Alhamisi, 8 Agosti 2013

YANGA YAITISHA MKUTANO WA WANACHAMA WOTE AUGUST 18 KUJADILI UDHAMINI WA AZAMTV.


Na Majuto Omary na Vicky Kimaro Mwananchi 
Yanga ndiyo klabu pekee kati ya 14 zitakazoshiriki Ligi Kuu Bara kugomea udhamini wa Azam, ikidai Sh100 milioni ambazo klabu zitapewa kila mwaka kwa miaka mitatu ni ndogo.
Azam Televisheni imekubali kudhamini Ligi Kuu Bara kwa kurusha ‘live’ mechi zote kwa miaka mitatu. Mkataba huo na Bodi ya Ligi una thamani ya Sh5.6 bilioni.
Kwa takriban wiki tatu sasa, Yanga imekuwa na malumbano na televisheni ya Azam ikidai kuwa siyo haki kwa kampuni hiyo kuonyesha mechi za Ligi Kuu Bara kwani wana timu inayoshiriki ligi hiyo.
Katika hoja nyingine ya msingi kupinga udhamini huo, uongozi wa Yanga unadai kuwa klabu husika hazikushirikishwa kikamilifu kujadili na hatimaye kukubali udhamini. Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema jana kuwa mkutano huo umepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa PTA Agosti 18 na ajenda kuu kujadili haki ambayo Azam wanatarajia kupewa.
Mwalusako alisema kuwa maandalizi ya mkutano huo yamekamilika na kuwataka wanachama kufika kwa wingi ili kuweka maazimio ambayo yatapelekwa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF).
“Katiba ya Yanga imewapa fursa wanachama kutoa uamuzi juu ya masuala mazito kama yaliyojitokeza kwa sasa. Uongozi umeyaona matatizo kwani yanapingana na utaratibu wa sheria za soka,” alisema Mwalusako.
“Klabu zimekutana na kufanya mkutano kutupinga sisi, hii ni ajabu sana, sisi hatujapingana na wao, sisi tumepinga bodi ya Ligi (TPL) na TFF kwa kusaini mkataba na Azam Televisheni,” aliongeza.
“Kuna klabu zimeundwa juzi tu, hazijawahi hata kutwaa ubingwa wa Bara, wameingia kwenye mkumbo wa suala hili bila kujua athari zake za baadaye. Sisi kama viongozi tunalinda na kutetea masilahi ya Yanga.”
Wakati huohuo, Yanga leo inacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kama alama ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Mchezo huo dhidi ya timu ya 3 Pillars ya Nigeria utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya timu nyingine ya Ligi Kuu, Mtibwa Sugar kwenye uwanja huohuo mwanzoni mwa wiki hii.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni