Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARI BBC. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo HABARI BBC. Onyesha machapisho yote

Jumatatu, 5 Agosti 2013

RAIS ZUMA WA AFRIKA YA KUSINI AMPONGEZA RAIS ROBERT MUGABE KWA KUSHINDA UCHAGUZI 2013.


Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ametoa zile alizoita, hongera nyingi kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye ameshinda muhula wa saba wa uongozi akiwa na umri wa miaka 89.
Zuma akikaribishwa na Mugabe alipozuru Harare zamani

Rais Zuma amesema uchaguzi mkuu wa Zimbabwe ulifanikiwa, na ametoa wito kwa pande zote zikubali matokeo.
Mpinzani mkuu wa Bwana Mugabe, Morgan Tsvangirai, mwenye umri wa miaka 61, amekataa matokeo na amesema atapeleka malalamiko mahakamani.
Viongozi wa mataifa ya magharibi yamesema yana wasi-wasi kama uchaguzi ulikuwa wa halali.
Bwana Mugabe alipata asili-mia-61 ya kura katika uchaguzi wa rais.
Na chama chake cha ZANU-PF kilipata thuluthi mbili ya viti vya bunge

Alhamisi, 11 Julai 2013

IJUE HISTORIA YA CHAMA CHA MURSI WA MISRI ALIYENG'OLEWA MADARAKANI. NI MUSLIM BROTHERHOOD.

Muslim Brotherhood ni nani?

Nembo ya Muslim Brotherhood
Ushindi wa kihistoria wa Mohammed Mursi wa chama cha al-Ikhwan al-Muslimun ( Muslim Brotherhood ) katika uchaguzi wa Rais wa Misri kunabainisha mapinduzi ya vuguvugu la wanaharakati wa Kiislamu nchini humo ambako liliasisiwa na kupigwa marufuku kwa miongo kadhaa.
Hilo ndilo vuguvugu kongwe na kubwa kabisa la Kiislamu katika Misri;ikimaanisha kua mafunzo ya Quraan ndio msingi wa itikadi zake.
Kundi la al-Ikhwan al-Muslimun lilianzishwa na Hassan al-Banna katika miaka ya 1920 na limeyahamasisha mavuguvugu ya harakati za kiislamu duniani kote kwa siasa zake pamoja na shughuli zake za hisani na ufadhili wa Kiislamu.
Mwanzoni vuguvugu hilo lilikua na lengo la kusambaza maadili ya Kiislamu,lakini mara likajiingiza katika siasa hasa katika mapambano ya kuungo'wa utawala wa kikoloni wa Uingereza na kuitakasa Misri na athari zote za nchi za Magharibi.
Ingawa kundi la Ikhwan linasema linaunga mkono misingi ya kidemokrasia moja ya malengo yake makuu ni kuunda taifa la Kiislamu linaloongozwa na mfumo wa Sharia za kiislamu. Mojawapo wa kauli mbiu zake inayotumika dunia nzima ni "uislamu ndio suluhisho".
Mapinduzi
Baada ya kuunda Muslim Brotherhood mnamo mwaka 1928, matawi yalianzishwa nchini kote--kila moja likiendesha msikiti,shule na klabu cha michezo.na wanachama wake wakaanza kukua kwa haraka.
Hassan al-Banna aliuwawa na mtu asiejulikana mnamo mwaka 1948. Na mwishoni mwa mwongo wa 1940, inaaminiwa kikundi hicho kilikua na takriban wafuasi millioni mbili nchini Misri na mawazo yake yalisambaa katika Bara Arabu yote.
Wakati huo huo, Banna alianzisha tawi la kijeshi lilioitwa "zana Maalum" ambao wafuasi wake walijiunga na mapambano dhidi ya utawala wa Uingereza na kuhusika na kampeni za mashambulizi ya mabomu na mauaji. .
Serikali ya Misri ilikivunja kikundi hicho mwishoni mwa mwaka 1948 kwa kushambulia maslahi ya Waingereza na Mayahudi.. Muda mfupi baadae kikundi hicho kilishtumiwa kwa kumuua Waziri Mkuu Mahmoud al-Nuqrashi.
Banna aliyalaani mauaji hayo lakini yeye mwenyewe hatimae aliuwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana--inaoaminiwa walikua askarfi wa usalama.
Mnamo mwaka 1952, uitawala wa kikoloni ulimalizika kufuatiya mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na kikundi cha maafisa vijana waliojiita "Maafisa Huru".
Kundi la Ikhwan lilichangia kiasi katika mapinduzi hayo. - Anwar al-Sadat, aliyeshika wadhifa wa Rais mnamo mwaka 1970 aliwahi kua afisa wa uhusiano wa Maafisa Huru- na kwanza lilishirikiana na serikali mpya laini uhusiano mara ukaharibika.
Baada ya kushindwa njama ya kumuuwa Rais Gamal Abdul Nasser mnamo mwaka 1954, kundi la Ikhwan ndilo lilioshtumiwa kuhusika na likapigwa marufuku na maelfu ya wafuasi wake walifungwa jela na kuteswa. Hata hicho kundi hilo liliendelea kuimarika chini kwa chini .
Mgongano huu na serikali ulisababisha mageuzi muhimu katika itikadi za Ikhwan, yaliobainishwa na maandishi ya mojawapo wa wafuasi wake mashuhuri , Sayyid Qutb.
Qutb alihamasisha matumizi ya mapambano ya jihad dhidi ya jamii "jahili" za kijinga., ziwe za nchi za Magharibi ama zinazojiita kua za kiislamu ambazo alihoji kwamba zilihitaji mageuzi makubwa.
Maadishi yake hasa yale katika kitabu chake cha kumbukumbu kilichochapishwa mwaka mwaka 1964 --kiliyahamasisha makundi mengi ya kiislamu mkiwemo Islamic Jihad na al-Qaeda.
Mnamo mwaka 1965, serikali kwa mara nyingine tena ililenga Ikhwan,ikimyonga Sayyid Qutb mnamo mwaka 1966 na kwa hiyo kumgeuza kua shujaa katika eneo kanda nzima. .
FYEKA FYEKA
Katika miaka ya 1980 Ikhwan ilijaribu kujiunga tena katika mkondo wa kisiasa.
Ikhwanl Muslimin -ni kundi ambalo rasmi limepigwa marufuku ambalo mara kwa mara limejikuta likikandamizwa. Viongozi kadhaa waliunda ushirikiano na chama cha Wafd mnamo mwaka 1984, na vyama vya Labour na Liberal mnamo mwaka 1987,na kua nguvu kuu ya upinzani nchini Misri . Mnamo mwaka 2000, Ikhwan ilishinda viti 17 katika bunge la wanannchi.
Miaka mitano baadae,Ikhwan ilipata matokeo bora kabisa ya uchaguzi ,wakati wagombea wanaojitegemea wanaoshirikiana nao waliposhinda asilimia 20 ya kura.
Matokeo haya yalimshtua sana Rais Mubarak. Serikali kisha ikakiandama Ikhwan na kuwawekakizuizini mamia ya wafuasi wake na kutangaza mageuzi kadha aya kisheria ili kukabiliana na muamko wa kundi hilo.
Katiba iliandikwa upya ambapo ilisisitiza kua vyama vya kisiasa visiwe na misingi ya kidini,wagombea huru walipigwa marufuku kugombea Urais na sheria za kupambana na ugaidi zilitangazwa ambazo zilitoa madaraka makubwa kwa vikosi vya usalama kuweza kuwakamata washukiwa na kuekea vikwazo mikusanyiko ya hadhara.
Viongozi wa chama tawala cha Rais Mubarak cha National Democratic Party (NDP) pia kilifanya bidii kuvunja nguvu za wapinzani katikauchaguzi wa bunge wa November 2010 .
Lakini juhudi zao ziligonga mwamba -baada ya madai ya njama za kuiba kura pale ilipobainika kwamba wagombea waliofungamana na Ikhwan hawakushinda hata kiti kimoja cha bunge.
Ikhwan kilisusia duru ya pili ya uchaguzi Novemba 2010. Kikunsi hicho kikajiunga na vyama vingine vya upinzani katika hatua ya kususia na chama tawala NDP kikafadhaika kwa kushinda asilimia 80 ya viti vya bunge.
Upinzani kuendelea kukandamizwa ni mojawapo wa vichocheo vikuu vya maandamano dhidi ya serikali mnamo Januari 2011, ambapo makao makuu ya chama tawala cha NDP mjini Cairo yaliteketezwa/.
Ikhwan ililaumiwa kwa kuchochea ghasia ,lakini naibu kiongozi wao Mahmoud Izzat, alisisitiza kwamba yalikua mapinduzi ya umma.
Ingawa wafuasi wengi wa Ikhwan walijiunga na maandamano hayo ,walifanya hivyo bila ya kujitokeza waziwazi Medani Tahrir .
Lakini jinsi maandamano yalivyozidi kuunngwa mkono kwa wingi na serikali kuridhia madai kadhaa mkiwemo Rais Mubarak kutogombea tena Urais ndipo kundi hili kubwa kabisa la upinzani nchini Misri likaanza kujitutumua.
Mwanzoni mwa Februari 2011, uongozi wa Ikhwan ukatoa kauli: "tunadai kwamba utawala huu upinduliwe na tunadai kuundwa serikali ya muungano wa kitaifa wa makundi yote."
Halikadhalika walihudhuria mkutano ambao haujawahi kufanyika kati ya serikali na upinzani. Mazungumzo hayo yaligeuka kua vita vya maneno huku Ikhwan wakikataa hoja ya Makamo Rais Omar Suleiman kwamba watafute maridhiano ,lakini mualiko huo ulikuwa ni kama wametambua kuwa kundi la Ikhwan linaungw amkono na wengi na pia ni muhimu katika vuguvugu la maandamano.
'Halmashauri ya wanazuoni '
Umaarufu huu wa Ikhwan ulizusha upya mjadala kuhusu wangefanya nini pindi wangeshika udhibiti wa siasa nchini Misri.
Wakosoaji wengi hasa nchini Marekani walikumbusha muongozo wa kisiasa uliochapishwa na kundi hilo mnamo mwaka 2007, ambao ulihimiza kuundwe halmashauri kuu ya wanazuoni kuthibitisha sheria zote zinzopitishwa na taasisi za kiraia za Misri.Muongozo huo pia ulisema kwamba wanawake na wakristo hawawezi kua Rais au makamo Rais.
Hata wafuasi wenye msimamo wa wastani hawakukubaliana na muongozo huo ingawa wakereketwa walisistiza kwamba katiba inasema waziwazi kwamba Uislamu nduio dini ya taifa na sharia za kiislamu ndio msingi wa sheria kuu nchini.
Ni wazi kwamba viongozi wa Ikhwan wamejitolea kuimarisha hadhi ya Uislamu katika maisha ya wananchi wa Misri ,na kuuweka zaidi mfumo wa Shariah katikati ya sera za taifa.
Lakini mjumbe mwaandamizi wa Ikhwan, Issam al-Aryan, ameiambia BBC kwamba wanataka "taifa la raia kwa mujibu wa misingi ya kiislamu". Taifa la kidemokrasia,lenye mfumo wa bunge ,lenye uhuru wa kuunda vyama,uhuru wa vyombo vya habari na mahakama huru na za haki.

Jumatano, 3 Julai 2013

MANDLA MANDELA ASHITAKIWA KWA KUHAMISHA MAKABURI.


Jamaa za familia ya aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, wamewasilisha kesi ya uhalifu dhidi ya mjukuu wa Mandela,Mandla Mandela.
Msemaji wa polisi, Mzukisi Fatyela aliambia BBC kuwa maafisa wa usalama watachunguza tuhuma dhidi ya Mandla za kufukua makaburi kinyume na sheriaMwendesha mashtaka wa umma, kisha ataamua ikiwa amshtaki Mandla au la.
Inahusisha maiti za watoto watatu wa Mandela ambao inaaminika walifukuliwa na Mandla kutoka makaburi ya familia miaka miwili iliyopita.
Katika kesi nyingine, jamaa kumi na sita wa familia ya Mandela, wanataka kurejesha miili hiyo katika kijiji cha Qunu, ambako Mandela, ambaye anaumwa sana hospitalini anataka kuzikwa akifa.
Kesi hiyo inayosikilizwa katika mahakama kuu ya Mthatha, katika mkoa wa Mashariki iliakhirishwa hapo jana kuanza kusikilizwa leo.
Wiki jana, mahakama ilitoa amri ya muda kwa maiti za watatu hao kuhamishwa kutoka nyumbani kwa Mandla katika kijiji cha Mvezo hadi Qunu, umbali wa kilomiya 22.
Lakini Mandla Mandela, ambaye alitawazwa kama kiongozi wa kijamii na babu yake, sasa anapinga vikali amri hiyo

Jumanne, 11 Desemba 2012

MABILIONI YA NOTI MPYA ZA NIGERIA YAIBIWA KABLA HAZIJASAMBAZWA NA BENKI KUU.

Mamilioni ya noti mpya zapotea Nigeria

Noti mpya za Nigeria
Kampuni inayochapisha noti kwa ajili ya benki kuu ya Nigeria inajaribu kubaini ni vipi noti mpya zenye thamani ya dola zaidi ya milioni kumi na tatu zilipotea.
Kampuni ya Nigeria ya usalama na uchapishaji wa pesa imemfuta kazi kwa muda mkurugenzi wake na mkuu wa usalama huku ikiendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Shirika la kupambana na ufisadi Transparency International, liliiweka Nigeria nambari Thelathini na tano miongoni mwa nchi zenye ufisadi zaidi duniani lakini serikali inapinga hilo

Ijumaa, 15 Juni 2012

BI FATOU BENSOUDA ATEULIWA KUWA MWENDESHA MASHTAKA MPYA WA ICC, AMRITHI MORENO OCAMPO.

Fatou Bensouda
Mwendesha Mashtaka Mkuu mpya wa Mahakama ya Kimataifa ya kukabiliana na Uhalifu wa Kivita ameapishwa mjini Hague hii leo.
Bi Fatou Bensouda, aliyekuwa wakati mmoja Waziri wa Haki nchini Gambia,ndiye Mwafrika na pia mwanamke wa kwanza kushikilia cheo hicho.
Mojawapo wa wajibu wake wa mwanzo ni kumleta Hague mwana wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muamar Gaddafi, Saif al-Islam Gadaffi, ambaye ameshtakiwa kwa makosa dhidi ya binadamu na wakati huohuo kuongoza mashtaka yanayomkabili aliyekuwa kiongozi wa Ivory Coast, Laurant Gbagbo.
Fatou Bensouda amechukua nafasi ya mtangulizi wake aliyeondoka, Luis Moreno Ocampo, ambaye ameongoza mahakama hiyo kwa zaidi ya mwongo mmoja.
Kesi ya rais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, ilisikizwa na mahakama mahakama ya Umoja wa mataifa inayosikiliza kesi za waliohusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe Sierra Leone.
Bi Bensouda amekuwa akihudumu kama naibu wa Luis Moreno-Ocampo anayemaliza kazi yake katika mahakama ya ICC.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa licha ya kwamba Bi Bensouda sio mgeni kwa mambo ya Hague, uteuzi wake unakuja wakati mfumo wa sheria ya kimataifa unahojiwa sana.
Pia anachukua jukumu hilo wakati kuna mtafaruku katika mahakama hiyo huku maafisa wanne wa mahakama hiyo wakiwa wanazuiliwa nchini Libya.
Mwandishi wa BBC anasema kuwa Bi Bensouda anasifika kwa kuwa mtulivu kitu ambacho huenda kimemsaidia katika kazi yake.
Ikizingatiwa kuwa washukiwa wengi ambao kesi zao ziko katika mahakama ya ICC ni waafrika na hili limekosolewa huku ofisi ya mwendesha mkuu wa mashtaka ikisemekana kuwalenga zaidi waafrika.
Inatarajiwa kuwa kwa sababu Bi Bensouda mwenyewe ni Mwafrika tena wakili, huenda akasaidiwa na hili kunyamazisha wakosoaji wake, kulingana na wadadisi.
Mwezi Machi mbabe wa kivita kutoka DRC, Thomas Lubanga alipokea hukumu ya kwanza ya kesi yake ikiwa hukumu ya kwanza kuwahi kutolewa na mahakama hiyo tangu kuundwa kwake miaka kumi iliuopita.
Kikosi cha viongozi wa mashtaka wanataka Lubanga apokee miaka 30 jela kwa makosa ya kutumia watoto kama wanajeshi wakati wa vita mashariki mwa nchi yo kati ya mwaka 2002 na 2003.

Jumanne, 5 Juni 2012

KILELE CHA MAADHIMISHO YA DIAMOND JUBILEE YA MALKIA WA UINGEREZA IMEFIKIA LEO.

Malkia Elizabeth wa Uingereza
Sherehe za Kuadhimisha miaka sitini ya utawala wa malikia Elizabeth zimefikia kilele hii leo Mjini London, Maelfu ya Watu walimshangilia wakati alipojitokeza kwenye Roshani (Balkoni) ya Kasri QASRI ya Buckingham, huku Ndege za Jeshi la ANGA zikipta Angani.
Mapema leo malkia Elizabeth alihudhuria Ibada Maalum ya Kutoa Shukurani katika Kanisa la St. Paul mjini London.Wanasiasa, Mabalozi na Viongozi wa Kigeni pia walihudhuria Ibada hio.
Kwenye hutuba yake kwa Waumini, Kiongozi Kanisa la Ki-Anglikana, Askofu Mkuu Rowan Williams, alimsifu Malkia Elizabeth kwa kujitolea kwake kwa Uingereza.
Baadaye Malkia alihudhuria dhifa ya chakula cha mchana iliyoandaliwa katika ukumbi wa Westminster ambapo baadaye alikwenda kwenye roshani ya nyumba ya Kifalme ya Malkia wa Uingereza ambapo alikuwa akisubiriwa kwa hamu kubwa na umati wa watu.
Maelfu ya watu walijipanga kando ya barabara kumuona Malkia akisindikizwa na walinzi wake.
Hii ndio kilele cha sherehe za kuadhimisha utawala wa miaka sitini wa Malkia. Wanasiasa, mabalozi na viongozi wa kigeni pia walihudhuria.
Kwenye hotuba yake kwa waumini, kiongozi wa ngazi ya juu zaidi katika kanisa la ki-Anglikana, Askofu mkuu Rowan Williams, alimsifu Malkia Elizabeth kwa kujitolea kutumikia raia wa Uingereza: Baadaye kidogo kwaya ilimuimbia Malkia wimbo huu.
Rais wa Marekani Barack Obama alituma pongezi kwa Malkia na raia wa Uingereza kwa siku hii

Jumanne, 29 Mei 2012

MLIPUKO WA NAIROBI WAHUSISHWA NA UGAIDI WA KUNDI LA AL SHABAAB.



Mlipuko wajeruhi 33 Nairobi Kenya, polisi wasema huenda ni ugaidi
Polisi nchini Kenya inasema mlipuko uliojeruhi watu 33 katika mji mkuu Nairobi unaweza kuwa umesababishwa na bomu, baada ya hapo awali kulaumu hitilafu za umeme.
Mlipuko huo uliharibu maduka katika barabara yaMoi Avenuewakati wa mchana.Mtu mmoja aliyeshuhudia alisema kifurushi kiliachwa karibu yake kabla ya mlipuko kutokea.
Waziri Mkuu Raila Odinga amesema mlipuko huo unahusiana na magaidi.
Mwandishi wa BBC Kevin Mwachiro anasema mlipuko huo umesababisha bidhaa mbali mbali kama viatu, nguo na vioo vilivyovunjika kusambaa sehemu yote ya eneohilo.
Picha za Televisheni nchini humo zilionyesha watu wakikimbia mbali na majengo yaliyo karibu katikati ya mji waNairobi.
Awali Kamishna wa Polisi nchini Kenya Mathew Iteere, alisema huenda "hitilafu ya umeme" ndio chanzo cha mlipuko huo, kwa mujibu wa Televisheni ya NTV. Hata hivyo mlipuko huo unaiwekaNairobikatika hali ya wasiwasi.
Kumekuwa na milipuko kadhaa hivi karibuni ndani na nje ya mji huo mkuu huku baadhi ikihusishwa na kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab.
Polisi waliweka kizuizi eneo la mlipuko huo Nairobi.
Timu ya waokoaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu imetumwa katika eneo la tukio kwenye barabara ya Moi. Mtaa huo ni barabara kuu ambayo wakati wa mchana huwa na watu wengi, Shirika la habari la AP linasema.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia kulikuwa na mlipuko mkubwa na huku vipande vipande vya vioo na vitu vingine vikiwarukia na kujeruhi watu waliokuwa karibu, Gazeti la Nation linaripoti

Jumatatu, 9 Aprili 2012

MALAWI YAPATA RAIS MWANAMKE ANAITWA BANDA, AANZA KWA KUMFUKUZA KAZI MKUU WA POLISI.

Rais Banda amfukuza kazi mkuu wa polisi

Rais Joyce Banda amemfukuza kazi mkuu wa Polisi nchini Malawi Peter Mukhito
Rais mpya wa Malawi Joyce Banda amemfuta kazi mkuu wa polisi Peter Mukhito, kwa mujibu wa taarifa zilizotangazwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali.
Bibi Banda aliapishwa kuwa Rais Jumaamosi baada ya kifo cha Rais Bingu wa Mutharika wiki iliyopita.Amekuwa makamu wa Rais tangu mwaka 2009, lakini alikorofishana na Bw Mutharika na kujiondoa kutoka chama chake kinachotawala.
Hakuna sababu iliyotolewa ya kuondolewa kwa Bw Mukhito, lakini mwandishi wa BBC nchini humo anasema ameshtumiwa kwa uongozi mbaya wakati wa ghasia za kuipinga serikali zilizotokea mwaka jana.
Bw Mutharika, mwenye umri wa miaka 78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alkhamisi iliyopita ingawa kifo chake hakikuthibitishwa mpaka siku ya Jumamosi.
Alitawala Malawi kwa kipindi cha miaka minane lakini hivi karibuni alishtumiwa kwa kufisidi uchumi na kutawala kwa mabavu.
Malawi imekumbwa na ukosefu wa mafuta na fedha za kigeni tangu Uingereza na wahisani wengine kufuta misaada yao.
Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani akiwa mjini Blantyre anasema aliyekuwa mkuu wa polisi alianza kupata sifa mbaya mwaka uliopita baada ya kumhoji mhadhiri mmoja kwa kulinganisha vuguvugu la upinzani katika nchi za Tunisia na Misri kuwa sawasawa na mgogoro wa mafuta nchini Malawi.
Tukio hilo hatimaye lilisababisha kufungwa kwa tawi moja la chuo kikuu cha Malawi.
Mnamo mwezi wa Julai mwaka jana ,takriban watu 19 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya kuipinga serikali kuhusu uchumi unaozidi kuzorota nchini humo.
Wakati huo huo maafisa wa serikali wanasema matayarisho yanafanywa kurudisha maiti ya Rais Muthariika kutoka Afrika ya Kusini ambako alisafirishwa baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo

Ijumaa, 6 Aprili 2012

RAIS WA MALAWI YU HOI HOSPITALI BAADA YA KUANGUKA GHAFLA.

Mutharika asafirishwa Afrika Kusini

Rais Bingu wa Mutharika kwa wakati huu amepoteza fahamu kufuatia mshituko wa moyo.
Mutharika apelekwa Afrika Kusini kwa matibabu Kutokana na hali hiyo,Mutharika amesafirishwa hadi Afrika Kusini kwa matibabu zaidi na

aliondoka katika uwanja wa ndege wa Lilongwe milango ya saa sita na nusu usiku kuelekea Johannesbuerg.
Alisafirishwa Afrika kusini katika hali ya usiri mkubwa na akiwa hana fahamu.
Walioandamana nae ni mkewe na jamaa wa karibu zaidi wa rais huyo
Hii imezuia hali ya hofu na utata mkubwa nchini Malawi kwani kwa muda mrefu kumekuwa na shinikizo za kumtaka Mutharika ang’atuke .
Radio ya kitaifa ilikuwa imetangaza kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 78 na ambaye alikuwa hali mahututi atapelekwa hadi afrika kusini kwa matibabu maalum.
Wakati huo huo viongozi wa Malawi walitaka nchi iwe na utulivu huku watu wakimuombea apate afueni.
Afisa mmoja mkuu wa serikali ya Malawi alinukuliwa akisema kuwa Rais Mutharika aliangua akiwa katika makaazi yake rasmi na kupelekwa hospitalini ambako aliwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Akiwa hospitalini chini Malawi, Mutharika alitembelewa na maafisa wakuu katika serikali yake wakiwemo mawaziri, mkewe na wanawe.
Makamu wa Rais Bi Jocye Banda alikuwa wakwanza kuthibitisha habari za kuugua kwa Mutharika.
Kabla ya tamko hilo Bi Banda vyombo vyote vya habari vilikuwa vimebana kutoa habari zozote kuhus hali ya raia Bingu wa Mutharika.
Lakini baada ya Makamu wa rais kufichua kuwa Kiongozi wao ni mgonjwa, ndipo Radio ya kitaifa ikatangaza kuwa Mutharika atapelekwa Afrika kusini kwa matibabu maalum.
Kulingana na katiba ya Malawi ikiwa Mutharika atashindwa kuendelea na kazi yake ya Urais basi Makamu wake Bi Joyce Banda atalazimika kushikilia hatamu za uongozi kwa kipindi kilichosalia .
Hata hivyo Bi banda na rais Mutharika walikuwa hawasikilizani kwani walikosana mwaka wa 2009 na Makamu huyo wa Rais akalazimika kuhamia upinzani

Ijumaa, 16 Machi 2012

BAE KUNUNUA VITABU KWA PESA YA RADA.

BAE yanunua vitabu pesa za Rada Tanzania

Moja ya ndege za BAE, itainunulia Tanzania vitabu vya elimu kwa fedha za rada
Kampuni ya kuuza vifaa vya kijeshi ya BAE Systems itatoa takriban £29.5m kwa miradi ya elimu nchini humo kufuatia makubaliano na Taasisi ya Kupambana na ufisadi ya Uingereza (SFO).
BAE ilipigwa faini ya £500,000 mwaka 2010 kwa kushindwa kutunza rekodi zake za malipo iliyofanya kwa mshauri wake.Malipo hayo yalitolewa kununua rada ya kijeshi kwaTanzaniakwa gharama ya £28m.
Kampuni hiyo ya BAE sasa imethibitisha makubaliano ambayo yatatumika kusaidia watanzaniakamailivyoafikiwa.
Itanunua vitabu vya kiada kwa shule 16,000 vya masomo muhimu ya Kiswahli, Kiingereza, Hisabati na Sayansi.
Fedha hizo pia zitatumika kuwapatia miongozo walimu na mwongozo wa muhtasari wa masomo kwa waalimu wote 175,000 wa shule za msingi, na muhtasari yenyewe, kampuni hiyo ya ulinzi imesema.
Taasisi ya SFO ilisema makubaliano hayo yalikuwa ya kwanza na ya aina yake, lakini ilikosolewa na jaji aliyetoa uamuzi wake kwa kampuni hiyo miaka miwili iliyopita.
"Makubaliano haya ni ya kwanza kwa SFO ambayo iliratibu kutumia mfumo wa sheria za Uingereza,’ mkurugenzi wa SFO Richard Alderman alisema.
'hatma ya jambo lenyewe'
"Tumefurahi kuwa hatimaye tumefikia mahali tunaweza kutoa malipo kwa serikali yaTanzaniana kufikia tamati ya suala hili." BAE ilisema.
BAE iliafikiana na SFO mpango huo mwaka 2010. Ilikubali kulipa faini ya na gharama ya £225,000 kwa SFO – na faini ilikokotolewa kutoka £30m iliyotoa kwa watanzania kumaliza kesi hiyo.
Wakati huo jaji wa mahakama ya Southwark Crown alikosoa makubaliano hayo kati ya SFO na BAE.
"Muundo wa makubaliano hayo unaweka shinikizo la kimaadili kwa mahakama kuifanya faini hiyo iwe kwenye kiwango cha chini kwa ajili ya maandalizi ya juu. " alisema Justice Bean, aliyeongeza kuwa alikuwa kwenye shinikizo la kuiweka faini ya mahakama kuwa ya chini.
Pia alikosoa sehemu nyingine ya makubaliano ambayo alisema yalimpa mjumbe yeyote wa kampuni ya BAE Systems "kinga kwa makosa yote yaliyofanywa nyuma yawe yamewekwa wazi au la".
Kampuni hiyo ililipa £7.7m kwa kampuni mbili zinazomilikiwa na mfanyabiashara Shailesh Vithlani kabla hata ya kushinda zabuni yenyewe ya kununua rada.

Alhamisi, 16 Februari 2012

LIBYA IMESHINDWA KUDHIBITI WAPIGANAJI


misrata
Watu weusi ndio wanateswa zaidi

Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International linasema visa vya mateso, mauaji na watu kuzuiliwa bila kufunguliwa mashataka vimekithiri nchini Libya.
Shirika hilo linasema ukiukaji huo unatekelezwa na makundi ya wapiganji waliojihami ambao walimng'oa Muammar Gaddafi madarakan
Walioathirika zaidi ni watu wanaohofiwa kuwa wafuasi wa Gaddafi, waafrika weusi na wahamiaji walioko Libya.
Kufuatia visa hivyo makundi ya watu waliolengwa sana na visa hivyo wamehama makaazi yao.
Shirika la Amnesty international linasema serikali mpya ya Libya imeshindwa kuwachukulia hatua watu wanaotekeleza vitendo hivyo.
Kuanzia mwezi uliopita BBC imekuwa ikikusanya ushaidi wa mateso yanaoendelea miji ya Misrata, Gharyan na kusini mwa mji mkuu Tripoli.
Ijumaa hii, sherehe zitafanyika kote nchini Libya kuadhimisha mwaka mmoja tangu mapinduzi yaanze ambayo yalitarajiwa kuleta mabadiliko.
Kuna wasiwasi mkubwa sasa kuwa watu waliosaidiwa na NATO kuupindua utawala wa zamani, sasa wanahatarisha siku za baadaye za nchi hii

Ijumaa, 27 Januari 2012

BAADA YA KUHUSISHWA NA MASHTAKA NA ICC, UHURU KENYATTA AJIUZULU UWAZIRI.

Kenyatta aachia ngazi

Uhuru
Uhuru anakabiliwa na mashtaka kutoka ICC
Waziri wa fedha wa Kenya, Uhuru Kenyatta ameachia nafasi yake kufuatia uamuzi kuwa atashtakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinaadam.
Hatua hiyo inakuja baada ya Mahakama ya Kimataifa (ICC) kusema ajibu mashtaka kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2008.
Lakini atasalia kuwa naibu waziri mkuu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais Mwai Kibaki.
Afisa mwingine wa ngazi ya juu serikalini, Francis Muthaura, pia amejiondoa madarakani.
Wawili hao ni miongoni mwa watu wanne waliotajwa na ICC, ambao wote wanakanusha kuhusika kwao katika ghasia za uchaguzi mwaka 2007-08.
Mwanasheria mkuu wa Kenya alisema sio lazima kwa viongozi hao kujiuzulu, akisema hatma yao ingejulikana baada ya matokeo ya rufaa yao kupatikana ya kuzuia kesi ya Mahakama ya Kimataifa kuendelea.
Bw Kenyatta, ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, na ambaye anatajwa kuwa mmoja wa wananchi tajiri zaidi nchini humo, anatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinaadam, ikiwemo mauaji na utesaji. Bw Muthaura anakabiliwa na mashtaka kama hayo pia.
Wawili hao ni washirika wa Rais Mwai Kibaki, ambaye alitoa wito kwa wananchi kuwa watulivu baada ya ICC kuthibitisha mashtaka yake dhidi ya watu hao.
Wanaharakati wamekuwa wakifanya kampeni kwa viongozi hao kuondolewa madarakani.
Mwandishi wa BBC mjini Nairobi amesema haijafahamika bado iwapo Bw Kenyatta ataachana na nia yake ya kuwania urais.
Zaidi ya watu 1,200 waliuawa katika wiki kadhaa za machafuko kati ya Disemba 2007 hadi Februari 2008, huku watu 600,000 wakilazimika kukimbia makazi yao. Wengi bado hawajapata makazi maalum hadi sasa.
Ghasia zilianza baada ya kuzuka mapigano kati ya wafuasi wa wagombea urais Raila Odinga na Mwai Kibaki, na baadaye kufikia kuuana katika misingi ya kikabila.
Waziri wa zamani wa elimu William Ruto na mtangazaji wa redio Joshua arap Sang, ambao walimpinga Bw Kibaki mwaka 2007, pia wanashtakiwa katika kesi nyingine

Jumapili, 8 Januari 2012

RAIS WA SUDAN ZIARAN LIBYA.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan - ambaye anasakwa na Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa kwa mauaji ya watu wengi - yuko nchini Libya kwa ziara ya siku mbili.
Rais Omar al-Bashir wa Sudan
Omar  Bashir wa Sudan.

Shirika la Human Rights Watch limesema, baada ya kuvumilia kwa miongo kadha uongozi wa kikatili wa Kanali Gaddafi, inatia wasiwasi kuwa serikali mpya mjini Tripoli inazungumza na kiongozi mwengine anayetuhumiwa mauaji vitani.
Sudan imesema iliwapatia silaha wapiganaji waliompindua Kanali Gaddafi mwaka jana.
Uhusiano wa Gaddafi na Sudan ulikuwa mbaya kwa sababu Gaddafi akiwasaidia wapiganaji wa Darfur.

Jumanne, 1 Novemba 2011

NDEGE ZA KIJESHI ZA KENYA ZASHAMBULIA AL SHABAAB.

Ndege zililenga kambi ya Al Shabaab

Raia 10 waripotiwa kuuawa na wengine 50 kujeruhiwa baada ya ndege za kivita za Kenya kuwashambulia wapiganaji wa al-shabaab kusini mwa Somalia.
Msemaji wa Jeshi la Kenya ameiambia BBC kuwa ndege hizo zilishambulia maeneo yaliyo viungani mwa mji wa Jilib.
Amesema waliouawa ni wapiganaji wa kundi hilo lililo na ushirikiano na mtandao wa Al-qaeda.
Lakini shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF) limesema kwa sasa linawatibu watu waliojeruhiwa baada ya kambi ya wakimbizi kushambuliwa na kusababisha vifo vya watu watatu.
Majeshi ya Kenya yaliingia hadi Somalia ili kukabiliana na wapiganaji wa al-shabaab.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inawalaumu wapiganaji wa al shabaab kwa kuvuka mpaka sehemu za Kaskazini Mashariki na kushambulia vikosi vya Kenya na pia kwa visa kadhaa vya utekaji nyara.
"Tulipokea taarifa za kijasusi kuwa kiongozi mmoja wa al-shabaab alikuwa amepanga kuzuru kambi ya Jilib na ndipo tukafanya mashabulio kutoka angani " msemaji wa jeshi la nchi kavu la Kenya Meja Emmanuel Chirchir ameiambia BBC.
" Taarifa tulizo nazo ni kuwa wapiganaji 10 wa al-shabaab wameuawa na wengine 47 kujeruhiwa", aliongezea kusema.
Amekanusha habari kuwa kambi ya raia ilishambuliwa akisema taarifa kuwa kambi ya wakimbizi ilishambuliwa na raia wa kawaida kuuawa ni propaganda za al-shabaab.
Hata hivyo katika taarifa yake ya Jumapili ,shirika la MSF limesema kuwa wahudumu katika hospitali iliyoko Marere inawahudumia watu kadhaa waliojeruhiwa kufuatia shambulio la angani katika mji wa Jilib.
Shirika hilo limesema kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani kwa ndani ilishambuliwa majira ya saa saba na nusu mchana, saa za Afrika mashariki na waliopokelewa ili watibiwe wengi wao ni wanawake na watoto.
Kundi hilo la al-Shabaab limekanusha kuwa linahusika na visa vya utekaji nyara nchini Kenya na linataka Kenya iondowe wanajeshi wake au wakabiliwe vikali

Ijumaa, 28 Oktoba 2011

VIPIMO VYA UKIMWI VYA NYUMBANI VINATIA SHAKA.

Onyo juu ya vipimo vya Ukimwi

Moja ya aina ya kipimo cha nyumabani cha HIV.
Vipimo haramu vya nyumbani vya kupimia HIV vinawapa watu matokeo yasiyo sahihi, shirika la kudhibiti dawa na huduma za afya (MHRA) limeonya.
Limesema kuna matatizo mengine pia kwenye vipimo vya magonjwa ya zinaa ambayo ni halali lakini huenda pia vikawa si sahihi.
Chombo hicho kinaufanyia uchunguzi mtandao wa Uingereza unaouza vifaa hivyo.
Wakala wa kulinda afya umewaandikia baadhi ya walioathirika na kuwaeleza kuwa vipimo hivyo havikubaliki.

Jumatano, 26 Oktoba 2011

POLISI WAKAMATA MABOMU NA BUNDUKI NAIROBI.

Usalama umeimarishwa

Mtu mmoja amekamatwa na polisi na silaha mbali mbali kunaswa katika mtaa mmoja mjini Nairobi,Kenya.
Katika nyumba hiyo polisi walinasa maguruneti 13 na bunduki kadhaa pamoja na risasi.
Kwa mujibu wa mkuu wa polisi nchini Kenya Mathew Iteere, mtu aliyekamatwa anashukiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi.
"Sina shaka kuwa tutapata habari muhimu kutoka kwake na kuweza kuwatia mbaroni wanachama wengine wa makundi ya kigaidi," alisema.
Majirani wanasema mtu huyo alihamia katika nyumba hiyo ya kupanga kama mwezi mmoja uliopita na kwamba hawajawahi kumuona mtu mwingine yeyote hapo.
Polisi wanasema walivamia nyumba hiyo kutokana na taarifa za kijasusi walizopata.
Hatua hiyo inakuja baada ya mashambulio mawili kutokea katika maeneo tofauti mjini Nairobi.Katika mashambulio hayo mtu mmoja alifariki dunia na wengine zaidi ishirini kujeruhiwa

Ijumaa, 21 Oktoba 2011

ICC YAISHUTUMU MALAWI KWA KUTOMKAMATA AL-BASHIR.

Rais Omar al-Bashir

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC imeitaka Malawi kueleza kwanini ilishindwa kumkamata Rais wa Sudan Omar al-Bashir katika ziara yake ya hivi karibuni.
ICC imetoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Bw Bashir kwa mashtaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita wakati wa mgogoro huko Darfur.
Malawi ni moja ya nchi zilizotia saini makubaliano ya kuridhia mahakama ya ICC lakini imesema "si kazi yake" kumkamata Bashir.
Bw Bashir amekana mashtaka hayo, akisema yamechochewa na masuala ya kisiasa.
Umoja wa Afrika ulishawishi hati hiyo ya kukamatwa iahirishwe, ikiishutumu ICC kwa kuchunguza tu madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika na kukamatwa kwa rais wa Sudan kutazuia utafutaji wa amani Drafur.
Bw Bashir alilakiwa na gwaride la heshima alipowasili kwenye mji mkuu, Lilongwe, katika mkutano wa masuala ya biashara mwishoni mwa juma.
Umoja wa Ulaya na makundi ya kutetea haki za binadamu yaliisihi Malawi kumkamata Bw Bashir.
Lakini waziri wa habari Patricia Kaliati aliiambia BBC kwamba wasingeweza kumkamata Bw Bashir kwani alikuwa akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika (comesa).
Alisema, " Anakuja kikazi na kukamatwa kwa Rais Bashiri hakutuhusu."
Kenya na Chad, ambao wote nao wametia saini mkataba huo wa ICC, wamemruhusu Bw Bashir kutembelea nchi zao.
ICC imeiandikia Malawi kuiomba kufanya "uangalizi" wa ziara ya Bw Bashir kabla ya Novemba 11.
Rais wa Malawi Bingu wa Mutharika ni miongoni mwa viongozi wengi wa Afrika wanaoishutumu ICC kwa kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita barani Afrika tu na si maeneo mengine.
Bw Bashir alikuwa rais wa kwanza kushtakiwa na ICC, iliyomshutumu kwa mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita Darfur

Ijumaa, 23 Septemba 2011

PATRIOTIC FRONT ZAMBIA YASHINDA UCHAGUZI

Kiongozi wa Upinzani aliyeshinda Uchaguzi Zambia, Michael Satta

Mpinzani ashinda uchaguzi Zambia

Kiongozi wa chama cha Patriotic Front, MichaEl Sata ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Zambia
Bw Sata alipata asilimia 43 ya kura zilizopigwa na kumshinda Rais Rupiah Banda wa chama tawala cha MMD ambacho kimekuwa mamlakani kwa muda wa miaka 20.
Michael Sata
Kiongozi wa Patriotic Front ameshinda uchaguzi wa urais Zambia


Tangazo hilo lilitolewa na Jaji Mkuu wa Zambia Ernest Sakala.
Awali watu wawili waliuawa kufuatia ghasia katika maeneo ambayo ni ngome ya upinzani.
Mkuu wa Polisi wa jimbo hilo maafuru kwa uzalishaji Shaba ameliambia shirika la habari la Reuters watu wamejitokeza katika barabara za mji wa Kitwe na Ndola wakivurumisha mawe.
Mwandishi wa BBC anasema ghadhabu hizi zimechochewa na agizo la serikali kupiga marufuku vyombo vya habari kutangaza matokeo bila ya idhini ya tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.
Mwandishi wa BBC Mutuna Chanda akiwa Lusaka kilomita 300 kusini mwa Kitwe, anasema huko Kitwe, waandamanaji waliteketeza soko moja usiku na Polisi wameweka vizuwizi katika mji wa Wusaikile.
Rais Banda alimshinda Bw Sata kwa kura 35,000 katika uchaguzi wa mwaka 2008, matokeo yaliozusha ghasia kutoka upande wa upinzani katika ngome zao za mijini.
Tangu uchaguzi wa mwaka 2008, watu wengine milioni moja wamejiandikisha kuwa wapiga kura,wengi wao vijana wasio na ajira

Ijumaa, 16 Septemba 2011

WALIOLIPUA MABOMU MGAHAWA WA WAETHIOPIA UGANDA WAHUKUMIWA

 
Eneo lilokumbwa na mashambulio ya bomu
Eneo lilokumbwa na mashambulio ya bomu
Raia wawili wa Uganda wamehukumiwa kifungo gerezani kwa kuhusika na mashambulizi ya bomu mwaka 2010 ambayo yalisababisha vifo vya watu 76 katika mji mkuu wa Uganda Kampala.
Edris Nsubuga, ambaye amekiri kutega mabomu amehukumiwa miaka 25 gerezani, ihali Muhamoud Mugisha amehukumiwa kifo cha miaka mitano kwa kuhusika katika njama ya kufanya mashambulizi hayo .
Wanamgambo wa Kiislamu wa Somalia al-Shabab walisema walitekeleza mashambulio hayo .
Mabomu hayo yalitegwa katika mkahawa mmoja ambao pia ulikuwa na sehemu ya baa ambako watu walikuwa wamekusanyika kutazama fainali ya kombe la dunia katika televisheni.
Al-Shabab, kundi ambalo linahusishwa na mtandao wa al-Qaeda, linasema kuwa mashambulio hayo yalifanywa kulipiza kisasi cha jeshi la Uganda kuunga mkono serikali ya mpito ya Somalia.
Edris Nsubuga ambaye alikuwa akabiliwe na hukumu ya kifo ,ameepuka hukumu hiyo baada ya kukiri makosa yake.
Mapema wiki hii alikiri mashtaka matatu ya ugaidi yanayohusisha pia "nia ya kupeleka na kutega mabomu".
Natumai atatumia wakati wake gerezani kutafakari aliyoyatenda ambayo yamenilazimu nimuweke kando na jamii
Jaji Alfonse Owiny-Dollo
Jaji Alfonse Owiny-Dollo alisema kuwa Nsubuga aliomba msahama na kusema alitumiwa wakati ambapo hangeweza kufanya maamuzi yafaayo kwani wakati huo alikuwa anakabiliwa na matatizo mengi ya nyumbani.
Muhamoud Mugisha nae alikiri kuhusika na njama za kutenda vitendo vya kigaidi.
Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo mwaka jana Mugisha alisema anauhusiano na al-Qaeda.
Washukiwa wengine 12 wamekanusha mashtaka hayo na kesi yao inaendelea.
Washukiwa watano walifutiwa mashtaka dhidi yao kutokana na upungufu wa ushahidi, walikuwa nipamoja mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya Al-Amin Kimathi ambaye alizuiliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja korokoroni.
Alikuwa ameishutumu serikali ya Kenya kwa kuwahamisha kinyume na sheria washukiwa hadi Uganda na alikuwa amekwenda Uganda kuwapa ushauri washukiwa hao wakati alipokamatwa na kuzuiliwa.
Amesema alikuwa anaadhibiwa kwa kazi yake ya kutetea haki za binadamu ambayo ilifichua mpango wa washikiwa kusafirishwa kwa siri hadi nchi nyengine ambako hufanyiwa mahojiano na maafisa wa upelelezi

Jumamosi, 27 Agosti 2011

RAIS WA KENYA AWAFUKUZA KAZI BAADHI YA MAWAZIRI

Waziri ambaye ni mmoja ya watuhumiwa sita wakuu wa machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Kenya Uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,300 amefutwa kazi.
William Ruto

Rais Mwai Kibaki pia amemrudisha kazini Waziri wa Maswala ya nchi za njee aliyekuwa amesimamishwa kazi kufuatia tuhuma za ufisadi.
William Ruto ambaye ni mmoja ya washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini kenya, amefutwa kazi kama Waziri wa Elimu ya Juu.
Kufutwa kazi kwa Ruto kunakuja wakati Bwana Luis Moreno Ocampo akimsubiri huko The the Haegue kuanzia 1 September, 2011 ili uthibitishaji wa kesi inayomkabili kuhusu ghasia za zilizoikumba kenya mwaka 2008 ianze kusikilizwa.
Taarifa kutoka idara ya habari za rais pia zimesema kuwa waziri wa Afrika Mashariki profesa Hellen Sambili pia ametimuliwa. Ruto na Sambili wanatoka eneo la Rift Valley
Nafasi zao zimechukuliwa na wabunge wengine kutoka jimbo hilo hilo la Rift valley ,Prof. Margaret Kamar kama waziri mpya wa Elimu ya juu na Musa Sirma akiwa waziri mpya wa Afrika Mashariki.
Waziri Mkuu Raila Odinga

Wengine walifutwa kazi ni manaibu waziri wanne ambao wamekuwa ni wapambe wa William Ruto. Huku wakiasi chama chao cha ODM cha waziri Mkuu Raila Odinga na kukipigia debe chama kidogo cha UDM chenye ufuasi mkubwa eneo la Rift valley.
Na waziri wa Maswala ya nchi za Njee, Moses Wetangula ambaye alisimamishwa kazi karibu mwaka mmoja ulipita kutokana na kashfa ya kuuza majumba ya ubalozi wa Kenya nchini Japan amerudishwa kazini .
Kurudishwa kazini kwa Wetangula kumempa siku moja peke yake ya kujiandaa kabla ya kusafiri moja kwa moja hadi Addis Ababa, Ethiopia kuwakilisha Kenya katika mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Umoja wa Afrika kwa minajili ya kukusanya pesa za kusaidia kukabiliana na njaa katika upembe wa Afrika.
Lakini taarifa hiyo fupi haikusema kama uchunguzi uliokuwa ukiendelea kumhusu bwana Wetangula umekamilika na kumundolea lawama.
Taarifa hiyo inasema kuwa Rais Kibaki amefanya madadiliko hayo baada ya kushauriana na waziri Mkuu Raila Odinga.
Hata hivyo halmashauri ya kukabiliana na ufisadi nchini kenya imeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya kumrudisha kazini bwana Wetangula. Tume hiyo imesema ilikuwa bado inamchunguza Waziri huyo