Jumatatu, 23 Januari 2012

DK. SLAA USO KWA USO NA DK. KIKWETE, ILIKUWA JUZI IKULU YA DAR KATIKA MAZUNGUMZO YA KATIBA MPYA.

Mheshimiwa Rais Kikwete akisalimiana na Dk. Slaa juzi usiku Ikulu alipowakaribisha viongozi wa CHADEMA kwa mazungumzo mafupi juu ya Katiba mpya
.
RAIS Jakaya Kikwete amekutana na uongozi wa Chadema Ikulu Jijini Dar es Salaam, akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, kuzungumzia mchakato wa Katiba Mpya.Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili, mkutano huo ulifanyika jana kuanzia saa 10:30 jioni na kuendelea hadi usiku, lakini walifanya mapumziko mafupi saa tatu usiku.

Ujumbe wa Chadema uliokuwa wa watu wanane, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe. Wengine waliofuatana naye pamoja na Dk Slaa ni  Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, John Mnyika, Said Arfi, John Mrema, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari. Hadi tunakwenda mitamboni kikao hicho kilikuwa kinaendelea.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Slaa kukutana na Rais Kikwete tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambao Dk Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34 akiwa nyuma ya Rais Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17, Dk Slaa hakuwahi kukutana na mkuu huyo wa nchi ana kwa ana.

Katika hafla ya kutangazwa matokeo ya urais iliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwenye Ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam, Dk Slaa hakuhudhuria tofauti na ilivyokuwa kwa waliokuwa wagombea wenzake wote.

Dk Slaa, ambaye alikataa kuyatambua matokeo hayo, tangu wakati huo hawakuwahi kukutana rasmi na Rais Kikwete huku uvumi ukizagaa kwamba  kwamba mwanasiasa huyo amekuwa akijaribu kukwepa asikutane ana kwa ana na Rais Kikwete kwenye mazingira yoyote.

Katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya chama hicho, Regia Mtema yaliyofanyika katika Kijiji cha Lipangalala, hivi karibuni Dk Slaa alidaiwa kumkwepa Rais Kikwete, kwa kutokwenda kukaa kwenye nafasi aliyoandaliwa jirani na kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Ilidfaiwa kuwa nyumba kulikofanyika shughuli za awali za mazishi, waandalizi waliandaa majukwaa mawili, moja maalumu kwa ajili ya wabunge huku jingine likiwa ni maalumu kwa ajili ya viongozi wakuu ambalo alikaa Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe.

Mbali ya kukaa viongozi hao, kulikuwa na nafasi ambayo ilikuwa imetengwa maalumu kwa ajili ya Rais. Mbali ya nafasi hiyo, pia kulikuwa na kiti ambacho ilitegemewa kwamba Dk Slaa angekalia.

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Chadema alidaiwa kukikwepa na kwenda kujichanganya katika jukwaa la wabunge na kiti hicho kubaki bila ya kukaliwa na mtu.

Hata hivyo Dk Slaa alikanusha uvumi huo na kudai kwamba asingeweza kwenda kukaa jukwaa alilokaa Rais Kikwete kwani yeye si kiongozi wa serikali hivyo kwa mujibu wa itifaki, asingeweza kumfuata Rais Kikwete na kwenda kumsalimia alipoketi.

Hii ni  mara ya pili kwa ujumbe wa Chadema kukutana na Rais Kikwete Ikulu  kuzungumzia mchakato wa Katiba Mpya

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni