomba wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu wa kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe.” Imeeleza taarifa

Jumamosi, 31 Machi 2012

WAZIRI EMMANUEL NCHIMBI KATIKA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA LIZABONI HUKO SONGEA JUZI.

DKT EMMANUEL NCHIMBI MBUNGE WA SONGEA MJINI NA WAZIRI WA HABARI UTAMADUNI NA MICHEZO ATINGA KAMPENI ZA UDIWANI KATA YA LIZABONI MANISPAA YA SONGEA

 Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo aliyesimama kushoto kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni juzi.
 Mamia ya wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni juzi.
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Dkt Emmanuel Nchimbi akimnadi mgombea wa Udiwani wa Kata ya Lizaboni, Manispaa ya Songea kupitia CCM  George Oddo kwenye mkutano uliofanyika kwenye ofisi za CCM kata ya Lizaboni juzi.(Habari na picha kwa hisani ya Stephano Mango)

Jumatano, 28 Desemba 2011

MAHAKAMA YASEMA KAFULILA BADO MBUNGE HALALI

MAHAKAMA Kuu imetoa amri kusitisha kutekelezwa kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya
Chama cha NCCRMageuzi wa kumfukuza uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila
hadi kesi aliyofungua itakapomalizika.

Uamuzi huo ulitolewa jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Jaji Alise Chingwile kutokana na maombi ya zuio yaliyowasilishwa na Kafulila kupitia Kampuni ya Uwakili ya Asyla ya Dar es Salaam.
David Kafulila
Wakili wa Kafulila kutoka kampuni hiyo, Daniel Welwel alisema maombi hayo waliyawasilisha Ijumaa iliyopita chini ya hati ya dharura, kupinga kuvuliwa uanachama.

Kwa mujibu wa Wakili huyo, katika maombi hayo, walidai kwamba uamuzi huo wa NCCR-Mageuzi ukitekelezwa dhidi ya Kafulila atakuwa amekosa sifa za ubunge na jimbo litakosa mbunge.

“Tukasema na kesi ya msingi itakuwa haina maana,” alidai Wakili wa mwanasiasa huyo kijana
aliyewahi pia kuwa mwanachama na kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika kesi ya msingi ambayo itatajwa Februari 21, mwakani, Kafulila kupitia kwa mawakili wake, anadai uamuzi wa NCCR Mageuzi haukuwa halali kwa sababu Katiba ya chama hicho haikufuatwa.

Vile vile anadai hakupewa haki ya kusikilizwa licha ya kwamba ni haki yake ya msingi.

Anadai pia kwamba wajumbe walioshiriki kupitisha uamuzi huo, wengine hawakuwa wajumbe halali.

Watu wanaomuunga mkono pamoja na walio karibu na mbunge huyo, akiwemo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), wameelezea kufurahishwa na uamuzi huo wa Mahakama.

“Kafulila kuendelea na ubunge..... Mahakama Kuu imetoa amri muda mfupi uliopita.

Ataendelea kuwa Mbunge mpaka hapo kesi ya msingi itakapokwisha. Mungu yupo pamoja na wanyonge siku zote,” alisema Zitto kupitia mtandao wa kijamii.
.”

Awali, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alikiri kwamba ofisi imekwishapokea barua ya
NCCR Mageuzi ya kumvua ubunge Kafulila na kwamba inafanyiwa kazi, ingawa hakuna muda maalumu wa kutenda kazi hiyo

Jumanne, 20 Desemba 2011

BAADHI YA WANANCHI WALAUMU KAFULILA KUFUKUZWA UANACHAMA NCCR

Mh. D. Kafulila


Mbunge huyo alionekana anastahili adhabu hiyo baada ya kupitia tuhuma nzito zilizotolewa juu ya Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia
Wajumbe walipokea na kujadili kina na kura zikapigwa na kuonekana mbunge huyo kutokuwa na imani na mwenyekiti wake na kwenda kinyume na taratibu za chama hicho.

Mbali na kuvuliwa uanachama kwa mbunge huyo pia Hashim Rungwe aliyewahi kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 nae amevuliwa uanachama.
Hivyo kwa kuvuliwa uanachama kwa mbunge huyo kwa mujibu wa sheria jimbo hilo litakabiliwa na uchaguzi mdogo kupatikana kwa mbunge

Kufuatia sakata hilo, msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amelaani vikali na kukitupia lawama chama hicho kwa kitendo cha kumvua uanachama mbunge huyo na kuita kitendo hicho ni cha kukomoana na kusababisha gharama zisizo za lazima kwa Taifa kugharamia Uchaguzi Mdogo katika jimbo hilo

Kwa upande wa Chama cha Chadema kimemkaribisha mbunge huyo kijana machachari kujiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa NCCR-Mageuzi.
"Milango yetu ipo wazi kwa mujibu wa Katiba, Kanuni na taratibu za chama chetu,"kilisema chama hicho

Hata hivyo baadhi ya wananchi nao walilaani kitendo hicho cha kumvua uanachama mbunge huyo ambaye alikubalika jimboni kwake kuokana na harakati zake za kutetea wanaanchi wa jimbo lake na kitendo hicho kimeonekana na sawa na kuwanyanyasa wananchi wa jimbo hilo

Ijumaa, 16 Desemba 2011

CUF NA NCCR MMEPATWA NA NINI!!?



Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed

Waandishi Wetu
WAKATI uongozi wa CUF, ukiwa bado haujamwita kwenye Kamati ya Maadili, Mbunge  wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema hatishwi na kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya chama chake cha NCCR-Mageuzi, kinachotarajiwa kuketi kesho kumjadili kama inavyodaiwa.
CUF na NCCR- Mageuzi vimekuwa katika migogoro ya ndani kwa muda mrefu na kadiri siku zinavyosonga mbele, migogoro hiyo inaonekana kuendelea kukua kiasi cha kutishia uhai wa vyama hivyo vya upanzani.
Upande wa CUF
Wakati uongozi wa chama hicho ukiwa bado unasuasua kumpa barua ya wito Hamad kama ilivyoahidiwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Julius Mtatiro, wanachama 4,000 wa chama hicho Kata ya Manzese, jijini Dar es Salaam wameonya kwamba kitendo cha kumzuia mbunge huyo kufanya mikutano, kinaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama.
Mtatiro jana aliliambia gazeti hili kuwa chama hicho bado hakijampekelea barua Hamad  kumwita kwenye kikao hicho cha maadili, lakini mpango wake huo, haujabadilika.
"Bado tutampelekea tu na tutamuita  katika Kamati ya Maadili ya chama muda wowote  kuanzia sasa,”alisema Mtatiro.
Akieleza sababu za kumwita mbunge huyo pekee na sio Maalim Seif Sharif Hamad, Mtatiro alisema Hamad Rashid, ndiye aliyeanza kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza matatizo yake aliyonayo ndiyo maana uongozi ukabaini kwamba kuna kila sababu za kumuita na kuzungumza naye.
Alisema baada ya kumwandikia barua,  vikao vya ndani vya chama vitakaa na kumhoji na maamuzi yatakayotafanyika kikatiba ndio yatakayoamua hatima yake. “Vikao vya ndani ndivyo hasa vitakavyojua  hatma ya Hamad Rashid na sio mimi. Kwa kweli siwezi kukueleza chochote kile sasa hivi,”alisema
Wakati chama kikipanga kumwita, Hamadi mwenyewe amezungumzia hatua hiyo kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba akieleza kuwa kimsingi alipaswa kuitwa katika vikao vya chama na sio kuhukumiwa na kushutumiwa kupitia vyombo vya habari.
Kauli ya mbunge huyo wa Wawi ilikuja baada ya Mtatiro kutoa kauli kwenye mkutano na wanahabari akidai kuwa kitendo cha Hamad kufanya mkutano na wanachama wa Tawi la Chechinya, Manzese  bila kibali  cha chama ni kwenda kinyume na taratibu.
Wananchama 4,000
Wakati uongozi huo  wa CUF ukisuasua kumpa barua Hamad wanachama 4,000 wa Kata ya Manzese jijini Dar es Salaam, wameonya kuhusu kitendo cha kumzuia mbunge huyo kuendelea na mikutano yake.
Wanachama hao waliyasema hayo jana kufuatia mbunge huyo kushindwa kukabidhi msaada wa samani za ofisi ya kata hiyo alizopaswa kuzikabidhi Desemba 11 mwaka huu, lakini akazuiwa na ulinzi wa chama hicho wanaojulikana kama Blue Guard.
Katibu wa Kata hiyo, Hamdan Kulangwa alisema kitendo cha mbunge huyo kuzuiwa na walinzi wa chama hicho kinakiuka taratibu za chama na hivyo kuwasikitisha sana wapenzi na wanachama wake katika kata hiyo.
“Sisi tulimwalika Hamad Rashid aje atukabidhi msaada wa samani za ofisi ambazo tulimwomba atusaidie, lakini siku ya tarehe 11 Disemba, alipofika kabla hajaanza kufanya lolote lilikuja kundi la Blue Guard na kumzuia kuzungumza na sisi,” alisema Kulangwa
Kafulila: Sina hofu kikao cha NEC
Wakati upepo ukivuma vibaya ndani ya CUF, NCCR nako mambo bado magumu baada ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kusema kuwa hana hofu na kikao cha NEC ya chama hicho inayoketi  kesho.
Kafulila ambaye anadaiwa kuzungumza mambo ya ndani ya chama katika vyombo vya habari pamoja na kupingana wazi wazi na mwenyekiti wake, James Mbatia kinyume alisema  hana wasiwasi kwa kuwa mpaka sasa hakuna ajenda zilizowekwa wazi juu ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho.
Kafulila alisema, “Mimi ni mjumbe wa kikao hicho na nitakuwepo, ila mpaka sasa sijaelezwa ajenda…, hili ni jambo dogo na kila kitu kitajulikana katika kikao, nadhani kikao kitajadili mambo mbalimbali,” alisema Kafulila.
Alipoulizwa hoja atakazoziwasilisha iwapo atajadiliwa katika kikao hicho, Kafulila alisisitiza kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa mpaka sasa hajui nini kitakachojadiliwa.


Imeandaliwa Fidelis Butahe, Hussein Issa na Aidan Mhando

Jumamosi, 10 Desemba 2011

JESHI LA WANANCHI WA TANZANIA LASHIRIKI KUADHIMISHA MIAKA HAMSINI YA UHURU WA TANGANYIKA.

MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA ILIVYOADHIMISHWA NA JESHI LA WANANCHI (JWTZ)

Mara baada ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Dk. Jakaya Kikwete kukagua vikosi vya ulinzi na usalama na vikosi hivyo kutoa heshima kwa Amiri Jeshi Mkuu huyo, kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania leo katika uwanja wa Uhuru, yalifuatia maonyesho ya vifaa vya kijeshi vilivyoonyeshwa na jeshi tukufu la Tanzania JWTZ, ambapo askari wa jeshi hilo wakiwa wakakamavu, walipita na kuonyesha vifaa vya kivita kama linavyoonekana na gari hili ni la Rada hutumiwa na jeshi la wanamaji likiwa na
Haya ni Magari maalumu yanayotumiwa na wanajeshi wa majini kama yanavyoonekana.
Haya ni magari ya kulinda amani katika programu za umoja wa mataifa.
haya ni magari ya makombora ya masafa marefu.
Vifaru vinavyopiga masafa marefu.
Vifaru vya Doria
Magari haya maalum pia ni kwa ajili ya Doria
Hili ni gari maalum kwa ajili ya madaraja
Hili ni gari lililotengenezwa na kiwanda cha Nyumbu kinachomilikiwa na JWTZ.
Hili ni gari lililotengenezwa na kiwanda cha Nyumbu kinachomilikiwa na JWTZ ambalo kazi yake kubeba mizigo.
Credits; Fullshangwe

Ijumaa, 9 Desemba 2011

PONGEZI WATANZANIA KWA KUADHIMISHA MIAKA HAMSINI YA UHURU WA TANGANYIKA LEO, TUZIDISHE JUHUDI KATIKA KUFANYA KAZI ILI TUJILETEE MAENDELEO.

Tarehe 09/12/1961 Tanganyika ilikabidhiwa madaraka kamili ya kuiongoza nchi yao toka kwa wakoloni wa Kiingereza, Mwalimu J K Nyerere akateuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru, baadaye 1962 akawa Rais wa kwanza wa Jamuhuri ya Tanganyika kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar 26/04/1964.

Tulinde amani na kuuenzi umoja wetu tunaojivunia kwa miaka mingi, tukumbuke historia wapi tumetoka na wapi tunaelekea, Mungu Ibariki Tanzania na watu wake. Amina.


Jumatano, 30 Novemba 2011

RAIS KIKWETE ATIA SAINI MSWADA WA KUUNDWA TUME YA KURATIBU UUNDWAJI WA KATIBA MPYA.

RAIS Jakaya Kikwete ametia saini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Kikwete alisaini muswada huo jana, ikiwa ni siku 11 tangu upitishwe na Mkutano wa Tano wa Bunge la 10 mjini Dodoma, Novemba 18, mwaka huu.

Hatua hiyo ya Rais kutia saini Muswada huo inakamilisha safari ya kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 baada ya Bunge kuwa limepitisha Muswada huo.

“Aidha, kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

“Pamoja na kutiwa saini hiyo, bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo.

“Hivyo, Mheshimiwa Rais Kikwete anatoa wito kwa mwananchi yeyote mwenye maoni ama mawazo ya namna ya kuboresha Sheria hiyo, ajisikie yuko huru kutoa maoni yake na Serikali itasikiliza na kuchukua hatua zipasazo,” iliongeza taarifa hiyo ya Ikulu.

Aidha, Rais Kikwete ametia saini Muswada huo siku moja baada ya kuwa amekutana kwa siku mbili mfululizo na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambao waliomba wakutane naye na kuzungumza kuhusu Muswada huo wenye kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Jumapili na Jumatatu, Rais Kikwete na baadhi ya watendaji wake na Chadema kwa upande mmoja, walikuwa na mazungumzo kuhusu Muswada huo ambao ulipitishwa na Bunge bila ushiriki wa wabunge wa Chadema na wa NCCR-Mageuzi ambao walisusa.

Kususia mjadala wa Muswada huo kwa wabunge hao wa vyama hivyo, ulitokana na madai yao ya kutaka Muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni wakidai haukuwa umesomwa na wananchi na kuuelewa, hivyo kukosa kuuchangia, lakini walikataliwa na Spika Anne Makinda.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa Ikulu juzi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi na Kaimu Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika, kutakuwa na haja ya sheria hiyo baada ya kusainiwa kuendelea kuboreshwa, ili ikidhi mahitaji ya kujenga na kuaminiana na mwafaka wa kitaifa.

Pia kutakuwa na mawasiliano na mashauriano ya mara kwa mara kati ya Serikali na wadau mbalimbali juu ya kuboresha sheria hiyo kwa lengo la kudumisha mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya.

Awali ilielezwa kuwa mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira ya uelewano ambapo Rais Kikwete aliwahakikishia Chadema kuwa yeye na Serikali yake wana dhamira ya kuhakikisha Tanzania inapata Katiba mpya.

Jumatatu, 24 Oktoba 2011

RUSHWA YA NGONO YATUMIKA ILI KUPATA UONGOZI

 
Utafutaji wa vyeo kama ubunge na vingine vya maofisini miongoni mwa wanawake wasiojiamini, ni sababu kubwa ya kuendelea kuwepo kwa rushwa ya ngono nchini. 
Mh. Hilda Ngoye.

 Aidha, imeelezwa kuwa matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na baadhi ya wanaume ni kichocheo kingine cha rushwa hiyo, inayochangia nchi kuwa na viongozi wasio na uwezo, maadili mema, kwa asilimia kubwa.

Akizungumza wakati wa mkutano wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi iliyokutana Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, kujielimisha kuhusu unyanyasaji wa jinsia nchini, Mbunge wa Viti Maalum, Hilda Ngoye (CCM) alisema rushwa hiyo ipo na inarindima hata kwa wabunge.

Huku akiungwa mkono na Waziri Kivuli wa Afya na Ustawi wa Jamii, ambaye pia ni Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CHADEMA), Dk.Gervas Mbassa, Ngoye alisema anachokizungumza kinafanyika si tu katika kuutafuta ubunge, bali hata katika kutafuta vyeo maofisini.

Wakati akisema hayo, Mbunge wa Viti Maalu, Margret Mkanga (CCM) alishtuka kwa mshangao ulioashiria kuisikia habari hiyo kwa mara ya kwaza na ndipo Ngoye alipomwambia, “Usishangae! It is a practical example, akimaanisha kuwa alichokizungumza ni mfano hai uliopo.

Kwa upande wake, Mbassa aliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo ipo kweli na kwamba inatokana na kukosa utu miongoni mwa wanaoomba na wanaotoa rushwa ya ngono.

Alisema, wengi wanaojihusisha na rushwa hiyo na kushindwa kupata wanachokitaka huishia kuaibika au kupata maambukizi ya VVU huku walioigawa na kuupata uongozi wakiiharibu nchi kwa njia tofauti kutokana na kukosa maadili ya uongozi pamoja na uwezo wa kazi, “Alichokisema Ngoye ni sahihi kabisa, rushwa ya ngono ipo hata kwa wabunge. Lakini pia ipo katika nyanja zingine ambazo si za siasa. Watu wanataka uongozi wakati wanajua hawana uwezo na matokeo yake wanaamua kutumia miili yao. “Ufike wakati Watanzania tuikatae na kuthamini utu vinginevyo nchi itajaa viongozi watakaotusababishia matokeo mabaya,” Ndassa alisema.

Wakati huo huo, baadhi ya wabunge wanaounda kamati hiyo wamewataka wanafunzi wanaoombwa rushwa ya ngono kutoa taarifa kwa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili wahusika wakamatwe na kushitakiwa, kwa sababu kitendo hicho, licha ya kuwa kosa la jinai, kinatumiwa na wengi kusambaza VVU.

Mbunge wa Viti Maalum, Rosweeta Kasikila (CCM) na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), walisema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakitoa michango yao, kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, unaohusisha ngono nchini.

Kasikila ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema kuwa wanafunzi ni waathirika wakubwa wa rushwa ya ngono na kwamba wanahitaji kupewa elimu zaidi juu ya athari za rushwa hiyo ya ngono kwa watu mbalimbali wanaowarubuni ili waikatae na kuwaripoti wanaowashawishi kuishiriki, “Wapo wasichana na hata wavulana jasiri wanaowaeleza maofisa wa Takukuru kuhusu kuombwa rushwa ya ngono na hivyo kuandaa mitego inayowezesha kunaswa kwa wengi wao na kushitakiwa.

Hiyo ni njia mojawapo inayoweza kusaidia kupunguza kuenea kwa maambukizi ya VVU ambayo wengi wao huyapata wanaposhiriki kujamiiana huko”, Kasikila alisema.

Naye Shelukindo alisema kuwa wanafunzi wanastahili kujengewa ujasiri wa kuwaeleza wakubwa wao na taasisi zinazoshughulikia masuala ya haki zao ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa dhidi yao, kama vile kuhisishwa katika masuala ya kujamiiana kwa kurubuniwa kupata wanachokihitaji.

Alisema, rushwa ya ngono haistahili kuwepo mahali popote pale kwa kuwa ni njia mojawapo inayochochea maambukizi kutokana na ukweli kuwa mara nyingi wahusika wanaoishiriki hawapati muda au kukumbuka kutumia kinga kama kondomu.


source: http://www.wavuti.com/

Ijumaa, 7 Oktoba 2011

MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU HUKO BUTIHAMA MUSOMA.


WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk Emmanuel Nchimbi (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kutoka kwa maofisa wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) katika banda la kampuni hiyo kijijini Butiama mkoani Mara, kwenye maonesho ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya wizara ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Pembeni mwa Waziri ni Meneja Uchapishaji, John Mcharo aliyemwakilisha Mhariri Mtendaji katika maadhimisho; wanaotoa maelezo ni ofisa Usambazaji wa TSN, Judith Ngomo (wa kwanza kulia) na Ofisa Masoko na Mauzo, John Koyi (Picha na Stella Nyemenohi).


Jumapili, 2 Oktoba 2011

LEO NDIO LEO IGUNGA, ASIYE NA MWANA AELEKE JIWE, NANI ATAIBUKA KIDEDEA UGOMBEA UBUNGE IGUNGA!!!?


Akina mama wa kijiji cha Isekenese wakimshangilia mgombea ubunge Jimbo la Igunga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Dalaly Kafumu wakati akiruka kwa helkopta baada ya kuwahutubia wananchi wa kijiji hicho. (Na Mpigapicha Maalumu).

Jumamosi, 1 Oktoba 2011

HII NDIO HOTUBA YA RAIS YA KILA MWISHO WA MWEZI-SEPTEMBA 2011

Ndugu Watanzania Wenzangu;

Kwa mara nyingine tena naomba tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima, na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. Mwezi huu tunaoumaliza leo ulijawa na mchanganyiko wa mambo, yalikuwepo mambo ya furaha na ya majonzi.

Tuliuanza mwezi kwa sherehe za Eid El-Fitr, kuadhimisha kumalizika kwa swaumu ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Nafurahi kwamba sherehe hizo zilifana na kuisha salama.

Lakini, usiku wa tarehe 10 Septemba, 2011 katika mkondo wa bahari wa Nungwi, Zanzibar kulitokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander iliyokuwa na watu wengi na shehena kubwa ya mizigo. Mara baada ya taarifa ya ajali kutufikia hatua zilichukuliwa za kuokoa watu, meli na mali iliyokuwamo. Bahati nzuri ndugu zetu 619 waliweza kuokolewa wakiwa hai na sasa wanaendelea na shughuli zao za ujenzi wa taifa na kujiletea maendeleo yao. Maiti 203 waliweza kupatikana na kuzikwa kwa heshima. Maiti 197 walipatikana
eneo la tukio, tano walipatikana Kenya na mmoja Tanga. Maiti waliopatikana eneo la tukio walizikwa Unguja na wale waliopatikana Kenya na Tanga walizikwa huko huko.

Meli iliyozama haikuweza kuopolewa. Wataalamu wa uzamiaji wanasema ipo kwenye kina kirefu cha mita 300 ambacho hawakuweza kuifikia. Wao walifikia mita 58 tu. Wametushauri kuwa haitakuwa rahisi kuifikia meli hiyo, hivyo tukubali kuwa ndiyo makazi yake ya kudumu na vyote vilivyokuwamo ndani yake.

Kwa kweli hatujui kwa uhakika kama wapo watu waliozama pamoja na meli hiyo au hapana. Bahati mbaya idadi kamili ya watu waliokuwamo katika meli hiyo haijulikani kwa uhakika. Orodha rasmi ya wenye meli inaonesha idadi ya watu waliokuwemo kwenye meli wakati inaondoka bandari ya Malindi, Zanzibar kuwa
pungufu kuliko idadi ya watu waliookolewa na maiti waliopatikana. Kwa sababu hiyo, huenda wapo watu waliozama na meli na kushindwa kutoka.

Ndugu Wananchi;

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein amekwishaunda Tume ya Uchunguzi ambayo baada ya kumaliza kazi yake ndipo undani kuhusu ajali hiyo utapoweza kujulikana. Tume hiyo imekwishaanza kazi na kama kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, baada ya mwezi mmoja wataimaliza kazi hiyo. Napenda kutumia fursa hii kuwaomba watu mwenye taarifa zinazoweza kufanikisha kazi ya Tume hiyo wafanye hivyo.

Kwa mara nyingine tena narudia kutoa mkono wa pole na rambirambi kwa ndugu zetu waliopoteza ndugu na jamaa zao katika ajali ile. Nawaomba waendelee kuwa na moyo wa subira na sisi wengine tujumuike nao kuwaombea marehemu wapate mapumziko mema. Kwa walionusurika tunaendelea kuwapa pole na
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaponya.

Ndugu Wananchi;

Narudia kutoa pongezi maalum kwa vyombo vyetu vya usalama na wale wote walioshiriki kuokoa maisha ya ndugu zetu waliozama na kuwaopoa maiti. Natoa pongezi za pekee kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamu wake wawili kwa uongozi wao thabiti. Aidha, nawapongeza sana viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wa Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya tangu kutokea kwa ajali, jitihada za uokoaji, maiti kuzikwa, majeruhi kutibiwa na kurejea makwao na kuwafariji wafiwa na walionusurika.

Mwisho, lakini siyo mwisho kwa umuhimu, nawapongeza sana wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kwa moyo wao wa upendo, ustahamilivu na mshikamano waliouonesha katika maafa haya ya kitaifa.

Safari ya Marekani

Ndugu Wananchi;

Kati ya tarehe 16 na 23 Septemba, 2011 nilifanya ziara ya kikazi nchini Marekani. Nilikwenda kuhudhuria Kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na shughuli zake. Pamoja na hayo nimehudhuria mikutano mingine kama vile  Mkutano wa Open Government, ulioitishwa na Rais Barrack Obama wa
Marekani,Mkutano wa Umoja wa Marais wa Afrika wa kupambana na malaria ,Mkutano wa Tatu wa Watanzania Waishio Marekani (DICOTA 3) na mkutano kuhusu Wanawake na Lishe ulioandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mama Hilary Clinton. Aidha, mimi na Waziri Mkuu, Stephem Harper wa Canada tulipata nafasi ya kuwasilisha taarifa ya Tume ya Afya ya Mama na Mtoto aliyoiunda Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambayo tulikuwa Wenyeviti wenza. Nafurahi kwamba taarifa yetu imepokelewa vizuri na kuelezwa kuwa itakuwa msingi mzuri wa kutatua matatizo ya vifo vya kina mama na watoto duniani.

Katika hotuba yangu kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, nilieleza jinsi nchi yetu ilivyoshiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa katika miaka 50 ya Uanachama wetu ambayo pia ndiyo miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Nchi yetu inayo historia iliyotukuka kwamba, pamoja na udogo na umaskini wetu, tumetoa mchango muhimu katika shughuli za Umoja wa Mataifa za kudumisha amani na usalama wa dunia na kuleta maendeleo. Tunayo fahari kwa mchango tuliotoa mpaka sasa. Niliwaahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Mataifa na
kuendelea kutoa mchango wake ipasavyo.

Maradhi Yasiyoambukiza

Ndugu Wananchi;

Katika kikao cha mwaka huu cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kulifanyika mkutano maalum kuhusu maradhi yasiyoambukiza kama vile kisukari, moyo, shinikizo la damu, figo na saratani. Kwa muda mrefu dunia imejishughulisha na maradhi yanayoambukiza kwa vile yamekuwa yanaua watu wengi, kwa mfano
malaria, UKIMWI, kifua kikuu n.k. Lakini, ni ukweli ulio wazi kwamba siku hizi maradhi yasiyoambukiza nayo yamekuwa chanzo kikubwa cha watu wengi kupoteza maisha.

Kwa kutambua ukweli huo, imeonekana upo umuhimu kwa Umoja wa Mataifa kujihusisha kwa karibu katika kupambana na maradhi hayo kama inavyofanya kwa maradhi ya kuambukiza. Baada ya mkutano maalum wa tarehe 19 – 20 Septemba, 2011, tutegemee mabadiliko makubwa yenye tija na manufaa kwa wanadamu katika kukabiliana na maradhi haya.

Ndugu Wananchi;

Kwa kushirikiana na nchi za Australia na Sweden, nchi yetu ilidhamini na kuongoza mjadala kuhusu maradhi ya kinywa ambayo ni sehemu ya maradhi yasiyoambukiza yanayoathiri watu wengi. Katika mkutano huo, juhudi za Tanzania kuendeleza tiba ya maradhi ya kinywa zimetambuliwa na kusifiwa. Aidha, tumepata ahadi za kuendelea kusaidiwa kuimarisha na kuendeleza mafanikio tuliyoyapata.

Kama mjuavyo, kwa msaada wa kibinadamu kutoka Marekani na mchango wa Serikali yetu katika miaka minne iliyopita, Kituo cha Tiba ya Maradhi ya Kinywa cha Hopitali ya Muhimbili kimekuwa ndicho cha kisasa zaidi kuliko vyote katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati.

Open Government Partnership
Ndugu Wananchi;

Nchi yetu imepata heshima nyingine kubwa kufuatia uamuzi wa Rais Barack Obama wa Marekani wa kuijumuisha katika kundi la nchi 46 duniani zitakazoshiriki katika mpango mpya unaoitwa Open Government
Partnership. Mpango ulianza na nchi nane, Afrika ya Kusini ikiwa ndiyo nchi pekee ya Afrika. Sasa
zimeongezeka nchi nne za Tanzania, Kenya, Ghana na Liberia na kufanya nchi za Afrika kuwa tano kati ya hizo 46 duniani.

Sifa kubwa ya nchi kujumuishwa katika mpango huo ni Serikali kuwekeza katika maendeleo ya watu wake na kuongoza kwa misingi ya kidemokrasia, utawala bora, utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Ni jambo la kutia faraja kwamba nchi yetu imetambuliwa kufanya vyema kwa mujibu wa misingi hiyo na kustahili kupewa heshima kubwa kiasi hicho. Ni sifa kubwa ambayo hatuna budi kujivunia, kuienzi na kujipa dhima ya kuhakikisha kuwa tunaidumisha na kuiendeleza.

Ndugu Wananchi;

Katika mpango wa Open Government, asasi za kijamii ni wadau na washiriki kamili. Jambo la sifa na faraja nyingine kwa nchi yetu ni kwamba miongoni mwa mashirika ya kijamii machache yaliyoshirikishwa ni Shirika la TWAWEZA la Tanzania. Lakini sifa kubwa zaidi kwetu ni kuwa Ndugu Rakesh Rajani, kiongozi wa Shirika hilo, ndiye aliyepewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wenzake. Alizungumza vizuri sana na kuiongezea sifa nchi yetu ya kutoa fursa kwa asasi za kijamii kutoa maoni yao na kushirikiana na Serikali
kujenga nchi yao.

Tuzo

Ndugu Wananchi;

Juhudi tuzifanyazo za kupambana na changamoto mbalimbali ili kujiletea maendeleo zimeonekana na kutambuliwa duniani. Bila ya kutarajia nchi yetu imepewa tuzo tatu za heshima kimataifa kutokana na mafanikio tunayoyapata katika nyanja mbalimbali. Kwanza, The United Nations Foundation wametupa
tuzo ijulikanayo kama “2011 Social Good Award”  kwa kuendeleza midia jamii na kutumia teknolojia ya kisasa kukabili changamoto za maendeleo ikiwa ni pamoja na huduma ya afya ya kina mama. Pili,tumepewa tuzo ya  "The South-South News Award"  kutokana na mafanikio tunayoyapata katika kuboresha
afya nchini na kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kwa ajili hiyo. Pia, kwa kutambua mchango tunaoutoa kwa maendeleo ya dunia. Na tatu,  kutoka Soko la Mitaji la NASDAQ tumepewa tuzo kwa kutambua mchango wangu na mafanikio tunayoyapata katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
Mh. Jakaya M. Kikwete.


Tuzo hizo za kimataifa nilizopewa mimi ni za nchi yetu na watu wake. Juhudi zetu za pamoja ndizo zilizotufanya tupate mafanikio yanayotambuliwa kimataifa. Ni fahari kubwa kwa juhudi zetu kutambuliwa kimataifa. Nawaomba ndugu zangu tusibweteke na kulimbuka na sifa bali tuongeze bidii na maarifa
maradufu huku nikiwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwawezesha kwa hali na mali wananchi, madaktari, wauguzi na watendaji wengine Serikalini na nje ya Serikali. Bado tunayo safari ndefu kuelekea kwenye maendeleo ya juu ya afya kwa Watanzania. Muelekeo wetu ni mzuri, hivyo hatuna budi tuudumishe na kuuendeleza.

Mkutano na Watanzania

Ndugu Wananchi;

Shughuli yangu ya mwisho kubwa niliyofanya nchini Marekani ilikuwa ni kukutana na Watanzania waishio Marekani. Ndugu zetu wana umoja wao ujulikanao kama Diaspora Community of Tanzania in America (DICOTA) na tarehe 23 Septemba, 2011, walikuwa wanafanya mkutano wao mkuu wa tatu. Walinialika
niende kuzungumza nao na kushiriki nao katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Kwa kweli mkutano wao ulikuwa mzuri, tulivu na ndugu zetu walikuwa wamejiandaa vizuri. Walikuwa na maonyesho ya mambo mazuri wanayoyafanya kule Marekani ambayo yanaweza kunufaisha nchi yetu na mengine tayari yanafanya hivyo.

Ndugu Wananchi;

Katika mazungumzo yangu nao, niliwapongeza sana kwa uamuzi wao na kwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi kifupi cha miaka mitatu. Niliwataka washike uzi huo huo ili waweze kupata mafanikio zaidi. Katika hotuba yangu niliwaelezea kwa muhtasari mafanikio tuliyoyapata katika nyanja mbalimbali na changamoto zilizo mbele yetu. Wakati mwingine ni muhimu kufanya hivyo kwani baadhi ya ndugu zetu wameondoka nyumbani miaka mingi na hawajabahatika kurudi. Hivyo kwao Tanzania wanayaoifahamu ni ile waliyoiacha miaka 15 au 20 iliyopita au hata zaidi.

Ndugu Wananchi;

Niliwakumbusha mambo matano muhimu ambayo niliwaambia nilipokutana nao kwa mara ya kwanza nikiwa Rais wan chi yetu mwezi Mei, 2006. Kwanza,*niliwaomba wawe raia wema katika nchi ya watu.
Niliwasihi wajiepushe kufanya vitendo vya uhalifu kama vile wizi, ujambazi,
kutumia au kufanya biashara ya dawa za kulevya, ubakaji n.k.

Niliwaeleza kuwa wakijihusisha na vitendo hivyo wasitegemee Serikali kuwatetea kwa sababu hata na sisi huku nyumbani watu wanaofanya makosa hayo wanakamatwa, kushtakiwa na kufungwa. Hata hivyo, niliwahakikishia kuwa iwapo wataonewa au kusingiziwa tutawasaidia na kuwatetea.

Pili, niliwataka wasisahau nyumbani kwao. Wametoka huku nyumbani kwenda nje kuchuma ili wajiletee maendeleo. Wakumbuke kujenga nyumba nzuri kwao ili wawe na mahali pazuri pa kufikia. Wakati mwingine kukosa mahali pazuri pa kufikia kunawafanya wasije nyumbani au wakija waishie mjini kwa sababu
nyumbani kwao hakuwafai kwa viwango vyao.

Aidha, niliwataka wasaidie kuwaendeleza wazazi na ndugu zao kwa elimu au hata kwa misaada mingine ya kuwaendeleza kiuchumi na kuwapatia kipato.

Ndugu Wananchi;

Niliwaeleza kuwa natambua tatizo la wao kupata viwanja na kupata watu waaminifu wa kusimamia ujenzi. Ni kweli kabisa kwamba wapo watu ambao wamedhulumiwa na watu waliowaamini kuwatafutia viwanja au kusimamia ujenzi.

Kuhusu upatikanaji wa viwanja niliwaambia kuwa nimeagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa washirikiane kuwasaidia kupata viwanja kwa urahisi na uhakika. Kuhusu ujenzi niliwaeleza kuwa wakikosa ndugu au jamaa waaminifu watumie Mashirika ya Hifadhi ya Jamii na Shirika la Nyumba la Taifa ambao wanajenga nyumba na kuuza. Wanaweza kuwauzia wanazojenga au hata kuwasaidia kujenga badala ya kutumia watu wasiokuwa waaminifu. Nafurahi kwamba baadhi ya mashirika hayo yalishiriki katika mkutano huo.

Tatu, niliwataka wachangie kwa namna mbalimbali maendeleo ya nchi yetu. Wanaweza kuhifadhi fedha zao kwenye Benki zetu hapa nchini na kuzitumia kwa shughuli zao hapa nchini na nje pia. Kama Watanzania wengi watafanya hivyo watakuwa wamechangia kukuza uchumi wa nchi. Zipo nchi nyingi duniani zinanufaika na utaratibu wa namna hiyo. Niliwasisitizia kuwa na sisi wakati umefika kwa Tanzania kunufaika na ndugu zetu waishio ughaibuni. Bahati nzuri CRDB wameanzisha mfumo wa kuwawezesha Watanzania kufanya hivyo kupitia Tanzanite Account.  Nimewakumbusha waitumie fursa hiyo. Nimesikia pia kuwa benki
nyingine nazo zinafikiria kufanya kama CRDB.

Nne, nimewataka wawekeze nyumbani au wawashawishi wawekezaji walete vitega uchumi nyumbani. Kufanya hivyo kutasaidia kukuza uchumi, kuongeza ajira na kipato kwa ndugu zao. Wafanye hivyo hivyo kuleta teknolojia za kisasa na taaluma mbalimbali. Wapo ambao wamehamasika na tayari wanawekeza na wapo ambao wamekuwa wanashawishi wawekezaji kuja nchini. Baadhi yao wameelezea matatizo ya urasimu na tabia ya kigeugeu kwa baadhi ya watendaji Serikalini hapa nchini. Nimewaelekeza kuwa watumie Kituo cha Uwekezaji kuwasaidia badala ya kutegemea sana wenyeji wao. Wanapokwama wazione mamlaka
zinazohusika na bahati nzuri siku hizi kuna Waziri maalum anayeshughulikia uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Jambo la  tano, ambalo niliwaomba wafanye ni kuwa wawe na umoja wao ili uwe ndicho chombo cha kuwaunganisha na kuratibu shughuli zao. Pia kiwe ni chombo cha wao kusaidiana wawapo na shida kama vile misiba n.k. Nafurahi kwamba wamekwishaunda chombo hicho yaani DICOTA. Bahati nzuri kwa upande wa
kusaidiana, viongozi wa DICOTA wameshazungumza na NSSF ambao wameanzisha aina fulani ya bima ya afya ambayo watu watachangia na mtu akipoteza maisha, mwili wake utasafirishwa kwa gharama ya NSSF. Aidha, huku nyumbani kwao nako, ndugu zake atakaowachagua watapata matibabu kwa gharama ya NSSF.

Uraia wa Nchi Mbili

Ndugu Wananchi;

Moja ya kilio cha siku nyingi cha Watanzania waishio nchi za nje ni kupata fursa ya kuwa na uraia wa nchi mbili, yaani wa Tanzania na wa ile nchi ya nje anayoishi. Niliwaeleza kuwa tumekisikia kilio chao na tunaelewa kuwa zipo nchi nyingi duniani zinao utaratibu huo. Bahati mbaya sisi hatuna utaratibu huo, lakini tunafikiria suala hilo liwe miongoni mwa mambo ambayo yatazungumzwa katika mjadala wa Katiba mpya ili wananchi waamue. Kuhusu fursa ya kupiga kura nje ya nchi ni suala ambalo tutalizungumza kupitia taasisi husika.

Niliwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini tunatambua na kuthamini mchango muhimu unaoweza kutolewa na Watanzania waishio nchi za nje. Ndiyo maana katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tumeunda Idara ya kushughulikia Watanzania walioko nchi za nje.

Uchaguzi wa Igunga

Ndugu Wananchi;

Kama mnavyofahamu siku ya Jumapili tarehe 2 Oktoba, 2011 ndugu zetu wa Jimbo la Igunga, Mkoani Tabora watapiga kura kuchagua Mbunge katika uchaguzi mdogo. Napenda kutumia fursa hii kuwatakia wananchi wa Igunga uchaguzi mwema na kuwaomba siku hiyo wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao ya
kikatiba ya kumchagua mtu wanayemtaka kuwa Mbunge wao kwa kupiga kura. Haitakuwa sawa hata kidogo kama ndugu zetu wa Igunga wataacha kutimiza wajibu wao huo wa msingi kama raia.

Ndugu Wananchi;

Ningependa kuwahakikishia kwamba Serikali imejiandaa vya kutosha kutimiza ipasavyo wajibu wake wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa Igunga katika kipindi hiki cha uchaguzi. Hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura bila wasiwasi wowote. Usalama utakuwa wa uhakika katika vituo vyote na kamwe hatavumiliwa mtu yeyote atakayefanya au hata kujaribu kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, vurugu au fujo. Hatukubali siku ya kupiga kura iwe ni siku ya watu kujifungia ndani au kuogopa kutoka nje.
Nawahakikishia hilo halitatokea huko Igunga. Na wanaodhani kuwa tunatania wathubutu,
watadhibitiwa ipasavyo.

Nawasihi, wananchi wa Igunga kuendelea kudumisha amani, kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya matokeo kutangazwa. Nawaomba msikubali wanasiasa wawageuze chambo cha kuendeleza maslahi yao binafsi ya kisiasa na tamaa zao za madaraka zilizovuka mipaka. Amani ya nchi yetu ni tunu adhimu ya taifa letu tuliyoirithi kutoka kwa waasisi wa taifa letu Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Mzee Abeid Amani Karume. Tumeapa kuidumisha na kuiendeleza na tumefanya hivyo kwa mafanikio
hadi hivi sasa.

Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshawahakikishia wapiga kura wa Igunga kwamba maandalizi yote yamekamilika na shughuli za uchaguzi kule Igunga zitakwenda kama inavyotarajiwa. Wamesema vifaa vyote tayari vimesambazwa katika Kata zote, Wasimamizi wa Vituo na Mawakala wa vyama wamekamilika. Kwa
jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyojipanga, ninayo imani kuwa mchakato mzima wa uchaguzi utakwenda vizuri.

Ni matumaini yangu kwamba Tume itaendelea kuwaelimisha wananchi taratibu za kufuata ili wananchi washiriki kwa ukamilifu katika kutimiza haki yao ya kikatiba. Ningependa kuona kuwa kila mtu aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anapata fursa ya kupiga kura kwa
uhuru na bila bugudha yoyote. Nawatakia uchaguzi mwema.

*Mungu Ibariki Afrika!*

*Mungu Ibariki Tanzania!*

*Asanteni kwa Kunisikiliza.*

Ijumaa, 30 Septemba 2011

HELIKOPTA YA CCM YAPOTEA ANGANI IKIJARIBU KUTAFUTA VITUO VYA MIKUTANO YA KAMPENI.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, helikopta inayotumiwa na  CCM katika kampeni za Igunga imeripotiwa kupotea ikiwa angani wakati ikijaribu kutafuta vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kumnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Dk Dalaly Kafumu.Taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo zilianza kuzagaa jana majira ya saa tano asubuhi mjini Igunga na baadaye zilithibitishwa na mmoja wa maofisa wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe kuwa walipotea mara kadhaa baada ya mtu wanayemtegemea kuwaongoza njia kupoteza ramani akiwa angani.
“Unajua tumemchukua mtu ambaye anaifahamu vizuri Igunga ili aweze kuielekeza helikopta mahala pa kwenda, lakini kwa bahati mbaya mtu huyo alipokuwa angani alishindwa kwa sababu ya kupoteza ramani,” alisema ofisa huyo.
Helikopta ya CCM.

Awali taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo zilitolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutano wa kampeni wa chama hicho uliofanyika katika Kata ya Nkinga jana asubuhi, akisema kuwa alipata habari kuwa helikopta ya CCM ilikuwa imepotea.Mmoja wa watu waliokuwa ndani ya helikopta hiyo alisema walipotea mara kadhaa na kwamba katika harakati hizo walitua kwenye kijiji kimojawapo cha Wilaya ya Igunga jana saa nne asubuhi, lakini walijikuta kwamba wamekosea, hivyo kuondoka kwani watu hawakuwa tayari kwa mkutano huo.
January Makamba ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Siasa na Mambo ya Nje) alikanusha taarifa za kupotea kwa helikopta hiyo na kuziita kuwa ni “uzushi wa kisiasa”.
Helikopta ya CCM ambayo iliwasili juzi asubuhi na kuanza kutumika katika kampeni, inadaiwa kutumia mmoja wa wenyeji wa wilayani hapo katika ziara yake kutokana na kutokuwapo  kwa maandalizi ya ramani inayojulikana kama GPRS.
“Hatuna ramani ya kumwogoza rubani, hivyo tunafanya kazi hii kwa kutumia wenyeji wanaoifahamu vizuri Igunga, kama unavyojua huko angani wakati mwingine ni vigumu kutambua eneo na hili ni tatizo kwetu," alisema ofisa huyo.Helikopta hiyo ya CCM ilirejea mjini Igunga jana majira ya saa tisa alasiri na haikufahamika iwapo kurejea huko mapema kulitokana na matatizo hayo yaliyoelezwa.

Mratibu wa Kampeni za CCM Igunga, Mwigulu Nchemba hakupatikana kuzungumzia suala hilo na pale alipotafutwa kwa simu, ilikuwa ikiita bila majibu.
Masanduku ya Kura
Katika hatua nyingine, Chadema kimesema kuna njama za kuingiza kura bandia Igunga na kwamba tayari karatasi na masanduku ya kura yamefikishwa mjini Nzega kwa ajili ya kuingizwa Igunga siku ya uchaguzi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jana majira ya saa tano asubuhi katika Kata ya Nkinga, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema Chadema kina taarifa za uhakika kwamba tayari karatasi hizo zimeshawasili wilyani Nzega.
“Ndugu waandishi mlioko katika mkutano huu, hii ni taarifa rasmi ya chama na kwamba tuna taarifa za uhakika kwamba karatasi hizo zimehifadhiwa nyumbani kwa ofisa mmoja wa Serikali,” alisema Mbowe.
Aliendelea kusema kuwa tayari karatasi hizo zimeshapigwa kura na kudumbukizwa kwenye maboksi ya kupigia kura tayari kwa kuyaingiza kwenye vituo vya kupiga kura.
Mbowe alisema kuwa tayari vijana wa Chadema wameshakwenda Nzega kuimarisha ulinzi ili kuhakikisha karatasi hizo haziingii Igunga.
Mbowe aliendelea kusema kuwa mpango huo wa CCM unatekelezwa kwa msaada mkubwa wa usalama wa taifa na kuonya kuwa iwapo zinaingia Igunga basi hapatakalika.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Chadema zimedai kuwa karatasi hizo pamoja na maboksi hayo ya kura yamehifadhiwa nyumbani kwa mkuu wa wilaya hiyo, taarifa ambazo zimekanushwa vikali na kiongozi huyo.
Mwananchi lilizungumza kwa simu na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Florence Horombe ambaye alisema kwamba, hana taarifa za kuwapo kwa masanduku hayo ya kura katika wilaya yake.
“Sina taarifa yoyote kuhusiana na karatasi hizo au jambo lolote kama hilo,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Nahodha: Hatumchagui mfalme Igunga
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha amesema Jeshi la Polisi litatumia ikiwezekana fedha zote lilizo nazo kuhakikisha kwamba linawapata wahusika wa kitendo cha kumwagiwa tindikali kwa mmoja wa wakazi wa Igunga, Mussa Tesha.Alisema mjini Igunga jana kuwa “tutafanya kila tuwezalo, tutatumia fedha zetu zote polisi tulizonazo, kuhakikisha watuhumiwa hawa wote wanne wanakamatwa na wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria”.
Nahodha alisema hayo wakati akijibu hoja mbalimbali za viongozi wa vyama vya siasa mjini Igunga, mkutano ambao uliibua hoja kwamba mtuhumiwa aliyekamatwa kisha kufikishwa mahakamani George Salum, alionewa.
Nahodha alisema kwa kuwa suala hilo lipo mahakamani wahusika wawe na subira na kwamba ikiwa mahakama itabaini kutohusika kwa mtuhumiwa huyo, basi ataachiwa.
Nahodha aliweka bayana kwamba juzi alimtembelea mtuhumiwa huyo gerezani na kubaini kwamba miongoni mwa wanaosakwa ni mtuhumiwa George Ernest Nyati na kwamba kufanana kwa majina hayo ndiyo chanzo cha manung’uniko hayo.
“Nimeambiwa kwamba yule mgonjwa (Tesha), anapata nafuu, sasa nami namuombea akipata nafuu hiyo hasa ya macho, tutaitisha gwaride la utambulisho na yeye atawatambua hata kama asipoweza kuwaona basi hata kwa sauti zao maana ni watu ambao aliwazoea na alikuwa akiwafahamu,”alisema Nahodha.
Katika mazungumzo yake waziri huyo alisema uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Igunga keshokutwa si wa kumchagua mfalme wala mwakilishi wa wananchi peponi, bali ni wa mbunge pekee.
Kutokana na hali hiyo, Nahodha ambaye yuko Igunga tangu Jumanne wiki hii alisema hakuna haja ya vyama vya siasa kuwa na uhasama na badala yake zifanyike siasa za kistaarabu ambazo zinawezesha wananchi wa Igunga kupata mwakilishi wanayemtaka.
“Ninachotaka kuwaeleza wenzangu hapa, ni kwamba hatuchagui mwakilishi wetu peponi, la hasha, ila tunamtafuta mbunge tu, hivyo kadhia hii yote haina maana, sidhani kama ni sahihi sana kuwa na mvutano mkubwa katika jimbo dogo tu la uchaguzi,”alisema Nahodha muda mfupi kabla ya kuingia katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa.
Nahodha alirudia kauli hiyo wakati alipozungumza na viongozi hao pale alipowaambia kwamba: “Hatumchagui mfalme wa Igunga”, hivyo kuwataka viongozi hao kuhakikisha wafuasi hao wanaendesha siasa za kistaarabu zisizo na uhasama.
Waitara wa Chadema alizungumzia suala la madai ya kutaka kutekwa kwa mbunge wa Viti Maalumu Ester Bulaya (CCM) na kurushiwa risasi ambapo baadaye kesi hiyo ilibadilishwa na yeye (Waitara) kutuhumiwa kurusha risasi huku polisi wakionekana kuegemea upande wa CCM."Ninachosema hapa kuwe na usawa wa kushughulikiwa matukio ya uhalifu na mtu anapofanya kosa, ashughulikiwe kama yeye na chama kisihusishwe, kwa sasa hakuna ugomvi na polisi bali ugomvi uliopo ni wa makada wa CCM na Chadema,  hapa kuna uhasama nasema ukweli," alisema.
Waitara alitaka kuhakikishiwa juu ya ushiriki wa polisi katika mchakato wa kuchakachua kura kwa kuwa katika chaguzi zingine polisi wamekuwa wakihusishwa.Kada wa CCM, Shaibu Akwilombe alitaka kuwapo kwa utaratibu mzuri kwa ajili ya watu wanaosubiri matokeo utakaoepusha vurugu kwa kuwa sheria iliyopo inasema mtu akipiga kura akae umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupiga kura jambo ambalo alisema ni hatari iwapo watajikusanya wengi wakiwa na itikadi tofauti.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adam, alikiri kutokea kwa mfululizo wa matukio ya kujeruhiana, kuchaniana picha na mabango, lakini alikanusha matukio hayo kuhusishwa na CCM ambapo aliitupia shutuma nzito Chadema kuwa ndio imekuwa ikitajwa mara kwa mara kuhusika na matukio hayo.
Polisi: Hatutapendelea chama chochote Igunga
Wakati huo huo, uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora ukitarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili, Jeshi la Polisi nchini limeweka wazi msimamo wake kwa kusema: "Tutahakikisha hatutumiki kwa maslahi ya chama chochote cha siasa".Kadhalika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupitia kwa Mwenyekiti wake wa muda, Profesa Amon Chaligha imesema, itahakikisha uchaguzi wa Igunga unakuwa huru na wa haki na kwamba mshindi halali ndiye atakayetangazwa.
Polisi katika tamko lililotolewa na Kamishna wake wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja imesema itahakikisha upigaji kura unafanyika kwa amani, bila vikwazo wala bughudha, kulinda usalama wa vifaa vya kupigia kura na kuhakikisha mchakato wa kupiga, kuhesabu kura na kutangaza matokeo unakuwa wazi, huru na wa haki.Chagonja aliwaambia waandishi wa habari jana mjini Igunga kuwa chombo cha umma, polisi watasimamia sheria, kanuni na taratibu zote za uchaguzi "bila upendeleo wowote" na kwamba usalama utaimarishwa kabla, wakati na baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
"Jeshi la polisi litaendelea kusimamia sheria, kanuni na taratibu zote bila upendeleo wowote. Kama chombo cha Umma, litahakikisha halitumiki kwa maslahi ya chama chochote cha siasa," alisema Chagonja.
Uchaguzi mdogo wa Igunga unatarajiwa kufanyika keshokutwa Jumapili, Oktoba 2, 2011 na vyama vinane vimesimamisha wagombea wakiwania kurithi nafasi iliyoachwa wazi na mbunge aliyejiuzulu, Rostam Aziz kutoka CCM.

Habari hii imeandikwa na Neville Meena, Geofrey Nyang'oro na Daniel Mjema, Igunga

CREDITS; Gazeti la Mwananchi.

Jumatano, 28 Septemba 2011

HELIKOPTA YA CHADEMA YATIKISA IGUNGA, YA CCM BADO KITENDAWILI.CUF NAO KURUSHA KWA MARA YA KWANZA LEO.

<>  WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilitikisa anga la Igunga baada ya kuanza kutumia helikopta kufanya kampeni zake, zile mbili za wapinzani wao, CCM zikishindwa kuwasili jimboni humo na kubaki Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kutokana na sababu za kiufundi.Wakati Chadema ikipasua anga na mbili za CCM zikibaki KIA, helikopta ya Chama cha Wananchi (CUF) nayo imeshindwa kutua Igunga jana na sasa inatarajiwa hapa leo.

Helikopta ya Chadema ilianza kuonekana katika anga la Igunga saa 10:40 jioni ikiwa na maandishi makubwa ya chama hicho na rangi ya bluu.Ujio wa helikopta hiyo ulivuta kwa muda idadi kubwa ya wananchi waliokuwa kwenye Viwanja vya Sabasaba wakisubiri ujio wa helikopta mbili za CCM, ambazo awali, ilielezwa kuwa zingewasili saa 8:00 mchana.

Baadaye ilielezwa kwamba helikopta hizo za CCM zingetua Igunga saa 11:30 jioni zikiwa na makada wa chama hicho akiwamo Katibu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba.

Hata hivyo, ilipofika saa 12:00 jioni, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akitumia gari la matangazo la Bendi ya muziki ya ToT Plus alitangaza kwamba helikopta hizo zisingeweza kutua Igunga kutokana na sababu za kiufundi.
Alisema zilichelewa kupata vibali kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam na kwamba baada ya kutua KIA ilishauriwa kuwa ni vyema zilale hapo.

Alisema kama helikopta hizo zingeondoka KIA jana jioni na kufika hapa usiku wakati tayari kungekuwa na giza kitu ambacho kisingekuwa kizuri kiusalama. Alisema helikopta hizo sasa zitawasili leo saa 4:00 asubuhi.

Matumizi hayo ya helikopta yanawafanya wananchi wa Igunga kushuhudia kampeni nzito na za aina yake tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kwanza wa vyama hivyo mwaka 1994 na Rostam Aziz kushinda.Jimbo hilo lenye wapiga kura 170,000 katika vijiji 96, halijawahi kushuhudia kampeni nzito kiasi hicho zinazohanikizwa na magari yenye vifaa vya kisasa vya muziki.

Habari kutoka ndani ya CCM, zinaeleza kuwa katika kujihakikishia kura katika kipindi hiki cha lala salama, chama hicho kitawatumia makada wake, Makamba na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli wanaoelezwa kuwa na ushawishi mkubwa.

Kulingana na vyanzo mbalimbali vya habari, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano wa ufunguzi wa kampeni za CCM anatarajiwa kurudi tena hapa keshokutwa.Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliwasili hapa jana kuongeza nguvu kwa viongozi wa chama hicho ambacho idadi kubwa ya wabunge wake wameweka kambi hapa.

Helikopta ya CUF
Kwa upande wake, CUF kinatarajiwa kuanza kutumia helikopta yake kuanzia leo huku Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Juma Duni Haji akitarajiwa kufunga pazia la kampeni za chama hicho ambazo, awali zilitarajiwa kufungwa na Katibu Mkuu wake ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.

Akizungumzia na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Julius Mtatiro alisema kampeni hizo sasa zitafungwa na Haji anayetarajia kuwasili wakati wowote katika kipindi hiki cha mwisho wa kampeni.Mtatiro alisema tayari wabunge wa chama hicho  akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar) Ismail Jussa wanaendelea na kampeni jimboni humo.

Chanzo; Mwananchi

WANAZUONI WALAANI CHADEMA KUSHINDWA KUOMBA RADHI KWA KUMVUA HIJAB BI. KIMARIO.


Katibu wa Sekretarieti ya Wanazuoni, Sherally Huseein (kulia) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)kukataa kuomba radhi kwa Waislamu kufuatia udhalilishaji wa kumvua hijabu Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mkoani Tabora, Fatma Kimario hivi karibuni. (Picha na Mwanakombo Jumaa- Maelezo

Jumanne, 27 Septemba 2011

WIKI YA LALA SALAMA IGUNGA, WASHINDANI NI CUF, CCM NA CHADEMA.

Daniel Mjema, Igunga
KAMPENI za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga, leo zinaingia katika wiki ya lala salama huku tathmini ikionyesha kuwa mchuano mkali ni baina ya vyama vitatu, licha ya vyama nane kusimamisha wagombea wake.

Vyama vyenye ushawishi mkubwa kisiasa jimboni humo katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2, ni CCM kilichomsimamisha Dk Dalaly Kafumu, CUF kilichomsimamisha Leopard Mahona na Chadema ambacho kimemsimaisha, Joseph Kashindye.

Uchaguzi huo pia unavishirikisha vyama vya SAU, UPDP, DP, AFP na Chausta, lakini baadhi yake kampeni zake zinaendeshwa kwa kusuasua, huku vingine vikishindwa kabisa kufanya kampeni hizo.

Katika muda wa wiki mbili za kampeni Igunga, kumekuwa na matukio baadhi ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kutuhumiana kwa matukio ya uhalifu, ukiwamokampeni chafu, ubakaji, kumwagiwa tindikali, udhalilishaji na hata vitisho vya kutumia silaha za moto kama bastola.

Mvutano mkali zaidi upo baina ya CCM na Chadema, ambavyo makada wake wamekuwa wakipiga kambi za muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kulala katika maeneo yenye idadi kubwa ya wapigakura.

Juzi Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wenye ushawishi alitua kukiongezea nguvu chama chake, lakini tayari CCM kilikwishaongeza wapiga kampeni wake wakiwamo, Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho Philip Mangula. Kwa upande wake CUF kinajivunia mtaji wa kura 11,000 ilizopata katika uchaguzi wa mwaka jana. 

Mbinu nyingine ambayo imekuwa ikitumiwa katika kampeni hizo ni wagombea kujinadi kwa lugha ya kisukuma kutokana na wapigakura wengi wa jimbo hilo kuzungumza lugha hiyo ikilinganishwa na Kiswahili.

Hali hiyo imekuwa ikiwapa wakati mgumu wanahabari kufuatilia mikutano hiyo kutokana na wengi kutofahamu lugha hiyo, isipokuwa pale anapokuwapo mkalimani wa kutafsiri maneno husika Kiswahili.

Katika wiki ya mwisho iyaoanza leo, viongozi wa kitaifa wa vyama vyenye ushindani, wanatarajiwa kuhamia Igunga, ili kunadi sera za wagombea wao ili kujihakikikisha ushindi.

Inachojivunia CCM
CCM ambacho kinadai kuwa na mtaji wa kura 39,000 ilizozipata katika uchaguzi mkuu uliomalizika Oktoba mwaka jana, kimekuwa kikijivunia mfumo wa uongozi kuanzia ngazi ya mabalozi, shina, kata hadi wilaya.

Chama hicho kinaamini kuwa kama viongozi wao hao hawatakisaliti basi kina uhakika wa kutetea kiti hicho kilichoachwa wazi na Rostam Aziz aliyejiuzulu huku kikiamini kushinda kwa zaidi ya asilimia 60.

Mbali na uongozi huo, lakini chama hicho kina madiwani 24 kati ya 26 na kinaamini kuwa madiwani hao pia wana ushawishi mkubwa kwa vile walichaguliwa na wananchi kwa kura.

Katibu Mkuu wa CCM, Willison Mukama wiki iliyopita alisema chama chake pia kinajivunia sera nzuri kwenye huduma za jamii ikiwamo mradi mkubwa wa maji wa Shinyanga-Nzega-Igunga ambao utafanya tatizo sugu la maji Igunga kuwa historia.

CCM kimejenga imani kwamba tuhuma dhidi ya Chadema kwamba wanafanya vurugu, zinaweza kukisadia kuendelea kuliongoza jimbo hilo ambalo halijapata kuwa na mwakilishi wa upinzani.

Baadhi ya makada wa CCM wanaweka wazi kwamba Chadema ambacho ni chama kikii cha upinzani nchini, kimejikuta kikisigana na CUF ambao pia ni wapinzani na kwamba CCM wanaweza kunufaishwa na hali hiyo.

Kwa mtizamo huo, CCM kinaamini CUF kitasaidia kupunguza kura za Chadema ambacho hakina mizizi jimboni humo ikilinganisha na CUF ambacho kilishiriki uchaguzi mkuu 2010 na kunyakua kura 11,000.

Hivyo ipo imani kwamba Chadema na CUF vinaweza kujikuta vikigawana kura za wale wanaounga mkono upinzani, hivyo CCM kushinda kwa urahisi. Vijana kuwabeba Chadema
Kwa upande wake Chadema ambacho ni chama kipya katika siasa za Igunga, kinaamini kitashinda uchaguzi huo kwa kile kinachodai ni kufanikiwa kujipenyeza katika kundi la vijana ambao ni wengi.

Hakuna ubishi kwamba katika mikutano ya chama hicho, kundi kubwa linaloonekana kukiunga mkono ni vijana ambao wanaamini matatizo makubwa ya ajira na maisha magumu yamesababishwa na CCM.

Jambo jingine, Chadema kinaamini mgawanyiko ndani ya CCM uliosababishwa na kujiuzulu kwa Rostam, pia utapunguza kura za chama tawala na kuwanufaisha wapinzani.

Wafuasi wa Rostam wanadaiwa ‘kununa’ na kufanya kampeni za chinichini ili kuhakikisha CCM hakishindi uchaguzi huo.

Jambo lingine ambalo Chadema kinaamini litapunguza kura za CCM ni hatua ya kumsimamisha Dk Kafumu katika wakati ambao kuna kelele nyingi kuhusu ufisadi katika sekta ya madini ambayo yanadaiwa kutowanufaisha Watanzania.

Kabla ya kuteuliwa kwake kupeperusha bendera ya CCM, Dk Kafumu alikuwa kamishina wa madini na Chadema na CUF vinatumia hilo kama silaha ya kummaliza mgombea huyo kwamba alishiriki ufisadi.

CUF na mtaji wa kura 11,000
CUF kwa upande wao wanaamini kuwa kura 11,000 kilizozipata 2010, mgawanyiko ndani ya CCM unaotokana na kundi la Rostam na vurugu zinazotokea jimboni humo zitasaidia kukivusha na kushinda.

Mbali na hayo lakini CUF kinaamini kuwa ndicho pekee kimeendesha kampeni za kistaarabu kulinganisha na vyama vingine na kutokana na hulka ya wenyeji kutoshabikia vurugu basi watakipa kura.

Pia CUF kinaamini kwamba mchuano mkali kati ya Chadema na CCM kutavifanya vyama hivyo viwili kugawana kura hivyo wao kupata ushindi kutokana na ushawishi walioufanya kwenye kampeni.

CUF kinaamini mgombea wake ndiye mwenye nguvu na anayekubalika zaidi na kwamba hata 2010 angeweza kuibuka mshindi lakini kutokana na ‘nguvu’ kubwa aliyoitumia Rostam ndio iliyochangia kumwangusha.

Kinachotarajiwa

Kutokana na hali ilivyo na ushindani mkubwa baina ya vyama vya Chadema, CUF na CCM, wadadisi wa siasa wanasema lolote linaweza kutokea katika jimbo hilo.

Wiki ya mwisho ya kampeni hizi inaweza kutoa mwelekeo wa nani atakuwa mshindi lakini kwa mtizamo wa kidadisi, hadi sasa hakuna chama chochote chenye uhakika wa ushindi.

Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2 huku wapiga kura waliojiandikisha wakiwa 170,000 lakini wanaweza wasijitokeze wote kama ilivyotokea mwaka jana ambapo ni asilimia 40 waliojitokeza

Jumapili, 21 Agosti 2011

DR. PETER KAMFUMU KUBEBA DHAMANA YA CCM UBUNGE WA IGUNGA TABORA.

Dr. Peter Kamfumu, kwa sasa ni Kamishna wa Madini Wizara ya Nishati na Madini, ndiye anayeongoza jahazi la CCM Igunga akijaribu kuvaa viatu vya Rostam Aziz.

KURA ZA MAONI CCM YAMPATA MRITHI WA ROSTAM IGUNGA , NI PETER KAMFUMU.

PETER KAMFUMU ameongoza kura za maoni za CCM zilizopigwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora kwa ajili ya kuomba kugombea Ubunge Jimbo la Igunga lililoachwa wazi na Rostam Azizi aliyejiuzulu.

Taarifa iliyotua hivi punde katika mtandao huu kutoka radio Uhuru Fm inadai kuwa Ndugu KAMFUMU ambaye pia ni Kamishna wa Nishati katika Wizara ya Nishati na Madini amepata kura 588 kati ya kura 928 zilizopigwa na Wajumbe wa Mkutano huo katika uchaguzi uliofanyika jana Mjini Igunga.
Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga Ndugu NEEMA ADAM ameiambia Uhuru FM kwa njia ya Simu kuwa jumla ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Kumi na Tatu wamepigiwa kura za maoni katika mkutano huo.
Wanachama wengine waliopigiwa kura ni pamoja na Ndugu JAFARI ALI OMAR kura 163, SHAMSI FEROUZ IBRAHIMU kura 36, Ndugu HAMIS MAPINDA kura 36, Ndugu NGASA NIKOLAUS kura 18, Ndugu SELF HAMIS kura 13 na Ndugu SHIRE MASHAURI kura 16.

Wengine ni Ndugu HAMAD SAFARI kura 5, Ndugu MKOBA SHABAN kura 5 Ndugu DANIEL MBOJE kura 4, Ndugu ADAM KAMANI kura Tatu na Ndugu AMINA FUNDIKILA kura Saba.

Kulingana na Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Igunga majina hayo yote yatapelekwa ngazi ya Mkoa ambayo nayo itayapitia na kisha kuyapeleka katika Kamati Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kwa maamuzi zaidi.