Jumapili, 8 Januari 2012

CHAZ BABA AIHAMA TWANGA PEPETA, HUENDA AKAJIUNGA NA MAPACHA WATATU.



NewsImages/6172494.jpg
Charles Gabriel au maarufu kwa jina la 'Chaz Baba'
Mwimbaji wa kutumainiwa wa bendi ya muziki wa dansi ya The African Stars 'Twanga Pepeta' Charles Gabriel au maarufu kwa jina la 'Chaz Baba' ametangaza kujitoa katika bendi hiyo na kufanya shughuli zake mwenyewe.
Chaz Baba alitangaza mbele ya waandishi wa habari kuwa kujitoa kwake Twanga Pepeta kumetokana na mambo mengi mojawapo ni kutokuwa na mkataba wa kazi.

Alisema tangu ajiunge na bendi hiyo mwaka 2005 hajawahi kupewa mkataba wowote wa kazi zaidi ya kulipwa mshahara tu kitu ambacho amekiona kama ni kinyume na utaratibu wa kazi.

Chaz Baba aliongeza kuwa kuanzia sasa atakuwa chini ya meneja wake aliyemtaja kwa jina la Benard Msekwa.

“Kwa sasa nitakuwa nasimamiwa na meneja wangu mpya (Msekwa) hivyo kila kitu kinachohusu masuala yangu ya kazi ama ya kisanii kwa ujumla kitakuwa chini yake, kama ni onyesho ama kuhamia bendi nyingine yeyote ni juu yake", alisema Chaz Baba.

Aidha mwimbaji huyo maarufu aliongeza kuwa baada ya kujitoa Twanga Pepeta anatarajia kuzindua albamu yake binafsi yenye nyimbo nane.

"Mpaka sasa nimeishakamilisha vibao kama sita hivi hivyo katika miezi ya karibuni nadhani albamu nzima itakuwa imekamilika", alisema Chaz Baba.

Alizitaja baadhi ya nyimbo kwenye albamu yake kuwa ni pamoja na "Nusu Chizi" ambayo amewashirikisha "Mapacha Watatu" na nyimbo zingine kama vile "Blandina", "Papa Fred", "Mayasa" na "Ninaelekea wapi".

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni