Jumatano, 14 Desemba 2011

BADO UTATA WAGUBIKA KIFO CHA KONSTEBO DAVID ALIYEJIUA LINDONI NMB.

Askari Polisi wakijaribu kuwatawanya wananchi waliokuja kushuhudia tukio hilo la askari kujiua nje ya Makao Makuu ya Benki ya NMB mtaa wa Azikiwe na Jamuhuri.

ASKARI Polisi, Konstebo David Selemani (22) aliyejiua kwa kujipiga risasi jijini Dar es Salaam inadaiwa kabla ya kuchukua uamuzi huo, aliwasiliana na ndugu zake wengi wakiwemo ambao hakuwa amewasiliana nao kwa muda mrefu.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile ambaye kwa mujibu wake polisi inaendelea na uchunguzi kubaini sababu za kufanya hivyo, alisema hatua hiyo iliwashangaza ndugu hao.


Shilogile alisema uchunguzi unaofanyika ni pamoja na kuwasiliana na kampuni ya simu ya mtandao aliokuwa akiutumia ili kufahamu mtu aliyekuwa akiwasiliana naye kabla ya kujiua.


Kwa upande wa ndugu na marafiki wa askari huyo waliozungumza na gazeti hili kabla ya mwili wake kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa maziko, walisema wanaendelea kujiuliza maswali bila majibu juu ya sababu za jamaa yao kuchukua uamuzi huo.


Katika kuaga mwili wa Konstebo David katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, mmoja wa ndugu aliyejitambulisha kwa jina moja la Danny, alisema siku moja kabla ya kujiua, alizungumza naye kwa simu akimtaka waonane.


“Mimi shughuli yangu ni dereva, na kwa bahati mbaya siku hiyo nilikuwa safarini, hivyo nilimtaka wakaonane na kaka yangu ili wazungumze kama kulikuwa na jambo la haraka la kuzungumza, sababu nilijua lingeweza kupatiwa majibu na kaka,” alisema Danny.


Alisema siku iliyofuata, akiwa njiani kurudi Dar es Salaam, alishitushwa kupata taarifa za msiba wa David, suala alilodai kuwa limemuacha na maswali mengi juu ya kile kilichosababisha ajiue.



Alisema David aliyezaliwa Desemba mwaka 1989, alikuwa ni mtoto pekee kwa wazazi wake ambao hata hivyo wote walishafariki kipindi akiwa anasoma kidato cha kwanza na hivyo kulazimika kulelewa na ndugu zake.


Kifo cha askari huyo, mbali na kuwashitua ndugu na jeshi la Polisi, pia majirani waliokuwa wakiishi jirani kwa mama yake mkubwa eneo la Kimara Baruti, walimsifu kijana huyo kwa upole.


Mwili wa marehemu unatarajia kuzikwa leo katika Kijiji cha Mambamiamba, Gonja, wilayani Same mkoani Kilimanjaro.


David alijiua kwa kujipiga risasi mbili, kidevuni na kwenye koromeo na kusababisha kichwa chake kufumuka.


Alichukua uamuzi huo wakati akiwa lindoni katika makao makuu ya Benki ya NMB iliyopo katika Mtaa wa Azikiwe, Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni