Jumatano, 7 Agosti 2013

BARAZA LA USHINDANI NCHINI(FCT) LAJINADI MBELE YA WAANDISHI WA HABARI JANA.



Mchumi Mshauri wa Baraza la Ushindani (FCT) Bw. Nzinyangwa Mchany (kulia) akieleza kwa waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya Baraza hilo tangu kuanzishwa na serikali chini ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003, leo jijini Dar es salaam kushoto Mwanasheria Mshauri wa Baraza hilo Bi. Hafsa Said.




Mwanasheria Mshauri wa Baraza la Ushindani (FCT) Bi. Hafsa Said(kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari sheria mbalimbali na kesi ambazo zimeshawahi kuendeshwa na baraza hilo, kwenye mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari, kulia ni Mchumi Mshauri wa Baraza hilo Bw. Nzinyangwa Mchany.

(Picha na Hassan Silayo)

 BARAZA LA USHINDANI (FAIR COMPETITION TRIBUNAL – FCT)

MADA KUHUSU BARAZA LA USHINDANI ILIYOWASILISHWA KWA WAANDISHI WA HABARI TAREHE 6 AGOSTI 2013, KATIKA UKUMBI WA HABARI MAELEZO, DAR ES SALAAM

Utangulizi
 
Ndugu Waandishi wa Habari, mada yetu inahusu Baraza la Ushindani. Katika mada hii tunatarajia kuliezea Baraza la Ushindani kuwa ni chombo cha namna gani, majukumu yake na uwezo wake kisheria. Hivyo, ili kuweza kuwapa maelezo yatakayoweza kuwasidia kuandika makala zenu vizuri mada hii imejengwa katika sehemu tatu kuu kama ifuatavyo:
  1. Chimbuko la Baraza la Ushindani;
  2.  Baraza la Ushindani ni nini
  3. Majukumu na Uwezo wa Baraza.
 
Chimbuko la Baraza la Ushindani
Bila shaka mtakumbuka kwamba katika jitihada za kuboresha na kuimarisha uchumi mwaka 1986, Serikali ya Tanzania iliamua kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa uchumi kutoka kwenye mfumo wa uchumi hodhi (planned economy) na kufuata mfumo wa uchumi wa soko (Market Economy). Kwa kifupi katika Mfumo wa uendeshaji wa uchumi hodhi maamuzi yote makubwa yanayohusisha uendeshaji wa uchumi hufanywa na Serikali, wakati katika mfumo wa uchumi wa soko, maamuzi yote makubwa hufanywa kwa kutegemea mwelekeo na nguvu ya soko.   Aidha, mfumo wa uchumi wa soko unashirikisha kwa kiasi kikubwa sekta binafsi. Katika mfumo huu huduma na bidhaa sokoni hutolewa na kuuzwa kwa ushindani. Uzoefu duniani umeonesha kuwa bila kuwa na usimamizi mzuri wa ushindani sokoni migongano na mivutano ya kimasilahi hutokea na kusababisha kutofikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuanzishwa mfumo wa uchumi wa soko.
Kwa hiyo ili kupata matunda yaliyokusudiwa kutoka kwenye mfumo wa uchumi wa soko, Serikali iliazimia kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa ushindani sokoni pamoja na udhibiti kwenye sekta za miundombinu, huduma za maji, nishati na mawasiliano.  Utekelezaji wa azma hiyo ya Serikali ukasababisha kuanzishwa kwa vyombo vya udhibiti katika sekta hizo. Vyombo hivyo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),  Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri wa Anga (TCAA), na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Aidha, Serikali kupitia Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003 iliunda vyombo vitatu muhimu ambavyo ni Tume ya Ushindani (FCC), Baraza la Ushindani (FCT) na Baraza la Taifa la Utetezi wa Mlaji (NCAC). Nia ya uanzishaji wa vyombo hivi vyote ni kusimamia biashara zizifanyike kiholela, kuhakikisha panakuwepo na ustawi wa mlaji na pia kuona kwamba kunakuwa na ufanisi katika utumiaji wa rasilimali zilizopo, soko na uchumi kwa ujumla. Kwa hiyo Baraza la Ushindani ni chombo kimojawapo  kilichoanzishwa kufuatia mabadiliko hayo ya kichumi.
Baraza la Ushindani ni nini na madhumuni yake ni nini
Baraza la Ushindani au kwa lugha ya Kiingereza “Fair Competition Tribunal” na kwa kifupi “FCT” ni chombo huru cha kimahakama kilichoanzishwa na Serikali chini ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 (Fair Competition Act, No. 8/2003). Madhumuni ya kuanzishwa Baraza hili ni kuwa chombo maalumu cha kimahakama kitakachopokea, kusikiliza na kuamua kwa haraka rufaa zitokanazo na maamuzi au amri za Tume ya Ushindani na Mamlaka nne za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi ya mawasiliano zilizotajwa kwenye aya zilizotangulia.
 
Majukumu na Uwezo wa Baraza
Jukumu kuu la Baraza la Ushindani ni kupokea, kusikiliza na kuamua kesi za rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission – FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti zifuatazo:
  1. Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA);
  2. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA);
  3. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA); na
  4. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano na Utangazaji (TCRA).
Uwezo wa Baraza la Ushindani umeainishwa kwenye Sheria ya Ushindani Na 8 ya mwaka 2003 pamoja na Kanuni za Baraza (The Fair Competition Tribunal Rules 2012) Tangazo la Serikali Na. 2019 la tarehe 22 Juni 2012.
Katika kutekeleza majukumu yake, Baraza la Ushindani linaweza kufanya, kwenye shauri la rufaa, lolote kati ya haya yafuatayo:-
1.                   Kuthibitisha, kugeuza au kubadilisha uamuzi wa Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika;
2.                   Kurejesha shauri kwenye Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika pamoja na maelekezo litakayoona yanafaa kutolewa;
3.                  Kuamuru Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika kuendesha shauri upya; na
4.                  Kutoa amri yoyote muhimu kufuatia uamuzi wake.
Kimsingi, kila mtu anaruhusiwa kuleta maombi ya rufaa kwenye Baraza la Ushindani, hii ni awe mtu binafsi ama ni kampuni ya Biashara au taasisi.  Hata hivyo kwa kuwa Baraza la ushindani ni Mamlaka  ya Rufaa, kama ilivyo katika Mahakama za kawaida, ili mtu binafsi, Kampuni au Taasisi yoyote iweze kuleta maombi ya rufaa kwenye Baraza la ushindani, ni lazima mtu, Kampuni au Taasisi hiyo iwe ni mdaawa (Party) katika mgogoro uliozaa uamuzi unaoombewa rufaa. Lakini pia mtu, Kampuni au Taasisi inaweza kuomba kuunganishwa kwenye rufaa kama muathirika wa uamuzi unaoombewa rufaa hata kama haikuwa mdaa katika shauri hilo.
Hivyo ndugu waandishi wa Habari kwa kifupi tumeweza kuona kuwa Baraza la Ushindani ni chombo cha kimahakama kilichoanzishwa na Serikali chini ya Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 kuwa chombo maalumu cha Rufaa kitakachopokea, kusikiliza na kuamua rufaa zitokanazo na maamuzi au amri za Tume ya Ushindani na Mamlaka nne za udhibiti kwenye sekta za miundombinu na matumizi ya mawasiliano zilizotajwa. Chimbuko la kuanzishwa Baraza la Ushindani ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa uchumi, pia tumeeleza kuhusu majukumu ya Baraza na kwamba katika kutekeleza majukumu yake, Baraza linaweza kuthibitisha, kugeuza au kubadilisha uamuzi wa Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika; Kurejesha shauri kwenye Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika pamoja na maelekezo litakayoona yanafaa kutolewa; Kuamuru Tume ya Ushindani au Mamlaka ya Udhibiti husika kuendesha shauri upya; na Kutoa amri yoyote muhimu kufuatia uamuzi wake.
Aidha kimsingi, mtu anayeleta  maombi ya rufaa kwenye Baraza la Ushindani anahitaji kufuata taratibu kama zilivyoainishwa katika Kanuni (Rules) za Baraza zilizotajwa hapo juu.
 
Nzinyangwa E. Mchany
MKUU WA KITENGO CHA MASUALA YA UCHUMI
Simu 0754 720007

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni