Jumanne, 24 Januari 2012

TAKUKURU YAICHUNGUZA SIMBA NA YANGA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) sasa imenyoosha makucha yake michezoni kwa kuivalia njuga kashfa ya upangaji wa matokeo ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga.



 
PCCB Chief, Edward Hoseah.


Jaribio hilo lakupanga matokeo lilifanyika siku chache kabla Simba na Yanga hazijakutana katika mechi ya mzunguko wa Kwanza Tanzania Bara iliyofanyika Oktoba 29, 2011 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi hiyo Yanga ilishinda 1-0.

Habari za uchunguzi zinaeleza kwamba tayari Takukuru imekwishawahoji watu kadhaa akiwemo kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Simba (jina linahifadhiwa) na wachezaji wa Yanga, wiki iliyopita.

Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alithibitisha kuwa suala hilo lilikuwa mezani kwao ingawa hakutaka kuingia kwa undani kuhusiana na uchunguzi wao.
“Suala hilo lipo mikononi mwetu linafanyiwa kazi, upelelezi ukikamilika tutatoa tamko,” alisema.

Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba upelelezi unamlenga zaidi kiongozi huyo wa Simba anayedaiwa kumpigia simu mshambuliaji wa Yanga, Pius Kisambale, siku chache kabla ya pambano lao wakati Yanga ikiwa kambini kwenye Hoteli Double Tree iliyoko Masaki, jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinasema, wakati Kisambale anapigiwa simu alikuwa na baadhi ya viongozi wa Yanga na kwamba simu hiyo iliwashtua viongozi hao, hivyo kumfanya mchezaji huyo aongeze sauti ili nao wasikie kilichozungumzwa.

Shuhuda wa tukio hilo anaeleza kwamba mshambuliaji huyo alirekodi maneno ya kiongozi huyo mzito wa Simba, kitendo ambacho pia kilifanywa na viongozi waliokuwa wamemzingira.

Katika mazungumzo hayo, inaelezwa kwamba kiongozi huyo wa Simba alimtaka Kisambale acheze chini ya kiwango ikiwa atapangwa na kuahidi kumpatia ‘mzigo’ huku akimwomba awaeleze na wenzake juu ya mpango huo.

Hali hiyo inaelezwa kuwakasirisha viongozi wa Yanga walioamua kulipeleka suala hilo Takukuru ili mhusika achukuliwe hatua za kisheria.

Taarifa zaidi zinasema wiki iliyopita Takukuru ilimhoji Kisambale na wachezaji kadhaa wa Yanga katika ofisi yao iliyoko Upanga jijini dare s Salaam.

Mbali ya Kisambale, kiongozi huyo wa Simba pia amehojiwa na Takukuru kuhusu kashfa hiyo inayoonyesha kukubuhu kwa vitendo vya rushwa michezoni kiasi cha kuporomosha kandanda nchini.

“Rushwa imetawala michezoni na watu wanalichukulia kama shamba la bibi bila kujali namna kiwango cha michezo kinavyoporomoka. Sasa watu wamechoka,” kilisema chanzo hicho.

Kisambale aligoma kuzungumzia suala hilo na kusema hafamu chochote, huku Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa akiruka kimanga na kusema hawezi kulizungumzia.

“Siwezi kuzungumzia,nendeni mkamuulize huyo kiongozi wa Simba mwenyewe, mambo haya yako kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa upelelezi umehusisha mawasiliano mbalimbali ya simu kati ya wachezaji wa Yanga na kigogo huyo wa Simba huku taarifa nyingine zikiongeza kwamba hata mawasiliano baina ya kiongozi huyo na baadhi ya waandishi wa habari za michezo nayo yanachunguzwa.

Mbali ya suala hilo, Takukuru pia inadaiwa kuchunguza kashfa inayomhusisha mshambuliaji wa Simba Ulimboka Mwakingwe aliyetaka kumhonga kipa wa zamani wa Mtibwa, Shabaan Kado katika msimu wa 2010/2011.

Ulimboka alikamatwa na walinzi wa kiwanda cha sukari Mtibwa akiwa na fedha zinazodaiwa zilikuwa rushwa kwenda kwa Kado ili aachie mabao katika mechi yao ya Ligi Kuu.

Vyanzo vya habari vinasema tayari Kado anayeidakia Yanga kwa sasa, amekwishahojiwa na Takukuru, ingawa mwenyewe amegoma kuzungumzia kilichoendelea kwenye mahojiano hayo.

Matokeo ya uchunguzi huo yanaweza kubadili sura ya soka la Tanzania ambalo kwa miaka kadhaa limekumbwa na kashfa nyingi za rushwa, upangaji wa matokeo na uamuzi mbovu, hasa likizihusisha timu za Simba na Yanga


Source: http://www.wavuti.com/

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni